Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 4/22 kur. 20-23
  • Sasa Ninafurahi Kuwa Hai!

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sasa Ninafurahi Kuwa Hai!
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Tamaa ya Kitu Bora Zaidi
  • Tena Natamani Kufa
  • Kukabili Matatizo
  • Nasongwa Kutumia Damu
  • Upasuaji—Wafanikiwa
  • Msaada wa Udugu Wetu
  • Nategemezwa na Tumaini Hakika
  • Wala Wafanya-Mizungu Wala Miungu
    Amkeni!—1994
  • Kukabili Hali ya Dharura ya Kitiba
    Amkeni!—1996
  • Maisha Yawapo Magumu
    Amkeni!—1994
  • Je! Ilifaa Nijitahidi Kushinda Watu Wote?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1977
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 4/22 kur. 20-23

Sasa Ninafurahi Kuwa Hai!

“Unatambua kwamba utakufa, sivyo?” daktari akauliza. Kwa kinyume, mara mbili hapo awali kifo kingekuwa kitulizo kizuri. Lakini si wakati huu. Ebu nieleze.

NILILELEWA katika Long Island, viungani mwa New York, ambako baba yangu alikuwa mashuhuri katika kuendesha magari ya mashindano. Yeye alitaka ukamilifu na alipenda sana mashindano. Alikuwa mwepesi kukasirika na mgumu sana kupendeza. Kwa upande mwingine, mama alikuwa mtulivu na mnyamavu zaidi, naye aliogopa sana mashindano ya baba ya magari hivi kwamba hangeweza kumtazama akishindana.

Mimi na ndugu yangu tulijifunza mapema maishani kutokuwa wenye kujitokeza nyumbani, jambo ambalo tayari mama alizoea. Lakini kufanya hivyo kukawa na hasara kubwa. Sote tulimwogopa baba. Iliniathiri kwa kadiri ambayo niliona siwezi kufanya jambo lolote vizuri. Sikujistahi hata zaidi wakati “rafiki” wa familia yetu alinisumbua kingono nilipokuwa naanza umri wa utineja. Kwa kuwa nilishindwa kukabiliana na hisia zangu, nilijaribu kujiua. Hiyo ilikuwa ndiyo mara ya kwanza nilipofikiri kwamba kifo kingekuwa kitulizo kizuri.

Nilihisi sifai na sipendwi na nikawa na tatizo la ulaji ambalo huwapata sana wanawake wachanga wasiojistahi. Nilianza kuishi maisha ya msisimko, dawa za kulevya, uasherati, na utoaji-mimba—“kutafuta mapenzi katika sehemu zote zisizofaa,” kama wimbo mmoja usemavyo. Nilikuwa naendesha pikipiki, nikishiriki mashindano ya magari, kupiga mbizi, na mara kwa mara nilienda Las Vegas kucheza kamari. Pia nilitafuta mashauri ya mpiga-ramli na kutumia ubao wa Ouija kwa kujifurahisha, bila kutambua hatari za uwasiliani-roho.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12.

Kwa kuongezea, kutafuta msisimko kulifanya nihusike na vitendo visivyo halali kama vile ulanguzi wa dawa za kulevya na kuiba vitu madukani. Utafutaji wangu wa mapenzi na kibali kulifanya niwe na mlolongo mrefu wa marafiki na wachumba. Hayo yote yalifanyiza mtindo-maisha ambao ulikuwa hatari kuliko nilivyotambua.

Usiku mmoja, baada ya kuchanganya alkoholi na dawa za kulevya katika sehemu za kurekebisha magari ya mashindano kwenye nyanja za mashindano ya magari, bila hekima nilimruhusu rafiki yangu mvulana anipeleke nyumbani kwa gari. Baada ya kuzimia kwenye kiti cha mbele, yaonekana hata yeye pia alizimia. Niligutushwa na kishindo cha mgongano. Nililazwa hospitalini nikiwa na majeraha mengi, lakini hatimaye nilipata nafuu ila goti langu la kulia ndilo lililobaki na dhara.

Tamaa ya Kitu Bora Zaidi

Ingawa sikuthamini sana maisha yangu, nilihangaikia sana usalama na haki za watoto na wanyama na kuhusu kulinda mazingira. Nilitamani kuona ulimwengu bora zaidi na nilikuwa mtendaji katika mashirika mengi katika kujaribu kusaidia kufanyiza ulimwengu kama huo. Tamaa hiyo ya ulimwengu bora ndiyo iliyonifanya nivutiwe na mambo yaliyosemwa na mfanyakazi mwenzangu ambaye alikuwa mmoja wa Mashahidi wa Yehova. Kila mara alikuwa akirejezea “mfumo huu” kwa njia ya kufadhaika wakati wowote mambo hayakuwa sawa kazini. Nilipomwuliza anamaanisha nini, yeye alieleza kwamba siku fulani iliyo karibu maisha hayatakuwa na mahangaiko yote. Kwa kuwa nilimstahi sana, nilimsikiliza kwa upendezi mwingi.

