Jikoni Kwaweza Kuvutia
“ONDOKA jikoni!” Watoto wengi wenye njaa wamepata hilo onyo la upole walipokuwa wakijaribu kuonja chakula cha jioni kabla ya hicho kupelekwa mezani. Hata hivyo, badala ya kuwafukuza, wazazi wana sababu nzuri ya kuwaalika watoto jikoni. Kwa nini? Kwa sababu jikoni ni darasa lenye kuvutia.
Jikoni ni mahali ambapo watoto wanaweza kukuza ubunifu na stadi za kutatua matatizo, mahali ambapo wanaweza kujifunza kutumikia wengine na kufanya kazi wakiwa sehemu ya kikundi, mahali ambapo mazungumzo yenye maana ambayo hugusa moyo yaweza kujitokeza yenyewe, mahali ambapo maadili yaweza kukazwa kwa njia isiyo ya moja kwa moja. Kwa kweli, wakati wa kupika jikoni, kuna mambo mengi yenye thamani yawezayo kufunzwa na kutumiwa wakati wa kutayarisha mlo utakaofuata.
Kwa nini utumie jikoni kuwa mahali pa kuzoeza watoto katika muhula huu wa tekinolojia na habari? Jibu ni wakati. Wazazi wengi hutambua kwamba hakuna kibadala cha kutumia wakati pamoja na watoto wao—wakati mwingi vya kutosha!a Tatizo ni kuupata. Wataalamu fulani huhimiza wazazi wafikirie kazi ya kawaida wanayoifanya nyumbani kuwa fursa ya kufanya mambo pamoja na watoto wao na kuwaelimisha. Hilo lapatana na amri ambayo Mungu aliwapa wazazi katika taifa la kale la Israeli: “Maneno haya ninayokuamuru leo, yatakuwa katika moyo wako; nawe uwafundishe watoto wako kwa bidii, na kuyanena uketipo katika nyumba yako, na utembeapo njiani, na ulalapo, na uondokapo.”—Kumbukumbu la Torati 6:6, 7.
Kwa sababu sisi kwa kawaida hutumia wakati jikoni hata iweje, basi yaonekana pangekuwa mahali dhahiri pa kushiriki katika utendaji unaoshirikiwa na familia. Na tofauti na ziara za kipekee za kwenda nje, ambazo mara nyingi huhitaji kungoja hadi tuwapo na wakati, nishati, au fedha ili kuzipangia, hamu za kula haziwezi kuahirishwa. Kando na hilo, jikoni pana uvutio wa kiasili kwa watoto. Kwa vyovyote, ni mahali gani pengine wafunzwapo kutumia visu kwa uangalifu na kushughulika na vyombo vinginevyo? Watoto wanaofurahia huenda hata wakaharibu mambo pindi kwa pindi! Ingawa hivyo, ni masomo gani yaandaliwayo jikoni?
Kujifunza Katika “Darasa” la Jikoni
Louise Smith—ajulikanaye kwa wanafunzi wake wenye umri wa miaka minne kuwa Bibi-Mkate-Tangawizi—alitoa maoni haya yategemeayo uzoefu wake wa miaka 17 katika kufundisha watoto wachanga kupika: “Chakula ni kifaa kikuu cha kufundishia kwa sababu ndicho jambo ambalo watoto wote hufahamu. Hisi zao za kunusa, kuonja, na kugusa zina umakini sana wanapokuwa na umri mchanga hivi kwamba wanaweza kuhusika kikamili. Na kupitia kupika chakula waweza kufundisha sayansi ya sauti, hisabati, na stadi za kutatua matatizo.” Kumwaga, kutwanga, kuambua, kuchunga, kukoroga, na kuviringa kwaweza kuwasaidia watoto kusitawisha wepesi wa kawaida wa kiakili na upatanifu wa jicho na mkono. Kudondoa (kutenganisha zabibu na kokwa) na kufuatanisha (kuweka vikombe vya kupimia kimoja ndani ya kingine kulingana na ukubwa kwa utaratibu) hufundisha dhana ambazo zaweza kutumika zikiwa msingi wa kujifunza hisabati. Kufuata maagizo ya njia ya kupika ni zoezi katika utumizi wa namba, vipimo, kupima wakati, mantiki, na lugha. Na mtu hawezi kujasiria kuingia katika ulimwengu tata wa jikoni uliojaa hatari bila kujifunza juu ya usalama, kuchukua daraka, kujipanga kibinafsi, na kufanya kazi ya kikundi.
Jambo la maana pia ni thamani ya kujifunza kupika. Ni jambo la kawaida kwa watoto ambao huanza kwa kusaidia jikoni kuweza kutayarisha milo yote kufikia wakati wanapokuwa katika miaka yao ya utineja. Ni mzazi yupi mwenye shughuli nyingi ambaye hatafurahia hilo pindi kwa pindi? Isitoshe, kupika husaidia vijana kusitawisha uhakika na kujitegemea—sifa ambazo zaweza kuwanufaisha wanapochukua madaraka ya watu wazima baadaye, iwe watafunga ndoa au watabaki waseja.—Linganisha 1 Timotheo 6:6.
Lee, ambaye alibaki mseja hadi alipofika miaka yake ya mapema ya 30 akumbuka: “Mama yangu alianza kunizoeza kawaida za msingi za jikoni nilipokuwa na umri wa miaka sita hivi. Mwanzoni, nilipendezwa tu na kutengeneza biskuti, keki, na vitamu vinginevyo. Lakini kufikia wakati nilipokuwa na umri wa miaka tisa, niliweza kupanga na kutayarisha mlo wote wa familia yetu, na nilifanya hivyo kwa ukawaida. Baadaye, nikiwa mtu mzima aliye mseja, nilipata kwamba kujua kushughulikia kazi kadhaa za nyumbani, kutia ndani kupika, kulifanya maisha yawe rahisi. Na naweza kusema kwa hakika kwamba hilo limechangia kufanya niwe na ndoa yenye mafanikio.”
Kupika Hufurahisha!
Mzazi aweza kupataje wakati wa kuzoeza watoto jikoni? Mama mmoja adokeza kuratibu wakati ambapo kuna vikengeusha-fikiria vichache iwezekanavyo. Ikiwa una watoto kadhaa, huenda mwanzoni ukataka kufanya kazi na mtoto mmoja kwa wakati wanapokuwa wakijifunza mambo ya jikoni. Ili kufanya hivi, chagua wakati ambapo wale watoto wengine wanapumzika kitandani mchana au wako shuleni. Panga utumie wakati mwingi zaidi ya ule ambao ungetumia ukiwa peke yako. Kisha uwe tayari kufurahia jikoni!
Kwa kipindi chako cha kwanza, waweza kumruhusu mtoto wako achague kitu ambacho yeye hufurahia kula. Tafuta njia rahisi ya kupika ambayo huleta matokeo haraka. Hakikisha inatia ndani kazi ambazo aweza kuzimaliza kwa mafanikio. Ili kumzuia mtoto wako kutotulia na kuchoshwa, mwache atafute vichanganyiko na vyombo vinavyohitajiwa kimbele. Waweza hata kutengeneza vichanganyiko fulani kwa sehemu kimbele ili kipindi hicho kisiwe kirefu na chenye kuchosha.
Isome njia yote ya kupika pamoja na mtoto wako, ukimwonyesha jinsi ya kufanya kila kazi. Mpe mtoto wako nafasi yake mwenyewe jikoni—labda saraka ikiwa na bakuli kadhaa na vyombo vichache—na umpe aproni. Badala ya mvulana kuvaa aproni ya mwanamke, waweza kumtafutia ile iliyotengenezewa mpishi wa kiume. Tangu mwanzoni, kazia umuhimu wa usalama na uweke kanuni zenye busara kwa ajili ya jikoni.—Ona sanduku lenye kichwa “Somo la Kwanza—Usalama,” ukurasa 18.
Zaidi ya yote, fanya ifurahishe. Usiache mtoto wako akutazame tu; mwambie anawe mikono, na umfanye awe na shughuli nyingi katika utayarishaji wenyewe wa chakula. Mpe fursa ya kuvumbua, kujaribu, na kuuliza maswali. Na chakula kisipotokea vizuri, usiwe na wasiwasi. Ikiwa mtoto wako alikitengeneza mwenyewe, yaelekea kwa vyovyote atakila!
Umoja wa Familia
Bila shaka, manufaa kuu zaidi zitokazo jikoni hutia ndani umoja na maadili ya familia. Huenda umeona kwamba katika nyumba fulani leo, washiriki wa familia hutenda shughuli zao tofauti bila kuwasiliana. Chini ya hali kama hizo, nyumbani kwaweza kuwa kama mahali ambapo mtu hutumia wakati mchache sana, kituo cha kula haraka na kuondoka. Kinyume cha hilo, familia ambayo hupika pamoja yaelekea zaidi itakula pamoja na kusafisha pamoja. Utendaji huu huwaandalia fursa za kawaida za kuwasiliana, kuchocheana, na kujuliana hali. “Nilikuwa na mazungumzo bora zaidi pamoja na wavulana wangu tulipokuwa tumesimama tukiosha vyombo,” mama mmoja akumbuka. Na Hermann, baba Mkristo, aongeza: “Tulipanga tusitumie mashine ya kuosha vyombo kwa miaka kadhaa, ili tulazimike kuviosha na kuvikausha kwa mkono. Wana wetu walipewa mgawo wa kuvikausha, wakipokezana zamu. Huo ndio ulikuwa wakati bora zaidi wa mawasiliano ya vivi hivi.”
