Je, Wanasayansi Wamegawanyika?
“INGAWA hatupaswi kupuuza wazo la kwamba sayansi ni utafutaji wa kweli kuhusu ulimwengu, tunapaswa kufikiria mambo ya kisaikolojia na ya kijamii ambayo mara nyingi hupinga utafutaji huo.” Ndivyo alivyoandika Tony Morton katika insha yenye kichwa “Maoni Yenye Kutofautiana: Nia na Mbinu za Wanasayansi.” Ndiyo, yaonekana kwamba umashuhuri, mapato ya kifedha, au hata kupendelea upande fulani kisiasa nyakati nyingine kumeathiri ugunduzi wa wanasayansi.
Kule nyuma katika 1873, Lord Jessel alionyesha hangaiko kuhusu mavutano kama hayo katika kesi za mahakamani aliposema hivi: “Uthibitisho utolewao na wataalamu . . . ni uthibitisho wa watu ambao nyakati nyingine hupata riziki kutokana na kazi hiyo, na katika visa vyote wao hulipwa kwa ajili ya uthibitisho wao. . . . Basi ni kawaida kwamba hata awe mwenye kufuatia haki kadiri gani, akili yake itapendelea mtu ambaye amemwajiri, na kwa njia hiyo sisi huona upendeleo kama huo.”
Kwa kielelezo, fikiria sayansi inayoshughulikia uhalifu. Mahakama moja ya rufani ilitaja kwamba wanasayansi wa kushughulikia uhalifu wanaweza kuwa wenye kupendelea upande mmoja. Jarida Search lasema: “Jambo la kwamba polisi hutafuta msaada wao laweza kukuza uhusiano kati ya polisi na wanasayansi wa kushughulikia uhalifu. . . . Wanasayansi wanaoshughulikia uhalifu ambao wanaajiriwa na serikali waweza kuanza kuona kazi zao kuwa za kuwasaidia polisi.” Jarida hili latoa kielelezo cha zile kesi za mabomu yaliyolipuliwa na wapiganaji wa IRA (Irish Republican Army) la Maguire (1989) na Ward (1974) nchini Uingereza kuwa ina “uthibitisho wenye nguvu juu ya utayari wa wanasayansi fulani wenye uzoefu sana na ambao wamesifika sana wa kuacha kutokuwamo kwao kisayansi na kuona madaraka yao kuwa kusaidia upande wa mashtaka.”
Kielelezo kingine chenye kutokeza ni kesi ya Lindy Chamberlain nchini Australia (1981-1982), ambayo ilikuja kuwa msingi wa sinema A Cry in the Dark. Yaonekana kwamba uthibitisho uliotolewa na wataalamu wa sayansi inayoshughulikia uhalifu ulikuwa na uvutano katika hukumu iliyotolewa dhidi ya Bi. Chamberlain, ambaye alishtakiwa kumwua kimakusudi mtoto wake Azaria. Ingawa alidai kwamba mtoto huyo aliuawa na mbwa-mwitu, yeye alipatikana na hatia na kufungwa gerezani. Miaka kadhaa baadaye, jaketi chafu na yenye damu ya mtoto huyo ilipopatikana, uthibitisho wa awali haukutosha kuthibitisha ni nani aliyekuwa amemwua huyo mtoto. Tokeo likawa kwamba Lindy aliachiliwa kutoka gerezani, hukumu yake ikabatilishwa, akalipwa ridhaa kwa sababu ya kufungwa kwa makosa.
Mwanasayansi abishanapo na mwanasayansi, ubishi waweza kuwa mkali. Miongo kadhaa iliyopita ushindani baina ya Dakt. William McBride na watengenezaji wa dawa inayoitwa thalidomide uliripotiwa katika habari kote ulimwenguni. Alipodokeza kwamba dawa hiyo, ambayo inauzwa ili kuondoa kichefuchefu cha asubuhi kwa wenye mimba, ilitokeza madhara katika watoto ambao bado hawajazaliwa, daktari huyo akawa shujaa mara hiyo. Lakini, miaka kadhaa baadaye, alipokuwa akifanya kazi katika mradi mwingine, daktari aliyekuwa mwandishi wa habari alimshtaki kwa kubadili data. McBride alipatikana na hatia ya udanganyifu wa kisayansi na utovu wa nidhamu kikazi. Aliondolewa kwenye orodha ya madaktari katika Australia.
