Hangaiko la Habari Husababishwa na Nini?
“HANGAIKO LA HABARI hutokezwa na pengo linalozidi kukua kati ya yale tunayoelewa na yale tunayofikiri twapaswa kuelewa. Hangaiko la habari hutokezwa na kinachokosekana kati ya data na ujuzi, na hutokea wakati ambapo habari hazituelezi tunachotaka au tunachohitaji kujua.” Ndivyo alivyoandika Richard S. Wurman katika kitabu chake Information Anxiety. “Kwa muda mrefu, watu hawakutambua kadiri ya mambo ambayo hawakujua—hawakujua kuwa kulikuwa mambo mengi ambayo hawakujua. Lakini sasa watu wanajua kwamba kuna mambo ambayo hawajui, na hilo lawafanya wahangaike.” Matokeo ni kwamba wengi wetu huenda tukahisi kwamba twapaswa kujua mengi kuliko tunayojua. Kukiwa na habari nyingi sana inayotolewa kwetu, tunachukua tu visehemu vidogo vya data. Lakini mara nyingi hatuna uhakika tufanye nini navyo. Wakati uleule, huenda tukafikiri kuwa kila mtu mwingine anajua na kuelewa mengi zaidi kuliko sisi. Hapo ndipo tuwapo na hangaiko!
David Shenk abisha kwamba habari zenye kuzidi mno zimekuwa kichafuzi ambacho chasababisha “ukungu wa data.” Yeye aongezea: “Ukungu wa data huzuia; hautoi nafasi ya dakika chache za kimya, na unakinza kufikiria kwa makini kwingi kunakohitajiwa. . . . Unatusababishia mkazo mwingi.”
Ni kweli kuwa habari nyingi kupita kiasi au mambo mengi mno yanaweza kusababisha hangaiko, lakini ndivyo ilivyo pia ikiwa hatuna habari za kutosha au, vibaya zaidi, ikiwa tuna habari zisizo sahihi. Kuwa na habari nyingi kupita kiasi ni kama kujihisi mpweke katika chumba kilichojaa watu. Kama vile John Naisbitt asemavyo katika kitabu chake Megatrends, “tunazama katika wingi wa habari lakini twafa njaa kwa ajili ya ujuzi.”
Jinsi Uhalifu wa Kompyuta Unavyoweza Kukuathiri
Sababu nyingine ya hangaiko ni kuongezeka kwa kasi kwa uhalifu wa kompyuta. Katika kitabu chake Protection and Security on the Information Superhighway, Dakt. Frederick B. Cohen, aelezea mahangaiko yake: “[Shirika la Upelelezi la] FBI lakadiria kuwa kila mwaka kiasi cha kufikia dola bilioni 5 hupotezwa kwa sababu ya uhalifu wa kompyuta. Na, kwa kushangaza, hiyo ni sehemu ndogo tu ya tatizo kubwa zaidi. Hitilafu katika mifumo ya kompyuta pia imetumiwa kwa kujifaidi ili kudhibiti majadiliano, kuharibu sifa, kushinda katika mapambano ya kijeshi, na hata kuua kimakusudi.” Kwa kuongezea hili ni hangaiko linaloongezeka kuhusu tatizo la watoto kuweza kufikia ponografia ya kompyuta—bila kutaja kuingiliwa kwa faragha.
Waraibu wa kompyuta wasio wanyoofu wameweka kimakusudi virusi katika mifumo ya kompyuta na kusababisha uharibifu mkubwa. Wahalifu stadi wa mambo ya kompyuta huingilia kiharamu mifumo ya elektroni na kupata habari za siri, wakati mwingine hata wanaiba pesa. Utendaji kama huo waweza kuwa na matokeo yenye kuangamiza kabisa kwa maelfu ya watumiaji wa kompyuta za kibinafsi. Uhalifu wa kompyuta ni tisho kwa biashara na serikali.
Uhitaji wa Kuwa Mwenye Kuarifiwa Vizuri
Bila shaka, sisi sote twahitaji kuwa wenye kuarifiwa vizuri, lakini kuwa na kiasi kikubwa sana cha habari kwa kweli hakutuelimishi, kwa kuwa nyingi za zile zinazoonekana kuwa habari huhusisha tu mambo matupu au data isiyo kamili, isiyohusiana na ujuzi wetu. Wengine hata wapendekeza kwamba badala ya lile “ongezeko kubwa la habari,” maneno “ongezeko kubwa la data” yangefaa zaidi jambo hili au kwa ubeuzi hata zaidi lile “ongezeko kubwa la ukosefu wa habari.” Hivi ndivyo mchanganuzi wa uchumi Hazel Henderson alionavyo: “Habari peke yake haielimishi. Hatuwezi kufafanua ni ipi habari yenye makosa, au habari iliyo kinyume, au propaganda katika mazingira yaliyotawalwa na habari. Kukazia fikira habari tu kumeongoza kwa mabilioni ya vipande vya data zisizo kamili na zisizopatana, badala ya kutafuta vigezo vipya vya ujuzi wenye maana.”
Joseph J. Esposito, msimamizi wa Kundi la Uchapishaji la Encyclopædia Britannica, atoa kadirio hili la wazi: “Habari nyingi za Enzi ya Habari hutumiwa vibaya tu; ni kelele tu isiyofaa. Ongezeko Kubwa la Habari ni ufafanuzi ufaao; ongezeko hilo huzuia uwezo wetu wa kusikia hasa mengi kuhusu chochote. Ikiwa hatuwezi kusikia, hatuwezi kujua.” Orrin E. Klapp atoa mchanganuo wake: “Nashuku kwamba hakuna yeyote ajuaye ni kiasi gani cha uwasiliano wa umma ambacho ni habari za uwongo, ambazo zadai kusema jambo fulani lakini kwa hakika hazisemi kitu.”
Bila shaka utakumbuka kuwa sehemu kubwa ya elimu yako shuleni ilikazia kujifunza mambo ya hakika ili uweze kupita mitihani. Nyakati nyingi ulikariri mambo ya hakika akilini mwako kabla tu ya wakati wa mtihani. Je, wakumbuka ukijifunza kwa moyo tarehe nyingi katika masomo ya historia? Kati ya matukio hayo na tarehe hizo ni ngapi uwezazo kukumbuka sasa? Je, mambo hayo yalikufunza kusababu na kufikia mikataa ya kimantiki?
Je, Kuwa na Habari Nyingi Ni Kwenye Faida Sikuzote?
Ukiwa haudhibitiwi vizuri, ujitoaji kwa kujipatia habari ya ziada waweza kugharimu mengi kwa habari ya wakati, usingizi, afya, na hata pesa. Ingawa habari nyingi zaidi hutoa nafasi nyingi zaidi, yaweza kumfanya mtafutaji kuwa na hangaiko, akijiuliza ikiwa amechunguza au amepata habari yote iwezayo kupatikana. Dakt. Hugh MacKay atoa onyo hili: “Kwa hakika, habari si njia ya kuelekea kuelimika. Habari yenyewe haitoi nuru juu ya maana ya maisha zetu. Habari haihusiani sana na kupata hekima. Kwa kweli, kama mali nyingine, yaweza kwa hakika kuzuia hekima. Twaweza kujua mengi mno kama vile tuwezavyo kuwa na vitu vingi mno.”
Mara nyingi, watu hawalemewi tu na habari nyingi zipatikanazo leo bali pia na kukatishwa tamaa kwa kujaribu kubadili habari iwe kitu kiwezacho kueleweka, chenye umaana, na chenye kuarifu kwelikweli. Imependekezwa kuwa twaweza kuwa kama “mtu mwenye kiu ambaye amehukumiwa kutumia kastabini ili kuchota maji kutoka kwenye bomba la maji la kuzimia moto. Habari nyingi zinazopatikana na namna ambayo kwa kawaida huwa zinatolewa inafanya habari nyingi zisiwe na faida kwetu.” Kwa hiyo, zinazotosha zapasa kukadiriwa, si kwa wingi, bali kwa ubora na manufaa yake kwetu binafsi.
Namna Gani Uhamishaji wa Data?
Usemi mwingine unaosikika sana leo ni “uhamishaji wa data.” Huo warejezea kupitisha habari kielektroni. Ingawa huo wathaminiwa, si uwasiliano mzuri katika maana halisi. Kwa nini? Kwa sababu twaitikia vizuri zaidi kwa watu, sio kwa mashine. Katika uhamishaji wa data, ishara za uso hazionekani na hamwonani ana kwa ana wala hakuna ishara za mwili, ambazo mara nyingi hupamba maongezi na huwasilisha hisia. Katika maongezi ya ana kwa ana, mambo haya huongezea maneno na mara nyingi huelewesha maneno yanayotumiwa. Misaada hii yenye thamani haiwezi kupatikana kupitia uhamishaji wa kielektroni, wala hata kupitia simu za redio ambazo sasa zimeenea sana. Nyakati nyingine, hata maongezi ya ana kwa ana hayawasilishi kikamili yale ambayo yako katika fikira za msemaji. Msikilizaji aweza kupokea na kuelewa maneno katika njia yake mwenyewe na kuyaona kuwa yamaanisha vingine. Kuna hatari kubwa hata zaidi kama nini kwa hili kutukia ikiwa msemaji haonekani!
Ni jambo la kuhuzunisha kwamba katika maisha ya kila siku kwamba wakati mwingi kupita kiasi ambao watu fulani hutumia mbele ya kompyuta na televisheni nyakati nyingine huwafanya washiriki wa familia wawe wageni kuelekeana katika nyumba yao wenyewe.
Umesikia Kuhusu Technophobia?
Neno “technophobia” lamaanisha tu “hofu ya tekinolojia,” kutia ndani matumizi ya kompyuta na vyombo vingine vya elektroni kama hivyo. Wengine waamini kuwa hili ni moja ya mahangaiko yaliyoenea zaidi sana yanayotokana na enzi ya habari. Makala fulani katika The Canberra Times, iliyotegemea taarifa ya Shirika la Habari la Associated Press ilisema hivi: “Wakuu wa Japani Waogopa Kompyuta.” Ilisemwa hivi juu ya mkurugenzi mkuu wa kampuni moja kubwa ya Japani: “[Yeye] hutoa amri kwa mamlaka na hadhi kubwa. Lakini akiketi mbele ya kompyuta, anakuwa mwenye wasiwasi sana.” Kulingana na uchunguzi wa kampuni 880 za Japani, ni asilimia 20 tu ya wakuu wao walioweza kutumia kompyuta.
Hilo technophobia lachochewa na misiba mikubwa kama ule uliosababisha kufungwa kwa simu 1991 katika New York City na ambao ulifanya viwanja vya ndege vya huko visiweze kufanya kazi kwa muda wa saa kadhaa. Na namna gani ile aksidenti katika Kituo cha Nyuklia cha Three Mile Island huko Marekani katika 1979? Iliwachukua wafanyakazi wa mahali hapo muda wa saa nyingi za maana kabla ya kuweza kuelewa maana ya ishara za king’ora zilizoongozwa na kompyuta.
Hivi ni vielelezo vichache tu vya jinsi ambavyo tekinolojia ya enzi ya habari imeathiri sana wanadamu. Katika kitabu chake, Dakt. Frederick B. Cohen auliza maswali haya yenye kuamsha kufikiri: “Je, umeenda benki karibuni? Ikiwa kompyuta hazikuwa zikifanya kazi, je, ungeweza kupata pesa zozote kutoka kwazo? Namna gani duka kuu? Je, wangeweza kukutoza kwa bidhaa ulizonunua bila kutumia kompyuta?”
Labda waweza kujihusisha na moja au zaidi ya hali hizi zenye kuwaziwa:
• Mashine yako mpya ya ukanda wa vidio (VCR) yaonekana kuwa na vidude vingi mno wakati unapotaka kuchagua programu unayotaka kurekodi. Ama kwa aibu wamwita mpwa wako mwenye umri wa miaka tisa akutayarishie mashine au waamua kuwa hakuna haja ya kurekodi programu hiyo tena.
• Una uhitaji mkubwa sana wa pesa. Waendesha gari hadi kwenye mashine iliyo karibu zaidi ya kutolea pesa lakini mara hiyo wakumbuka kuwa mara ya mwisho ulipoitumia ulichanganyikiwa, ukabonyeza vidude visivyo sahihi.
• Simu ya ofisini yalia. Simu hiyo ilipitishwa kwako kwa makosa. Simu hiyo ilikuwa ya mkubwa wako kwenye orofa ya juu. Kuna njia rahisi ya kumpitishia simu hiyo, lakini, bila kuwa na uhakika, waamua kumwacha opareta kwenye swichibodi ya simu aipitishe simu hiyo.
• Dashibodi ya gari lako ulilonunua karibuni yaonekana kana kwamba ni ya ndege. Kwa ghafula taa nyekundu inamweka, na waanza kuhangaika kwa sababu hujui taa hiyo yaashiria nini. Kisha inakubidi uchunguze kitabu chenye maagizo kamili.
Hivi ni vielelezo vichache tu vya technophobia. Twaweza kuwa na uhakika kuwa tekinolojia itaendelea kutokeza vifaa tata hata zaidi, ambavyo watu wa vizazi vilivyopita bila shaka wangeviita “muujiza.” Kila bidhaa mpya ianzayo kuuzwa yahitaji ujuzi mwingi zaidi ikiwa itatumika kwa manufaa. Vitabu vya maagizo vilivyoandikwa na wataalamu katika lugha yao ya kitaalamu,a vyenyewe vyaogopesha inapodhaniwa kuwa mtumiaji aelewa msamiati huo na kuwa ana ujuzi na ustadi fulani.
Mwananadharia wa habari Paul Kaufman ajumlisha hali hiyo katika njia hii: “Jamii yetu ina maoni ya habari ambayo, zijapokuwa zenye kuvutia sana, mwishowe zaelekea kuzuia lengo lililokusudiwa. . . . Sababu moja ni kwamba uangalifu mwingi sana umeelekezwa kwenye kompyuta na vifaa na uangalifu mdogo sana kwa watu ambao hutumia habari ili waweze kupata maana ya ulimwengu na kufanya mambo yenye mafaa kwa mmoja na mwenzake. . . . Tatizo si kwamba twafikiria kompyuta kuwa za hali ya juu sana lakini ni kwamba twawafikiria wanadamu kuwa wa hali ya chini sana.” Yaelekea kuwa shughuli nyingi ili kupata sifa ya kutokeza vitu vipya vya ajabu vya kitekinolojia mara nyingi imewaacha watu wakiwa na wasiwasi juu ya ni nini kitakachotukia hatimaye. Edward Mendelson asema: “Watu wenye maoni yasiyotumika kitekinolojia hawawezi kamwe kutambua tofauti kati ya yawezayo kufanywa na yapendezayo. Ikiwa mashine yaweza kutengenezwa ili ifanye kazi yenye kutatanisha sana, basi mtu mwenye maoni yasiyotumika adhani kuwa kazi hiyo ni yenye manufaa ikifanywa.”
Ni huku kupuuza wanadamu katika tekinolojia ambako kumeongezea sana hangaiko la habari.
Je, Utokezaji wa Kazi Umeboreka Kweli?
Mwandishi wa makala Paul Attewell, akiandika katika The Australian, atoa maelezo yake kuhusu utafiti alioufanya kuonyesha ni kiasi gani cha wakati na pesa kimeweza kuokolewa kwa sababu ya utumizi wa kompyuta katika miaka ya karibuni. Hapa pana machache ya maoni yake yaliyotolewa vizuri: “Ijapokuwa miaka mingi ya kutega uchumi katika mifumo ya kompyuta iliyobuniwa ili kushughulikia kazi za usimamizi na kudhibiti gharama, vyuo vikuu na vyuo vingi hukuta kwamba wafanyakazi-wasimamizi wao huzidi kuongezeka. . . . Kwa miongo kadhaa, watengeneza-kompyuta wamesisitiza kwamba tekinolojia waliokuwa wakiuza ingeweza kufanya utokezaji uongezeke mara moja, hili likifanya iwezekane kazi ya idadi fulani ya usimamizi iweze kufanywa na wafanyakazi wachache zaidi na kwa gharama kidogo zaidi. Badala ya hivyo, kama tunavyokuja kuona, tekinolojia ya habari imeongoza kwenye kutofanya bidii: mambo mengi mapya yanafanywa na wafanyakazi walewale au hata wengi zaidi kuliko kazi ya zamani kufanywa na wafanyakazi wachache. Mara nyingi, hakuna pesa zinazookolewa. Kielelezo kimoja cha hali hiyo ni kuwa watu wanatumia tekinolojia kufanya hati zionekane kuwa nzuri zaidi badala ya kufanya kazi ya ukarani haraka zaidi.”
Sasa yaonekana kama barabara kuu ya habari, ambayo ni hatari sana kwa Wakristo, itadumu. Lakini twaweza kuepukaje hangaiko la habari—angalau kwa kiasi fulani? Twatoa mapendekezo machache yenye kutumika katika makala fupi ifuatayo.
[Maelezo ya Chini]
a Vielelezo vya lugha ya kitaalamu ya kompyuta: log on, yamaanisha “unganisha mtambo”; boot up, “anzisha au weka katika mwendo”; portrait position, “wima”; landscape position, “mlazo.”
[Sanduku katika ukurasa wa 6]
Takataka Nyingi Sana za Habari
“Kama tujuavyo kutokana na mambo yaliyoonwa, jamii inazidi kuwa chafu. Tunaona enzi mpya ya vipindi vya televisheni visivyofaa, vipindi vya redio vya kuchochea chuki, watangazaji wa redio wenye kushtusha, mashtaka ya kisheria, njia zisizo za kawaida za kutafuta umashuhuri, usemi wenye jeuri kupita kiasi na wenye kukejeli sana. Sinema zinaonyesha ngono waziwazi na jeuri kuliko wakati mwingine wowote. Matangazo ya kibiashara yana kelele zaidi, yaenea zaidi, na mara nyingi yakikaribia hali ya kutopendeza . . . Matusi yaongezeka na adabu za kawaida zashuka. . . . Kile ambacho watu wengi wamekiita ‘tatizo katika viwango vya familia’ kinahusiana zaidi na mabadiliko makubwa ya habari kuliko inavyohusiana na ukosefu wa staha wa sinema za Hollywood kwa utaratibu wa familia.”—Data Smog—Surviving the Information Glut, kilichoandikwa na David Shenk.
[Sanduku katika ukurasa wa 7]
Hekima—Ile Njia ya Kizamani
“Mwanangu, kama ukiyakubali maneno yangu, na kuyaweka akiba maagizo yangu; hata ukatega sikio lako kusikia hekima, ukauelekeza moyo wako upate kufahamu; naam, ukiita busara, na kupaza sauti yako upate ufahamu; ukiutafuta kama fedha, na kuutafutia kama hazina iliyositirika; ndipo utakapofahamu kumcha BWANA, na kupata kumjua Mungu. Kwa kuwa BWANA huwapa watu hekima; kinywani mwake hutoka maarifa na ufahamu. Maana hekima itaingia moyoni mwako, na maarifa yatakupendeza nafsi yako; busara itakulinda; ufahamu utakuhifadhi.”—Mithali 2:1-6, 10, 11.
[Picha katika ukurasa wa 8, 9]
Habari nyingi kupita kiasi imefananishwa na kujaribu kujaza kastabini kutoka kwenye bomba la maji