Jihadhari! Walaghai Wamechacha
EBU wazia hii mandhari. Dhoruba imepita. Pepo haribifu zimeacha mapigo yake, na mafuriko yamekoma. Waokokaji ambao wameshtuka watoka kwenye maficho yao, huku kwa umbali kidogo, wahamishwa wenye wasiwasi na hofu warudi kuchunguza matokeo ya dhoruba hiyo. Paa zimeng’olewa kutoka kwenye nyumba; miti imeng’olewa na imelalia nyumba zisizo na paa na ambazo zimenyeshewa sana. Nyaya za umeme zimekatika, zikifanya kusiwezekane kupiga simu za dharura au kupeleka ujumbe. Nyumba fulani, ambazo zamani zilikuwa makao ya familia zenye furaha, zimeharibiwa—zimeharibika kiasi cha kwamba haziwezi kurekebika tena. Kile ambacho pindi moja kilikuwa jumuiya tulivu sasa ni mandhari ya uharibifu na kukata tamaa.
Jumuiya hiyo yaamka—ikiwa imeazimia kujenga upya. Jirani asaidia jirani; wengine hata hawakujuana kwa majina kabla ya wakati huo. Wanaume washirikiana vifaa na ufundi. Wanawake walisha wafanyakazi huku watoto wenye umri mkubwa wakiwalea walio wachanga zaidi. Kutoka nje ya hiyo jumuiya, misafara ya wafanyakazi walio tayari kujitolea kusaidia yaingia—wataalamu wa paa, waondoa-miti, maseremala, wapakaji wa rangi. Lakini, pamoja na hao pia waja walaghai, wakiwa tayari kuwatumia waokokaji kwa kujifaidi.
Malipo makubwa ya kwanza yanadaiwa kabla ya kuanza kazi ya urekebishaji. Wenye nyumba waliokata tumaini watoa pesa zao, ila tu kugundua kwamba wafanyakazi hao wametoroka na pesa zao, wasionekane tena. Watengenezaji wa paa, ambao “huahidi” kwamba kazi zao ni nzuri, hurekebisha nyufa kijuu-juu tu, na hizo huvuja yakinyeshewa mara ya kwanza. Kwa kisingizio cha kukodi mashine kubwa kwa ajili ya kazi ya kesho, waondoa-miti huwafyonza wahasiriwa maelfu ya dola kabla ya kufanya kazi zao. Hawarudi kesho.
Zaidi ya huo uharibifu na upotezo kuna mvunjiko wa moyo wa wenye makao ambao walilipa pesa nyingi kwa makampuni ya bima yaliyofilisika au yaliyo bandia ambayo sasa hukataa kulipia hasara iliyopatwa au ambayo ofisi zake zimekuwa mahame, wenyewe wakiwa tayari wametoroka. Wale waliofanikiwa kupata malipo ya bima kwa hasara walizopata hupata kwamba mara nyingi wanakandarasi wasio wanyoofu na ambao hawastahili hujazia nafasi wakati ambapo wale wachache wanaostahili hawawezi kufanya kazi hizo zote. Tokeo ni kwamba kazi inafanywa kwa njia mbovu, jambo linalotokeza huzuni kubwa kwa wenye nyumba ambao tayari wana matatizo.
Wahasiriwa wa msiba hutumiwa vibaya tena na tena. Kile ambacho huanza kwa jumuiya iliyoharibiwa kabisa kujiunga pamoja kwa ajili ya mema kwa watu wote, hugeuka kuwa ndoto yenye kuvunja moyo kabisa.
Baada ya kimbunga, katika jumuiya moja peremende fulani ilipanda bei sana kufikia dola 4, na chakula cha watoto kiliwagharimu akina mama dola 6 kwa mkebe mmoja. Katika duka moja haikuwezekana kununua betri bila kununua televisheni au redio. Wenye kuuza vifaa vya ujenzi walipata faida kubwa sana kwa kuuza bidhaa kwa bei za juu zaidi. Katika kisa kingine wenye nyumba za kukokotwa ambao nyumba zao zilivurutwa hadi sehemu zilizoinuka wakati wa mafuriko waliongezewa bei kwa asilimia 600. Baada ya tetemeko la dunia, mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 84 ambaye nyumba yake ilikuwa imeharibiwa alipokea simu kutoka kwa mtu aliyejifanya mfanyakazi wa serikali. Mwanamke huyo alidhani kwamba hati ambazo baadaye alitia sahihi zilikuwa maombi ya kutaka msaada wa serikali na chakula. Kumbe, zilikuwa rehani ya dola 18,000 kwa nyumba yake ya kugharimia kile kilichothibitika kuwa kazi ya urekebishaji ya dola 5,000 tu.
Upunjaji wa Uuzaji Kupitia Simu
‘Hongera, Bi. S——! Una bahati leo.’ Hayo huenda yakawa maneno ya utangulizi ya simu hiyo ya ghafula. ‘Wewe ni mshindi wetu mkubwa wa . . .’ Watu wengi wamepokea simu kama hizo zikisema kwamba “tayari wameshinda,” kwamba zawadi zao “zimehakikishwa.” “Zawadi” ya kushinda inaweza kuwa gari jipya, makabati ya kuwekea vifaa vya vitumbuizo, au labda pete ya almasi.
Je, umepata kupokea simu kama hiyo ikitangaza kwamba umepokea zawadi ya bure? Je, ulisisimuka? Je, ulishindwa kuamini? Ikiwa ulijibu simu kama hiyo, je, ulipata zawadi yako? Au ulikuwa mhasiriwa wa upunjaji wa uuzaji kupitia simu? Ikiwa umepatwa na jambo kama hilo, basi si wewe peke yako. Kulingana na gazeti Consumers’ Research, katika Marekani pekee, wauzaji bandia kupitia simu huwapunja watu wapatao kumi kwa kila dakika. Kila mwaka walaghai huwalaghai watu dola bilioni 10 hadi dola bilioni 40, karibu dola 7,500 kwa kila dakika.
“Kila mwaka kotekote Kanada,” likaripoti Reader’s Digest, “zaidi ya watu 150,000 hujibu simu kutoka kwa wauzaji wapunjaji ambao huwaambia kwamba ‘wameshinda’ au ‘wameteuliwa’ kwa ajili ya zawadi kubwa. Na kila mwaka maelfu ya Wakanada hudanganywa na simu hizo, wakitumia wastani wa dola 2,000 kila mmoja ili wapate zawadi zao.” Ofisa mmoja wa Polisi wa Mkoa wa Ontario alitangaza: “Udanganyifu kupitia simu ni mmojawapo wa upunjaji mkubwa zaidi katika historia ya Kanada.” Yeye aongezea: “Twajua kwamba inagharimu Wakanada mamilioni ya dola kwa mwaka.” Tarakimu hizo zawakilisha hasa visa vinavyoripotiwa kwa polisi. Lakini, kwa kuwa imekadiriwa kwamba ni asilimia 10 ya wahasiriwa ndio huripoti upotezo wao, haiwezekani kujua kwa usahihi kadiri kamili ya tatizo.
“Tunawaambia watu wameshinda ili washindwe kufikiri vizuri,” akakiri laghai mmoja stadi. Aliongezea: “Kisha sisi huwasonga watuletee pesa, na tunasisitiza hata wakikataa.” Mara tu mhasiriwa anapokuwa amedanganywa, jina lake linaweza kuuziwa mashirika mengine ya uuzaji wa kupitia simu na kuwekwa katika orodha ya “wapumbavu.” Majina yao yanaweza kuuziwa wengine, ambao nao watawapigia simu kwa kurudia-rudia. “Tunapofanya kazi kutokana na orodha ya wapumbavu,” akasema mmoja aliyekuwa mwendeshaji wa uuzaji wa kupitia simu wa Toronto, “asilimia 75 ya watu hukubali mara ya kwanza. Hilo hurudi chini hadi karibu asilimia 50 kwa mara ya tatu tupitiapo hiyo orodha. Lakini wakiwa wamenaswa, watu fulani huendelea tu; wakifuatia pesa zao.”
Hao waliodanganywa na wauzaji kupitia simu watafikia wapi wakifuatia ndoto yao ya kushinda zawadi kubwa? “Imetulazimu kushirikiana na benki ili kufunga akaunti za wazee-wazee fulani wasinyonywe kabisa,” akasema mpelelezi mmoja wa polisi. Mwanamke mmoja ambaye hivi majuzi alifiwa na mumewe alipatikana kwamba alipeleka malipo 36 kwa wauzaji kupitia simu 16 tofauti-tofauti, zikijumlika kuwa dola 85,000. Naye alikuwa amepokea tu “kiasi kikubwa cha vitu visivyo na thamani.”
Udanganyifu Wenye Kupangwa kwa Uangalifu Dhidi ya Werevu
Hata hivyo, watu wanaoendeleza udanganyifu huo hawabagui. Wahasiriwa wao ni watu wa matabaka yote ya kiuchumi katika jumuiya. Hata wale waonwao eti wataalamu wenye elimu wamedanganywa. Udanganyifu unaotumiwa waweza kuwa wa kichini-chini hivi kwamba hata mnunuzi aliye chonjo zaidi aweza kuhasiriwa. Udanganyifu wa kiasi kikubwa cha fedha ambao huwalenga wanunuzi werevu waweza kutangazwa katika televisheni au katika broshua zenye rangi zinazopelekwa kupitia barua. Zinaweza kutia ndani vitega-uchumi vyenye kuahidi mapato makubwa—vitega-uchumi katika studio za sinema, dhahabu na machimbo ya dhahabu, visima vya mafuta. Orodha hiyo ni kama haina kikomo. Hata hivyo, matokeo ni yaleyale—hasara kabisa.
“Kadiri ya udanganyifu wao hauaminiki kabisa,” akasema mwanamke mmoja mwenye elimu aliyehasiriwa. “Nikiwa mwalimu wa shule, nilifikiri kuwa mimi ni mtu mwenye akili. . . . Ahadi hazikukoma.” Alipoteza dola 20,000 katika udanganyifu uliohusu kampuni fulani ya sinema ambayo haikuwapo.
Upunjaji wa uuzaji kupitia simu ni tatizo la kimataifa. Wapelelezi watabiri kwamba “hiyo itazidi kuwa mbaya zaidi katika mwongo huu.” Lakini, jihadhari! Kuna aina nyinginezo za ulaghai, na wadanganyifu fulani stadi wana lengo fulani walipendalo—wazee-wazee.
[Picha katika ukurasa wa 4]
Jihadhari na walaghai wanaokuja baada ya dhoruba!
[Picha katika ukurasa wa 5]
“Umeshinda zawadi ya bure!”—je, ni kweli?