Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/22 kur. 6-8
  • Wanalenga Wazee-Wazee

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Wanalenga Wazee-Wazee
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kutana na Walaghai wa Japani
  • Kuwalaghai Wazee-Wazee Nchini Italia
  • Kulaghai kwa Jina la Dini
    Amkeni!—1997
  • Jihadhari! Walaghai Wamechacha
    Amkeni!—1997
  • Jinsi ya Kujilinda Dhidi ya Ulaghai
    Amkeni!—2004
  • Familia ya Kikristo Huwasaidia Wazee-Wazee
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/22 kur. 6-8

Wanalenga Wazee-Wazee

USIDANGANYIKE. Wadanganyifu stadi wamejitayarisha vizuri. Wao wanafahamu mambo ambayo yanawafanya wazee-wazee hasa kuwa rahisi zaidi kulaghaiwa. Kwa kielelezo, nchini Marekani watu wenye umri wa zaidi ya miaka 65 ni asilimia 12 tu ya jumla ya wakazi wote. Lakini, wao wana jumla ya mapato yazidiyo dola bilioni 800, ambayo ni karibu asilimia 70 ya jumla ya mapato ya familia za Marekani. Haishangazi kwamba wazee-wazee kama hao ni asilimia 30 kati ya wahasiriwa wote wa upunjaji.

Ni nini huwafanya wazee-wazee wawe rahisi kupunjwa? “Wao wana mwelekeo wa kiasili wa kuitibari na huenda wasijue njia za kisasa za vitega-uchumi,” laeleza gazeti Consumers’ Research. Ofisa mmoja wa polisi alilalamika kwamba upunjaji wa uuzaji kupitia simu “hulenga hasa watu walio wapweke na walio rahisi kudanganywa—wazee-wazee—ambao ndio wengi kati ya wahasiriwa wao. Hawa ni watu ambao walikua katika enzi ambayo salamu ya mkono ilitosha kuhakikisha kwamba mkataba umefanywa.” Mwakilishi wa Shirika la Marekani la Watu Waliostaafu alinukuliwa akisema: “Mara nyingi husemwa kwamba pupa huingiza mtu katika matatizo. Kwa watu wazee-wazee, si pupa. Wao wana hofu ya kuishiwa pesa kabla ya wao kufa. Hawataki kuwa mzigo wenye kulemea kwa watoto wao. Kisha wanaogopa kuripoti [huo upunjaji] kwa sababu wanaogopa watoto wao watawafikiria kuwa hawawezi kujitunza.”

Si kwamba wahasiriwa wazee-wazee wa upunjaji hudanganywa au kuongozwa vibaya sikuzote. Nyakati nyingine wao ni wapweke, labda wakihitaji “kununua” urafiki. Katika jumuiya moja wajane fulani wapweke walidanganywa wakalipa dola 20,000 kwanza kwa ajili ya “masomo ya kufaa sana ya kucheza dansi,” akaandika ripota mmoja wa gazeti la habari. “Wengine walikuwa wadhaifu mno wasiweze kutembea. Hawakuwa wajinga, walikuwa wamekata tu tamaa.” Klabu moja ya kucheza dansi inawapa wanachama wapya mahali pa kuwa na marafiki zao wapya, ambao mara nyingi ni marika yao. Ni vigumu kwao kumkinza mfanya-biashara mwenye kurairai, mwenye maneno matamu na aliye mchangamfu, ambaye pia aweza kuwa mfunzi wao wa kucheza dansi.

Kutana na Walaghai wa Japani

Walaghai fulani hutumia wazee-wazee walio wapweke katika njia nyinginezo. Nchini Japani wadanganyifu stadi wamejifanya kuwa watu wenye kujali, wakitumia wakati mwingi kupiga-gumzo na wahasiriwa wao walio wazee-wazee, na kuwasikiliza. Hatua kwa hatua wao huzidisha ziara zao, na baada ya kujua kwamba mhasiriwa huyo anawatumaini kabisa, wao huwatokezea mauzo ya upunjaji. Kielelezo halisi cha upunjaji huo wenye hila kilikuwa udanganyifu wa dhahabu ambamo watu wapatao 30,000, kutia ndani na wengi wanaopokea malipo ya uzeeni, waliripotiwa kuwa walilaghaiwa yen bilioni 200 (dola bilioni 1.5). “Hakuna Uwezekano wa Kuondoa Hasara ya Wahasiriwa,” gazeti la Japani la Asahi Evening News likaripoti katika kichwa-kikuu.

Gazeti Asahi Shimbun la Tokyo liliripoti hivi katika kisa hicho: Mfanya-biashara mwanamke mwenye umri wa makamo alimzuru mtu mmoja aliye mzee-mzee, akisema: “Mbali na kazi yangu, ninakuhangaikia, Bw. K., kwa kuwa unaishi peke yako.” Huyo mwanamke alisikiliza hadithi zake nyingi, naye alidanganywa na haiba ya huyo mwanamke. Alipokuwa akiondoka, mwanamke huyo aliomba arudi siku ifuatayo. “Bila shaka,” akajibiwa.

Ziara za kawaida zikafuata; wakawa wanakula chakula cha jioni pamoja, naye hata akawa anamletea Bw. K. chakula. “Nitakutunza mpaka ufe,” akaahidi. Ndipo mambo ya biashara yakaanza: “Nitasimamia mali yako kwa ajili yako. Kampuni ninayofanyia kazi hivi majuzi ilipata njia nzuri sana ya kutumia mali.” Mpango huo ulihitaji mzee aweke nyumba yake na mali yake rehani, kisha anunue kinoo cha dhahabu na akiweke akiba katika kampuni ya huyo mwanamke. Mtego ukawa umetegwa. Bw. K. akawa mhasiriwa mwingine katika orodha ndefu za wenye kulaghaiwa. Mara tu shughuli hizo zilipomalizwa, mwanamke huyo hakurudi.

“Nilipokuwa mwanajeshi,” akasema Bw. K., “kifo kilinikodolea macho sana. Lakini ni vigumu hata zaidi kustahimili kulaghaiwa mali yangu na mtu ambaye anatumia udhaifu wa sisi wazee-wazee ambao tunaishi peke yetu bila ya watu wa ukoo wa kuwategemea. Yaonekana ulimwengu umefikia enzi ambayo watu wanataka pesa, hata kwa njia zenye upunjaji.”

Kuwalaghai Wazee-Wazee Nchini Italia

Kitabu L’Italia che truffa (Italia Inayolaghai) kiliripoti juu ya mpango uliopangwa kwa uangalifu sana na walaghai nchini Italia wa kuwanyonya wazee-wazee akiba zao zote zenye thamani. Mwaka wa 1993 serikali iliyoongozwa na aliyekuwa gavana wa Benki ya Italia ilifanyizwa. Bila shaka sahihi zake zilitokea katika pesa za noti (bila shaka zikiwa zingali halali) ambazo zilikuwa zimetolewa wakati alipokuwa gavana. Baada ya kujitokeza kwenye milango ya wazee-wazee, walaghai kadhaa, ambao walijitambulisha kuwa maofisa wa Benki ya Italia na ambao walibeba vitambulisho bandia ili kuthibitisha hivyo, wakaambia kila mhasiriwa wao: “Unajua kwamba gavana wa Benki ya Italia amekuwa rais wa Baraza la Mawaziri; basi, sahihi yake inayoonekana katika pesa za noti haitumiki tena. Tuna daraka la kukusanya noti zote za zamani kutoka katika familia mbalimbali na kuzibadilisha kwa noti mpya zilizotiwa sahihi na mwandamani wake . . . Chukua hii risiti. Enda kwenye benki yako ukiwa nayo kesho kutwa, nawe utapokea kiasi cha pesa kinachotoshana na pesa ambazo umetupa sasa.” Kwa njia hii, walaghai hao walikusanya lire milioni 15 (karibu dola 9,000) kwa siku moja!

Walaghai fulani nchini Italia huwasiliana na watu wasiotahadhari, kutia ndani wazee-wazee, barabarani. Wao huwaomba watu wasio na habari kushiriki katika uchunguzi fulani na kuwapa makaratasi ya kutia sahihi, akisema kwamba sahihi zao ni kuthibitisha tu kwamba walishiriki katika uchunguzi huu. Kwa hakika wao wanatia sahihi mkataba ambao unawalazimu kufanya kitu au kununua kitu fulani.

Kisha, wakati fulani baadaye, mhasiriwa hupokea kifurushi chenye bidhaa fulani, labda kikiwa na onyo la wazi kwamba akikataa bidhaa hizo, ataadhibiwa kwa njia fulani. Wengine, hasa watu walio wazee-wazee, huogopa, wakiona kwamba ni afadhali walipe pesa kidogo na kubaki na bidhaa hizo zisizo na thamani kuliko kupelekwa mahakamani.

Ulaghai umeenea kadiri gani nchini Italia? Kulingana na L’Italia che truffa, idadi ya ulaghai ambayo inaripotiwa inafikia karibu 500,000 kwa mwaka. Karibu mara tatu za ulaghai haziripotiwi. Mwandishi mmoja wa habari za televisheni alisema: “Jumla ni karibu mitego milioni mbili ya aina mbalimbali kila mwaka, au kitu kama elfu tano hadi sita kwa siku.”

Kwa kusikitisha hali hiyo inaendelea. Hakuna rika fulani (au kabila, au jamii, au taifa kwa habari hiyo) ambayo haiachwi na walaghai wanaowalaghai watu pesa zao—na mara nyingi akiba zao zote za maisha. Jihadhari! Unaweza kulaghaiwa.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]

Jinsi ya Kuepuka Kulaghaiwa

SI MASHIRIKA yote ya kufanya biashara kwa njia ya simu hayafuati haki. Kwa kielelezo, nchini Marekani kulikuwa na makampuni 140,000 yaliyofanya biashara kwa njia ya simu katika mwaka wa 1994, kulingana na Shirika la Marekani la Wastaafu (AARP). Inakadiriwa kwamba asilimia 10, au 14,000 yalikuwa yenye upunjaji. Basi, inalazimu kuwa macho wakati unapopata toleo lionekanalo kuwa zuri mno. Hapa pana madokezo ya kukusaidia kuepuka kulaghaiwa kwa njia ya simu.

◆ Mtu akikupigia simu akisema umeshinda zawadi ya bure, labda jambo bora zaidi uwezalo kufanya ni kukata hiyo simu.

◆ Muuzaji wa kupitia simu akisisitiza kwamba ni lazima ununue leo au sivyo utachelewa mno, mara nyingi hiyo ni ishara ya kwamba huo ni ulaghai.

◆ Linda nambari ya kadi yako ya mkopo. Usiitoe kwa watu usiowajua watafutao fedha.

◆ Usinunue kitu chochote kupitia simu ila tu kama ni wewe mwenyewe umepiga simu na unashughulika na kampuni ya kuagiza bidhaa ambayo imejulikana.

Wenye nyumba wanahitaji kuwa waangalifu juu ya udanganyifu wa kurekebisha nyumba. Hapa pana tahadhari chache, kama ambavyo zimetajwa na Masuala ya Wanunuzi ya AARP:

◆ Usimwajiri mtu usiyemjua mpaka uwe umeangalia kwa ukamili watu wanaompendekeza; uwe umeuliza majina na nambari za simu za wateja wengine ambao amewahudumia.

◆ Usitie sahihi kitu chochote bila kukiangalia kwa usahihi, na uwe na hakika kwamba unaelewa na unakubaliana na matakwa katika mkataba wowote au mapatano yoyote.

◆ Usimtegemee mtu mwingine akufafanulie mapatano ila tu kama ni mtu unayemjua na kumwitibari. Jisomee mwenyewe matakwa.

◆ Usilipie marekebisho kabla ya kazi kufanywa. Uwe na hakika kwamba umeridhika na kazi kabla ya kutoa malipo ya mwisho.

Uwe chonjo. Tumia akili ya kawaida. Usisite kukataa ikiwa hutaki kununua hicho kitu. Na kumbuka: Ikiwa toleo hilo laonekana kuwa zuri mno, labda ni ulaghai.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Wadanganyifu stadi waweza kujifanya kuwa wenye kujali, ili kuwalaghai wazee-wazee

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki