Kuutazama Ulimwengu
Hakuna Dawa “Chemchemi ya Ujana”
Kulingana na daktari wa magonjwa ya wazee Andréa Prates, kutumia dawa mpya ili kuhifadhi ujana, kama vile homoni za aina fulani, huenda “kukatokeza aina fulani ya manufaa lakini pia kwaweza kuharibu sana afya yako.” Katika pigano dhidi ya kuzeeka, “mitindo mipya ya tabia ni yenye matokeo mazuri zaidi ya dawa mpya,” ashauri Dakt. Prates. Tabia nzuri ambazo zaweza kuongeza muda wa kuishi, lasema gazeti la Brazili Superinteressante, zatia ndani kupata usingizi wa kutosha, kudumisha mwelekeo wa utulivu, kujinyoosha na kufanya mazoezi ya kiasi, kutumia akili sana na kuepuka vyakula vyenye mafuta. Pia ni muhimu kula vitamini na madini, ambayo hupatikana katika matunda na mboga za majani. Kuzeeka huhusisha chembe zote katika mwili na kitu kimoja hakiwezi kuleta manufaa mara moja kwa viungo tofauti-tofauti vya mwili.
Ufanyizaji wa Mamalia wa Kwanza Aliyekomaa
Watafiti katika Scotland waliushangaza ulimwengu mwishoni mwa Februari uliopita kwa kutangaza kwamba walikuwa wamefanyiza mwana-kondoo kutokana na DNA ya kondoo aliyekomaa. Ingawa ufanyizaji wa chembe za kiinitete ulikuwa umefanywa kwa miaka kadhaa, hadi sasa ufanyizaji wa jeni pacha ya mamalia aliyekomaa ulifikiriwa na wanasayansi wengi kuwa hauwezekani. Watafiti hao walisema kwamba, kinadharia, mbinu hiyo ingeweza kutumika kwa binadamu—kwamba DNA ya chembe iliyotolewa kwa mtu mzima ingeweza kufanyizwa itokeze pacha ya huyo anayefanana na yeye kabisa, ingawa mchanga zaidi. Lakini, kulingana na International Herald Tribune, Ian Wilmut, mwanasayansi aliyeongoza mradi huo, afikiri kwamba wazo hilo halikubaliki kimaadili. Shirika la Afya Ulimwenguni lakubaliana naye likipinga ufanyizaji wa binadamu kuwa ‘aina ya majaribio yenye kuvuka mpaka,’ laripoti The Journal of the American Medical Association.
Jihadhari na Mkazo Mwingi!
“Mamilioni ya Wabrazili wanapigana kwa ukawaida na mkazo,” laripoti gazeti Veja. Wengi wao huenda waamini kwamba kufanya kazi kwa bidii kwa vipindi virefu ni kipimo cha ubora wao kikazi, lakini mwelekeo huu waweza kuwa hatari kwa afya. “Mfanyakazi hufanya vema anapokuwa chini ya mkazo wa kadiri, lakini afikia utendaji wa juu kabisa wakati, bila kujua, tayari amesha pita kikomo,” aeleza Dakt. Marilda Lipp wa Pontifical Catholic University. “Chini ya mkazo mkubwa, mwanadamu hufanya maajabu kwa muda mfupi. Kisha, yeye huisha tu ghafula.” Wale ambao huona ugumu wa kuwapa wengine madaraka hupatwa na mkazo mkubwa, yasema ripoti hiyo. Mkazo mkubwa huwakumba wale ambao kulingana na maneno ya Dakt. Lipp, “wana ugumu katika kueleza hisia zao, ambao huelekea kufoka katika nyakati za mkazo na kisha kufanya jitihada kuwa wapole na waungwana.”
Vifaranga vya Kuku vya Kielektroni
Vifaranga vya kuku vya kielektroni vimekuwa mtindo katika Japani, liliripoti gazeti la Asahi Evening News mwanzoni mwa mwaka huu. Kichezeo chenye umbo la yai kina kiwambo ambacho huonyesha kifaranga katika hatua tofauti za ukuzi. Bonyeza swichi, na baada ya dakika tano kifaranga cha kuku kitatokea kutoka katika gamba lake katika kiwambo. Kisha “kifaranga” hicho hutoa sauti ili mwenyewe “akilishe” na kukitunza kwa mahitaji yake mengine kwa kubonyeza swichi nyinginezo. Kinaweza kutoa sauti wakati wowote, hata usiku. Kushindwa kukihudumia kwaweza kuongoza katika “kifo” cha mapema cha kifaranga hicho. Kwa vyovyote, baada ya juma moja hivi, kifaranga hicho hufa. Kisha kichezeo hicho chaweza kutengenezwa upya ili kwamba kifaranga kingine, kikiwa na utu tofauti, “kizaliwe.” Baadhi ya watu wameripotiwa kuwa karibu sana na vifaranga vyao vya kielektroni kama ambavyo wangekuwa na mtoto wao. Daktari mmoja hata alisema hivi kuhusu kifaranga chake: “Kilipokufa nilihuzunika zaidi kuliko wakati mmoja kati ya wagonjwa ninaowatibu alipokufa.”
Kutumia Watoto Vibaya
“Karibu watoto milioni mbili duniani pote wanaaminiwa kuwa wahasiriwa wa biashara ya ngono,” lasema ENI Bulletin. Kutenda vibaya watoto kulikopangwa kitengenezo namna hiyo ambako tayari kumeenea katika sehemu fulani za Asia, sasa kunaongezeka katika nchi za Amerika. Rodrigo Quintana, mtaalamu katika Inter-American Institute of the Child, alisema kwamba mwongo uliopita umepata tatizo hili likiongezeka haraka katika Amerika ya Latini. Takwimu zilizotajwa na Quintana zaonyesha kwamba makumi ya maelfu ya watoto wadogo katika nchi zote za Amerika ya Latini sasa wanaajiriwa kuwa malaya.
Kipande cha Kipinga-Mata Chagunduliwa
Hivi karibuni wanaastrofizikia waligundua kile kionekanacho kuwa kipande cha kipinga-mata chenye urefu wa miaka-nuru-3,500 kitokacho katika kiini cha galaksi yetu, Njia ya Kimaziwa, laripoti gazeti The New York Times. Kipinga-mata hutia ndani visehemu vya atomi ambavyo vinafanana kabisa na mata ya kawaida isipokuwa kwamba vina chaji ya umeme iliyo kinyume. Mgusano pamoja na mata ya kawaida hutokeza uangamizo wa vitu vyote viwili na kutolewa kwa miale ya gama yenye nguvu ikiwa na nishati maalumu. Wanasayansi walitambua kipande hicho kuwa kipinga-mata kwa kurekebisha setilaiti ya Compton Gamma Ray Observatory kwa usawa huo. Kuhusu athari ya kipande hicho, “wanaastrofizikia walisema hakitishi Dunia, [kilitisha] galaksi.”
Kifukuza-Tembo
“Katika Asia, tembo huharibu mazao yenye thamani ya maelfu ya dola kila mwaka,” asema mwanazuolojia Loki Osborn wa Chuo Kikuu cha Cambridge. Kama ilivyoripotiwa katika gazeti New Scientist, tembo katika Afrika wanazidi kuvutiwa na mazao ya shambani. Kidesturi, wakulima wamejitahidi kuwafukuza wanyama hao kwa kupiga ngoma au kutupa mawe. Tembo wengi wanaovamia wameuawa kwa kupigwa risasi, asema Osborn, “lakini hatua hizo hazipunguzi uharibifu wa mazao.” Osborn na mvumbuzi fulani waamini kwamba wamegundua zana iliyo bora: kopo moja la rasharasha lenye kilogramu moja ya pilipili na mafuta ambalo laweza kurushwa karibu na eneo alipo tembo kwa kutumia kirusha-vitu chenye kutumia msongo wa hewa. Aeleza kwamba pua ndefu ya tembo ni moja kati ya vitu viliyo nyetivu zaidi katika dola ya wanyama. Wakati wa majaribio katika Zimbabwe, “kwanza tembo wangesimama tuli, kisha wangepiga chafya kabla ya kuondoka mbio.” Ripoti yasema kwamba pilipili hiyo haileti madhara ya kudumu.
