Mungu—Je, Ni Mcheza-kamari au Muumba?
“HAKUNA shaka kwamba wanasayansi wengi wanapinga kabisa hoja za kuwapo kwa nguvu zenye kupita uwezo wa wanadamu. Wao wanapuuza wazo la kwamba huenda Mungu yupo, au hata kuwapo kwa chanzo fulani chenye uwezo wa kuumba . . . Mimi binafsi sikubaliani na dhihaka zao.” Ndivyo asemavyo Paul Davies, profesa wa fizikia ya hisabati katika Chuo Kikuu cha Adelaide, Australia Kusini, katika kitabu chake The Mind of God.
Pia Davies asema: “Uchunguzi wenye uangalifu waonyesha kwamba sheria za ulimwengu wote mzima zafaa kabisa kutokea kwa viumbe vingi tofauti-tofauti. Kwa habari ya viumbe hai, kuwapo kwao yaonekana hutegemea matukio kadhaa mazuri ambayo baadhi ya wanasayansi na wanafalsafa wamedai kuwa ya ajabu mno.”
Yeye aendelea kusema: “Utafutaji wa kisayansi ni safari ya kwenda kusikojulikana. . . . Na katika utafutaji huo wote kuna jambo lilelile la akili na utaratibu. Tutaona kwamba utaratibu huo mzuri wa ulimwengu unaungwa mkono na sheria fulani hususa za hisabati ambazo hupatana na kufanyiza muungano usioonekana lakini wenye umoja. Sheria hizo ni sahili sana.”
Davies amalizia kwa kusema: “Sababu hasa inayofanya binadamu ndiye awe na akili ya kufahamu ulimwengu wote mzima, ni fumbo kubwa sana. . . . Siwezi kuamini kwamba kuwapo kwetu katika ulimwengu wote mzima kulitukia tu kwenyewe, kukiwa aksidenti fulani tu katika historia na kasoro fulani katika matukio ya ulimwengu wote mzima. Tumehusika sana na ulimwengu. . . . Hakika tumekusudiwa kuwa hapa.” Lakini, Davies hafikii mkataa wa kwamba kuna Mbuni, Mungu. Lakini wewe wafikia mkataa upi? Je, ilikusudiwa wanadamu wawepo? Ikiwa ndivyo, ni nani aliyekusudia tuwepo?
Funguo za “Fumbo”
Katika Biblia mtume Paulo atoa dokezo la kuelewa kile Davies akiitacho “fumbo kubwa sana.” Paulo aonyesha jinsi Mungu amejifunua: “Kwa sababu lile liwezalo kujulikana juu ya Mungu ni dhahiri miongoni mwao [“watu wanaokandamiza kweli”], kwa maana Mungu alilifanya dhahiri kwao. Kwa maana sifa zake zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea, kwa sababu zafahamiwa kwa vitu vilivyofanywa, hata nguvu zake za milele na Uungu, hivi kwamba hawana sababu ya kujitetea.” (Waroma 1:18-20)a Ndiyo, aina nyingi sana za uhai, utata wao ajabu sana, ubuni wao bora zaidi, wapaswa kufanya mtu ambaye ni mnyenyekevu na wa kimungu atambue kwamba kuna uwezo mkuu zaidi na akili, ipitayo kitu chochote ambacho mwanadamu amepata kujua.—Zaburi 8:3, 4.
Maneno zaidi ya Paulo kuhusu wale wanaomkataa Mungu hufanya mtu atue na kufikiri: “Ijapokuwa walisisitiza kuwa ni wenye hekima, wakawa wapumbavu . . . , hata wale walioibadili kweli ya Mungu kwa uwongo nao waliheshimu mno na kutoa utumishi mtakatifu kwa kiumbe badala ya Yeye aliyeumba, ambaye abarikiwa milele. Ameni.” (Waroma 1:22, 25) Wale wanaoheshimu “asili” na kumkataa Mungu kwa hakika si wenye hekima kwa maoni ya Yehova. Wakiwa wamekwama katika nadharia nyingi zenye kupingana za mageuzi, wao hawatambui Muumba na vilevile utata na ubuni wa uumbaji wake.
“Mfululizo wa Aksidenti Kubwa-Kubwa”
Paulo aliandika pia: “Bila imani haiwezekani kumpendeza [Mungu] vema, kwa maana amkaribiaye Mungu lazima aamini kwamba yeye yuko na kwamba yeye huwa mthawabishaji wa wale wanaomtafuta kwa bidii.” (Waebrania 11:6) Imani inayotegemea ujuzi sahihi, wala si kukubali mambo bila msingi, yaweza kufanya tuelewe ni kwa nini tupo. (Wakolosai 1:9, 10) Kwa hakika, kukubali mambo bila msingi hutokea wakati wanasayansi fulani wanataka tuamini kwamba uhai upo kwa sababu ni “kana kwamba tumeshinda bahati nasibu ya dola milioni moja mara mamilioni mfululizo.”
Mwanasayansi wa Uingereza Fred Hoyle alinadharia kwamba utendanaji wa nyuklia ambao ulitokeza mfanyizo wa elementi mbili zilizo muhimu kwa uhai, yaani kaboni na oksijeni, ulitokeza kiasi chenye usawaziko cha elementi hizo kwa aksidenti nzuri.
Yeye atoa mfano mwingine: “Kama jumla ya protoni na elektroni zingeongezeka kidogo tu zaidi badala ya kupungua kidogo zaidi kuliko jumla ya nutroni, matokeo yangekuwa mabaya zaidi. . . . Kotekote katika Ulimwengu Wote Mzima atomu zote za hidrojeni zingevunjika-vunjika mara moja ili kufanyiza nutroni na nutrinosi. Bila fueli yalo ya nyuklia, Jua lingefifia na kuporomoka.” Na ndivyo ingekuwa na mabilioni ya nyota nyinginezo katika ulimwengu wote mzima.
Hoyle alifikia mkataa huu: “Orodha ya . . . zile zionekanazo kuwa aksidenti za asili zisizo za kibiolojia bila kaboni na hivyo uhai wa kibinadamu usiweze kuwapo, ni kubwa na kustaajabisha.” Yeye asema: “Mambo hayo [muhimu kwa uhai] yaonekana yameshikamana na ulimwengu wa asili kama mfululizo wa aksidenti nzuri. Lakini kuna matukio hayo yasiyo ya kawaida mengi yaliyo muhimu kwa uhai hivi kwamba twahitaji yafafanuliwe.”—Italiki ni zetu.
Pia alitaja: “Tatizo ni kuamua kama matukio hayo ya kiaksidenti kwa kweli yalikuwa aksidenti au la, na basi kama uhai ulitukia kwa aksidenti au la. Hakuna mwanasayansi apendaye kuuliza swali kama hilo, lakini ni lazima swali hilo liulizwe. Je, yawezekana kwamba matukio hayo yanafanywa na akili fulani?”
Paul Davies aandika: “Hoyle alivutiwa sana na ‘mfululizo wa aksidenti kubwa-kubwa,’ mpaka akasema ilikuwa kana kwamba ‘sheria za fizikia zimebuniwa kwa kufikiria matokeo yazo ndani ya nyota.’” Ni nani au ni nini kimesababisha “mfululizo wa aksidenti [nzuri] kubwa-kubwa”? Ni nani au ni nini kilichotokeza sayari hii ndogo sana, iliyojaa mamilioni ya viumbe na mimea iliyo tofauti-tofauti?
Jibu la Biblia
Mtunga-zaburi aliandika kwa staha sana miaka ipatayo 3,000 iliyopita: “Ee BWANA, jinsi yalivyo mengi matendo yako! Kwa hekima umevifanya vyote pia. Dunia imejaa mali zako. Bahari iko kule, kubwa na upana, ndimo mlimo viendavyo visivyohesabika, viumbe hai vidogo kwa vikubwa.”—Zaburi 104:24, 25.
Mtume Yohana alisema: “Wewe wastahili, Yehova, naam, Mungu wetu, kupokea utukufu na heshima na nguvu, kwa sababu uliumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yako vilikuwako na vikaumbwa.” (Ufunuo 4:11) Uhai si tokeo la nasibu tu, la bahati nasibu ambayo ilitukia kutokeza washindi wa mamilioni ya aina za uhai.
Ukweli ni kwamba Mungu ‘aliumba vitu vyote, na kwa sababu ya mapenzi yake vilikuwapo na kuumbwa.’ Yesu Kristo mwenyewe aliwaambia Mafarisayo: “Je, hamkusoma kwamba yeye aliyewaumba wao kutoka mwanzo aliwafanya wa kiume na wa kike?” Yesu alijua Muumba! Akiwa Mfanyakazi Stadi wa Yehova, alikuwa pamoja na Yeye wakati wa uumbaji.—Mathayo 19:4; Mithali 8:22-31.
Hata hivyo, inahitaji imani na unyenyekevu kuona na kukubali kweli ya msingi kuhusu Muumba. Imani hiyo si kuamini tu mambo bila msingi. Inategemea uthibitisho uonekanao. Ndiyo, “Sifa [za Mungu] zisizoonekana zaonwa waziwazi tangu uumbaji wa ulimwengu na kuendelea.”—Waroma 1:20.
Kwa ujuzi wetu kidogo wa sasa juu ya mambo ya kisayansi, hatuwezi kueleza jinsi Mungu alivyoumba. Basi, twapaswa kutambua kwamba kwa wakati huu hatuwezi kujua wala kuelewa kila kitu kuhusu mwanzo wa uhai. Twakumbushwa jambo hili tusomapo maneno ya Yehova: “Mawazo yangu si mawazo yenu, wala njia zenu si njia zangu . . . Kwa maana kama vile mbingu zilivyo juu sana kuliko nchi, kadhalika njia zangu zi juu sana kuliko njia zenu, na mawazo yangu kuliko mawazo yenu.”—Isaya 55:8, 9.
Chaguo ni lako: ama uamini mambo ya mageuzi yasiyo na msingi, zile kamari nyingi sana ambazo zasemekana eti zilikuwa na matokeo mazuri, ama uamini katika Mkusudiaji-Muumba-Mbuni, Yehova Mungu. Nabii aliyepuliziwa alisema hivi kwa usahihi: “Yeye Mungu wa milele, BWANA, Muumba miisho ya dunia, hazimii, wala hachoki; akili zake hazichunguziki.”—Isaya 40:28.
Basi, utaamini nini? Uamuzi wako utafanyiza tofauti kubwa sana katika matazamio yako ya wakati ujao. Kama mageuzi yangekuwa kweli, basi kifo kingemaanisha utupu kabisa, japo hoja zisizo za kweli za theolojia za Katoliki, ambazo zinajaribu kuingiza “nafsi” katika mageuzi.b Mwanadamu hana nafsi isiyoweza kufa iwezayo kupunguza pigo la kifo.—Mwanzo 2:7; Ezekieli 18:4, 20.
Tukikubali kwamba Biblia ni kweli na kwamba Mungu aishiye ni Muumba, basi kuna ahadi ya ufufuo kwenye uhai udumuo milele, uhai mkamilifu, katika dunia iliyorekebishwa kwenye hali yayo ya awali ya usawaziko na upatano. (Yohana 5:28, 29) Utaweka imani yako wapi? Katika kamari isiyoweza kuaminiwa ya nadharia ya Darwin ya mageuzi? Au katika Muumba, ambaye ametenda kwa kusudi na aendelea kufanya hivyo?c
[Maelezo ya Chini]
a “Tangu Mungu aumbe ulimwengu uwezo wake na uungu wake wa milele—hata kama hauonekani—umekuwapo tuuone kwa akili katika vitu ambavyo ameumba.”—Waroma 1:20, Jerusalem Bible.
b Ona “Kuutazama Ulimwengu,” ukurasa wa 28, “Papa Ahakikisha Tena Mageuzi.”
c Kwa mazungumzo marefu juu ya jambo hili, ona kitabu Life—How Did It Get Here? By Evolution or by Creation?, kilichochapishwa na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Blabu katika ukurasa wa 14]
Wanamageuzi fulani wasema kwamba kuwapo kwetu duniani ni “kana kwamba tumeshinda bahati nasibu ya dola milioni moja mara mamilioni mfululizo.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]
Viumbe Vingi Sana vya Aina na Ubuni Mbalimbali
Wadudu “Wanasayansi hugundua spishi mpya 7,000 hadi 10,000 za wadudu kila mwaka,” yasema The World Book Encyclopedia. Na bado, “yawezekana kwamba kuna spishi milioni 1 hadi milioni 10 ambazo hazijagunduliwa.” Gazeti la habari la Ufaransa Le Monde, kama lilivyonukuliwa katika Guardian Weekly, katika makala moja iliyoandikwa na Catherine Vincent, lasema juu ya spishi ambazo zimejulikana kuwa “idadi ndogo sana kwa kulinganisha na idadi halisi . . . inayokadiriwa kuwa kati ya milioni 5 na, kwa kushangaza sana, milioni 50.”
Fikiria ulimwengu wa wadudu wa ajabu—nyuki, chungu, manyigu, vipepeo, mende, bibiarusi, vimulimuli, mchwa, nondo, nzi, kereng’ende, mbu, silverfish, panzi, chawa, chenene, viroboto—kwa kutaja wachache tu! Orodha yaonekana kuwa ndefu sana!
Ndege Twaweza kusema nini kuhusu ndege ambaye ana uzito unaopungua gramu 14? “Ebu mfikirie akihama zaidi ya kilometa 16,000 kwa mwaka kutoka misitu ya Alaska hadi misitu ya mvua ya Amerika Kusini na kurudi, akipita juu ya vilele vya milima vyenye misitu, orofa ndefu za majiji, na kuvuka upana mkubwa sana wa Bahari-kuu ya Atlantiki na Ghuba ya Mexico.” Ndege huyo wa ajabu ni yupi? “Ni blackpoll warbler [Dendroica striata], ndege mwenye nguvu ambaye umahiri wake wa kusafiri hauna kifani miongoni mwa ndege wa bara la Amerika Kaskazini.” (Book of North American Birds) Tena twajiuliza: Je, hilo ni tokeo la aksidenti nyingi za asili ambazo zimetukia tu zenyewe? Au je, ni ajabu ya ubuni wa akili?
Ongezea mifano hiyo ndege wanaoonekana kuwa na orodha ndefu isiyo na mwisho ya nyimbo: nightingale, ajulikanaye kotekote Ulaya na sehemu za Afrika na Asia kwa nyimbo zake tamu; mockingbird wa Amerika Kaskazini, ndege ambaye ni “mwigaji stadi ambaye huimba pia mafungu ya maneno aliyokariri katika wimbo wake”; lyrebird aliye stadi sana wa Australia, mwenye “wimbo wa hali ya juu sana, na mwenye uwezo sana wa kuiga.”—Birds of the World.
Kwa kuongezea, rangi kamili na ubuni wa mabawa na manyoya ya ndege wengi sana hustaajabisha. Ongezea uwezo wao wa kufuma na kutengeneza viota, ardhini, magengeni, au mitini. Akili hiyo ya asili ni lazima ivutie wanyenyekevu. Walikujaje kuwapo? Kwa nasibu au kwa ubuni?
Ubongo wa Kibinadamu “Inawezekana kwamba kuna sinapsi kati ya trilioni kumi hadi trilioni 100 katika ubongo, na kila moja hutenda kama kikokotozi kidogo sana ambacho huhesabu ishara zinazofika kwa njia ya mipwito ya elektroni.” (The Brain) Tuna mwelekeo wa kupuuza ubongo, lakini ni kama ulimwengu wote mzima uliowekwa na kulindwa na fuvu. Sisi tulipataje kuwa na kiungo hicho ambacho hufanya wanadamu wafikiri, wasababu, na kusema maelfu ya lugha? Je, ni kupitia mamilioni ya kamari zenye bahati nzuri? Au ni kupitia ubuni wenye akili?
[Mchoro katika ukurasa wa 16, 17]
Mchoro Sahili wa Sehemu ya Nje ya Ubongo
Koteksi ya fahamu
Huchanganua mipwito ya fahamu inayotoka mwilini kote
Occipital lobe
Huchakata ishara za kuona
Ubongo-kati
Hudhibiti usawaziko na uratibu wa mwili
Sehemu ya mbele ya koteksi
Hudhibiti uratibu wa misuli
Koteksi ya miendo ya neva
Husaidia kudhibiti miendo ya mwili
Frontal lobe
Husaidia kudhibiti kusababu, hisia, usemi, miendo
Temporal lobe
Huchakata sauti; huongoza hali ya kujifunza, kumbukumbu, lugha, hisia
[Mchoro katika ukurasa wa 16]
Kituo cha aksoni
Vipitisha-neva
Dendira
Sinapsi
[Mchoro katika ukurasa wa 16, 17]
Nyuroni
Dendira
Aksoni
Dendira
Sinapsi
Nyuroni
Aksoni
“Inawezekana kwamba kuna sinapsi kati ya trilioni kumi hadi trilioni 100 katika ubongo, na kila moja hutenda kama kikokotozi kidogo sana ambacho huhesabu jumla ya ishara zinazofika kwa njia ya mipwito ya elektroni.”—THE BRAIN
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]
Mwezi na sayari: Picha ya NASA