Kwa kusikitisha, tulipoteza uwasiliano, lakini sikusahau kamwe mambo aliyokuwa amesema. Nilitambua kwamba siku moja nitalazimika kufanya mabadiliko makubwa ili kumpendeza Mungu. Lakini sikuwa tayari. Lakini, ningewaambia wale waliotazamia kufunga ndoa nami kwamba siku moja nitakuwa Shahidi na kama hawapendi jambo hilo, huu ndio wakati wa kuachana.

Tokeo likawa kwamba mvulana rafiki yangu wa mwisho alitaka kujua zaidi, akisema kwamba ikiwa ninapendezwa, hata yeye anaweza kupendezwa. Basi tukaanza kuwatafuta Mashahidi. Badala ya kuwapata, ni wao waliotupata walipobisha mlango wangu wa mbele. Funzo la Biblia lilianzishwa, lakini hatimaye, rafiki yangu akaamua kuacha kujifunza na kumrudia mke wake.

Funzo langu la Biblia mara nyingi halikuwa la kawaida. Ilinichukua muda kuthamini maoni ya Yehova juu ya utakatifu wa uhai. Lakini mara niliporekebisha kufikiri kwangu, niliona uhitaji wa kuacha ziara zangu za kuruka angani na kuacha kuvuta sigareti. Uhai wangu ulipokuja kuwa wenye thamani sana kwangu, nilikuwa tayari kutulia na kutohatarisha uhai wangu tena. Oktoba 18, 1985, nilionyesha wakfu wangu kwa Yehova kwa ubatizo wa maji. Sikujua kwamba uhai wangu ungekuwa hatarini.

Tena Natamani Kufa

Miezi michache baadaye—usiku wa Machi 22, 1986—nilikuwa mbele ya nyumba yangu, nikiondoa nguo ndani ya gari langu, wakati gari lililokuwa likienda kwa kasi liliponigonga na kunivuta zaidi meta 30! Nilikuwa nimegongwa na gari lililotoroka. Ingawa nilipata majeraha ya kichwa, sikupoteza fahamu muda huo wote.

Nikiwa nimelala kifudifudi katikati ya barabara yenye giza, nilihofia kugongwa tena. Maumivu yalikuwa makali sana na singeweza kuyavumilia. Basi nikafuliza kusali kwa Yehova aniache nife. (Ayubu 14:13) Mwanamke mmoja akatokea ambaye kumbe alikuwa muuguzi. Nikamwomba anirekebishie mkao wa miguu yangu kwa kuwa ilikuwa imevunjika-vunjika. Alifanya hivyo na pia akafinyiza kitambaa kutoka kwa nguo yake ili kukomesha mvujo wa damu kwa mguu mmoja uliokuwa umevunjika-vunjika. Viatu vyangu vilipatikana mbali kandokando ya barabara, vikiwa vimejaa damu!

Wapita-njia, bila kutambua kwamba niligongwa nikitembea kwa miguu, walifuliza kuniuliza gari langu lilikuwa wapi. Bila kujua nimevutwa umbali gani, nilidhani nilikuwa kando yalo! Madaktari wa dharura walipofika, walidhani nilikuwa nakaribia kufa. Waliita wapelelezi wa polisi, kwa kuwa mauaji kwa kutumia gari yaweza kuwa kosa baya sana. Hatimaye dereva huyo alikamatwa. Walifunga eneo hilo la uhalifu na kushika gari langu kuwa uthibitisho. Milango yote miwili kwenye upande mmoja wa gari ilikuwa imeng’oka kabisa.

Kukabili Matatizo

Kwa wakati huo, nilipofika kituo cha dharura cha mahali hapo, nilikuwa nikirudia-rudia, hata kupitia kipasha-oksijeni: “Msinitie damu, msinitie damu. Mimi ni mmoja wa Mashahidi wa Yehova!” Jambo la mwisho nakumbuka ni kuhisi mkasi mkubwa ukikata nguo zangu na kusikia kikundi hicho cha dharura kikitoa amri kwa udharura.

Nilipoamka, nilishangaa kwamba bado nilikuwa hai. Nikawa napoteza na kurudia fahamu. Kila wakati nilipoamka, niliomba familia yangu iwasiliane na wenzi walionifundisha Biblia. Familia yangu haikufurahi kwamba nilikuwa nimekuwa Shahidi, basi wao “wakasahau” kuwaarifu. Lakini sikukoma—lilikuwa jambo la kwanza nililouliza kila wakati nilipofungua macho yangu. Hatimaye, udumifu wangu ukathawabishwa, na siku moja nilipoamka, Mashahidi hao walikuwapo. Nilipata kitulizo kama nini! Watu wa Yehova walijua mahali nilipokuwa.

Hata hivyo, shangwe yangu ilikuwa ya muda mfupi kwa sababu damu yangu ilianza kupunguka nikawa na joto jingi sana. Mifupa iliyoshukiwa kusababisha maambukizo ilitolewa, na vyuma vinne vikawekwa katika mguu wangu. Lakini punde si punde, nikawa tena na joto jingi, na mguu wangu ukawa mweusi. Ulikuwa umeanza kuoza, na uhai wangu ulitegemea kukatwa kwa mguu wangu.

Nasongwa Kutumia Damu

Kwa kuwa damu yangu ilikuwa imepunguka sana, ilionekana siwezi kufanyiwa upasuaji bila kutiwa damu mshipani. Madaktari, wauguzi, washiriki wa familia, na marafiki wa zamani waliitwa ili kunisonga nikubali damu. Kisha, minong’ono ikaanza mlangoni. Nilisikia madaktari wakila njama, lakini sikuelewa ni njama gani. Kwa uzuri, Shahidi aliyenitembelea wakati huo akasikia mpango wao wa kunitia damu kwa nguvu. Mara moja akawasiliana na wazee wa huko wa Kikristo, ambao walikuja kunisaidia.

Mtaalamu wa akili aliletwa kuchanganua hali ya akili yangu. Kwa wazi makusudi yao yalikuwa kunitangaza kwamba sijiwezi na hivyo kufanya matakwa yangu yapuuzwe. Mpango huo ulitibuka. Kisha, mshiriki wa makasisi, ambaye mwenyewe alikubali kutiwa damu mshipani, aliletwa kunisadikisha kwamba si vibaya kutiwa damu. Hatimaye, familia yangu ilitafuta amri ya mahakama ya kunilazimisha kutiwa damu.

Saa nane hivi za usiku, kikundi cha madaktari, karani wa mahakama, wakili wa serikali, na wakili wanaowakilisha hospitali hiyo na hakimu waliingia katika chumba changu cha hospitali. Mahakama ilikuwa imeketi. Sikufahamishwa kimbele, sikuwa na Biblia, sikuwakilishwa, nami nilikuwa nimetumia dawa nyingi sana za kuzuia maumivu. Matokeo ya kikao hicho? Hakimu huyo alikataa mahakama isitoe amri, akisema kwamba yeye alivutiwa hata zaidi na uaminifu-maadili wa Mashahidi wa Yehova kupita wakati mwingine wowote.

Hospitali moja katika Camden, New Jersey, ilikubali kunishughulikia. Kwa kuwa wasimamizi wa hospitali hiyo katika New York walikuwa wameghadhabika, walininyima tiba zote, kutia ndani dawa za kutuliza maumivu. Pia walikataa kuruhusu helikopta kutua ili kunipeleka kwenye hospitali ya New Jersey. Kwa uzuri, niliweza kuokoka safari katika gari la kubebea wagonjwa mpaka huko. Mara tu nilipofika huko, nilisikia yale maneno yaliyotajwa mwanzoni wa masimulizi haya: “Unatambua kwamba utakufa, sivyo?”

Upasuaji—Wafanikiwa

Nilikuwa dhaifu hivi kwamba muuguzi alihitajika kunisaidia kuweka alama X kwenye fomu ya kukubali kufanyiwa upasuaji. Mguu wangu wa kulia ulikuwa lazima ukatwe juu ya goti. Baadaye kiwango cha hemoglobini kilipungua hadi chini ya 2, na madaktari wakashuku kwamba nilikuwa nimepata mvujo mkubwa wa damu katika ubongo. Hiyo ni kwa sababu sikuitikia walipoita kwenye masikio yangu, “Virginia, Virginia,”—ambalo ni jina lililokuwa kwenye kadi zangu za kulazwa hospitalini. Lakini niliposikia tu, “Ginger, Ginger,” likiitwa polepole baadaye, nilifumbua macho yangu nikamwona mtu ambaye sikuwa nimepata kumwona.

Bill Turpin alikuwa mshiriki wa mojayapo makutaniko ya Mashahidi wa Yehova katika New Jersey. Alikuwa amejua jina langu la utani Ginger—ambalo nimetumia maishani mwangu mwote—kutoka kwa Mashahidi wa New York. Aliuliza maswali ambayo ningeweza kujibu kwa kufumba na kufumbua macho, kwa kuwa nilikuwa nimeweka chombo cha kupumulia na singeweza kuongea. “Je, unataka niendelee kujaribu kukutembelea,” akauliza, “na kuwaambia Mashahidi wa New York kukuhusu?” Nilifumba na kufumbua macho mara nyingi sana! Ndugu Turpin alikuwa amejasiria kwa kuingia kisiri katika chumba changu kwa kuwa familia yangu ilikuwa imeamuru kwamba Mashahidi wasiruhusiwe kunizuru.

