Wanawake Waishi Zaidi Lakini si Lazima Maisha Bora
ULIMWENGUNI kote wanawake wanaolewa wakiwa na umri mkubwa zaidi, wana watoto wachache, na wanaishi maisha marefu zaidi. “Maisha ya wanawake yanabadilika,” laripoti gazeti UNESCO Sources. Kati ya 1970 na 1990, matazamio ya urefu wa maisha ya wanawake wakati wa kuzaliwa yaliongezeka kwa miaka minne katika nchi zilizoendelea na kwa karibu miaka tisa katika nchi zinazoendelea. “Hii yamaanisha kwamba leo katika nchi zilizoendelea, wanawake huishi kwa wastani wa miaka 6.5 zaidi ya wanaume. Katika nchi zinazoendelea tofauti ni miaka mitano katika Amerika ya Latini na Karibea, miaka 3.5 katika Afrika na miaka mitatu katika Asia na Pasifiki.”
Hata hivyo, kwa wanawake wengi, kuishi muda mrefu hakumaanishi kuishi maisha bora. Our Planet, gazeti la Umoja wa Mataifa, lasema kwamba kwa wengi wa wanawake wa ulimwengu, haki za msingi za kibinadamu bado “zinatamaniwa sana lakini bado hawajazipata. Bado watafuta haki za msingi kabisa.” Bado, hata haki za msingi za kibinadamu, lasema Umoja wa Mataifa, haziwezi kupatikana na mamilioni kwa sababu idadi kubwa sana ya watu wa ulimwengu wasiojua kusoma na kuandika, wakimbizi, na maskini ni wanawake. Ingawa kuna maendeleo fulani, lamalizia UNESCO Sources, “wakati ujao wa wanawake . . . hauna matumaini.”