Osteoporosis—Maradhi ya ‘Mifupa Dhaifu’
“‘Osteoporosis’ ni hali ambayo kiwango cha tishu ya mifupa kiko chini sana hivi kwamba mifupa yavunjika kwa urahisi kwa uzito mchache sana. Mtu aliye na “osteoporosis” aweza kuvunja kiwiko au nyonga kwa kuanguka barafuni au kuvunjika ubavu kwa kukumbatiwa kwa shauku. . . . Kwa hakika, kiwango cha tishu ya mifupa chaweza kuwa chini sana hivi kwamba mtu huvunjika uti wa mgongo kwa kubeba uzito wa mwili wake tu.”—“Osteoporosis—A Guide to Prevention & Treatment,” kilichoandikwa na John F. Aloia, M.D.
JE, UNAUGUA osteoporosis? Tatizo hilo la kudhoofika kwa mifupa ni la kawaida miongoni mwa wanawake waliopita komahedhi. Hata hivyo, laweza pia kuwapata wanawake wachanga na wanaume vilevile. Kulingana na Taasisi za Kitaifa za Afya za Marekani, osteoporosis huathiri “watu wengi sana kama milioni 15 hadi 20 katika Marekani.” Kila mwaka katika Marekani, osteoporosis husababisha mivunjiko ya mifupa milioni 1.3 ya watu wenye umri wa miaka 45 na zaidi. Hilo hugharimu dola bilioni 3.8 kila mwaka.
Kichapo Health Tips, cha Wakfu wa Elimu na Utafiti wa Kitiba wa California, chaeleza: “Ingawa dalili za osteoporosis huonekana sana katika umri wa uzee, utaratibu ambao hudhoofisha mifupa huanza hasa miaka 30-40 kabla ya mvunjiko wa mfupa wa kwanza kutokea. Baada ya umri wa miaka 35 wote wanaume na wanawake huanza kupoteza tishu ya mfupa. Kadiri mifupa izidivyo kuwa myepesi zaidi na dhaifu zaidi, mivunjiko yaweza kutokea kwa urahisi zaidi na huenda ikapona polepole kwa sababu mwili hauwezi kutengeneza mfupa mpya kwa urahisi kama ulivyoweza wakati fulani. Kisababishi hususa cha osteoporosis hakijulikani, lakini uhaba wa kalsiamu na vitamini D katika chakula, kupungua kwa viwango vya homoni za kike na kutofanya mazoezi ya kutosha kwaweza kuchangia hali hiyo.”
Kitabu Understanding Your Body—Every Woman’s Guide to a Lifetime of Health chaonelea kwamba moja ya dalili za kawaida zinazohusiana na komahedhi ni kupungua kwa nguvu ya mifupa. Hicho hutaarifu hivi: “Osteoporosis, kihalisi mifupa yenye kuvuja, ni tatizo kuu la kiafya na la kawaida kwa wanawake baada ya komahedhi.”
Utafiti wadokeza kwamba huenda osteoporosis ikaweza kuzuilika na kutibika. Hatua ya kuzuia ni kuhakikisha kwamba mwili una kiwango kifaacho cha kalsiamu pamoja na vitamini D, ambayo ni muhimu ili kalsiamu ifyonzwe. Hatua nyingine ya kuzuia ni mazoezi ya kawaida yanayoongeza uzito kwenye mifupa, kama vile kutembea au kukimbia-kimbia.
Dakt. Carol E. Goodman alisema hivi katika Geriatrics: “Urekebishaji wa kikao na mazoezi ya kutia nguvu yapaswa kuagizwa—na twapaswa kuwa waangalifu na maagizo hayo kama vile tuwavyo waangalifu na maagizo ya dawa. Programu ifaayo ya mazoezi kwa mgonjwa wa osteoporosis mwenye umri mkubwa yaweza kuwa rahisi kuelewa, rahisi kufanya, na salama.”
Ingawa osteoporosis haiwezi kutibiwa, dawa mpya za kupambana nayo zaanza kupatikana. Isitoshe, yaweza kuzuiwa kwa ulaji ufaao, mazoezi ya kutosha, na kwa wengine, tiba ya kurudisha homoni. Ili kuwa na matokeo bora zaidi, ni lazima hatua hizi zichukuliwe kabla ya kudhoofika kwa mifupa kuanza na zapaswa kuendelea kwa muda wote wa maisha.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Kujikinga Dhidi ya Osteoporosis
1. Kalsiamu
2. Vitamini D
3. Jua
4. Mkao mzuri
5. Tahadhari za utunzaji wa mgongo
6. Mazoezi
7. Kutovuta sigareti
Kalsiamu Katika Vyakula vya Kawaida
Kalsiamu ya Chakula (miligramu)
Maziwa yasiyo na mafuta, kikombe 1 300
Jibini aina ya Cheddar, kipande cha inchi 1 130
Mtindi, kikombe 1 300
Nyama ya ng’ombe, kuku, samaki, gramu 170 30-80
Samaki wa mkebe aina ya salmoni, gramu 85 170
Mkate, nafaka, wali, kikombe 1 20-50
Tofu (maziwa ya mgando ya soya), gramu 100 150
Lozi, 1/2 kikombe 160
Walnuts, 1/2 kikombe 50
Brokoli, bua 1 150
Spinachi, kikombe 1 200
Majani mabichi ya tanipu, kikombe 1 250
Mboga nyingine nyingi, kikombe 1 40-80
Aprikoti, zilizokaushwa, kikombe 1 100
Tende, zilizotolewa kokwa, kikombe 1 100
Rhubarb, kikombe 1 200
Matunda mengine mengi, kikombe 1 20-70
Kutoka kichapo Understanding Your Body, kilichoandikwa na Felicia Stewart, Gary Stewart, Felicia Guest, na Robert Hatcher, ukurasa wa 596.
[Sanduku katika ukurasa wa 17]
Baadhi ya Visababishi vya Osteoporosis
Visababishi vya Kurithiwa
Kuwa wa kike
Kutokuwa wa asili ya Kiafrika
Uzao wa Ulaya-Kaskazini
Kuwa mweupe
Wembamba
Udogo wa umbo (sentimeta 157 au chini)
Visababishi vya Mtindo-Maisha
Nuru ya jua ya nje, chini ya saa tatu kwa juma
Kutokuwa na kalsiamu nyingi katika ulaji
Kuwa na kafeni na/au fosfati nyingi katika ulaji
Dawa
Vizimaasidi vyenye aluminiamu
Thiroidi au levothyroxine
Steroidi (cortisone)
Dilantin (matibabu ya muda mrefu)
Furosemide (dawa ya kukojoza)
Matatizo ya Kitiba
Komahedhi ya mapema au ya kabla ya wakati wayo
Amenorrhea (kutokuwapo kwa damu ya mwezi)
Anorexia nervosa (ugonjwa wa kukosa hamu ya chakula)
Hyperthyroidism (thiroidi nyingi kupita kiasi)
Maradhi ya figo au vijiwe vya figo
Ugonjwa wa kisukari
Uhaba wa laktasi (kuwa mnyetivu isivyo kawaida kwa maziwa)
Maradhi ya matumbo (uvimbe wa utumbo mpana na uvimbe wa sehemu ya mwisho ya utumbo mwembamba)
Uraibu wa alkoholi
Kukaa kwa mgonjwa kitandani kwa muda mrefu au kutoweza kuondoka kwa muda uzidio majuma matatu
Baridi yabisi