Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Ustahimilivu Nina umri wa miaka 22, na nataka kuwashukuru kwa sababu ya mfululizo “Ustahimilivu—Je, Ulimwengu Umepita Kiasi?” (Januari 22, 1997) Vijana Wakristo walazimika kukabili matatizo mengi. Makala hizi zilinitia moyo kutovuka mipaka na kuimarisha azimio langu la kumtumikia Yehova japo mikazo ya ulimwengu huu.
M. B., Italia
Kunguru Nilipenda sana makala yenye kufundisha “Kunguru—Ni Nini Kinachomfanya Awe Tofauti?” (Januari 8, 1997) Nina umri wa miaka 18 na hivi karibuni nilipata kazi ya muda nikiwa mwanaviumbe katika kituo cha viumbe cha kwetu. Miongoni mwa wanyama tuwatunzao ni kunguru wazuri wawili. Nimewagundua kuwa sawa kabisa kama mlivyoeleza katika makala yenu—wenye akili sana. Ninapanga kushiriki makala hii pamoja na wafanyakazi wenzangu.
J. C., Marekani
Habari mlizoandaa zilikuwa za kweli na za kufurahisha sana. Ukweli kwamba ndege wa familia ya kunguru ni wezi sana unajulikana sana hapa katika eneo la chuo kikuu ambacho ninasomea katika Ghana. Inajulikana hapa kwamba kunguru huiba kila kitu kuanzia samaki hadi sabuni. Hata imeripotiwa kwamba kunguru wamefungua baadhi ya sufuria za wanafunzi na kula vyakula vyao!
F. A. A., Ghana
Jikoni Kwavutia Asanteni kwa makala “Jikoni Kwaweza Kuvutia.” (Januari 8, 1997) Mimi vilevile nimefaidika na maongezi yafanywayo jikoni. Wakati wa kumenya vitunguu na viazi, mama yangu alikuwa akinifundisha kumpenda Yehova na alikuwa akinitia moyo kumtumikia kwa ukamili. Maongezi haya ya jikoni yalithibitika kuwa yenye manufaa sana hasa katika ule wakati mgumu ambao baba yangu alitupinga kidini. Sasa mama yangu na mimi tuna furaha ya kumwona baba yangu akiwa mtumishi wa Yehova. Pia nimejifunza jinsi ya kupika vyakula mbalimbali vitamu!
A. M. M., Italia
Nafanya kazi nikiwa mpishi wa nyumbani kwa mwajiri ambaye ni mtumbuizaji. Kwa sababu hiyo nimekuwa na fursa nyingi kushiriki chakula cha kiroho na wageni—kutia ndani baadhi ya watumbuizaji maarufu—ninapofanya kazi jikoni. Huweka baadhi ya fasihi za Biblia katika mtoto wa meza huko jikoni. Wakati fulani niliingia katika mazungumzo ya Biblia na mgeni fulani. Baadaye alirudi tena jikoni kwa ajili ya mazungumzo zaidi ya Biblia. Nilipokuwa mwenye shughuli ya kukaanga kuku, alisoma kwa sauti nakala ya kitabu changu Ufunuo—Upeo Wao Mtukufu U Karibu! Ndiyo, mlisema kweli. Jikoni kwaweza kufurahisha!
A. R., Marekani
Kuungama Dhambi Natumikia nikiwa mzee wa kutaniko, na nataka kueleza uthamini wangu kwa ajili ya makala “Vijana Huuliza . . . Je, Niungame Dhambi Yangu?” (Januari 22, 1997) Makala hiyo iliwatia moyo vijana kadhaa kuungama dhambi zao nzito walizofanya wakati fulani uliopita. Ilikuwa ni furaha kuona kwamba baada ya kupokea msaada, vijana hawa waliimarisha uhusiano wao na Yehova. Wameazimia kujitunza wakiwa safi.
O. B., Italia
Makala hiyo ilinisaidia kutambua kwamba kuficha siri kwaweza kudhuru sana. Kuungama kwaweza kuleta aibu na fedheha, lakini uungamapo dhambi zako kwa Yehova na kwa wazazi wako, wapata uhusiano ulio imara, na wa karibu nao.
B. K., Guyana
Makala hiyo ilikuja wakati barabara nilipoihitaji. Ilinisaidia kuona kwamba ilinipasa kuwaambia wazazi wangu na wazee wa kutaniko kile nilichokuwa nimefanya. Nilihisi kana kwamba makala hiyo iliandikwa kwa ajili yangu. Hatimaye nilipowaambia kuhusu tatizo langu, nilihisi vizuri zaidi!
A. A., Marekani