Sababu Inayofanya Watoto Wawe Wapiganaji Bora
JE, ULIUA?“La.”
ULIKUWA NA BUNDUKI?“Ndiyo.”
ULILENGA BUNDUKI?“Ndiyo.”
ULIFYATUA RISASI?“Ndiyo.”
NI NINI KILICHOTOKEA?“Walianguka tu.”—World Press Review, Januari 1996.
MAZUNGUMZO hayo yenye kushtusha sana kati ya mfanyakazi mmoja wa kijamii na mtoto mmoja aliye askari-jeshi katika Afrika yafunua mvurugo ulio katika akili ya mtoto anayejaribu kujipatanisha na maisha ya kawaida.
Katika miaka ya majuzi, katika nchi 25, watoto walio chini ya umri wa miaka 16 wamejiunga katika mapigano. Katika mwaka wa 1988 pekee, watoto wapatao 200,000 walikuwa wakishiriki vitani. Kwa sababu wametumiwa vibaya na watu wazima, watoto walio wapiganaji pia ni wahasiriwa.
Ubora Wao Wakiwa Askari-Jeshi
Katika wakati uliopita, majeshi yalipopigana kwa mikuki na mapanga, mtoto hangeweza kuokoka kupigana na mtu mzima mwenye silaha kama hiyo. Lakini hii ni enzi ya silaha nyepesi. Leo, mtoto aliye na bunduki—aina ya AK-47 iliyotengenezwa Sovieti au aina ya M16 iliyotengenezwa Marekani—atoshana na mtu mzima.
Silaha hizi ni nyepesi na pia rahisi kutumia na kudumisha. Bunduki ya AK-47 inaweza kufunguliwa vipande-vipande na kuunganishwa tena na mtoto mwenye umri wa miaka kumi. Bunduki hizi pia zimejaa tele. Bunduki zipatazo milioni 55 za AK-47 tayari zimeuzwa. Katika nchi moja ya Afrika, hizo huuzwa kwa dola 6 tu (za Marekani). Bunduki za M16 pia hupatikana kwa wingi na kwa bei rahisi.
Mbali na kuweza kubeba bunduki, watoto huthaminiwa sana wakiwa askari-jeshi kwa sababu nyinginezo. Wao hawadai kulipwa mishahara, na ni nadra sana watoroke. Isitoshe, watoto wana tamaa sana ya kuwapendeza wakubwa wao. Hisia yao ya lililo sawa na lisilo sawa hufunikwa na tamaa ya kutaka kukubaliwa na kikundi chochote kile cha kupigania uhuru au jeshi la kuvizia ambalo limekuwa kama “familia” yao.
Wengi wao pia huelekea kuwa wasiohofu. Mfafanuzi mmoja wa kijeshi alieleza hivi katika Afrika Magharibi: “Kwa kuwa [watoto] hawaonekani kuelewa kifo kama ilivyo [na] askari-jeshi walio watu wazima, hawaelekei sana kusalimu amri katika hali ambazo hakuna tumaini.” Mvulana mmoja wa Liberia aliyebandikwa jina Kapteni Muuaji alijigamba hivi: “Watu wazima walipoogopa na kutoroka, sisi watoto tulibaki na kuendelea na vita.”
Kwa kushangaza, ingawa wavulana huwa askari-jeshi wazuri, mara nyingi ni wao huonwa kuwa wenye kuweza kutolewa mhanga. Katika vita fulani katika Mashariki ya Kati, vikosi vya askari-jeshi walio watoto viliamriwa kuongoza njia katika sehemu zilizotegwa mabomu ya chini ya ardhi.
Kusajiliwa na Kufundishwa
Watoto wengine hujiunga na majeshi au vikundi vya waasi kwa sababu wanatafuta msisimuko. Pia, kunapotokea hatari na familia imevurugika, kikosi cha kijeshi huwatolea usalama na kuwa kama familia ya badala. Lasema Shirika la Hazina ya Watoto la Umoja wa Mataifa: “Watoto ambao wamelelewa wakiwa wamezingirwa na ujeuri huona ujeuri kuwa njia ya daima ya maisha. Wakiwa wapweke, mayatima, waoga, wenye kuchoshwa na kufadhaishwa, mara nyingi hatimaye wao wataamua kupigana.”
Watoto wengine hujiunga na majeshi kwa sababu huenda ikawa hakuna chaguo jingine bora. Nyakati nyingine, kama kuna uhaba wa chakula na kuna hatari, kujiunga na jeshi huenda kukaonekana kuwa njia ya pekee ya kuweza kuishi.
