Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g97 12/8 kur. 5-8
  • Malezi ya Mtoto—Dini na Sheria

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Malezi ya Mtoto—Dini na Sheria
  • Amkeni!—1997
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Haki za Msingi za Wazazi na Watoto
  • Haki za Wazazi Wasio Walezi
  • Upatanisho Nje ya Mahakama
  • Malezi ya Mtoto—Maoni Yaliyosawazika
    Amkeni!—1997
  • Matatizo ya Jamaa Yatatuliwa na Mashauri ya Biblia
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1986
  • Ni Nini Kingekuwa Bora Zaidi kwa Mtoto?
    Amkeni!—1997
  • Mzazi Mmoja, Matatizo Mengi
    Amkeni!—2002
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1997
g97 12/8 kur. 5-8

Malezi ya Mtoto—Dini na Sheria

KATIKA kesi za talaka na malezi ya mtoto, dini yaweza kuwa jambo la maana—na lililo tata. Kwa kielelezo, maswali kama haya yafuatayo yaweza kutokea.

Je, hakimu apaswa kufikiria ushuhuda akidai kuwa mzazi mmoja ni asiyestahili kuwa mlezi wa mtoto kwa sababu mzazi huyo ni mshiriki wa dini fulani, hasa dini isiyo mashuhuri? Je, hakimu apaswa kufikiria ushuhuda kuhusu itikadi na mazoea ya kidini ya wazazi ili aweze kuamua ni dini ipi ingekuwa bora zaidi kwa mtoto, kulingana na maoni yake? Je, basi apaswa kuamuru kwamba mtoto alelewe katika dini hiyo na akataze kabisa mtoto kufunuliwa kwa dini nyinginezo?

Leo, watu wengi zaidi na zaidi wanaoa au kuolewa katika dini na malezi ya kabila tofauti na yao. Kwa hiyo wenzi hawa wanapotalikana, watoto huenda tayari wakawa na uhusiano katika dini mbili tofauti. Wakati mwingine, mzazi anayehusika katika mashauri ya talaka huenda karibuni akawa amekubali kirasmi dini fulani ambayo ni tofauti na ile aliyokuwa nayo hapo awali. Ushirika wa dini mpya huenda ukawa jambo la kuimarisha katika maisha ya mzazi huyo na la maana sana kwake lakini usiojulikana kwa watoto. Hivyo swali jingine latokea, Je, mahakama yaweza kumzuia mzazi kuwapeleka watoto katika ibada za kidini za dini hiyo kwa sababu tu ni tofauti na dini ambayo wazazi hao waliizoea hapo awali?

Haya ni maswali magumu. Yahitaji hakimu kufikiria si mahitaji ya mtoto tu bali pia mapendezi na haki za wazazi.

Haki za Msingi za Wazazi na Watoto

Ni kweli kuwa mahakimu waweza kushawishiwa na maoni yao ya kibinafsi ya kidini. Lakini katika nchi nyingi si rahisi kwa haki za kidini za wazazi au za mtoto kupuuzwa. Nchi hizi huenda zikawa na katiba ambazo huwakataza mahakimu kutozuia haki za msingi za wazazi za kuelekeza malezi ya mtoto, kutia ndani elimu na mafunzo ya kidini ya mtoto.

Kwa upande ule mwingine, mtoto vilevile ana haki ya kupokea mazoezi kama haya kutoka kwa wazazi wake. Kabla ya hakimu kuingilia kisheria mazoezi ya kidini ya mtoto, mahakama lazima isikie uthibitisho wenye kusadikisha kwamba “mazoea hususa ya kidini yanatokeza tisho la papohapo na kubwa kwa hali njema ya kimwili ya mtoto.” (Italiki ni zetu.) Tofauti za kidini tu au hata uhasama kati ya wazazi kuhusu dini haitoshi kuipa serikali haki ya kuingilia.

Katika Nebraska, Marekani, msimamo wenye ufikirio uliochukuliwa na mama aliye mmoja wa Mashahidi wa Yehova katika bishano la malezi watolea kielezi jinsi ambavyo maandalizi ya kisheria huwalinda wazazi wote wawili na watoto. Baba asiye Shahidi hakutaka binti yao ahudhurie ibada za kidini za Mashahidi wa Yehova katika Jumba la Ufalme. Mahakama ya chini zaidi ilikubaliana na baba huyo.

