Je, Kweli Ngoma za Kiafrika Huzungumza?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Nigeria
KATIKA safari yake ya kuteremka Mto Kongo miaka ya 1876 na 1877, mvumbuzi Henry Stanley hakupata fursa ya kufikiria mazuri ya ngoma za wenyeji. Kwake na kwa wasafiri wenzake, ujumbe uliowasilishwa na ngoma ulikuwa mmoja tu: vita. Ule mdundo mzito waliosikia ulimaanisha kwamba walikuwa karibu kushambuliwa na wapiganaji wakali waliojihami kwa mikuki.
Ni baadaye tu katika nyakati za amani kwamba Stanley alijifunza jinsi ambavyo ngoma zingeweza kuwasilisha ujumbe zaidi ya kuita watu vitani. Akifafanua kabila moja lililoishi kando ya Mto Kongo, Stanley aliandika: “[Wao] hawajaanza kutumia ishara za umeme, lakini wao wana mfumo wa kuwasiliana ambao ni wenye matokeo sana. Ngoma zao kubwa zinapopigwa pande tofauti-tofauti, hizo huwasilisha lugha ambayo ni dhahiri sana kwa wale wanaofahamu lugha hiyo kama vile tu usemi wa kawaida ulivyo dhahiri.” Stanley alitambua kwamba wapiga-ngoma walipeleka zaidi ya ujumbe ambao ishara za buruji au king’ora zingewasilisha; ngoma zingeweza kuwasilisha ujumbe hususa.
Ujumbe ungeweza kuwasilishwa kutoka kijiji hadi kijiji. Baadhi ya ngoma zingeweza kusikika umbali wa kilometa 8 hadi 11, hasa kama zingepigwa usiku kutoka kwenye chelezo au kutoka juu mlimani. Wapiga-ngoma walio mbali walisikiliza, wakaelewa, na kupitisha ujumbe kwa wengine. Msafiri Mwingereza A. B. Lloyd aliandika katika 1899: “Niliambiwa kwamba kutoka kijiji fulani hadi kingine, zaidi ya kilometa 160, ujumbe ungepelekwa kwa muda upunguao saa mbili, nami naamini kabisa kwamba inawezekana kuwasilisha ujumbe kwa muda mfupi hata zaidi.”
Muda mrefu baada ya kuanza kwa karne ya 20, ngoma ziliendelea kutimiza fungu kubwa katika kuwasilisha habari. Kitabu Musical Instruments of Africa, kilichochapishwa mwaka wa 1965, kilisema: “Ngoma zenye kuzungumza hutumiwa kama simu na telegrafu. Ujumbe wa aina yoyote hupelekwa—kutangaza kuzaliwa kwa watoto, vifo, na ndoa; michezo, dansi, na sherehe za unyago; ujumbe wa serikali, na vita. Nyakati nyingine ngoma ziliwasilisha porojo au mizaha.”
Lakini ngoma ziliwasilishaje ujumbe? Katika Ulaya na kwingineko, ujumbe ulipelekwa kwa ishara za umeme kupitia nyaya za simu. Kila herufi ya alfabeti ilipata ishara yake yenyewe ili maneno na sentensi ziweze kuendelezwa mojamoja. Hata hivyo, watu wa Afrika ya Kati hawakuwa na lugha iliyoandikwa, na basi ngoma hazikuendeleza maneno. Wapiga-ngoma wa Afrika walitumia njia nyingine.
Lugha ya Ngoma
Njia ya kufahamu uwasiliano wa ngoma hutegemea kufahamu lugha zenyewe za Kiafrika. Lugha nyingi katika Afrika ya Kati na ya Magharibi hasa ni za toni mbili—kila silabi ya neno lisemwalo lina toni mbili za msingi, ama toni ya juu ama ya chini. Badiliko la toni hugeuza maana ya neno. Kwa mfano, fikiria neno lisaka, la lugha ya Kikele nchini Zaire. Silabi zote tatu zinapotamkwa katika toni za chini, neno hilo lamaanisha “kidimbwi au bwawa”; toni ya chini-chini-juu ya silabi hizo yamaanisha “ahadi”; toni ya chini-juu-juu yamaanisha “sumu.”
Ngoma za Kiafrika zilizopasuliwa mianya ambazo hutumiwa kuwasilisha ujumbe pia zina toni mbili, ya juu na ya chini. Vivyo hivyo, ngoma zilizowambwa kwa ngozi zipelekapo ujumbe, hizo hutumiwa zikiwa mbili, ngoma moja ikiwa na toni ya juu na ngoma nyingine ikiwa na toni ya chini. Basi, mpiga-ngoma mwenye ustadi huwasilisha ujumbe kwa kuiga violezo vya toni za lugha ya kawaida. Kitabu Talking Drums of Africa chasema: “Hiyo iitwayo lugha ya ngoma ni sawa tu na lugha ya kabila hilo.”
Bila shaka, lugha ya toni mbili mara nyingi ina maneno mengi yasemwayo na toni na silabi zinazofanana. Kwa mfano, katika lugha ya Kikele, nomino zipatazo 130 zina sauti zilezile (juu-juu) kama sango (baba). Zaidi ya 200 zina sauti zilezile (chini-juu) kama nyango (mama). Ili kuepuka kueleweka vibaya, wapiga-ngoma huandaa muktadha wa maneno kama hayo, kutia ndani fungu fupi la maneno lijulikanalo sana lenye utofauti uwezao kumwezesha msikilizaji aelewe jambo linalosemwa.
Kuzungumza Kupitia Ngoma Zilizopasuliwa
Mojawapo ya aina ya ngoma inayozungumza ni ile ya mbao ambayo imepasuliwa. (Ona picha iliyo katika ukurasa wa 23.) Ngoma hizo hufanyizwa kwa kutoboa gogo. Ngoma hizo hazina ngozi kwenye pande zake. Ingawa ngoma iliyo katika picha imepasuliwa mianya miwili, nyingi zimepasuliwa mwanya mmoja mrefu. Kupiga upande mmoja wa mwanya hutokeza toni ya juu; kupiga upande mwingine wa mwanya hutokeza toni ya chini. Mara nyingi ngoma zilizopasuliwa zina kimo cha meta moja, ingawa zaweza kuwa fupi kufikia nusu meta au ndefu kufikia meta mbili. Kipenyo chaweza kuanzia sentimeta 20 hadi kufikia meta moja.
Ngoma zilizopasuliwa zilitumiwa kwa makusudi mengi kuliko kupeleka tu ujumbe kutoka kijiji hadi kijiji. Mtungaji wa vitabu wa Kamerun, Francis Bebey alifafanua fungu la ngoma hizo katika michuano ya mieleka. Timu mbili zenye kuchuana zinapojitayarisha kukutana katika baraza la kijiji, ile timu bingwa ilicheza midundo ya ngoma zilizopasuliwa huku ngoma hizo zikiwasifu. Ngoma za upande mwingine zingesema: “Ee, bingwa, umewahi kupata mshindani? Nani awezaye kushindana na wewe, nani? Maskini hao . . . wadhani kwamba waweza kukushinda kwa kinyangarika fulani hoi wakiitacho eti bingwa . . . , lakini hakuna mtu kamwe awezaye kukushinda.” Wanamuziki katika kambi ya wapinzani wangeelewa mizaha hiyo nao wangejibu kwa methali: “Tumbili mdogo . . . tumbili mdogo . . . anataka kupanda mti lakini kila mtu anaona kwamba ataanguka. Lakini ng’o! yeye hataanguka, atafika kileleni, huyu tumbili mdogo.” Ngoma zingeendelea kusisimua na kutumbuiza katika mchuano wote wa mweleka.
Ngoma Zizungumzazo kwa Njia Bora Kuliko Zote
Ngoma zenye msongo zimepiga hatua kubwa hata zaidi. Ngoma unayoona katika picha iliyo kulia inaitwa dundun; nayo ni ngoma maarufu inayozungumza ya Wayoruba, nchini Nigeria. Ikiwa nyembamba katikati, ngoma hii inapigwa kwa sehemu mbili, ambazo zimewambwa kwa ngozi laini na nyembamba ya mbuzi. Nazo sehemu za mwisho zimeunganishwa kwa vikanda vya ngozi. Vikanda hivyo vikazwapo, mkazo ulio juu ya ngoma huongezeka ili iweze kutokeza sauti tofauti-tofauti katika ubeti mmoja au zaidi. Kwa kutumia mikwiro iliyopinda na kubadili uzito na mdundo wa sauti, mpiga-ngoma stadi aweza kuiga mwinuko na mshuko wa sauti ya kibinadamu. Basi, wapiga-ngoma waweza “kuzungumza” na wapiga-ngoma wengine ambao wanaweza kufasiri na kucheza lugha hiyohiyo ya ngoma.
Mnamo Mei 1976 uwezo mkubwa wa wapiga-ngoma wa kuwasiliana kupitia ngoma ulionyeshwa na wapiga-ngoma wa makao ya chifu fulani wa Wayoruba. Wenye kujitolea miongoni mwa wahudhuriaji walinong’ona maagizo fulani kwa mpiga-ngoma stadi ambaye aliwasilisha maagizo hayo kwa mwingine aliyekuwa mbali na makao hayo kwa ngoma. Akiitikia maagizo hayo yaliyowasilishwa kwa ngoma, yule mpiga-ngoma aliye mbali alitoka mahali fulani na kwenda mahali pengine na kutekeleza yale aliyoagizwa.
Si rahisi kujifunza ujumbe uliowasilishwa kwa ngoma. Mwandishi mmoja I. Laoye alisema: “Ngoma za Wayoruba ni utaalamu ulio mgumu sana ambao unahitaji miaka mingi ya kujifunza. Mpiga-ngoma hahitajiki tu kuwa na ustadi mwingi wa kupiga ngoma na kufahamu sana midundo, bali pia awe na kumbukumbu nzuri ya kushika mashairi na historia ya mji anaoupelekea ujumbe kupitia ngoma.”
Katika miongo ya majuzi ngoma za Kiafrika hazizungumzi sana kama zilivyokuwa zikizungumza zamani, ingawa zingali zinatimiza fungu kubwa katika muziki. Chasema kitabu Musical Instruments of Africa: “Ni vigumu sana kujifunza kupeleka ujumbe kupitia ngoma; kwa hiyo, sanaa hii inapotea haraka sana katika Afrika.” Aongezea mtaalamu wa vyombo vya habari Robert Nicholls: “Ngoma kubwa za wakati uliopita, zenye sauti ambazo zilisafiri mbali sana na ambazo zilitumika kihususa katika kupitisha ujumbe, zimeelekea kutoweka.” Siku hizi watu wengi huona ikiwa rahisi kutumia simu.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Ngoma iliyopasuliwa
[Picha katika ukurasa wa 23]
Ngoma inayozungumza ya Wayoruba