Vito vya Kingo za Mto
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Hispania
WAKATI wowote nitembeapo kando-kando za mto, au kidimbwi, mimi hutafuta kimojawapo vito nivipendavyo zaidi—chaweza kuwa chekundu, cha buluu, au cha kijani-kibichi. Nyakati nyingine mimi huona kimoja kikiwa kimetulia tuli kwenye jani; naweza kuona kingine kikirukaruka juu ya maji au hata kukimbiakimbia mbele yangu. Kito nitafutacho ni kereng’ende—yule “helikopta” mwenye kuvutia wa ulimwengu wa wadudu.
Vito hivi vyenye kuruka vilinasa uangalifu wangu kwa mara ya kwanza miaka mingi iliyopita nilipopata kwa ghafula kijito fulani chenye kwenda polepole kikipitia msitu. Kulikuwa na kereng’ende kadhaa wakirukaruka kwenye jua na kivuli—wengine walikuwa wenye rangi ya buluu yenye kung’aa na wengine walikuwa waking’aa kwa rangi ya manjano ya kijani. Nikakaa kwa muda wa saa moja nikitazama michezo yao hewani, ambayo ilifanya sehemu peupe katika msitu kuwa uwanja mdogo wa kucheza dansi. Wamenivutia tangu wakati huo.
Kadiri nilivyojifunza kuhusu kereng’ende, ndivyo nilivyokuja kuthamini umaridadi wao na hadhi yao. Uvumbuzi wangu wa kwanza ukawa kwamba kuna tofauti kati ya kereng’ende na damselflies. Kereng’ende ni warukaji wenye nguvu na kwa kawaida wao ni wakubwa, huku damselflies wakiwa warembo zaidi nao hawaruki kwa nguvu. Tofauti kubwa kati yao ni njia wanayoweka mabawa yao. Kereng’ende hunyoosha mabawa yao kandokando wapumzikapo, huku damselfly akifunga mabawa yake yote pamoja juu ya mwili wake.a
Nikaanza kujiuliza jinsi ambavyo kereng’ende wawezavyo kushika mbu hewani kwa ustadi sana. Mimi huona ikiwa vigumu sana kupiga nzi mkubwa anayeota jua kwenye ukuta wa jikoni. ‘Ni nini,’ nikajiuliza, ‘ambacho kereng’ende anacho ambacho sina?’ Vitu viwili: kudhibiti kabisa hewa na vilevile macho yenye uwezo mkubwa sana.
Mruko wa Kereng’ende
Kwa kweli kuita kereng’ende helikopta—jina la kubandika la kawaida nchini Hispania—ni ulinganifu wenye kumshusha hadhi kabisa. Sarakasi zao za angani ni za kasi sana hivi kwamba nyakati nyingine haiwezekani kuwafuata kwa macho. Kwa miendo mifupi ya kasi, spishi fulani zaweza kufikia mwendo wa kilometa 96 hivi kwa saa. Wao pia waweza kusimama hewani au kwenda kinyumenyume, mbele au kandokando kwa ghafula. Isitoshe, kereng’ende apigapo kona kali hewani, wanasayansi hukadiria kwamba ni lazima astahimili nguvu za karibu G 2.5.
Kereng’ende wana mabawa mawili yenye kupindika na yaliyo mepesi. Ingawa mabawa hayo huonekana kuwa dhaifu, hayo yaweza kupiga mara 40 kwa sekunde moja nayo huweza kustahimili kugongwagongwa bila kupatwa na madhara. Mwanabiolojia Robin J. Wootton ayafafanua kuwa “maajabu madogo ya ubuni wenye ustadi.”
“Kadiri tuelewavyo zaidi kazi ya mabawa ya mdudu,” yeye aongezea, “ndivyo ubuni wayo na umaridadi wa uumbaji wayo uzidivyo kuonekana. . . . Mabawa ya wadudu hayana kifani katika tekinolojia.” Haishangazi kwamba mbinu za mruko wa kereng’ende zinachunguzwa sasa na wahandisi wa ndege.
Kichwa Kilichojaa Macho
Ikiwa mruko wa kereng’ende ni wa ajabu, basi macho yake ni ya ajabu vilevile. Macho mawili makubwa hufunika karibu kichwa chote cha kereng’ende. Kila jicho limejigawanya kwa maumbo madogo-madogo ya pembesita yapatayo 30,000 ambayo ni kama macho madogo-madogo ndani ya jicho, kwa kuwa kila jicho dogo huwasilisha picha tofauti katika ubongo. Lakini, hiyo haimaanishi kwamba kereng’ende huona maelfu ya picha tofauti-tofauti, zote kwa wakati mmoja. Badala ya kuona picha nzima kama sisi, yeye hutambua miendo, vigezo, utofauti, na maumbo.
Picha hizo zote huhitaji kuchanganuliwa. Kwa hiyo, asilimia 80 ya ubongo wa kereng’ende hasa ni ya kuchanganua habari zinazoletwa na macho. Ni vifaa vichache sana vya macho ambavyo vina uwezo kama wake—kereng’ende aweza kuona mbu kwa umbali wa meta 20. Hata jioni-jioni, wakati ambapo nuru ni hafifu sana hivi kwamba hata mwanadamu atazamaye hawezi kuona nzi wadogo, kereng’ende wa kitropiki huwashika kwa urahisi sana.