Baada ya kulazwa hospitalini kwa miezi sita, bado niliweza kufanya mambo ya msingi pekee ya kila siku, kama vile kujilisha na kupiga mswaki. Hatimaye, nilipokea mguu-bandia nami niliweza kutembea kidogo-kidogo kwa chombo cha kunisaidia kutembea. Niliporuhusiwa kuondoka hospitalini katika Septemba 1986 na kurudi kwangu, msaidizi wa kiafya aliishi nami kwa miezi mingine sita hivi ili kunisaidia.

Msaada wa Udugu Wetu

Hata kabla ya kurudi nyumbani, kwa kweli nilianza kuthamini umaana wa kuwa sehemu ya udugu wa Kikristo. (Marko 10:29, 30) Kwa upendo ndugu na dada walihudumia mahitaji yangu ya kimwili na kiroho vilevile. Kwa msaada wao wenye upendo, niliweza kuanza kuhudhuria tena mikutano ya Kikristo na baada ya muda hata nikaanza kushiriki katika kile kinachoitwa huduma ya painia msaidizi.

Mashtaka ya madai dhidi ya dereva wa lile gari, ambayo mara nyingi huchukua angalau miaka mitano ndipo yatokee tu katika ratiba ya mahakama, yalisuluhishwa kwa miezi kadhaa tu—kwa mshangao wa wakili wangu. Kutokana na ridhaa niliyopata, niliweza kuhamia nyumba iliyo rahisi zaidi kufikika. Pia nilinunua gari lenye kuinua kiti chenye magurudumu na lenye vidhibiti vya mkono. Hivyo, katika 1988, niliingia katika utumishi wa upainia wa kawaida, nikitumia angalau muda wa saa 1,000 katika kazi ya kuhubiri kila mwaka. Katika miaka ambayo imepita, nimefurahia kufanya kazi katika maeneo ya majimbo ya North Dakota, Alabama, na Kentucky. Nimetumia zaidi ya kilometa 150,000 kwenye gari langu, nyingi katika utumishi wa Kikristo.

Nimepata mambo mengi ya kuchekesha ninapotumia skuta yangu ya umeme yenye magurudumu matatu. Mara mbili nimepinduka nayo nikihubiri na wake za waangalizi wasafirio. Pindi moja, katika Alabama, nilidhani kimakosa kwamba ningeweza kuruka nayo kibonde kidogo lakini nikaanguka, nikalowa matope chepechepe. Lakini, nikidumisha hali ya ucheshi na kutojichukua kwa uzito mno kumenisaidia sana kudumisha mtazamo ufaao.

Nategemezwa na Tumaini Hakika

Nyakati nyingine matatizo ya afya karibu yanishinde kabisa. Nililazimika kuacha upainia mara mbili miaka michache iliyopita kwa sababu ilionekana kwamba mguu wangu mwingine ungehitaji kukatwa. Tisho la kukatwa mguu ni la kudumu sasa, na katika miaka mitano ambayo imepita, nimelazimika kutumia kiti chenye magurudumu kabisa. Katika 1994 nilivunjika mkono. Nilihitaji msaada katika kuoga, kuvaa, kupika, na katika kufanya usafi na kusafirishwa popote nilipoenda. Lakini kwa sababu ya msaada wa ndugu, niliweza kuendelea na upainia japo magumu hayo.

Maishani mwangu mwote nimetafuta kile kilichoonekana kuwa msisimko, lakini sasa natambua kwamba nyakati zenye msisimko ziko mbele. Usadikisho wangu kwamba Mungu ataponyesha magonjwa ya sasa katika ulimwengu wake mpya unaokuja kwa kasi ndio unaonifanya niwe mwenye furaha sasa. (Isaya 35:4-6) Katika ulimwengu huo mpya, natazamia kuogelea na nyangumi na dolfini, nikichunguza milima nikiwa pamoja na simba na watoto wake, na kufanya jambo sahili kama kutembea kwenye ufuo. Nafurahi sana kuwazia kufanya mambo hayo yote ambayo Mungu ametuumba kufurahia katika Paradiso hiyo duniani.—Kama ilivyosimuliwa na Ginger Klauss.

[Picha katika ukurasa wa 21]

Kamari ilipokuwa sehemu ya maisha yangu

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ahadi za Mungu hunitegemeza

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki