Ulimwengu Maridadi wa Miamba ya Matumbawe
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA PAPUA NEW GUINEA
MIAMBA ya matumbawe imeenea karibu pwani yote ya Papua New Guinea. Katika siku zilizopita mabaharia waliiona kuwa hatari tu. Lakini wale ambao wamevinjari maji yanayoizunguka, miamba ya matumbawe ni kiingilio cha ulimwengu wa umaridadi, rangi, na utulivu mwingi—nelibini ya chini ya maji!
Kujaribu kupiga picha ulimwengu huu wa chini ya maji ni jambo gumu sana. Kwanza, vitu vilivyo chini ya maji huonekana kana kwamba viko robo tatu ya umbali wake hususa; kwa hiyo ni vigumu kulenga picha. Maji hufyonza, kutapanya, na kupinda nuru. Rangi pia zaweza kutofautiana sana kulingana na halihewa, mahali ambapo jua limefika, kuwapo kwa miani na planktoni, kina cha maji, na aina na rangi ya sakafu ya bahari. Isitoshe, maji, kitu kinachopigwa picha, na mpigaji-picha mwenyewe huwa katika hali ya kusogea daima!
Hata hivyo, wapiga-picha fulani wamekuwa na mafanikio ya kiasi fulani kuhusiana na hilo. Picha unazoona hapa zimepigwa wakati wa kwenda chini ya maji. Acheni tuwajulishe kwa viumbe vinne vyenye kuvutia vilivyopigwa picha chini ya mawimbi.
Picha ya 1 yaonyesha mkazi mwenye kuvutia wa baharini aitwaye kauri simbamarara (Cypraea tigris). Jina hilo si la kawaida kwa sababu kauri yake yenye vigezo vingi ina madoa, wala si milia. Kauri simbamarara hupatikana hapa, kwa kuwa hujilisha matumbawe na sifongo. Wachina wa kale walipendezwa naye sana hivi kwamba walitumia kauri yake kuwa namna ya pesa. Hapa katika Papua New Guinea, kauri bado hutumika kuwa chenji katika masoko ya wenyeji. Ingawa hivyo, kwa sehemu kubwa wakazi wenyeji huzikusanya kwa ajili ya umaridadi tu.
Picha ya 2 ni mnyoo neli mwenye rangi maridadi (Spirobranchus giganteus). Aweza kuishi katika matumbawe yaliyokufa au aweza kuchimba katika matumbawe yanayoishi. Akiwa amepumzika, huonekana kama ua. Lakini awapo na njaa, yeye huyumbisha minyiri yake na kufanyiza “wavu” wa kuzuia vipande vidogo vya chakula vipitavyo haraka. Kwa minyiri yake yenye manyoya-manyoya inayoyumbayumba, huonekana kama safu ya wacheza-dansi wadogo wakipunga mapepeo yao. Kiolezo hiki kilikuwa milimeta kumi kwa upana. Lakini ni lazima mpiga-picha awe mwangalifu asisogee kwa ghafula. Kwa ishara ya kwanza tu ya hatari, haraka sana, viumbe hivi vidogo vyenye kupendeza huingia haraka kwenye makao yao ya matumbawe.
Picha ya 3 ni sifongo. Haifanani sana na ile sifongo ya sanisia ieleayo katika hodhi yako. Sifongo kwa hakika ni mnyama anayeishi, si mmea. Ni mkusanyo wa chembe zenye vinyweleo ambazo hufanya kazi pamoja katika njia ya kipekee sana. Kitabu The Undersea chasema kwamba chembe za sifongo hazitendi kwa ukaribu sana wala hazihusiani. Hivyo, sifongo iliyo hai inaporaruliwa vipande, kila kisehemu hatimaye hufanyiza sifongo mpya. Hata ikiwa chembe mojamoja zatenganishwa, hizo hugaagaa kama amiba hadi zijapo pamoja na kutengeneza sifongo nzima tena.”
Tofauti na mmea, ambao hufanyiza chakula chake wenyewe, sifongo “huwinda” chakula chake. Hiyo huvuta maji yaliyo karibu na kuyachuja ili kupata vitu vinavyotokana na viumbe hai. Kama mnyama mwingine yeyote, hiyo humeng’enya chakula chake na kuondosha uchafu wake. Waweza kupata sifongo zikijishikamanisha kwenye miamba au kwenye makombe katika sakafu ya bahari.
Mwishowe, katika picha ya 4 kuna kivaaute wa hali ya chini. Yeye hukaa mahali pamoja na aweza kwa urahisi kupatikana katika miamba ya matumbawe au akiwa tu kwenye sakafu ya bahari. Wengi hujilisha kwa kuchuja planktoni kutoka katika maji. Kivaaute huitwa moluska wa vali mbili kwa sababu ana makombe mawili, au vali mbili. Hizo zimeshikamana kwa kano na zinafunguliwa na kufungwa na misuli miwili yenye nguvu. Kivaaute ahitajipo kusogea, yeye hujifunua na mguu wake wenye nyama hutokeza kidogo. Lakini adui akikaribia, yeye hurudi katika kombe lake na kujifunika!
Picha hizi zatoa mwono mfupi tu wa mandhari tukufu ziwezazo kuonwa katika bahari zenye matumbawe—mahali pengine tena ambapo hekima ya uumbaji ya Yehova inaonyeshwa.—Waroma 1:20.
[Picha katika ukurasa wa 17]
1. Kauri simbamarara bado hutumika kama pesa
2. “Maua” haya ni minyoo neli hasa
3. Sifongo ni mnyama, si mmea
4. Kivaaute hujilisha planktoni (mdomo umeonyeshwa)