Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Redio Asanteni sana kwa makala nzuri sana yenye kichwa “Redio—Uvumbuzi Uliobadili Ulimwengu.” (Oktoba 8, 1996) Nina umri wa miaka 18, na mimi hupenda sana kusikiliza redio. Niliona mazungumzo hayo juu ya maendeleo ya redio kuwa yenye kupendeza sana. Ilipendeza hasa kujua kwamba katika nyakati zilizopita Mashahidi wa Yehova walitumia redio ili kueneza habari njema ya Ufalme.
F. B., Italia
Vipepeo Nilikuwa nikihubiri peke yangu katika eneo la mashambani na kuamua kukazia ile makala “Msafiri Dhaifu Lakini Hodari.” (Oktoba 8, 1996) Nilikutana na mkulima mmoja pandikizi kwelikweli—si mtu ambaye kwa kawaida ningezungumza naye kuhusu vipepeo! Lakini, baada ya kuona picha hizo zenye kuvutia, alichukua magazeti hayo na kusema kwamba spishi nyingi ambazo ni nadra zaweza kupatikana katika shamba lake. Nilipoondoka, mke wake alikuwa amezama katika gazeti hilo akilisoma. Basi, kama kipepeo, nitarudi—na kuwaonyesha zaidi kuhusu Ufalme wa Mungu!
B. B., Uingereza
Hiyo ilikuwa mojawapo ya makala zenye kupendeza zaidi nilizopata kusoma. Siku chache tu baada ya magazeti hayo kufika, niliona miti yetu imejaa vipepeo-maliki! Nilimshukuru Mungu kwa uumbaji huu wa ajabu.
S. M., Marekani
Kuruhusiwa kwa Uovu Asanteni kwa ile makala “Vijana Huuliza . . . Kwa Nini Mungu Huruhusu Maovu Yatokee?” (Oktoba 22, 1996) Baada ya kuteseka sana kwa upweke, kudhalilishwa, na kuwa na huzuni kubwa katika ndoa ya miaka 18 na mume asiye mwaminifu ambaye hastahi wanawake, kusoma kwamba Yehova ni Mungu mwenye upendo ambaye anatujali kulikuwa kitulizo kikubwa. Ilikuwa kana kwamba Yehova alikuwa akinifariji.
H. T., Marekani
Sigareti Ningependa kusema juu ya makala “Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?” (Oktoba 22, 1996) Inasikitisha kama nini kwamba sikuipata miaka iliyopita! Mume wangu alikufa kwa kansa ya mapafu mwaka huu. Amekuwa mvutaji sana wa sigareti kwa miaka 50. Mimi binafsi sikujua kwamba sigareti ilikuwa na madhara mabaya sana hivyo.
H. G., Ujerumani
Akee Makala yenu “Akee—Chakula cha Kitaifa cha Jamaika” (Oktoba 22, 1996) ilikuwa nzuri sana. Nikiwa mzaliwa wa Jamaika, sijapata kamwe kumwandalia mtu akee ambaye alisema hakukipenda. Ninatia moyo mtu yeyote aendaye Jamaika aonje akee!
E. B., Marekani
Inapendeza kama nini kuona mazungumzo mengine juu ya kazi za Muumba wetu! Miti ya akee imejaa hapa Ghana nayo hutumika katika miji fulani na vijiji fulani kuwa miti ya kutoa kivuli. Katika misitu miti hiyo huwa mirefu sana. Popo, kasuku, na ndege wengine hupumzikia matawi yake. Mti wa akee ni zawadi nyingine nzuri sana kutoka kwa Mungu.
P. A. E., Ghana
Farasi Ni lazima niandike ili kuonyesha uthamini wangu kwa ile makala “Bado Wanalima Mashamba kwa Kutumia Farasi.” (Oktoba 22, 1996) Mimi hupenda wanyama, na makala hiyo ilinigusa moyo. Napenda jinsi mlivyoonyesha uhusiano ambao mtu aweza kuwa nao na wanyama, hasa sehemu inayohusu mtu kufurahia “mazungumzo” pamoja na farasi zake.
V. H., Marekani
Nimeishi maisha yangu yote katika eneo la miji, na tamaa yangu ya kuwa karibu na uumbaji wa Yehova haijaridhishwa. Kwa kusoma makala yenu, niliweza kulima kwa kutumia farasi katika akili yangu. Asanteni sana kwa makala hizo zenye kupendeza sana.
L. A. D., Marekani