Uvutaji wa Moshi Wafisha
“Zaidi ya vifo 50,000 kwa mwaka kutokana na maradhi ya moyo na ateri husababishwa na uvutaji wa moshi,” ule moshi kutokana na matumizi ya tumbaku ya watu wengine, yasema ripoti katika gazeti la Marekani Good Housekeeping. Kwa kuongezea, wasiovuta sigareti ambao kwa kawaida hutumia wakati fulani katika mazingira yenye moshi wa sigareti wamo katika hatari kubwa ya kupata maradhi ya mchochota wa mirija ya mapafu na nimonia na wamo katika hatari kubwa zaidi kupatwa na kansa za aina mbalimbali. Harufu isiyopendeza inayobaki katika chumba kwa siku kadhaa baada ya mtu fulani kuvuta sigareti haifikiriwi kuwa ni yenye hatari. Lakini, “vyumba vyenye kujaa moshi wa sigareti vyaweza kuwa na uchafuzi wa hewa kwa mara sita zaidi ya uchafuzi wa hewa wa barabara kuu zenye shughuli nyingi,” ilisema makala hiyo. Pia ilisema kwamba “moja katika kila vifo vinane visababishwavyo na uvutaji wa sigareti ni matokeo ya uvutaji wa moshi.”
Je, Ni Mmea wa Wakati Ujao?
Mianzi ilikuwa mingi sana karibu na ikweta kabla wakoloni hawajaikata ili kutayarisha mashamba, lasema The UNESCO Courier. Katika Afrika pekee, kuna aina 1,500 za mianzi. Mmea huu una matumizi mengi tofauti-tofauti. Ukiwa na uwezo mkubwa wa kustahimili kuliko feleji, mwanzi ni kifaa bora cha ujenzi. Majengo fulani ya orofa tatu katika Kolombia yana umri wa zaidi ya miaka mia moja na bado yanatumika. Mwanzi pia ni wenye mafaa ukiwa bomba, kwa fueli, na kwa matumizi mengineyo mengi. Matawi mororo ya mwanzi hata hutumiwa katika upishi wa Kichina na Kijapani. Mafaa ya mwanzi huenda yalipuuzwa katika nyakati zilizopita. Lakini sifa zake zenye mafaa sana na kukua kwake kwa haraka—hukomaa kwa miaka mitano tu—zimevuta baadhi ya watu kuiona katika njia mpya, kuwa “mmea wa wakati ujao uwezao kufanywa upya.”
Mende Wahusishwa na Ugonjwa wa Pumu kwa Watoto
Uchunguzi wa miaka mitano kwa ajili ya Taasisi za Kitaifa za Afya za Marekani unalaumu mende kwa kuongeza visa vya ugonjwa wa pumu miongoni mwa watoto waishio ndani ya mji, laripoti gazeti la New York Daily News. Kati ya watoto 1,528 wenye ugonjwa wa pumu ambao walichunguzwa katika miji saba, asilimia 37 walikuwa na mizio mikali kutokana na mende. Wale waliokuwa na huo mzio na kuwekewa mende wengi katika vyumba vyao vya kulala walielekea mara tatu zaidi kuhitaji kulazwa hospitalini kuliko watoto wengine wenye ugonjwa wa pumu. Dakt. David Rosenstreich, kiongozi wa uchunguzi huo, alitia moyo kupambana na mende kwa kutumia mitego ya mende, dawa za kuua wadudu, asidi boriki, na usafishaji kabisa. Alisema kuvuta vumbi nyumba nzima kwa kutumia mashine husaidia kumaliza mavi ya mende yaliyo katika vumbi. “Wapaswa kuondoa vyakula na maji ambayo huwavutia mende,” aongeza Dakt. Rosenstreich, “hasa mivujo ya maji au ya vioevu. Ni lazima mende wanywe ili waishi.”