OSCE—Hilo Ni Nini? Je, Litafaulu?
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Ureno
BAADA ya Vita ya Ulimwengu ya Pili, kulizuka mng’ang’ano wa mamlaka baina ya nchi za kidemokrasi za kibepari za Magharibi na jumuiya ya Sovieti ya nchi za Kikomunisti za Mashariki. Kila jumuiya ilianzisha shirika lake lenyewe la usalama: Shirika la Kujihami la NATO katika Magharibi na Mwafaka wa Warsaw katika Mashariki.
Kufikia 1975 Vita Baridi ilikuwa imepoa kwa kadiri ya Mataifa 35, kutia na Marekani na Urusi, kutia sahihi kile kilichokuja kuitwa Mwafaka wa Helsinki. Basi Mkutano wa Usalama na Ushirikiano wa Ulaya (CSCE) ukafanyizwa. Huo ulikuwa mahali pa mazungumzo na majadiliano kati ya zile jumuiya mbili.
Katika Mkutano wa Budapest mwaka wa 1994, mkutano wa CSCE ulibadili jina lake na kuwa Shirika la Usalama na Ushirikiano la Ulaya (OSCE). Leo, limefanyizwa na Mataifa yanachama 54, kutia ndani Marekani, Kanada, na nchi zote za ule uliokuwa Muungano wa Sovieti.
Lengo Lake
Mradi wa mataifa yanachama ya OSCE ni kuhakikisha usalama wa Ulaya na vilevile kuendeleza kutekelezwa kwa haki za kibinadamu, kupunguza silaha, kupata uhuru wa kidemokrasi na kudhibiti mapambano katika eneo hilo.
Mkutano wa OSCE ulifanywa Lisbon, Ureno Desemba 2-3, 1996. Mara ya kwanza, uangalifu ulikaziwa NATO, kwa kuwa washiriki kadhaa wa NATO, kutia ndani Marekani, wanapendelea kupanuliwa kwa NATO ili litie ndani mataifa mengi zaidi ya Ulaya ya Kati na Mashariki. Lakini badala ya kuunga mkono kupanuliwa kwa NATO ili litie ndani nchi zilizokuwa zamani jumuiya ya Mashariki, Urusi na baadhi ya nchi za zamani zilizoshirikiana nayo za jumuiya ya Mashariki zinataka OSCE liwe mahali pa kujadili masuala yahusuyo usalama wa Ulaya.
Waziri mkuu wa Urusi, Viktor Chernomyrdin, alisema hivi katika mkutano: “Sisi tunapendelea kuimarishwa kwa OSCE, ambapo ni mahali pa pekee katika Ulaya ambapo Mataifa yote yanaweza kushirikiana pamoja. Ndipo mahali bora zaidi pa kimataifa pa kuzungumzia usalama na ulinzi.”
Jua jangavu la alasiri lilionekana kutokeza hali ya kutazamia mazuri kwa ujumla mkutano ulipomalizika, japo maelezo ya vyombo vya habari kuhusu matokeo yake yasiyo dhahiri. Hata OSCE lipate mafanikio gani au liambulie patupu kivipi, wapendao amani kila mahali waweza kuhakikishiwa kwamba amani na usalama za kweli zitapatikana karibuni duniani pote chini ya utawala wa Ufalme wa Mungu.—Zaburi 72:1, 7, 8.
[Picha katika ukurasa wa 31]
Kituo cha Utamaduni cha Belém, Lisbon, Ureno, ambako mkutano ulifanywa