Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 9/22 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Magari Yaendeshwayo kwa Umeme na Hali ya Mazingira
  • Tahadhari: Mbega Wanavuka
  • Onyo: Simu Zaweza Kuwa Hatari
  • Hila ya Tumbaku
  • Kichaa cha Mileani
  • Matetemeko ya Dunia Hayatabiriki
  • Mimea Yala Vilipukaji
  • Uchezaji wa Dansi Ulio Hatari
  • Aksidenti za Magari Je, U Salama?
    Amkeni!—2002
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
  • Ghadhabu za Barabarani—Waweza Kukabilianaje?
    Amkeni!—1997
  • Uchovu—Mtego Usiotambuliwa na Madereva wa Lori
    Amkeni!—1997
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 9/22 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Magari Yaendeshwayo kwa Umeme na Hali ya Mazingira

Kampuni ya Magari ya Ujerumani ilifanya uchunguzi ili kugundua ikiwa magari yatumiayo umeme ni bora kuliko magari yatumiayo injini za mafuta kwa utunzaji wa mazingira. Kulingana na gazeti la habari Süddeutsche Zeitung, uchunguzi huo ulihusisha madereva 100 ambao walisafiri kilometa milioni 1.3 kati ya 1992 na 1996. Magari yatumiayo umeme yalionekana kuwa na faida kadhaa, ingawa yana mwendo mfupi kabla hayajaongezewa nguvu: Hayo yalienda kwa ukimya, bila kutoa moshi yanapotumiwa. Hata hivyo, faida zote hizi zinazidiwa na tatizo moja kubwa. Kuchaji upya betri hutumia nishati nyingi za msingi kuliko magari yatumiayo mafuta—kutoka mara 1.5 hadi mara 4, ikitegemea matumizi—na nishati hiyo inapaswa kutengenezwa mahali fulani. Ikitegemea jinsi ambavyo nishati hiyo hutengenezwa, inawezekana kwamba “madhara kwa mazingira kutokana na magari yatumiayo umeme ni makubwa zaidi ya magari yatumiayo mafuta,” lilitaja gazeti hilo.

Tahadhari: Mbega Wanavuka

Msitu wa Diani, ulio karibu na pwani ya kusini mwa Kenya, ni moja kati ya sehemu chache katika Afrika Mashariki ambapo mbega bado wanaishi. Tatizo linalowakabili wanyama hao ni jinsi ya kuvuka kwa usalama barabara iliyo kando ya ufuo wenye shughuli nyingi. Kulingana na kadirio fulani, angalau mbega 12 huuawa na magari kila mwezi katika barabara hiyo, laripoti Swara, gazeti la Shirika la Wanyama wa Pori la Afrika Mashariki. Kikundi cha watu wenye hangaiko waishio katika ujirani wa pwani ya Diani kilichukua hatua kupunguza vifo hivyo. Zaidi ya kuwahimiza madereva wawe waangalifu zaidi, hivi karibuni walitengeneza daraja la kamba lililo juu sana ya barabara. Wakitiwa moyo kuona mbega hao wakitumia daraja hilo, wakazi hao wanafanya mipango ya kutengeneza madaraja zaidi.

Onyo: Simu Zaweza Kuwa Hatari

Simu zaweza kuwa hatari ikitumiwa wakati wa kuendesha gari. Uchunguzi uliochapishwa katika New England Journal of Medicine wadokeza kwamba madereva watumiao simu zilizo katika gari wana mwelekeo wa mara nne zaidi wa kuhusika katika aksidenti kuliko madereva ambao wanakazia fikira tu katika uendeshaji. Hii yaweza kufanya hatari ya kuendesha gari ukitumia simu kuwe sawa na kuendesha gari ukiwa na kiasi cha alkoholi cha asilimia 0.1 katika damu. Na madereva ambao hawakuhitaji kushika simu mikononi mwao walikabili hatari hiyo hiyo kama madereva walioshika simu mikononi. Watafiti wa uchunguzi huo walitaja kwamba simu zenyewe hazisababishi aksidenti bali zinahusika tu nazo, kama vile ubishi utokeapo na mtu kukengeushwa fikira. Licha ya hayo, asilimia 39 ya madereva waliohusika katika aksidenti, baadaye waliweza kutumia simu zilizo katika magari yao kuomba msaada. Inapendekezwa kwamba wale wenye simu zilizo katika magari waepuke simu zote zizizo za lazima waendeshapo na wafanye mazungumzo yao kuwa mafupi. Baadhi ya nchi, kama vile Brazili, Israeli, na Uswisi, tayari zina sheria ambazo zinazuia madereva kutumia simu za mkononi.

Hila ya Tumbaku

“Je, washangaa kwa nini kampuni za tumbaku hazijatumia uvutano wao wa kisiasa kufanya Bunge la Marekani kupunguza au kuondoa vibandiko vya onyo vinavyotakiwa katika matangazo na pakiti zote za sigareti [katika Marekani]?” liliuliza The Christian Century. “Jibu ni rahisi: onyo hilo la hatari ya kuvuta sigareti hulinda kampuni za tumbaku kutokana na hatua za kisheria. Ukianza kuvuta sigareti ukiwa na umri wa miaka 12 na yakutokezea kifo kutokana na kansa ya mapafu ukiwa na umri wa miaka 45, na unaamua kushtaki kampuni hiyo ya sigareti kwa kukufanya uwe mraibu, watengenezaji wana jibu rahisi: ‘Tulikuonya kwamba uvutaji wa sigareti una hatari za kiafya.’” Moja kati ya mbinu ya karibuni zaidi ya kutia moyo uvutaji wa sigareti ni kwa kuonyesha wachezaji wa sinema na warembo wa kuonyesha mitindo wakivuta sigareti ili kuidhinisha sigareti. Hata hivyo, biri huchafua zaidi ya sigareti na kuleta hatari kubwa zaidi ya kiafya. “Uvutaji wa biri haumsaidii mwanamke isipokuwa kumwongezea hatari ya magonjwa yatishayo uhai, na kumnyang’anya nguvu na uwezo ambao anauhitaji sana katika maisha,” asema Dakt. Neil Schachter, wa New York City’s Mount Sinai Medical Center.

Kichaa cha Mileani

“Karne ya 20, ambayo ilianza na Vita ya Ulimwengu ya 1 na kukua hadi Enzi ya Atomu, yaonekana ikiisha ikiwa Enzi ya Vitumbuizo,” lasema gazeti la Newsweek. “Hoteli tufeni pote tayari zimejaa” kwa ajili ya sherehe za Mkesha wa Mwaka Mpya wa 1999. Lakini ubishi umekuwa ukiendelea juu ya mahali ambapo hasa mileani itaanza. “Tatizo lilianza katika taifa la Kiribati,” laeleza U.S.News & World Report. “Mstari wa kimataifa wa tarehe ulitumiwa kukata katikati ya kikundi cha visiwa hivyo: Ilipokuwa Jumapili katika mashariki mwa Kiribati, ilikuwa Jumatatu katika magharibi mwa Kiribati.” Taifa hili lilimaliza tatizo hilo kwa kuamua kwamba kuanzia Januari 1, 1995, na kuendelea, mstari wa tarehe ungepita kando ya kisiwa cha Caroline, kilichopo mashariki zaidi. Hii ingemaanisha kwamba Kiribati ingekuwa bara la kwanza kuona mwanzo wa mwaka mpya. Lakini, mataifa mengine, kama vile, Tonga na New Zealand, yalitaka heshima za “kwanza.” Kulingana na Royal Greenwich Observatory, umuhimu wa suala hilo ni muhimu sana. “Kwa vile jua huangaza katika Ncha ya Kusini kuanzia ikwinoksi ya Septemba hadi ikwinoksi ya Machi, hivyo basi, mileani yaanza kwanza katika kizio cha chini cha Dunia,” yasema ripoti hiyo. Hata hivyo, yaongeza Observatory, hiyo haitakuwa hadi baada ya Januari 1, 2001—si mwaka 2000.

Matetemeko ya Dunia Hayatabiriki

Hivi karibuni, kikundi cha wataalamu wa tetemeko la dunia walikutana huko London ili kujadili utabiri wa kisayansi wa matetemeko ya dunia. Uchanganuzi wao ulikuwa nini? “Kwa zaidi ya miaka 100 wanasayansi wengi wa jeolojia ya Dunia wamekuwa wakifikiri kwamba [matetemeko makubwa ya dunia] bila shaka lazima yatangulizwe na viishara vyenye kuonekana na kutambulika ambavyo vingeweza kutumiwa kuwa msingi wa kutoa maonyo,” aandika Dakt. Robert Geller, wa Chuo Kikuu cha Tokyo, katika kichapo Eos. Badala yake, mabadiliko makubwa ya kufikiri yanahitajiwa kwani “yaonekana inaelekea kwamba kutokea kwa tetemeko la dunia hakuwezi kutabiriwa.” Ingawa utabiri sahihi kabisa pengine usiwezekane, wanasayansi waweza kukadiria uwezekano na ukubwa wa tetemeko la dunia kwa maeneo yenye rekodi za matetemeko mengi ya dunia. Kwa mfano, ramani mpya iliyotolewa na U.S. Geological Survey yaonyesha maeneo ambayo mtikisiko mkubwa waweza kutokea katika bara lote la Marekani kwa kipindi cha miaka 50 ijayo. Kwa kutegemea habari hizo, mashirika ya serikali yalidokeza kwamba zaidi ya asilimia 70 ya idadi ya watu wa California wanaishi katika maeneo yawezayo kuwa katika hatari.

Mimea Yala Vilipukaji

Mimea ya kiazi-sukari na aina fulani ya magugu yapatikanayo katika vidimbwi yana uwezo wa kutoa vilipukaji kutoka katika ardhi na maji katika maeneo ya zamani ya kuwekea silaha na kuvivunja-vunja kwa usalama, laripoti gazeti la New Scientist. Wanasayansi katika Chuo Kikuu cha Rice, katika Houston, Texas, waliilisha mmea periwinkle na parrot feather, ambao ni aina ya kawaida ya magugu ya vidimbwi sumu ya TNT (trinitrotoluene). Katika muda wa juma moja hakukuonekana sehemu yoyote ya vilipukaji katika tishu zake, na kuchoma mimea hiyo hakukutokeza mlipuko wowote. Wakati huohuo, watafiti katika Chuo Kikuu cha Maryland waligundua kwamba chembe za mimea ya kawaida ya kiazi-sukari na vitolewaji vyake vyaweza kufyonza na kuvunja-vunja aina ya sumu iitwayo nitroglycerin. Makundi yote mawili ya wanasayansi yalihasi mimea kwanza ili kuhakikisha kwamba havipati msaada kutoka kwa vijiumbe. “Kwa wakati huu, kwa kawaida ni hatari sana na gharama mno kurudisha katika hali nzuri maeneo yaliyo na silaha za vita ili kujenga juu yake, lakini hilo laweza kubadilika ikiwa mimea iwezayo kupandwa kwa urahisi ingeweza kutumiwa kuvuta vilipukaji kutoka katika ardhi na majini na kuzivunja-vunja kwa usalama,” ilisema makala hiyo. Kuna uhitaji wa haraka kwa sababu “zoea la sasa la kutupa takataka zenye sumu katika bahari linaondolewa.”

Uchezaji wa Dansi Ulio Hatari

Uchezaji wa dansi fulani katika ukumbi wa kuchezea dansi umegeuka kutoka kwa ustadi wenye madaha hadi “mchezo wenye mashindano makali sana ambamo pesa nyingi sana zapatikana,” laripoti gazeti The Times la London. Migongano wakiwa katika miendo ya kasi sana na teke za juu ambazo huwajeruhi kiaksidenti washindanaji wengine wa kucheza dansi zinakuwa hatari katika ukumbi wa kuchezea dansi. Kwa ubaya zaidi, uchezaji fulani wa dansi ulio hatari unafanywa kimakusudi kwa “nia mbaya sana,” kulingana na Harry Smith-Hampshire, mwamuzi mashuhuri wa uchezaji wa dansi. Washindanaji wa kucheza dansi wanaingiza “tabia zinazopatikana katika stediamu za mpira na jukwaa la ndondi,” kulingana na The Times. Kukiwa na matazamio ya kutambuliwa kwa uchezaji wa dansi katika ukumbi kuwa mchezo wa Olimpiki, makocha stadi na waamuzi wameweka “kanuni ya tabia” iliyo rasmi ili kuudhibiti mchezo huo.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki