Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • w94 2/15 kur. 3-4
  • Vidhehebu—Hivyo Ni Nini?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Vidhehebu—Hivyo Ni Nini?
  • Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Kidhehebu Ni Nini?
  • Je, Mashahidi wa Yehova Ni Dhehebu?
    Maswali Yanayoulizwa Mara Nyingi Kuhusu Mashahidi wa Yehova
  • Je! Mashahidi wa Yehova Ni Kidhehebu?
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Siri—Katika Jina la Bwana
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1997
  • Ubikira—Kwa Nini?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
w94 2/15 kur. 3-4

Vidhehebu—Hivyo Ni Nini?

FEBRUARI 28, 1993—polisi zaidi ya mia moja wa vikosi kadhaa vya kutekeleza sheria walishambulia majengo yenye wanaume, wanawake na watoto wengi. Kusudi lilikuwa kutafuta silaha haramu na kukamata mtu fulani aliyeshukiwa kuwa mhalifu. Hata hivyo, polisi hao walikumbwa kwa ghafula na mfululizo wa risasi kutoka katika majengo hayo. Wao pia wakaanza kupiga risasi.

Pigano hilo lilisababisha vifo vya watu kumi na kuwajeruhi watu kadhaa. Katika siku 50 zilizofuata, mamia ya polisi wa serikali walizingira majengo hayo wakiwa na bunduki za kutosha kuweza kupigana vita ndogo. Mgogoro huo uliisha katika kabiliano lililosababisha vifo vya watu 86, kutia na angalau watoto 17.

Lakini adui alikuwa nani? Genge la walanguzi wa dawa za kulevya? Kikundi cha wapiganaji wa kuvizia? La. Kama vile huenda ukajua, “adui” alikuwa kikundi cha wajitoaji wa kidini, washiriki wa kidhehebu. Msiba wao ulifanya jumuiya ndogo kwenye nyanda za Teksasi ya kati, U.S.A., ikaziwe fikira na mataifa yote. Vyombo vya habari vilijaza redio na magazeti kwa ripoti, machanganuzi, na maelezo mengi mno juu ya hatari za vidhehebu vyenye ushupavu.

Umma ulikumbushwa juu ya matukio ya nyakati zilizopita ambamo washiriki wa kidhehebu fulani waliongozwa kwenye kifo na viongozi wao: mauaji ya kimakusudi ya Manson ya 1969 katika Kalifornia; kule kujiua kwa kikundi cha washiriki wa kidhehebu mwaka wa 1978 katika Jonestown, Guyana; ule mkataba wa uuaji wa kimakusudi na wa kujiua wa 1987 uliofanyizwa na kiongozi wa kidhehebu fulani Park Soon-ja wa Korea, uliosababisha vifo vya washiriki 32. Ni jambo la maana kwamba walio wengi wa watu hao walidai kuwa Wakristo na walidai kuwa na imani katika Biblia.

Kwa kueleweka, wengi wanaostahi Biblia kuwa Neno la Mungu wanachukizwa na jinsi vidhehebu hivyo vimetumia vibaya Maandiko kwa ukaidi. Likiwa tokeo, kwa muda wa miaka ambayo imepita mamia ya mashirika yameanzishwa kwa kusudi la kuchunguza mwenendo wa vidhehebu na kufunua mazoea yavyo ya hatari. Wastadi juu ya mwenendo wa vidhehebu hutabiri kwamba kuja kwa mileani mpya katika miaka michache huenda kukachochea kuongezeka kwa vidhehebu. Gazeti moja la habari lilionyesha kwamba kulingana na vikundi vipingavyo vidhehebu, kuna maelfu ya vidhehebu “huko nje vilivyo tayari kutwaa kwa nguvu mwili wako, kudhibiti akili yako, kufisidi nafsi yako. . . . Ni vichache vilivyo na silaha lakini vingi vinaonwa kuwa hatari. Vitakudanganya na kupokonya mali zako, vitapanga ndoa yako na kufanya maziko yako.”

Kidhehebu Ni Nini?

Neno “kidhehebu” hutumiwa bila usahihi na wengi ambao huenda wasitambue maana yalo kikamili. Ili kuzuia mvurugo, wanatheolojia fulani huepuka kihalisi kutumia neno hilo.

The World Book Encyclopedia yaeleza kwamba “zamani, neno kidhehebu lilirejezea namna yoyote ya ibada au desturi ya kisherehe.” Kwa kiwango hicho, matengenezo yote ya kidini yangeweza kuitwa vidhehebu. Hata hivyo, katika matumizi ya kawaida leo, neno “kidhehebu” lina maana tofauti. Ensaiklopedia iyo hiyo yaonyesha kwamba “tangu miaka ya katikati ya 1900, kutangazwa sana kwa vidhehebu kumegeuza maana ya neno hilo. Leo, neno hilo hutumiwa kuhusiana na vikundi vinavyofuata kiongozi aliye hai aendelezaye mafundisho na mazoea mapya na yasiyo ya kawaida.”

Likikubaliana na matumizi ya kawaida ya neno hilo, gazeti Newsweek laeleza kwamba “kwa kawaida [vidhehebu] ni vikundi vidogo vyenye maoni ya kupita kiasi ambavyo washiriki wavyo hupata umoja na kusudi lao kutoka kwa mtu mmoja, mwenye uwezo mwingi wa kuvutia watu.” Vivyo hivyo, gazeti Asiaweek laonyesha kwamba “neno [kidhehebu] lenyewe si dhahiri, lakini kwa kawaida humaanisha imani mpya ya kidini iliyotegemea kiongozi mwenye uwezo mwingi wa kuwavutia watu, ambaye mara nyingi hujitangaza kuwa ufananisho wa Mungu.”

Usemi uliotumiwa katika azimio moja la pamoja la Baraza la 100 la Jimbo la Maryland, U.S.A., waonyesha pia maana yenye dharau ya neno kidhehebu. Azimio hilo lasema kwamba “kidhehebu ni kikundi au harakati inayoonyesha ujitoaji wa kupita kiasi kwa mtu au wazo fulani na kutumia ufundi usio wa kiadili wa kuvuta kwa hila na kudhibiti ili kuendeleza miradi ya viongozi wacho.”

Kwa wazi, vidhehebu vinaeleweka kwa kawaida kuwa vikundi vya kidini vyenye maoni na mazoea tofauti sana yanayopingana na mwenendo wa kijamii unaokubaliwa kuwa wa kawaida leo. Kwa kawaida hivyo hufanya utendaji wavyo wa kidini kisiri. Vingi kati ya vikundi hivyo vya kidhehebu hujitenga kihalisi katika jumuiya ndogo-ndogo. Ujitoaji wavyo kwa kiongozi wa kibinadamu wa kujitangaza unaelekea kuwa bila masharti na usiotia ndani mwingine. Mara nyingi viongozi hao hujivunia kuwa wamechaguliwa kimungu au hata kuwa wenye asili ya kimungu wenyewe.

Pindi nyingine, mashirika yapingayo vidhehebu na vyombo vya habari vimewarejezea Mashahidi wa Yehova kuwa kidhehebu. Makala kadhaa za karibuni za magazeti ya habari zawatia Mashahidi pamoja na vikundi vinavyojulikana kwa ajili ya mazoea yao yenye kutilika shaka. Lakini je, ingekuwa sahihi kurejezea Mashahidi wa Yehova kuwa kikundi kidogo cha kidini chenye maoni ya kupita kiasi? Mara nyingi washiriki wa kidhehebu hujitenga na marafiki, familia, na hata jamii kwa ujumla. Je! ndivyo ilivyo na Mashahidi wa Yehova? Je! Mashahidi wanatumia ufundi na udanganyifu usio wa kiadili ili kupata washiriki?

Viongozi wa kidhehebu wanajulikana kutumia njia za kuvuta kwa hila ili kudhibiti akili za wafuasi wao. Je! kuna ithibati yoyote kwamba Mashahidi wa Yehova hufanya hivyo? Je! ibada yao hufanywa kisiri? Je! wao wanafuata na kumpa kiongozi wa kibinadamu heshima ya kiibada? Kwa wazi, je, Mashahidi wa Yehova ni kidhehebu?

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 3]

Jerry Hoefer/Fort Worth Star Telegram/Sipa Press

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki