Huduma na Vyanzo vya Habari vya Internet
CHANZO cha kawaida cha habari kinachoandaliwa na Internet ni mfumo wa ulimwenguni pote wa kupeleka na kupokea barua kielektroni, uitwao E-mail. Kwa hakika, E-mail huwakilisha sehemu kubwa ya shughuli za Internet na kwa wengi ndiyo chanzo cha habari pekee cha Internet wanachotumia. Mfumo huo hufanyaje kazi? Ili kujibu swali hilo, acheni tupitie mfumo wa kawaida wa upelekaji wa barua kwanza.
Wazia kwamba waishi Kanada na wataka kupeleka barua kwa binti yako anayeishi Moscow. Baada ya kuweka anwani kwenye bahasha ifaavyo, waipeleka, hivyo ukianzisha safari ya barua hiyo. Katika posta, barua hiyo yapitishwa hadi mahali pafuatapo, labda kitovu cha usambazaji cha kimkoa au cha kitaifa, kisha hadi kwenye ofisi ya posta ya mahali inapoenda iliyo karibu na binti yako.
Utaratibu kama huo hutokea na E-mail. Baada ya barua yako kupangwa kwenye kompyuta yako, ni lazima uweke anwani hususa ya E-mail inayomtambulisha binti yako. Mara upelekapo barua hii ya kielektroni, hiyo husafiri kutoka kwenye kompyuta yako, mara nyingi kupitia kifaa kiitwacho modemu, ambacho huunganisha kompyuta yako kwenye Internet kupitia mfumo wa simu. Yaanza safari yake, ikielekea kompyuta tofauti-tofauti ambazo hutenda kama posta za mahali fulani au za kitaifa. Zina habari ya kutosha kufikisha barua hiyo kwenye kompyuta ya kikomo chake, mahali ambapo binti yako aweza kuitoa.
Tofauti na barua ya kawaida, E-mail mara nyingi hufikia kikomo chake, hata katika kontinenti nyinginezo, kwa kipindi cha dakika chache au chini ya hicho isipokuwa sehemu fulani ya mfumo huo imesongamana sana au haifanyi kazi kwa muda. Binti yako akaguapo kisanduku chake cha barua cha kielektroni, atapata E-mail yako. Mwendo wa kasi wa E-mail na urahisi wake wa kupelekwa hata kwa watu kadhaa popote ulimwenguni huifanya iwe namna ya mawasiliano ipendwayo na wengi.
Vikundi vya Habari
Huduma nyingine ipendwayo na wengi huitwa Usenet. Usenet huwezesha kufikia vikundi vya habari kwa ajili ya mazungumzo ya vikundi kuhusu vichwa hususa vya habari. Baadhi ya vikundi vya habari hushughulikia hasa ununuzi na uuzaji wa bidhaa tofauti-tofauti za utumizi. Kuna maelfu ya vikundi vya habari, na mara tu mtu atumiaye Internet afikiapo Usenet, hakuna gharama ya kujiandikisha.
Ebu tuwazie kwamba mtu fulani amejiunga na kikundi cha habari kinachohusika na ukusanyaji wa stampu. Ujumbe mpya kuhusu hobi hii upelekwapo na wengine waliojiandikisha kwa kikundi hiki, ujumbe huo hupatikana kwa mtu huyu mpya. Mtu huyu hupitia si kile ambacho mtu fulani alipelekea kikundi hicho cha habari tu bali pia kile ambacho wengine wameandika kwa kujibu. Kwa kielelezo, ikiwa mtu fulani aomba habari kuhusu mfululizo fulani hususa wa stampu, muda mfupi baada ya hapo huenda kukawa na majibu mengi kutoka ulimwenguni pote, yakiandaa habari ambayo itapatikana mara hiyo kwa wote waliojiandikisha kwa kikundi hiki.
Tofauti ya wazo hilo ni Bulletin Board System (BBS). Mifumo hiyo ya BBS inafanana na Usenet, isipokuwa kwamba faili zote ziko katika kompyuta moja, ambayo kwa kawaida huwa na mtu mmoja au kikundi. Mazungumzo ya vikundi vya habari huonyesha mapendezi, maoni, na maadili yanayotofautiana ya watumizi, kwa hiyo busara yahitajiwa.
Kushiriki Faili na Kutafuta Kichwa cha Habari
Mmojawapo miradi ya awali ya Internet ulikuwa kushiriki habari duniani pote. Mwalimu aliyetajwa katika makala iliyotangulia alimpata mwelimishaji mwingine kwenye Internet ambaye alikuwa na nia ya kushiriki habari za mitaala iliyokuwa imetayarishwa. Kwa muda wa dakika chache faili zilihamishwa, japo umbali wa kilometa 3,000.
Ni msaada gani upatikanao kwa mtu ambaye hajui mahali ambapo habari fulani ipo katika Internet? Kama tu vile tupatavyo nambari ya simu kwa kutumia kitabu cha nambari za simu, mtumizi aweza kupata mahali anapotaka kwenye Internet kwa kufikia kwanza sehemu ziitwazo mahali pa utafutaji. Mtumizi hutoa neno au fungu la maneno; kisha mahali hapo hujibu kwa kutoa orodha ya mahali ndani ya Internet ambapo habari yaweza kupatikana. Kwa kawaida, utafutaji huo hauna malipo na huchukua sekunde chache tu!
Mkulima aliyetajwa mapema alikuwa amesikia juu ya ufundi mpya uitwao ukulima wenye usahihi, ambao hutumia kompyuta na ramani za setilaiti. Alipoandaa fungu hilo la maneno mahali pa utafutaji, alipata majina ya wakulima ambao wanatumia ufundi huo mpya na vilevile habari ya kina kuhusu namna hiyo ya ukulima.
Mfumo wa World Wide Web
Sehemu ya Internet iitwayo World Wide Web (au, Web) huruhusu watungaji watumie wazo la kale—lile la vielezi-chini—katika njia mpya. Mtungaji wa makala ya gazeti au kitabu aingizapo ishara ya kielezi-chini, twatafuta sehemu ya chini ya ukurasa na yawezekana twaelekezwa kwenye ukurasa au kitabu kingine. Watungaji wa hati za kompyuta za Internet wanaweza kufanya jambo lilo hilo kwa kutumia ufundi utakaopiga mstari au kutokeza neno, fungu la maneno, au picha katika hati yao.
Neno au picha iliyotokezwa ni kidokezi kwa msomaji kwamba kuna chanzo fulani cha habari, mara nyingi hati nyingineyo inayohusiana na Internet. Hati hii ya Internet yaweza kutolewa na msomaji kuonyeshwa mara hiyo. Hati hiyo yaweza kuwa hata katika kompyuta tofauti iliyo katika nchi nyingineyo. David Peal, mtungaji wa kitabu Access the Internet!, ataja kwamba ufundi huu “hukuunganisha kwenye hati zenyewe, si tu marejezo ya hizo hati.”
Mfumo wa Web pia hutegemeza uhifadhi na utoaji, au uchezaji, wa picha, michoro, katuni zilizohuishwa, vidio, na sauti. Loma, mke nyumbani aliyetajwa mwanzoni mwa makala iliyotangulia, alipata na kucheza sinema fupi yenye rangi kuhusu nadharia za sasa zinazohusiana na ulimwengu wote mzima. Alisikiliza masimulizi kupitia mfumo wake wa sauti wa kompyuta.
Kupitia-Pitia Internet
Kwa kutumia kifaa cha kupitia-pitia cha Web, mtu anaweza kwa urahisi na kwa uharaka kuona habari na michoro yenye rangi nyingi ambayo yaweza kuhifadhiwa kwenye kompyuta katika nchi nyingi tofauti. Kutumia kifaa cha kupitia-pitia cha Web kwaweza katika njia fulani kuwa sawa na kusafiri kwenyewe, isipokuwa kutumia kifaa hicho ni rahisi zaidi. Mtu aweza kuzuru maonyesho ya Web ya Hati-Kunjo za Bahari Iliyokufa au Jumba la Makumbusho ya Maangamizi Makubwa. Uwezo huu wa kwenda huku na huku katika Web ya Internet kwa kawaida huitwa kupitia-pitia Internet.
Biashara na mashirika mengineyo yamekuwa na upendezi kwa Web yakiutumia kuwa njia ya kutangaza bidhaa na huduma zake na vilevile kutoa habari za namna nyinginezo. Hayo hufanyiza ukurasa wa Web, namna fulani ya dirisha la chumba cha madukani cha kielektroni. Mara wajuapo tu ukurasa wa Web wa shirika fulani, watu wawezao kuwa wateja waweza kutumia kifaa cha kupitia-pitia ili kwenda kufanya “ununuzi,” au kupitia-pitia habari. Hata hivyo, kama ilivyo katika soko lolote lile, si bidhaa, huduma, au habari zote zinazoandaliwa na Internet zafaa.
Watafiti wanajaribu kufanya Internet iwe salama vya kutosha kwa ajili ya shughuli za siri na zilizolindwa salama. (Tutazungumzia usalama baadaye.) Internet nyingine ya ulimwenguni pote—iliyopewa na watu fulani jina Internet ya 2—inafanyizwa kwa sababu ya shughuli zinazoongezeka ambazo utendaji huu wa kibiashara umetokeza.
“Kupiga Gumzo” Ni Nini?
Huduma nyingine ya kawaida ya Internet ni Upigaji wa Gumzo wa Kupitishiana Ujumbe wa Internet, au Kupiga Gumzo. Kupiga gumzo huwezesha kikundi cha watu, wakitumia majina bandia, kupelekeana ujumbe kwa haraka. Ingawa hutumiwa na marika tofauti-tofauti, hiyo, hupendwa sana hasa miongoni mwa vijana. Mara aunganishwapo, mtumizi huwezeshwa kuwasiliana na idadi kubwa ya watumizi wengine kutoka ulimwenguni pote.
Pale paitwapo kwa kawaida mahali, au miunganisho ya kupigia gumzo, hufanyizwa pakiwa hasa na kichwa hususa, kama vile hadithi zenye kubuniwa za sayansi, sinema, michezo, au mahaba. Ujumbe wote unaopigwa chapa katika mahali pa kupigia gumzo huonekana karibu kwa wakati mmoja kwenye viwambo vya kompyuta vya washiriki wote wa mahali hapo pa kupigia gumzo.
Mahali pa kupigia gumzo ni kama kikundi cha watu wanaochangamana na kuzungumza kwa wakati mmoja, isipokuwa wote wanapiga chapa ujumbe mfupi-mfupi badala ya kuzungumza. Kwa kawaida mahali pa kupigia gumzo hufanya kazi kwa muda wa saa 24 kwa siku. Bila shaka Wakristo wanatambua kwamba kanuni za Biblia kuhusu mashirika, kama ile ipatikanayo kwenye 1 Wakorintho 15:33, hutumika kwa kushiriki katika vikundi vya kupiga gumzo kama tu vile itumikavyo katika sehemu zote za maisha.a
Ni Nani Hulipia Internet?
Huenda ukawa unajiuliza, ‘Ni nani hulipa gharama za umbali mkubwa ambao mtu aweza kusafiri katika Internet?’ Gharama hushirikiwa na watumizi wote, mashirika na watu mmoja-mmoja. Hata hivyo, si lazima mtumizi alipishwe gharama ya simu ya mbali, hata ikiwa alizuru mahali pengi pa kimataifa. Watumizi wengi wana akaunti na kampuni ya kuandaa huduma ya Internet, ambayo katika visa vingi humlipisha mtumizi kiwango fulani kilichowekwa kila mwezi. Makampuni hayo kwa kawaida huandaa nambari ya simu ya mahali fulani ili kuepuka gharama za ziada. Ada ya kawaida ya kila mwezi ni dola 20 hivi (za Marekani).
Kama uwezavyo kuona, uwezo wa Internet ni mkubwa sana. Lakini je, uingie kwenye hii njia kuu bora ya habari?
[Maelezo ya Chini]
a Uhitaji wa tahadhari kuhusu mahali pa kupigia gumzo utazungumziwa baadaye.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Anwani za Internet—Hizo Ni Nini?
Kutambulisha watu waliounganishwa kwenye Internet hutimizwa na anwani za E-mail. Wazia kwamba wataka kupeleka E-mail kwa rafiki ambaye anwani yake ya E-mail ni drg@tekwriting.com.b Katika kielelezo hiki, utambulisho wa mtu huyo ni “drg.” Mara nyingi watu hutumia kifupi cha majina au majina yao kamili kuwa utambulisho wao. Neno lifuatalo ishara “@” laweza kuwa mwajiri wao, mahali pao pa kazi, au kampuni inayowaandalia huduma za E-mail. Katika kisa hiki, “tekwriting” hutambulisha kampuni hiyo. Sehemu ya mwisho ya anwani hiyo hutambulisha aina ya shirika ambalo rafiki yako anajitambulisha nalo. Katika kisa hiki, “com” hurejezea shirika la kibiashara. Mashirika ya kielimu yana utambulisho wa aina hiyohiyo isipokuwa huishia kwa “edu,” na mashirika yasiyo ya kibiashara huishia kwa “org.” Kiwango kingine cha E-mail huishia kwa maandishi yaliyofupishwa ya nchi anakotoka mtu huyo. Kwa kielelezo, anwani lvg@spicyfoods.ar huonyesha kwamba mtu ambaye utambulisho wake ni “lvg” anahusiana na shirika liitwalo “spicyfoods” katika Argentina.
Namna nyingine ya anwani hutafuta hati za Web kwenye Internet. Tuseme kwamba habari kuhusu utafiti wa misitu ya mvua yaweza kupatikana katika hati ya Web iliyoko kwenye http://www.ecosystems.com/research/forests/rf. Herufi “http” (Hypertext Transfer Protocol) hutambulisha itifaki ya kushughulikia aina ya hati ya Web, na “www.ecosystems.com” huonyesha jina la server ya Web, kompyuta fulani—katika kisa hiki shirika la kibiashara linaloitwa “ecosystems.” Hati yenyewe ya Web ndiyo sehemu ya mwisho ya anwani—“/research/forests/rf.” Anwani za Web mara nyingi huitwa Uniform Resource Locators, au URL, kwa kifupi.
[Maelezo ya Chini]
b Anwani za Internet zilizonukuliwa hapa ni za kubuniwa.