Mruko wa haraka-haraka wa kereng’ende kupitia majani yaliyo kando ya mto huhitaji kufanya mamia ya maamuzi haraka sana. Yeye aweza kutimiza kazi hiyo ngumu kwa sababu aweza kuona picha mia moja tofauti-tofauti kwa sekunde moja, zaidi ya mara tano kuliko sisi. Kwa hiyo, sinema ambayo hutokeza picha 24 kwa sekunde moja, ingefanana na mfululizo wa picha zisizosonga kwa kereng’ende.
Badiliko la Mtindo-Maisha
Kereng’ende aanzapo maisha, hakuna dalili kwamba hatimaye atakuwa mrukaji mwenye kuvutia. Baada ya kuanguliwa, buu lake hubaki tuli katika kidimbwi au kijito, likingoja kunasa chakula chochote kisongeacho karibu. Baada ya kutoa ngozi mara kadhaa—miezi kadhaa baadaye au hata miaka kadhaa baadaye katika spishi fulani—buu hutoka nje na kupanda juu ya tete. Hapo, badiliko kubwa sana latokea.
Ngozi hupasuka kwenye kifua, halafu kereng’ende kamili hutokea. Kama kipepeo, kereng’ende huyo ni lazima angoje muda wa saa chache kabla ya mabawa yake kuwa thabiti na maisha mapya huanza. Kwa siku chache tu, hekima yake ya kisilika humwezesha kuwinda kwa mafanikio na kudhibiti magumu ya kuruka.
Upesi kereng’ende mchanga huwa stadi wa kushika nzi na mbu hewani. Akila wadudu wanaolingana na uzani wake mwenyewe kila siku, yeye hutekeleza utumishi muhimu. Ili kuhakikisha kwamba ugavi wa chakula hauishi, kereng’ende wengi wa kiume huweka maeneo, ambayo wao huyalinda kwa wivu.
Spishi fulani wa kereng’ende huwinda wadudu-wanyonyao au mbawakavu, wengine hushika vyura wadogo-wadogo, na damselfly fulani wa kitropiki hata hula buibui. Yeye husimama hewani karibu na utando wa buibui mkubwa aitwaye orb-spider na kushika buibui wadogo ambao huzuru utando wa buibui huyo ili kula masazo ya chakula ambayo mwenye utando huacha.
Uthibitisho Dhidi ya Mageuzi
Wanasayansi wengi wa mageuzi humfikiria kereng’ende kuwa mdudu wa kuruka wa mapema zaidi kati ya wadudu. Kisukuku kimoja kilichovumbuliwa nchini Ufaransa kilitokeza kwenye miamba kereng’ende fulani mwenye mabawa yenye upana wa sentimeta 75! Ndiye mdudu mkubwa zaidi ajulikanaye, akiwa mkubwa zaidi ya mara tatu kuliko kereng’ende yeyote aishiye.
‘Ingewezekanaje,’ nikajiuliza, ‘kwa muundo ulio tata zaidi wa mruko ujulikanao kwa binadamu kutokea tu wenyewe, ukiwa kamili kabisa?’ “Hakuna visukuku vya wadudu ambavyo viko kati ya wenye mabawa na wasio na mabawa,” chakiri kitabu Alien Empire—An Exploration of the Lives of Insects. Ni wazi kwamba kereng’ende ni kazi ya Mbuni Stadi mwenye akili.
Kereng’ende wanaishi kwa mafanikio karibu kila sehemu ya dunia. Wao hustarehe kando ya ziwa la mlimani, kando ya bwawa la ikweta, au hata katika vidimbwi vya kuogelea vya viunga vya miji.
Nimetazama makundi makubwa ya kereng’ende katika bichi moja ya kitropiki katika Afrika na vilevile kereng’ende maliki mmoja-mmoja walio peke yao wakishika doria kwenye kidimbwi chao wakipendacho katika Ulaya. Na niliposafiri kwa mtumbwi kupitia bonde lenye majani mengi nchini Filipino, damselflies wenye rangi za kung’aa walinisindikiza, hata wakitua katika mikono yangu.
Ingawa kereng’ende waweza kuwa mojawapo ya mashine zenye utata zaidi zinazoruka duniani, sikuzote nimevutiwa na umadaha wao na umaridadi wao kuliko uwezo wao wa kuruka. Kuwapo kwao huongezea umaridadi fulani kwenye vidimbwi na kando-kando za mto. Wao ni vito vifaavyo kabisa—wakiwapo sikuzote ili kufurahiwa.
[Maelezo ya Chini]
a Pindi kwa pindi, kereng’ende hulaza mabawa yao kuelekea chini na kuelekeza mwili wao juu kuelekea jua. Wao hukaa hivyo ili kupunguza joto, kwa kuwa kufanya hivyo hufanya sehemu kubwa ya mwili isiwe kwenye jua.
[Picha katika ukurasa wa 17]
Kereng’ende, ambao huweka mabawa yao yakiwa yamenyooshwa kandokando, kwa kawaida ni wakubwa kuliko “damselflies,” ambao hufunga mabawa yao juu ya miili yao