Ndiyo, wakati unaoutumia jikoni pamoja na watoto wako—juma baada ya juma, mwaka baada ya mwaka—huandaa msingi ambao juu yao thamani za kiroho na sifa za kimungu zaweza kusitawishwa. Ni wakati wa muda kama huo wenye utulivu na umoja kwamba mazungumzo ya kutoka moyoni kati ya mzazi na mtoto yawezapo kuzuka kiasili na kwamba uvutano wa kielelezo cha mzazi uwezapo kuathiri moyo wa mtoto. Uzoezaji huo waweza kumnufaisha mtoto kwa muda wote wa maisha, kwa kuwa Mithali 22:6 husema: “Mlee mtoto katika njia impasayo, naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee.”
Kwa hiyo ikiwa wewe ukiwa mzazi unatafuta njia za kutumia wakati zaidi pamoja na watoto wako, kwa nini usiwakaribishe wakusaidie kutengeneza keki au chakula chote? Huenda ukapata kwamba kufanya kazi pamoja nao jikoni ni njia ya kulisha na kulea familia yako.
[Maelezo ya Chini]
a Kwa mazungumzo juu ya habari hii, ona makala “‘Wakati Bora’ Watumiwa Kidogo-Kidogo,” katika toleo la Amkeni! la Mei 22, 1993, kurasa 16-17.
[Sanduku katika ukurasa wa18]
Somo la Kwanza—Usalama
Kazia Uangalifu Usalama
•Kwa uzito lakini kwa njia isiyotia hofu, eleza hatari za kufanya kazi jikoni, kwa njia ile ambayo ungeeleza hatari za magari kwenye barabara yenye magari mengi. Weka kielelezo kizuri mwenyewe.
•Andaa usimamizi wa mtu mzima wakati wowote watoto wafanyapo kazi jikoni. Usiruhusu mtoto atumie chombo au kifaa, hasa cha umeme, hadi awezapo kukitumia kwa njia salama.
•Panga jiko lako kwa utaratibu. Safisha mimwagiko na uondoe mara moja vitu vyenye kuzuia-zuia njiani. Wanyama rafiki na vikengeusha-fikira vinginevyo vyapasa kuondolewa jikoni wakati wa kupika.
Linda Vidole
•Vikorogeo, na viyeyushi vya umeme, na vitengeneza chakula vya umeme vyapaswa kutumiwa tu kukiwa na usimamizi wa mtu mzima. Hakikisha kwamba kifaa hicho chazimwa na kutolewa kwenye plagi kabla ya mtoto kutumia kijiko kukoroga katika bakuli la kifaa hicho.
•Dumisha visu vikiwa vikali, kwa kuwa kisu kisicho kikali huhitaji kutumiwa kwa nguvu zaidi na kwa hiyo chaweza kuteleza.
•Mtoto wako anapokuwa akijifunza kutumia kisu, mfanye afuate hatua hizi: (1) chukua kisu kwa kutumia mpini wacho, (2) weka kisu juu ya chakula, (3) weka mkono ule mwingine juu ya sehemu ya nyuma ya kisu na (4) usukume ili kukata chakula.
•Tumia ubao wa kukatia. Ili kuzuia mboga kubiringika wakati mtoto wako anapozikata, zikate nusu kwanza na uweke sehemu iliyo bapa upande wa chini juu ya ubao wa kukatia.
Linda Dhidi ya Kuchomeka
•Sikuzote zima mahali ambapo moto huwakia na viwashio vya jiko la kuokea wakati ambapo havitumiki. Weka taulo, vitabu vya mapishi, na vitambaa vya kushikia sufuria mbali na mahali ambapo moto huwakia.
•Weka vishikio vya sufuria kuelekea katikati mwa jiko, mahali ambapo haviwezi kugongwa kwa urahisi na kusababisha mimwagiko.
•Ukimruhusu mtoto wako afanye kazi karibu na jiko, hakikisha kwamba anasimama mahali palipo imara.
•Usichukue kitu chenye joto isipokuwa tayari unajua mahali pa kukiweka. Hakikisha kwamba wengine jikoni wanajua wakati unapobeba kitu chenye joto, hasa ikiwa utatembea nyuma yao.