Kwa Nini Almasi Ni Ghali Mno?
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA HISPANIA
NYAKATI nyingine urembo waweza kugunduliwa. Nyakati nyingine ni lazima uundwe. Lakini, almasi ni lazima igunduliwe na kuundwa.
Bila shaka, almasi ambazo hazijakatwa ni urembo wa asili. Msongo wa juu sana na halijoto za juu sana chini ya ardhi hufinyanga polepole kaboni sahili kuwa fuwele ngumu zenye kupenyeka nuru. Lakini mara nyingi mawe hayo hayagunduliwi kwa urahisi. Baadhi ya mashimo makubwa zaidi yaliyochimbwa na mwanadamu—yakiwa hapa na pale katika Australia, Siberia, na Afrika Kusini—yamechimbwa katika kutafuta mawe haya yenye thamani. Ili kupata almasi kadhaa zenye uzani wa gramu sita hivi, huenda mamia ya tani ya udongo yakachimbwa na kuchekechwa!
Almasi zigunduliwapo, wafanyakazi stadi ni lazima wazichonge kwa uangalifu sana ili urembo wake uliofichika utokeze kabla ya almasi kuwekwa kwenye pete au mkufu.
Bila shaka, jitihada hizo zote na ustadi ni wenye gharama. Lakini wanawake wengi—na wanaume—wanahisi kwamba gharama hiyo inafaa, hasa ikiwa almasi ni zawadi inayopewa mwenzi wa ndoa au mchumba kuwa wonyesho wa upendo wa kudumu. Umaridadi na mahaba umefanya almasi kuwa fuwele iliyo ghali zaidi duniani.a
Nazuru Antwerp
Nilipozuru Antwerp, Ubelgiji, jiji ambalo utajiri wake wategemea hasa almasi, upendezi wangu kwa mawe haya ya kipekee uliamshwa. ‘Ni nini,’ nikajiuliza, ‘hufanya almasi ivutie sana? Ni nini siri ya kuunda almasi?’
Ili kujibu maswali hayo, nilizungumza na Dirk Loots ambaye familia yake imefanya kazi za almasi kwa vizazi vitatu. “Sisi huita Antwerp rafiki bora zaidi wa almasi,” akaeleza, “kwa kuwa jiji hili ni mojawapo ya vituo vikubwa zaidi vya almasi ulimwenguni. Basi umekuja mahali bora kabisa pa kugundua siri za sonara wa almasi.”
Kwanza, akanionyesha almasi kadhaa ambazo hazijakatwa alizokuwa ametoka tu kununua. Ingawa ziligharimu dola 350,000, hazikuonekana nzuri sana nilipozitazama kwa mara ya kwanza—zilifanana zaidi na vipande vya kioo. Lakini nilipotazama kwa ukaribu zaidi niliona mng’ao wa ndani ambao ulionyesha umaridadi ambao sonara wa almasi angetokeza. Nikaanza kuelewa ule uvutio wake.
“Pindi kwa pindi nionapo almasi kubwa ambayo haijakatwa, mimi huhisi uvutio fulani kana kwamba kuna uvutano wa kihisia-moyo,” akakiri Dirk. “Mara moja mimi huhisi msukumo wa kuinunua. Inanikumbusha kielezi cha Yesu juu ya mtu aliyepata lulu bora sana, lulu bora sana hivi kwamba akawa tayari kuuza kila kitu alichokuwa nacho ili kuinunua. Sijafikia kamwe hatua hiyo,” akasema akitabasamu, “lakini ni lazima nikiri kwamba almasi nzuri huvutia sana, hata kwetu sisi ambao hutumia maisha zetu kuzinunua na kuziuza. Bila shaka, kutengeneza kito kutokana na almasi ambayo haijakatwa, hata ivutie kadiri gani, kuna matatizo.”
Kung’arisha Almasi Ambayo Haijakatwa
Nilikuwa nimesikia kwamba almasi ambayo ina thamani sana yaweza kuharibiwa na sonara wa almasi asiye mwangalifu. Niliuliza kama hilo hutukia mara nyingi. “Si nadra sana,” akakiri Dirk. “Na hilo laweza kutukia si wakati tu jiwe hilo linapopasuliwa. Hata mng’arisha-almasi pindi kwa pindi aweza kugusa mahali penye kasoro na kuharibu almasi hiyo. Sikuzote sisi huchunguza kwa uangalifu almasi ambayo haijakatwa kupitia nuru aina ya polarized light, ambayo huonyesha sehemu zenye matatizo; lakini kwa kusikitisha hakuna mfumo bora kabisa.
“Ingawa kuvunjika kwa almasi ndiko ogofyo letu kuu, hilo si tatizo pekee. Nyakati nyingine almasi hubadilika na kuwa nyeusi kidogo baada ya pande zake kukatwa na kung’arishwa, na basi thamani yake hupunguka. Na lazima ukumbuke kwamba ni lazima tuondoe asilimia 60 au zaidi ya almasi ambayo haijakatwa ili kufanyiza kito bora zaidi.”
Niliona hilo kama kupoteza pesa nyingi mno, hadi nilipotambua yale yote yanayohusika katika kufanyiza almasi. Dirk alinionyesha almasi kubwa yenye umbo la moyo ambayo ilikuwa imetoka tu kukatwa na kung’arishwa. “Je, waona jinsi inavyong’aa?” akaniuliza. “Huo ‘mng’ao’ ulio ndani ya almasi ni nuru tu ambayo imeakisiwa.
“Kile ambacho sonara apaswa kufanya ni kukata pande zote kwa njia ya kwamba nuru inanaswa mle ndani ya almasi na kuakisiwa kumrudia mtazamaji. Maumbo fulani ya kidesturi, kama vile mkato-mviringo, huakisi nuru kwa njia bora zaidi. Lakini hata miundo yenye kuvutia, kama huu wenye umbo la moyo, hujaribu kuakisi nuru nyingi zaidi kwa kadiri iwezekanavyo. Huo ndio ustadi muhimu kabisa wa sonara wa almasi. Kwa hakika, sonara mmoja wa almasi ajulikanaye sana amechagua maneno, ‘Urembo unafanyizwa na sonara,’ kuwa shime yake ya kibiashara.”
“Unaamuaje umbo utakalokatia almasi?” nikamwuliza Dirk. “Sisi huanza kwa kutazama kwa uangalifu sana jiwe la awali tununualo,” akasema. “Na kwa uangalifu sana! Nakumbuka jiwe moja kubwa ambalo tulichunguza kwa mwezi mmoja kabla ya kufanya uamuzi wa mwisho juu ya jinsi ya kulikata. Nyakati nyingine ni rahisi kwa sababu jiwe ambalo halijakatwa linakuwa rahisi kukatwa katika umbo fulani. Katika kila kisa lengo ni kuamua umbo lifaalo zaidi jiwe fulani hususa ili tusipoteze mawe kwa kadiri iwezekanavyo. Lakini kila upande tukatao—na almasi ya kawaida ina zaidi ya pande 50—humaanisha kupoteza uzani wa almasi.”
Kisha Dirk akaniambia nitazame kwa uangalifu almasi fulani. “Je, waona kasoro iliyopo ndani katika upande wa kulia wa almasi hiyo?” akauliza, akinipa kiookuzi cha sonara. Niliona mistari fulani kama ile ipatikanayo katika kioo kilichovunjika, ndani katika kona moja ya almasi hiyo. “Kasoro ya aina hiyo hupunguza sana thamani ya almasi. Bila shaka, tunaweza kuondoa sehemu hiyo lakini kufanya hivyo kwaweza kufanya tupoteze sehemu kubwa ya almasi. Ikiwa kasoro hiyo haionekani kwa macho, bado tunaweza kuuza almasi hiyo kwa bei ya chini.”
Nilitaka kujua ni kwa nini almasi ambazo ni ndogo-ndogo zina thamani kubwa sana. Kwa wazi, kuna mambo kadhaa yanayohusika.
“Ule usemi ‘almasi hudumu milele’—ingawa ni wa kibiashara—una ukweli fulani,” akasema Dirk. “Almasi hazififii, na mng’ao wazo hauishi. Hizo ni nadra kupatikana, ingawa si nadra kama zilivyokuwa zamani, nazo ni maridadi sana—hakuna shaka kuhusu jambo hilo! Lakini labda jambo kubwa zaidi linaloamua thamani yazo ni mahitaji makubwa ya almasi ulimwenguni pote. Hilo hutegemea sana matangazo ya biashara.
“Ni kwa nini mwanamke anataka pete ya almasi?” Dirk akauliza. “Labda anahusisha almasi na mapenzi na mahaba. Almasi ni kitu cha kipekee, kitu cha kuhaziniwa, cha kumkumbusha juu ya upendo wao unaotumainiwa utadumu kama almasi. Wazo hilo, au fumbo, kama vile wengine huliita, limetokezwa kwa ujanja sana. Pesa zipatazo dola 180,000,000 zilitumiwa mwaka wa 1995 katika kutangaza almasi, ujumbe ambao hufanya watu duniani kote wanunue almasi.”
Thamani ya Almasi
“Nafikiri thamani ya almasi iliyomalizika inategemea ukubwa wake,” nikasema. “Si hivyo hasa,” akajibu Dirk. “Wafanya-biashara wa almasi husema kwamba thamani ya almasi hutegemea mambo manne: mkato, karati, rangi, na wangavu. Kila mojawapo ya mambo hayo huhusika na umaridadi wake—na hivyo thamani—ya almasi.
“Ebu tuanze na mkato. Mkato mzuri ni sanaa kwelikweli, ni mchongo mdogo sana, waweza kusema. Angalia kwa ukaribu zaidi almasi yenye umbo la moyo ambayo ulikuwa ukiistaajabia. Si rahisi kuunda umbo hilo, nalo ni aina inayohitaji kuondoa kiasi kingi zaidi cha jiwe la awali kuliko maumbo mengine. Ona jinsi ambavyo pande zote zimewekwa kwa mtindo fulani ili kuboresha umaridadi wa almasi. Tunaweza kusema kwamba almasi hii hasa imekatwa vizuri sana.
“Kwanza ulivutiwa na ukubwa wake, na hilo laeleweka kwa sababu hiyo ni almasi kubwa ya karati 8. Karati moja ni sawa na gramu 0.2, na acha nitaje kwamba sisi hupima thamani ya karati kwa kupima uzani wa almasi. Kwa kawaida, kadiri karati ziwavyo nyingi ndivyo thamani ya almasi hupanda, lakini thamani yake itaathiriwa pia na rangi na wangavu.
“Almasi huwa na maumbo mengi na rangi nyingi, kama ulivyoona na zile almasi ambazo hazijakatwa. Jambo la kwanza tufanyalo ni kuziainisha kulingana na rangi, zile nyeupe zikiwa na thamani zaidi. Ingawa ni almasi chache ambazo zina rangi tuwezazo kusema kuwa za kuvutia, kama vile pinki, buluu, au nyekundu; na hizo ni zenye thamani zaidi kuliko almasi nyeupe, kwa kuwa hizo ni nadra sana kupatikana.
“Hatimaye, ni lazima tuainishe almasi kulingana na wangavu wake. Almasi ikiainishwa kuwa haina kasoro, yamaanisha kwamba ukitazama almasi hiyo—hata kwa kutumia kiookuzi—hutaona kasoro zozote. Hivyo, mkato, wangavu, na rangi za almasi zaweza kuwa muhimu kama tu uzani wake kwa karati. Kwa mfano, katika 1995, ile iwezayo kuwa almasi kubwa zaidi iliyopata kung’arishwa (karati 546.67) iliwekwa katika wonyesho. Lakini japo ukubwa wake—ikikaribia kulingana na mpira wa gofu—hiyo si almasi ghali zaidi ulimwenguni, kwa sababu si yenye wangavu sana nayo ina rangi ya kahawia ya kimanjano.”
Kabla ya kuondoka Antwerp, nilizungumza na Hans Wins, ambaye amehusika na biashara ya almasi kwa miaka 50. Nilitaka kuuliza swali moja la mwisho, Ni nini hufanya almasi kuwa ya kipekee sana?
“Almasi ndogo-ndogo hazinisisimui sana—hizo hata zaweza kuchongwa na mashine,” akajibu. “Lakini almasi kubwa-kubwa hunivutia sana. Kila almasi ni tofauti—uumbaji wa kipekee uliofanyizwa kwa msongo mkubwa wa kaboni kwa mamilioni ya miaka ya msongo wa volkeno. Unapochunguza almasi, unaweza kuona hasa mistari ya ukuzi, kwa njia fulani kama ile iliyo katika shina la mti. Mtaalamu wa almasi hata aweza kukuambia almasi hiyo imetoka katika mgodi gani.
“Sonara wa almasi hutazama jiwe kama vile tu mchongaji hutazama jiwe la marmar. Tayari anaona akilini kile awezacho kuunda. Akilini mwake, yeye akata na kung’arisha na kito chenye fahari kinatokea. Mimi hupenda kufikiri kwamba almasi hiyo ipatapo mahali katika pete au mkufu fulani, itampa mwenyewe furaha hiyohiyo.”
Baada ya mambo yote, hiyo ndiyo sababu inayofanya ifae kutengeneza almasi.
[Maelezo ya Chini]
a Sababu kuu inayofanya almasi iwe ghali mno ni udhibiti wa Shirika Kuu la Uuzaji.
[Sanduku katika ukurasa wa 15]
Almasi yenye umbo la moyo la karati 8 (huo ukubwa si wa almasi hizo kihalisi)
Mkato wa umbo la pea
Mkato wa “kofia ya Kadinali”
Kujua uzani wa karati wa almasi ambayo haijakatwa
Kuainisha almasi ambazo hazijakatwa kulingana na rangi
Kuchunguza pande za almasi ili kujua kama bado inahitaji kung’arishwa