Kulaghai kwa Jina la Dini
IKIWA unashtuka na kuhuzunishwa na ulaghai ambao umetajwa kufikia hapa, basi si wewe peke yako. Lakini kuna ulaghai ambao ni mbaya hata zaidi—kwa jina la dini. Mmojawapo ulio wa kawaida sana ni itikadi ya kwamba nafsi huendelea kuishi baada ya kifo na kwamba walio hai wanaweza kuwanufaisha wafu. Mamilioni ya watu wenye mioyo myeupe ulimwenguni kote wamefanywa waamini kuwa kwa kulipa pesa nyingi, wao waweza kuwasaidia au kuwatuliza wapendwa wao waliokufa.
Leo, katika nchi fulani, kuna jambo jipya kuhusu udanganyifu huu wa kale. Kwa kielelezo, majuzi nchini Japani, makuhani wa kiume na wa kike wa Dini ya Buddha waliodai kuwa na nguvu za kiroho walikamatwa kwa kushukiwa kuwa waliwalaghai wahudhuriaji mamia ya milioni ya yen. Wale waliokamatwa walikuwa wametangaza utumishi wao wa kuponya na wa kutoa mashauri. Walioitikia matangazo hayo walitia ndani wake wanne wa nyumbani ambao waliambiwa kwamba walikuwa wanasumbuliwa na roho za watoto wao waliokufa. “Kisha wanawake hao waliombwa walipe jumla ya yen milioni 10 [dola 80,000 za Marekani] kwa ajili ya ibada za ukumbusho,” likaripoti Mainichi Daily News. Mwanamke mmoja mwenye umri wa miaka 64 alitoa zaidi ya yen milioni 6.65 (karibu dola 53,000). Mwanamke huyo alikuwa ameenda kwa kuhani huyo kuhusu afya ya mtoto wake. “Yasemekana walimwambia mwanamke huyo kwamba angepatwa na balaa ikiwa hangefanya ibada ya kipekee ya kuzikumbuka nafsi za wazazi wake wa kale na kuziondosha roho,” likasema The Daily Yomiuri.
Ujuzi sahihi juu ya Biblia ungewaokoa watu hawa wasio na habari wasilaghaiwe. Unaonyesha wazi kwamba nafsi inaweza kufa. (Ezekieli 18:4, Zaire Swahili Bible) Wafu “hawajui neno lo lote,” lasema Mhubiri 9:5. Basi wafu hawawezi kuwadhuru wanaoishi. Wala wanaoishi hawawezi kuwanufaisha wafu.
Pande Mbalimbali za Ulaghai wa Kidini
Kwa sababu ya pupa yao wenyewe, wengine hudanganywa na udanganyifu wa kidini. Nchini Australia wenzi fulani wa ndoa wanaodai kuwa na nguvu zinazozidi zile za kibinadamu za kuweza kubariki pesa na kufanya ziongezeke walipewa dola 100,000 na mtu ambaye alitaka pesa zake ziongezeke. Aliambiwa aweke pesa katika sanduku na kuwapa ili “zitakaswe.” Wenzi hao walipeleka sanduku hilo katika chumba kingine ili kuzibariki huku akingoja. Waliporudi, walimrudishia sanduku, wakimwonya kwamba asilifungue kamwe sanduku hilo mpaka mwaka wa 2000. Na kama angelifungua? Aliambiwa kwamba “dawa ingeharibika, naye angekuwa kipofu, nywele zake zingeng’oka, angepatwa na kansa, na kufa kutokana na maradhi ya moyo.” Lakini, baada ya majuma mawili mtu huyo akawa na shaka akalifungua lile sanduku. Lahaula! Lilijaa karatasi zilizokatwa-katwa. Anajilaumu, gazeti lililoripoti tukio hilo likasema, na kwa kushangaza, “ameanza kupata upaa.”
Nchini Italia ulaghai wa kidini umepatwa na mbinu mpya: Makasisi fulani wamelaghaiwa na wadanganyifu stadi wanaojifanya kuwa Wakatoliki wa dhati. Walaghai hao hutumia kwa kujifaidi desturi ya Kikatoliki ya kulipia Misa ya mtu fulani aliyekufa. Wanafanyaje hivyo? Gazeti la Katoliki Famiglia Cristiana laeleza kwamba wadanganyifu hao hujitoa kulipia mapema Misa 12 za wafu wakitumia hundi bandia ambayo ina kiasi kikubwa sana cha pesa kuliko zile zinazotakikana. Wao humdanganya kasisi mwenye kudanganyika kwa urahisi awarudishie chenji kwa pesa taslimu. Hao walaghai wapokea pesa taslimu, na kasisi apokea cheki isiyokubalika!
Nchini Marekani, wazee-wazee mara nyingi husongwa pande zote na madhehebu za kidini ambazo zinatafuta watu wapya wa kujaza masanduku yao kwa upaji. “Katika taifa lote, madhehebu zinatii kanuni kubwa ya kuwa na uhakika: Fuata pesa,” likaandika gazeti Modern Maturity. “Wao nao huahidi kila kitu tokea afya nzuri hadi mabadiliko ya kisiasa hadi ufalme wa mbinguni.” Mtu mmoja ambaye huwatibu watu ambao awali walikuwa washiriki wa madhehebu alinukuliwa akisema: “Wazee-wazee ndio riziki ya madhehebu.”
Mapato ya kifedha yanaweza kuwa makubwa sana. “Najua visa kadhaa ambamo watu wamekuwa fukara sana,” akasema wakili mmoja wa New York ambaye amepata kushughulikia kesi nyingi za madhehebu. “Kuna kesi nyingi za watu ambao waliombwa upaji wa mamia ya maelfu ya dola hadi wale ambao hawakuwa na lolote ila hundi zao za Malipo ya Uzeeni ya kutoa.” Aliongezea: “Ni vibaya sana—kwa watu hao mmoja-mmoja na kwa familia zao.”
Basi jihadhari! Walaghai wamechacha. Udanganyifu wa kurekebishiwa nyumba, upunjaji wa uuzaji kupitia simu, na ulaghai wa kidini ni vielelezo vichache tu vya jinsi wanavyotenda. Haiwezekani kutaja kihususa mbinu zao zote, kwa kuwa sikuzote wao bado hugundua ulaghai mpya. Lakini yale ambayo yametajwa hapa ndani bila shaka yatakutahadharisha uwe mwangalifu, na labda hiyo ndiyo kinga yako bora zaidi. (Ona sanduku kwenye ukurasa wa 8, “Jinsi ya Kuepuka Kulaghaiwa.”) Onyo la mithali moja ya kale ya Biblia lafaa sana: “Mjinga huamini kila neno; bali mwenye busara huangalia sana aendavyo.”—Mithali 14:15.
[Picha katika ukurasa wa 10]
Mamilioni ya watu huamini kwamba kwa kulipa pesa wao waweza kuwasaidia au kuwatuliza wapendwa wao waliokufa