Nyakati nyingine huenda watoto wakajiona kuwa wapiganiaji haki ya kijamii, itikadi za kidini, au wa kutetea tamaduni zao. Kwa mfano, nchini Peru, watoto ambao wamelazimishwa kujiunga na vikundi vya wapiganaji wa kuvizia hupitia vipindi virefu vya kufundishwa kisiasa. Hata hivyo, mara nyingi hilo halihitajiki. Brian Milne, mwanthropolojia wa kijamii ambaye aliwachunguza watoto walio askari-jeshi katika Asia ya Kusini-Mashariki alisema hivi: “Watoto hawafuati mafundisho au mawazo fulani. Wao hushawishwa tu na upande mmoja au mwingine na kuanza kutumiwa.”
Lakini watoto wengine hulazimishwa kujiunga na vita. Katika vita fulani vya Afrika, vikundi hushambulia vijiji ili kuteka watoto, ambao nao hulazimishwa kushuhudia au kushiriki katika kutesa na kuua familia zao wenyewe. Nyakati nyingine wao hulazimishwa kuwapiga risasi wazazi wao wenyewe au kuwakata koo. Baada ya kutishwa mno, wavulana hao huwatisha wengine. Vijana hao waliotendwa kikatili mara nyingi hutenda matendo ya ukatili mno ambayo hata askari-jeshi walio watu wazima hawawezi kuyatenda.
Kuyarudia Maisha ya Kawaida
Si rahisi kwa watoto kama hao kubadilika na kuishi maisha yasiyo na jeuri. Mkurugenzi mmoja wa kituo cha watoto katika nchi moja ya Afrika Magharibi alisema hivi: “Watoto ambao tumewashughulikia wote wamefadhaika kwa kadiri mbalimbali. Wao wamebaka, wameua na kutesa watu. Wengi wao walipewa alkoholi au dawa za kulevya, hasa bangi, lakini nyakati nyingine heroini. . . . Unaweza kuwazia athari mbaya sana ambayo vitu hivyo hutokeza katika akili za watoto, wengine wao wakiwa wachanga mno wa miaka minane au tisa hivi.”
Hali ni hiyohiyo katika nchi jirani ya Liberia, ambako makumi ya maelfu ya watoto wametumia utoto wao wakiwaogofya wakazi wa mashambani. Si rahisi kwa matineja walio meja na majenerali kuacha vyeo vyao na uwezo wanaopata kutokana na bunduki za AK-47. Mkazi mmoja wa Somalia alisema: “Ukiwa na bunduki, una uhai. Bila bunduki, huna uhai.”
Mara nyingi, wapiganaji walio watoto hawawezi kurudi nyumbani kwa sababu ya kulipiziwa kisasi au kukataliwa na familia zao. Mshauri mmoja wa watoto katika Liberia alisema: “Mama zao husema, ‘Mbaki naye. Hatumtaki nyang’au huyu nyumbani kwetu.’”
Ingawa watoto wengine wamejirekebisha na kuishi maisha yenye amani, kufanya hivyo kwahitaji upendo, tegemezo, na uelewevu mwingi sana wa wale walio karibu nao. Si rahisi kwa ama watoto ama familia zao. Mfanyakazi mmoja wa kijamii nchini Msumbiji alieleza: “Linganisha maisha ya kuweza kuchukua chochote utakacho na ya kuamuru wengine na maisha yako urudipo kijijini. Hasa kama una umri wa miaka 17 na huwezi kusoma na huna stadi zozote zile. Unatumbukia maisha ya kuchosha. Ni vigumu sana kuyarudia maisha ya kuamuriwa na kuanza kusoma tena.”
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 5]
Anwar mwenye umri wa miaka 13 aishi Afghanistan. Akiwa amepigana vita sita, aliua kwa mara ya kwanza katika vita ya saba. Aliwapiga risasi askari-jeshi wawili kwa ukaribu kisha akadunga miili yao kwa matako ya bunduki kuhakikisha kwamba wamekufa. Alipoulizwa alihisije kuhusu kisa hicho, Anwar alionekana kushangazwa na swali hilo. “Nilifurahi kwa sababu niliwaua,” akasema.
Katika vita iyo hiyo, askari-jeshi wenzake Anwar waliwateka askari-jeshi wanne wa maadui. Hawa walioshikwa walifungwa, wakafungwa macho na kupigwa risasi. Anwar alihisije juu ya hilo? Huyo mpiganaji mchanga alionyesha tu mshangao na kujibu polepole na kimakusudi, kana kwamba anamjibu punguani. “Nilifurahi.”
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Mfungwa aliye karibu kuachiliwa huru katika Afrika Magharibi alikuwa amewekwa pingu, lakini kamanda wa jeshi aliupoteza ufunguo. Kamanda alisuluhisha tatizo hilo kwa kumwamrisha mvulana aliye askari kuikata mikono ya huyo mfungwa. “Katika ndoto zangu mimi bado husikia mayowe ya mwanamume huyo,” asema mvulana huyo. “Kila wakati ninapomfikiria, naghairi.”