Kutoka Kuwa Jiwe Hadi Kuwa Kito
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ubelgiji
WA SABABU ya umaridadi wake mkubwa, limekuwa kito chenye kupendwa sana kwa enzi nyingi. Kwa sababu ya ugumu wake—ndicho kitu kigumu sana kiasili kijulikanacho na mwanadamu—hutumiwa sana katika utengenezaji wa vifaa na mashine. Jiwe hili lenye kuvutia sana ni almasi.
Kuna hadithi nyingi zenye kuvutia kuhusu baadhi ya almasi zinazojulikana sana. Almasi iitwayo Koh-i-noor, jina limaanishalo “Mlima wa Nuru,” iligunduliwa karne saba zilizopita huko India. Mwanzoni, jiwe hilo lenye mabongemabonge lilikuwa na uzito wa karati 191, lakini baadaye lilipunguzwa kufikia karati 109.a Tena , kuna ile almasi iitwayo Cullinan, ambayo ni mojawapo ya vito vya taji la Uingereza na ambayo ndiyo almasi kubwa zaidi iliyowahi kupatikana na kukatwa.
Kutoka Kuwa Jiwe Hadi Kuwa Kito
Mwanzoni almasi si vito maridadi. Ni lazima nyingi zichimbwe kutoka kwenye ardhi. Kwa wastani, tani 250 za mchanga lazima ziondolewe na kuchujwa ili kupata karati moja ya almasi safi. Ni sehemu ndogo sana ya zile karati milioni 40 hadi 50 zichimbwazo kila mwaka inayostahili kutumiwa kuwa mapambo ya vito.
Almasi ambazo hazijang’arishwa lazima zitengwe kulingana na ukubwa, usafi, rangi, na umbo. Katika hali yake ya asili, karibu kila almasi ina kasoro. Lakini nyakati nyingine kisehemu fulani chaweza kuwa safi kwa kiasi fulani. Katika hali hizo kisehemu kilicho safi hutengwa kwa kukipasua au kukikata kwa msumeno. Mawe makubwa yenye thamani kubwa yatumikapo, wakati mwingine wachongaji hufikiri na kujadiliana kwa miezi kadhaa kabla ya kuyakata popote. Ni rahisi kuelewa hilo ufikiriapo kwamba kosa moja tu upasuapo laweza kupunguza sana thamani ya almasi au hata kuliharibu jiwe lote.
Hatimaye, kung’arisha huifanya almasi iwe na pande zake, ambazo lazima zipatane na umbo lake. Pande hizo hukiwezesha kito hicho kuwa na uwezo wa kuakisa nuru, na kuifanya almasi iwe na mng’ao wake maarufu.
Wakati ujao almasi ivutiapo uangalifu wako kwa sababu ya mng’ao wake na umaridadi wake, kumbuka ile kazi ngumu waliyoifanya wachimba-migodi na ule usahihi na ustadi wa wachongaji. Bila wao almasi haingeweza kamwe kubadilishwa kutoka jiwe lisilopendeza lililo kama kioo na kuwa johari maridadi.
[Maelezo ya Chini]
a Karati moja ni kipimo cha uzito kinachotoshana na sehemu moja kwa tano ya gramu moja.