Internet—Ni Nini?
KWA kutumia Internet, David, mwalimu katika Marekani, alipata habari ya kutumia katika kufundisha mtaala. Baba fulani Mkanada aliitumia kuwasiliana na binti yake Urusi. Loma, mke nyumbani, aliitumia kuchunguza utafiti wa kisayansi wa mianzo ya mapema ya ulimwengu wote mzima. Mkulima mmoja aliitumia kupata habari kuhusu njia za kupanda ambazo hutumia setilaiti. Mashirika huvutiwa nayo kwa sababu ya uwezo wake wa kutangaza bidhaa na huduma za mashirika hayo kwa mamilioni ya watu wawezao kuwa wateja. Watu tufeni pote husoma habari mpya zaidi za kitaifa na kimataifa kwa kutumia huduma zake nyingi zaidi za kuripoti na za habari.
Ni nini ajabu hii ya kikompyuta iitwayo Internet, au Net? Je, wewe binafsi unaihitaji? Kabla ya kuamua kutumia Internet, huenda ukataka kujua jambo fulani kuihusu. Japo kutangazwa kwake kwa kupita kiasi, kuna sababu za kutahadhari, hasa ikiwa kuna watoto nyumbani.
Hiyo Ni Nini?
Wazia chumba kilichojaa buibui wengi, kila buibui akisokota utando wake mwenyewe. Tando hizo zinafungamana kwa ukaribu sana hivi kwamba buibui hao wanaweza kusafiri kwa uhuru katika mzingile huu. Sasa umepata mwono uliofanywa kuwa sahili wa Internet—mkusanyo wa tufeni pote wa aina tofauti za kompyuta na mifumo ya kompyuta ambayo imeunganishwa pamoja. Kama tu vile simu hukuwezesha kuzungumza na mtu fulani upande ule mwingine wa dunia ambaye pia ana simu, ndivyo Internet huwezesha mtu kuketi kwenye kompyuta yake na kubadilishana habari na kompyuta nyinginezo na watumizi wengine wa kompyuta mahali popote ulimwenguni.
Wengine hurejezea Internet kuwa njia kuu bora ya habari. Kama tu vile barabara iwezeshavyo usafiri kupitia maeneo mbalimbali ya nchi, ndivyo Internet iwezeshavyo habari kutiririka kupitia mifumo ya kompyuta mbalimbali iliyounganishwa. Ujumbe usafiripo, kila mfumo ufikiwao huwa na habari inayosaidia katika kuunganisha kwenye mfumo ufuatao. Kikomo cha ujumbe huo chaweza kuwa jiji au nchi tofauti.
Kila mfumo waweza “kuzungumza” na mfumo ulio jirani yake kwa njia ya kanuni za kawaida zilizofanyizwa na wabuni wa Internet. Ni mifumo mingapi iliyounganishwa ulimwenguni pote? Makadirio fulani husema zaidi ya 30,000. Kulingana na chunguzi za hivi majuzi, mifumo hii huunganisha zaidi ya kompyuta 10,000,000 na watumizi wapatao 30,000,000 ulimwenguni pote. Inakadiriwa kwamba idadi ya kompyuta zinazounganishwa hurudufika kila mwaka.
Ni habari gani wawezazo kupata watu kwenye Internet? Hiyo huandaa mkusanyo wenye kuongezeka haraka sana wa habari, kukiwa na vichwa kuanzia tiba hadi sayansi na tekinolojia. Ina habari za kina juu ya sanaa na vilevile habari za utafiti kwa wanafunzi na yashughulikia tafrija, vitumbuizo, michezo, ununuzi, na fursa za kazi ya kuajiriwa. Internet hufanya iwezekane kufikia shajara za mwaka, kamusi, ensaiklopedia, na ramani.
Hata hivyo, kuna sehemu zisizo nzuri za kufikiria. Je, kila kitu kwenye Internet chaweza kuonwa kuwa chenye mafaa? Ni utumishi gani na vyanzo vipi vya habari vinavyoandaliwa na Internet? Tahadhari gani zihitajiwazo kuchukuliwa? Makala zifuatazo zitazungumzia maswali haya.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 4]
Chanzo na Mfanyizo wa Internet
Internet ilianza kama jaribio lililofanywa na Wizara ya Ulinzi ya Marekani katika miaka ya 1960 ili kusaidia wanasayansi na watafiti kutoka maeneo yaliyotapakaa sana kufanya kazi pamoja kwa kushiriki kompyuta chache na zilizo ghali na faili za habari. Mradi huo ulihitaji kufanyizwa kwa kikundi cha mifumo ambayo ingetenda kama mfumo ulioshikamana.
Vita Baridi ilichochea upendezi katika mfumo “usioweza kuharibiwa kwa bomu.” Ikiwa sehemu fulani ya mfumo huo ingeharibiwa, bado habari ingesafiri hadi kikomo chake kwa msaada wa sehemu zilizobaki. Hilo likitokeza mfumo wa Internet, daraka la kuelekeza ujumbe likaenezwa kotekote kwenye mfumo huo badala ya kuwekwa mahali pamoja tu.
Kwa sehemu kubwa Internet, sasa ikiwa na muda wa miongo zaidi ya miwili, imekuja kuwa mashuhuri kwa sababu ya utumizi wa vipitiaji-pitiaji. Kipitiaji-pitiaji ni kifaa cha programu ya kompyuta ambacho hurahisisha sana utaratibu wa mtumizi wa “kuzuru” mahali tofauti-tofauti kwenye Internet.