Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Singapore Ile makala “Singapore—Kito cha Asia Kilichopoteza Mng’ao” (Juni 8, 1997) ilifichua njia yenye kushtua ambayo serikali hii ya kisasa imewatendea Wakristo wapenda-amani. Mimi binafsi nawajua wengi wa wanaume na wanawake Wakristo huko, na wote ni watu wenye kuheshimika, wenye upendo. Ninatiwa moyo kwamba wanamtumikia Yehova licha ya mnyanyaso.
I. O., Malasia
Hasira Katika ile makala “Kwa Nini Udhibiti Hasira Yako?” (Juni 8, 1997), mwasema kwamba Simeoni na Lawi walilaaniwa na baba yao. Nina hakika nimesoma mahali fulani kwamba ni hasira yao iliyolaaniwa na Yakobo.
S. L., Marekani
Msomaji wetu yuko sahihi katika jambo hili. “Mnara wa Mlinzi” la Juni 15, 1962 (la Kiingereza), lilieleza: “Yakobo alipokuwa akifa, hakuwalaani Simeoni na Lawi. Aliilaani hasira yao, ‘kwa sababu ni yenye ukatili.’ Alilaani kiruu chao, ‘kwa sababu kinatenda kwa ukali.’”—Mhariri.
Ulaji Ile makala “Ulaji Wako—Je, Waweza Kukuua?” (Juni 22, 1997) iliokoa maisha yangu. Baada ya kuisoma, nilimwambia mke wangu amwite daktari mara moja, kwa kuwa makala hiyo ilisimulia kikamili hali yangu. Baada ya kunichunguza, daktari wangu alipanga nifanyiwe upasuaji asubuhi iliyofuata. Alifanya mipango nilazwe hospitalini mara moja, kwa kuwa aliogopa kuwa singeokoka usiku huo. Sasa niko nyumbani, nikipata nguvu kutokana na upasuaji wa moyo.
F. S., Marekani
Nyakati nyingine, mimi na mume wangu hulipata kuwa jambo gumu kujidhibiti wakati wa milo. Nimesoma makala nyingine juu ya ulaji, lakini hii ilizungumzia habari kwa njia sahili na yenye kutumika. Nina hakika kuwa kwa kutumia madokezo yenu, tutaweza kudumisha afya yetu ikiwa njema.
V. A., Brazili
Asanteni kwa ule mfululizo “Ulaji Wako—Sababu ya Kukufanya Uuhangaikie.” Ulinisaidia kuona hatari za kuwa mzito kupita kiasi. Nimeanza kufuata madokezo yote yaliyokuwa ndani yake, na kwa msaada wa Yehova, najua nitadhibiti ulaji wangu.
V. Y. D., Liberia
Kereng’ende Asanteni sana kwa ajili ya makala yenye kufurahisha sana “Vito vya Kingo za Mto.” (Juni 22, 1997) Ilihusu moja ya wachezaji wa hewani niwapendao sana, kereng’ende. Ninapofanya kazi katika bustani yangu, karibu sikuzote kereng’ende hupaa au kupumzika hapo karibu. Nilimwuliza mtu fulani ambaye hutunza mandhari kwa nini huwa hivyo. Alisema kwamba mlo wa kereng’ende hutia ndani mbu na kwamba mbu huvutiwa na watu. Kwa hiyo sasa mimi humwona kiumbe huyu mwenye kupendeza kuwa mlinzi wa kibinafsi wa aina fulani!
J. F., Marekani
Utafutaji wa Haki Nilifurahia kusoma ile makala “Utafutaji Wetu wa Haki.” (Juni 22, 1997) Bila shaka sifa adilifu za Mungu huwavuta wale wanaotweta na kulia kwa sababu ya ukosefu wa haki. Mimi hasa huwa na hisia nyepesi kuelekea ukosefu wa haki, na ninahitaji kufanya jitihada kikweli kurekebisha maoni yangu na matendo kulingana na viwango vya Mungu.
D. L., Taiwan
Sikubaliani na utangulizi. Mnaposema juu ya watetezi wa Texas wa Alamo, hamsemi walikuwa magaidi waliojaribu kunyakua eneo lililokuwa la Mexico.
A. C., Mexico
Hatukuzungumzia masuala yaliyo tata yaliyotiwa ndani ya pigano hilo huko Alamo, kwa kuwa hayakuhusiana na historia ya kibinafsi ya Antonio Villa. Hata hivyo, nakala yetu ya “Amkeni!” ya Mei 22, 1971 (la Kiingereza), ilitaarifu hivi: “Wamarekani wengi husahau, au labda hawakujua kamwe, kwamba San Antonio ilikuwa sehemu ya Mexico. Mexico iliona pigano hilo kuwa kukomeshwa kwa uasi katika eneo lake. Marekani ililitumia . . . kutetea uingiliaji wake wa mambo ya Mexico.”—Mhariri.