Kisha mama huyo akakata rufani kwenye Mahakama Kuu Kuliko Zote ya Nebraska. Mama huyo alibisha kuwa hakukuwa na uthibitisho wowote wa papohapo au mkubwa wa tisho kwa hali njema ya mtoto katika utendaji wowote wa Mashahidi wa Yehova. Mama huyo alitoa ushuhuda “kwamba kuhudhuria na kushiriki katika utendaji wa kidini wa wazazi wote wawili kungemwandalia . . . mtoto msingi wa kuamua ni dini ipi ambayo angependelea afikapo umri wa kutosha kuelewa.”

Mahakama ya juu zaidi ilibadili uamuzi wa mahakama ya chini zaidi na ikatoa hukumu kuwa “mahakama ya chini zaidi ilitumia vibaya busara yake katika kuwekea mipaka haki ya mama mlezi ya kuongoza malezi ya kidini ya mtoto wake mchanga.” Hakukuwa na uthibitisho wowote kuwa huyo mtoto alikuwa akidhuriwa na kuhudhuria ibada za kidini katika Jumba la Ufalme la Mashahidi wa Yehova.

Haki za Wazazi Wasio Walezi

Wakati mwingine, wazazi waliotalikana hujaribu kutumia mabishano kuhusu mazoezi ya kidini kama njia ya kupata udhibiti wa watoto. Kwa kielelezo, katika Khalsa v. Khalsa, kesi katika jimbo la New Mexico, Marekani, wazazi wote wawili walikuwa wamezoea Dini ya Sikh wakati wa ndoa yao. Lakini muda mfupi baada ya kutalikana, mama huyo akageuka kuwa Mkatoliki na akaanza kuwavunja moyo watoto wasizoee Dini ya Sikh.

Baba alikasirika, akalipeleka jambo hilo mahakamani katika jaribio la kupata mamlaka zaidi ya kuelekeza mazoezi ya kidini ya watoto wake kuelekea Dini yake ya Sikh. Mahakama iliitikiaje ombi la baba huyo? Ilikataa ombi lake. Mahakama iliamuru kuwa “wakati watoto walipokuwa [naye], hawangeweza kushiriki kwa hiari ama kwa kulazimishwa katika utendaji wowote wa Sikh, kutia ndani utendaji wowote wa kanisa, kambi ya Sikh au siku ya utunzaji katika kitovu cha Sikh.”

Baba huyo alikata rufani uamuzi huo kwenye Mahakama ya Rufani ya New Mexico. Mahakama hii ya juu zaidi ilikubaliana na baba huyo na ikabadili uamuzi wa mahakama hiyo ya chini. Mahakama ya rufani ilitaarifu hivi: “Mahakama zapaswa kushikamana sana na sera ya kutopendelea kati ya dini, na yapaswa kuingilia katika eneo hili nyetivu na lenye kulindwa kikatiba ambapo tu kuna uthibitisho wa wazi na wenye kuthibitika wa dhara kwa watoto. Vizuizi katika eneo hili vyatokeza hatari ya kwamba mipaka iliyowekwa na mahakama itaingilia kwa njia inayopinga katiba uhuru wa kuabudu wa mzazi au itaonwa kuwa na athari hiyo.”

Uamuzi kama huo wafuata mstari mrefu wa kanuni ambazo zimeimarishwa vema katika nchi nyingi. Mzazi mwenye kukubali sababu atafikiria kanuni hizi. Kwa kuongezea, mzazi Mkristo atafikiria kwa uangalifu uhitaji wa mtoto wa kuwasiliana na wazazi wote wawili, na pia jukumu la mtoto la kuonyesha heshima kwa mama na baba.—Waefeso 6:1-3.

Upatanisho Nje ya Mahakama

Ijapokuwa upatanisho nje ya mahakama huenda usiwe rasmi sana kama kusikia mbele ya hakimu, mzazi hapaswi kuuchukulia kwa njia isiyo rasmi. Makubaliano yoyote ya pamoja au mkataba wowote uliofikiwa katika utaratibu huu wa malezi waweza kufungwa kwa maagizo ya mahakama ya baadaye. Kwa hiyo, lingekuwa jambo la hekima kwa mzazi kutafuta habari kutoka kwa mwanasheria wa mambo ya familia mwenye uzoefu ili kuhakikisha kwamba mambo yote yanayohusiana na malezi yanashughulikiwa ifaavyo na kwa usawa.

Kila mzazi lazima achukue wakati wa kujitayarisha kwa ajili ya utaratibu wa upatanisho. Tabia ya mzazi kuelekea wengine na mwenendo wake wakati wa utaratibu wa upatanisho waweza kuathiri sana matokeo. Mara nyingi sana, wazazi wanaotalikana huwa na hisia nyingi sana kuelekea hatua hiyo ya talaka hivi kwamba wanakosa kuona masuala ya maana: Ni nini lililo bora zaidi kwa mtoto? Mtoto anahitaji nini ili akue kiakili, kihisia-moyo, na kimwili?

Kumbuka kwamba katika maoni ya kisheria, jambo la msingi katika upatanisho si tofauti ya kidini au ya jambo jingine lolote la kibinafsi, bali ni jinsi wazazi wawezavyo kupata njia ya kukubaliana na kutafuta mapatano kwa ajili ya manufaa ya watoto. Huenda mzazi akakabiliwa na ubaguzi wa kidini, au ubaguzi mwingine wowote, maswali yasiyotazamiwa, au miongozo ya hila iliyokusudiwa kufadhaisha na kukasirisha. Kasoro za kila mzazi huenda zikatokezwa wazi au hata kutiliwa chumvi. Hata hivyo, wanaohusika wanapobaki wakiwa wenye kukubali sababu, azimio laweza kufikiwa.

Wakati mwingine, utaratibu wa upatanisho waweza kuonekana ukichukua muda mrefu na wenye kuvunja moyo. Kibadala ni hatua ya mahakama yenye kuchukua wakati mrefu, pamoja na kutiwa aibu kwa waziwazi, mzigo wenye kulemea wa kifedha, na athari zenye hasara kwa mtoto. Hili kwa hakika si lenye kutamanika. Kama vile na matatizo mazito yote maishani, mzazi Mkristo atataka kufikia utaratibu wa upatanisho kwa sala, akikumbuka mwaliko uliopuliziwa “umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini, naye atafanya.”—Zaburi 37:5.

Lakini namna gani ikiwa suluhisho haliwezi kufikiwa na hakimu anampa malezi ya mtoto yule mzazi mwingine? Au namna gani ikiwa mmoja wa wazazi wanaotalikana ametengwa na ushirika wa kutaniko la Kikristo? Pia, mmoja apaswa kuonaje malezi ya pamoja na ya mzazi mmoja tu? Maswali haya na kanuni za Biblia zinazohusiana zitazungumziwa katika makala ifuatayo.

[Sanduku katika ukurasa wa 6]

Sifa Tatu za Maana

Hakimu mmoja wa mahakama ya familia aliyehojiwa na Amkeni! alisema kuwa kati ya sifa zilizo muhimu atafutazo katika mzazi ni hizi tatu zifuatazo:

Kukubali Sababu—kuwa tayari kumruhusu mzazi yule mwingine wakati wa kuwa na mtoto (ikiwa tu hakuna tisho la kimwili au la kiadili kwa mtoto)

Kuwa Mwenye Hisia Nyepesi—ufahamu wa mahitaji ya kihisia-moyo ya mtoto

Kujidhibiti—maisha ya kinyumbani yenye usawaziko ambayo yangechangia hali yenye utulivu ambapo mtoto angenawiri

Miongozo ya Kihukumu

Kwa kuweka miongozo, mahakimu fulani wamejaribu kuepuka mizozano isiyo ya lazima kuhusu viwango vya kidini vya mzazi. Kwa kielelezo:

1. Uhusiano wenye maana kati ya mtoto na wazazi wote wawili wapasa kukaziwa. Hakimu John Sopinka wa Mahakama Kuu Zaidi ya Kanada alionelea kwamba kila mzazi apaswa kukubaliwa “kushiriki katika utendaji ambao utachangia kumtambulisha mzazi kuwa alivyo hasa [kutia ndani mazoea ya dini yake]. Mzazi asiye mlezi hatarajiwi kujifanya asivyo au kuchukulia mtindo-maisha wenye udanganyifu wakati anapokuwa na watoto.”

2. Kumzuia mzazi asiye mlezi asimfunze mtoto itikadi zake za kidini ni kuhalifu uhuru wa kidini wa huyo mzazi, isipokuwa pale ambapo kuna uthibitisho wa wazi wa madhara ya papohapo au makubwa kwa mtoto.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Mahakimu wana jukumu zito katika kesi za malezi

[Picha katika ukurasa wa 8]

Mpatanishi anaweza kuwasaidia wazazi kusuluhisha tofauti bila kuwa na utaratibu wa mahakama wenye kuchukua muda mrefu

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki