Kuutazama Ulimwengu
Wafa Wakiwa Wangali Wachanga
Kwa kulinganisha na watoto walio katika nchi nyinginezo 25 zilizoendelea kiviwanda, watoto walio Marekani wana uwezekano wa mara 12 zaidi wa kufa kwa risasi, uwezekano wa mara 5 zaidi wa kuuawa, na uwezekano wa mara mbili zaidi wa kujiua, laripoti The Dallas Morning News. “Tulitarajia Marekani iwe na viwango vya juu zaidi, lakini tulishangaa kwa tofauti kubwa sana iliyopo,” asema Etienne Krug, mratibu wa ripoti ya Vitovu vya Kudhibiti Maradhi kule Atlanta, Georgia. Baadhi ya mambo yanayohusika na vifo vyenye jeuri miongoni mwa watoto ni dawa za kulevya, umaskini, familia zilizovunjika, na kukosa fursa za kupata elimu.
Maambukizo Yasababishwayo na Chakula
Ongezeko la matumizi ya “bidhaa zilizotoka tu shambani wakati wote mwakani” pamoja na “soko la ulimwengu ambalo linaweza kusafirisha bidhaa ulimwenguni kote kwa usiku mmoja tu” zinachangia kutokea kwa magonjwa mapya yasababishwayo na chakula nchini Marekani, laripoti JAMA (The Journal of the American Medical Association). Kwa kutegemea uchunguzi uliofanywa zaidi ya miaka kumi iliyopita, wanasayansi wakadiria kwamba vijiumbe vya maradhi yasababishwayo na chakula “huambukiza kati ya watu milioni 6.5 hadi milioni 81 na kusababisha vifo vipatavyo 9000 Marekani kila mwaka.” Wataalamu fulani pia waamini kwamba ongezeko la kula vyakula vinavyokuzwa kwa kutumia mbolea ya wanyama laweza kuchangia tatizo hilo. Kulingana na ripoti ya JAMA, “E coli chaweza kuishi katika samadi ya ng’ombe kwa siku 70 nacho chaweza kuongezeka katika vyakula vinavyokuzwa kwa kutumia samadi, ila tu moto au viongezi kama vile chumvi au vihifadhi vitumiwe kuua vijiumbe hivyo vya maradhi.”
Tumbili “Watakatifu”—Ni Kero
Tumbili waitwao ngedere wameishi Vrindavan, India, kwa muda mrefu sana, asema mtaalamu wa nyani Iqbal Malik. Watu wengi huwaona tumbili hao kuwa watakatifu nao wamekuwa huru kuzurura-zurura katika jiji takatifu la Hindu bila woga wa kukamatwa—yaani, mpaka sasa. Kulingana na gazeti New Scientist, idadi ya ngedere imeongezeka haraka sana katika miaka ya majuzi kwa sababu idadi ya mapilgrimu wanaowalisha imeongezeka pia. Inadhaniwa kwamba kuwalisha tumbili hao huleta ufanisi. Hata hivyo, katika miaka ambayo imepita tumbili hao wamekuwa wakitegemea sana kupewa chakula kwa sababu hakuna mimea. “Wameanza kuiba mifuko na kuingia katika nyumba za watu ili kutafuta chakula.” Wakazi wamekubali kwamba asilimia 60 ya idadi ya hao tumbili ishikwe na kupelekwa maeneo ya mashambani. Asema Malik: “Miungu imekuwa misumbufu.”
Viatu Vyenye Kufinya?
Hata ingawa mifupa ya nyayo zetu huacha kukua tukiwa katika umri wa baadaye wa ubalehe, nyayo zetu hubadilika maishani mwetu mwote. Neil Koven, msimamizi wa Shirika la Tiba ya Nyayo la Kanada, asema: “Tuendeleapo kuongeza umri, nyayo zetu huelekea kuwa bapa kidogo na kusambaa pande zote hivi kwamba nyayo hurefuka na kupanuka. Hiyo ni kwa sababu kano zetu hujiachilia zaidi.” Wataalamu wa viatu wakadiria kwamba kufikia nusu ya watu wazima huvaa viatu visivyowatosha vizuri—tatizo la kawaida zaidi likiwa ni upana ufaao wa viatu—ambavyo husababisha sagamba, sugu, vivimbe, na kasoro za vidole vya miguu. Je, viatu vyako vinakufinya mno? “Kanyaga karatasi kwa nyayo zako tupu kisha uchore nyayo zako kwenye hiyo karatasi. Kisha weka viatu vyako juu ya karatasi na uvichore pia. Kwa kulinganisha michoro hiyo, utaweza kuona ni kiasi gani cha nyayo zako unachofinya ndani ya viatu vyako,” lasema gazeti la habari The Toronto Star. Ili uweze kupata viatu vinavyokutosha kabisa, upimwe nyayo kila wakati unaponunua viatu, na uhakikishe unanunua viatu alasiri au jioni baada ya kutembea-tembea.
Kuwawinda “Maadui Wasiojulikana”
Mnamo 1997, mizio ilianza miezi miwili mapema kuliko kawaida kwa watu wanaoishi Roma, Italia, lasema Corriere della Sera. Hayo mashambulizi ya mapema yanafikiriwa na mtaalamu mmoja wa mizio kuwa yamesababishwa na “ongezeko la jumla la wastani wa hali-joto la sayari, ambalo limepunguza sana kipindi cha kipupwe.” Hilo gazeti lasema kwamba “hali nzuri ya hewa imeleta chavuo zisizojulikana, ambazo wataalamu wa mambo hayo hawajaweza kuzizuia.” Tayari “uwindaji wa kisababishi kisichojulikana” umeanza, lakini kwa wakati huu, “wagonjwa wanaugua mizio, ambayo haijulikani imesababishwa na nini.”
Wachunga-Mikate wa Ushirika Mtakatifu
Kanisa Katoliki la St. Charles lililoko Picayune, Mississippi, limeanza kuweka walinzi wa kuhakikisha kwamba hakuna mtu anayetoka kanisani bila kuumeza mkate mtakatifu wa Komunyo. Hatua hii ilichukuliwa kufuatia visa kadhaa ambavyo watu waliondoka kanisani wakiwa na hiyo mikate, ambayo Wakatoliki huiona kuwa mitakatifu. Kulingana na The Dallas Morning News, kasisi John Noone adai kwamba “waabudu wa Shetani wanataka hiyo mikate” ili “kuitia unajisi.” Kazi ya walinzi wa Komunyo ni kuwatazama wahudhuriaji na kuona ikiwa kweli waliumeza. Wasipoumeza, wahudhuriaji wa kanisa huombwa kwa upole ama waumeze huo Mkate ama waurudishe.
Kumbukumbu la Vidio
Kulingana na taarifa iliyochapishwa katika gazeti Pediatrics, “chunguzi kadhaa za majaribio zaonyesha kwamba vidio za muziki zinaweza kuathiri sana tabia kwa kufisha hisia za watazamaji kwa habari ya ujeuri na kwa kuwafanya matineja waelekee zaidi kukubali ngono ya kabla ya ndoa.” Jambo la kuwahangaisha zaidi wazazi ni maneno ya muziki wenye midundo mizito na rapu ya lugha ya mitaani. “Kwa kikundi kidogo cha matineja, chaguo lao la muziki laweza kuwaathiri sana. Uchunguzi mwingi waonyesha kwamba kupendelea zaidi muziki wa mdundo mzito kwaweza kuwa ishara kubwa ya kujitenga, kutumia vibaya vitu vya kulevya, matatizo ya akili, kuweza kujiua, kuiga mambo ya kingono, au tabia ya kujasiria wakati wa ubalehe.” Hiyo ripoti, ambayo ilikusanywa na madaktari wanane wa kitiba kati ya mwaka wa 1995 na 1996, yasema hivi: “Watazamaji wakisikia wimbo baada ya kuona vidio ya wimbo huo, mara moja wao ‘hukumbuka’ zile picha za vidio.”
Karatasi ya Mavi ya Tembo
Majirani walipomwona Mike Bugara akichemsha mitungi ya mavi ya tembo katika ua wake, kwa kueleweka walikuwa wenye wasiwasi sana. Wengine walidhani kwamba alikuwa akifanya uchawi, lakini, kumbe alikuwa akitengeneza karatasi. Mara ya kwanza Bw. Bugara alitengeneza karatasi kutokana na majani ya mgomba, ya mhindi, na ya mkalitusi. Lakini kupatikana kwingi kwa mavi yenye nyuzinyuzi nyingi ya tembo wa Kenya kulimfanya huyo mpenzi wa uhifadhi afikirie kuyatumia kufanyiza karatasi. Aliamua kwamba hiyo ingekuwa njia nzuri ya “kutahadharisha watu juu ya mafaa ya kuwahifadhi tembo,” laripoti gazeti New Scientist. Sasa karatasi yake ya mavi ya tembo inatumiwa kuwa kadi za mialiko kwa ajili ya sherehe ya miaka 50 tangu Shirika la Wanyama wa Pori la Kenya lianzishwe.
Desturi za Kula
Televisheni ndiyo “hukaziwa fikira katika tabia nyingi za desturi za kisasa,” lasema The New York Times. Mfano mmoja uliotolewa ni zoea la kula unapotazama televisheni—ambayo sasa ni desturi katika nchi nyingi ulimwenguni kote. Mathalani, nchini Mexico, familia nyingi hula chakula cha jioni zinapotazama vipindi ambavyo huendelezwa kila wakati. Uchunguzi wa majuzi nchini Ufaransa ulifunua kwamba “asilimia 62 kati ya milo yote huliwa wakati televisheni imewashwa.” Nchini China, watazamaji hufurahia kutazama matukio ya kipekee ya televisheni wanapokula mbegu zilizochomwa za tikitimaji. Mbegu hizi nyeusi pia zinapendwa na watazamaji wa televisheni nchini Israeli, pamoja na mbegu za alizeti na pistachio. Vyakula vyepesi vya wakati wa kutazama televisheni nchini Filipino hutia ndani miguu ya kuku, masikio ya nguruwe yaliyochomwa, na mshikaki wa matumbo ya kuku. Chakula chepesi kipendwacho ni balut—“vijusi vya bata ambavyo havijaanguliwa na ambavyo huchemshwa na kuliwa kutoka kwenye kaka vikiwa vimenyunyiziwa chumvi ya mawe,” lasema Times.
Uzuiaji wa Kipindupindu Bila Gharama
Wanasayansi waamini kwamba wamepata njia ya kuzuia kipindupindu bila gharama—kuchuja maji ya kunywa kwa sari! Watafiti katika Chuo Kikuu cha Maryland, nchini Marekani, na Kituo cha Kimataifa cha Utafiti wa Maradhi ya Kuhara, kule Dacca, Bangladesh, walipata kwamba bakteria isababishayo kipindupindu hukaa katika tumbo la aina ya kaa, ambao ni krasteshia wafananao na planktoni waishio majini. Kwa kuchuja maji kupitia tabaka nne za sari, zaidi ya asilimia 99 za bakteria za kipindupindu zinaweza kuondolewa. Kisha bakteria zilizo katika hizo sari zinaweza kuondolewa kwa kuanika sari katika jua kwa muda wa saa mbili, au, katika msimu wa mvua, kuifua kwa sabuni isiyo ghali. Gazeti la habari la London The Independent laripoti kwamba majaribio yataanza kufanywa mwaka huu, wakati ambapo watu waishio katika maeneo yaliyoathiriwa watakapofundishwa jinsi ya kufanya mambo haya.
Wamarekani Wapenda Bunduki
“Wamarekani walio watu wazima 4 kati ya 10 huishi katika nyumba zenye bunduki, na kila nyumba hizo zina wastani wa bunduki mbili, kulingana na mahoji ya kitaifa,” laripoti Daily News la New York. “Katika mahoji hayo, asilimia 25 walisema kwamba wana bastola, asilimia 27 walisema wana bunduki ya marisau na asilimia 29 walisema wana bunduki kubwa yenye mifuo.” Nyumba nyingi zina bunduki zaidi ya aina moja.