Kuyarudia Mambo ya Msingi Katika Kupigana na MALARIA
Fikira za ulimwengu zikiwa zimekaziwa vita vya wenyewe kwa wenyewe, uhalifu, ukosefu wa kazi za kuajiriwa, na matatizo mengine, vifo vinavyosababishwa na malaria havitajwi hata kidogo na habari za jioni. Hata hivyo, karibu nusu ya idadi ya watu ulimwenguni, lasema Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO), wanatishwa na malaria, na watu wapatao milioni 300 hadi milioni 500 huambukizwa malaria kila mwaka, hiyo ikifanya malaria iwe “maradhi ambayo yameenea zaidi ya maradhi yote ya kitropiki na pia mojawapo ya maradhi yaliyo hatari zaidi.” Hayo ni hatari kadiri gani?
Kila sekunde 20 mtu fulani hufa kutokana na malaria. Hiyo hujumlika kuwa vifo vya watu zaidi ya milioni 1.5 kila mwaka—idadi itoshanayo na watu wote wa taifa la Botswana katika Afrika. Vifo tisa kati ya kumi hutukia katika tropiki ya Afrika, ambako wengi wa wanaokufa ni watoto wachanga. Katika mabara ya Amerika, Shirika la Afya Ulimwenguni lilirekodi visa vingi zaidi vya malaria katika eneo la Amazon. Ukataji wa miti na mabadiliko mengine ya mazingira yamefanya wengi zaidi waambukizwe malaria katika sehemu hizo za ulimwengu. Katika jumuiya fulani za Brazili zilizo katika eneo la Amazon, tatizo hilo sasa limekuwa baya sana hivi kwamba zaidi ya wakazi 500 kati ya kila wakazi 1,000 huambukizwa.
Iwe ni katika Afrika, mabara ya Amerika, Asia, au kwingineko, malaria hasa huambukiza jamii zilizo maskini zaidi. Watu hao, lasema Shirika la Afya Ulimwenguni, “hawana uwezo sana wa kupata huduma za afya, hawawezi kugharimia kinga ya kibinafsi nao wako mbali zaidi na sehemu za utendaji wa kudhibiti malaria.” Hata hivyo, si kwamba wale walio maskini hawana tumaini. Katika miaka ya majuzi, TDR News, kijarida cha utafiti wa maradhi ya kitropiki, mojawapo ya njia zenye kuonekana kufaa zaidi katika kuzuia vifo vinavyotokana na malaria imepatikana. Kitu hicho cha kuokoa uhai ni nini? Vyandarua vyenye dawa za kuua wadudu.
Chandarua Chashinda
Ingawa kutumia vyandarua ni suluhisho linaloturudisha kwenye mambo ya msingi, Dakt. Ebrahim Samba, ambaye ni mkurugenzi wa Shirika la Afya Ulimwenguni, eneo la Afrika, alikiambia Panos Features, kijarida cha Taasisi ya Panos, kwamba majaribio ya kuona jinsi vyandarua vinavyofanya kazi katika kupigana na malaria yameonyesha “matokeo yenye kusisimua sana.” Kwa mfano, nchini Kenya, kutumia vyandarua vyenye dawa za kuua wadudu ziwezazo kuvundishwa na bakteria kumepunguza jumla ya vifo kwa thuluthi moja, na si tu vile vinavyosababishwa na malaria, miongoni mwa watoto walio chini ya umri wa miaka mitano. Mbali na kuokoa uhai, “vyandarua vyaweza kupunguza sana mzigo ulio katika huduma za afya” kwa sababu ni wagonjwa wachache watakaohitaji kutibiwa hospitalini kwa ajili ya malaria.
Hata hivyo, kuna tatizo moja ambalo bado halijasuluhishwa: Ni nani anayegharimia hivyo vyandarua? Watu katika nchi moja ya Afrika walipoambiwa wachangie, walikataa. Na hiyo haishangazi, kwa sababu kwa watu wanaoishi katika nchi zinazotumia kiasi kinachopungua dola tano (za Marekani) kwa kila mtu kwa mwaka kwa ajili ya matibabu, hata chandarua—chenye dawa ya kuua wadudu au kisicho na dawa ya kuua wadudu—ni anasa. Lakini, kwa kuwa njia hiyo ya kuzuia haigharimu sana kama kutibu wagonjwa wa malaria, wataalamu wa UM wasema kwamba “kugawanya na kununua vyandarua vyenye dawa za kuua wadudu kungekuwa njia nzuri sana ya kutumia fedha chache za serikali.” Hakika, kwa serikali, kutoa vyandarua kwaweza kuwa njia ya kuhifadhi fedha. Lakini, kwa mamilioni ya wakazi walio maskini—hiyo yamaanisha kuokoa uhai wao.
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
CDC, Atlanta, Ga.