Ubishi wa Kisayansi
Ubishi wa karibuni zaidi ni kama nguvu za sumakuumeme zinadhuru afya za wanadamu na wanyama au hazidhuru. Uthibitisho fulani wadokeza kwamba kuna uchafuzi mwingi sana wa mazingira unaotokezwa na sumakuumeme, ambazo vyanzo vyake vyaanzia nyaya za kupitishia umeme wenye nguvu nyingi sana hadi kompyuta za kibinafsi na joko la microwave [lililo] katika nyumba yako. Wengine hata wanadai kwamba baada ya miaka fulani, simu za mkononi zaweza kuharibu ubongo wako. Na bado wengine waonyesha uchunguzi wa kisayansi unaodokeza kwamba mnururisho wa sumakuumeme waweza kusababisha kansa na kifo. Kwa kutoa kielelezo cha jambo hilo, gazeti la habari The Australian laripoti: “Shirika moja la umeme la Uingereza linashtakiwa juu ya kifo cha mvulana mmoja ambaye yasemekana alishikwa na kansa alipokuwa akilala chini ya nyaya zenye nguvu nyingi sana za umeme.” Mshauri mmoja wa Melbourne wa tiba ya magonjwa yatokanayo na kazi, Dakt. Bruce Hocking, alipata kwamba “watoto wanaoishi umbali upatao kilometa nne kutoka kwenye vinara vya kituo cha televisheni cha Sydney walikuwa na visa vya kuambukizwa leukemia kwa kiwango cha mara mbili kuliko watoto walioishi nje ya umbali huo wa kilometa nne.”
Ingawa wanamazingira wanaendeleza madai kama hayo, biashara kubwa-kubwa na mashirika ya kibiashara yanaweza kupoteza mabilioni ya dola kutokana na kile yanachoita “kampeni za bure za kuwaogofya watu.” Kwa hiyo hizo zinashambulia pia na kuungwa mkono na sehemu nyinginezo za jumuiya ya kisayansi.
Kisha kuna ubishi juu ya uchafuzi wa kemikali. Wengine wamefafanua dioksini kuwa “kemikali yenye sumu zaidi iliyopata kutengenezwa na mwanadamu.” Kemikali hiyo, inayofafanuliwa na Michael Fumento kuwa “zaotuka tu lisiloweza kuepukika katika utengenezaji wa dawa fulani za kuua magugu” (Science Under Siege), iliitwa na wengine “sehemu kubwa ya dawa ya kuua magugu iitwayo Agent Orange.”a Hiyo ilitangazwa sana baada ya vita ya Vietnam. Mapambano makubwa ya kisheria yalifuata baina ya mashujaa wa vita na makampuni ya kemikali, kila kikundi kikiwa na wataalamu wake wa kisayansi wenye maoni yanayotofautiana.
Vivyo hivyo, masuala ya kimazingira kama vile kuongezeka kwa joto la dunia, athari ya kuongezeka kwa joto, na kupunguka kwa tabaka ya ozoni yanashika uangalifu mwingi wa umma. Kuhusu hofu za kimazingira kwa ajili ya Antaktika, gazeti la habari The Canberra Times laripoti: “Utafiti uliofanywa na wanasayansi katika Kituo cha Palmer, ambacho ni kituo cha kisayansi cha Marekani kilichoko katika Kisiwa cha Anvers, waonyesha kwamba mnururisho mwingi wa urujuanimno huharibu aina ndogondogo za uhai kama vile plankitoni na moluska nao waweza kuanza kuathiri mfuatano wa ulishano wa wanyama.” Lakini uchunguzi mwingine mwingi wa kisayansi waonekana kupinga wazo kama hilo na kuondosha hofu kuhusu kupunguka kwa ozoni na kuongezeka kwa joto la tufe.
Kwa hiyo ni nani asemaye kweli? Inaonekana kwamba kila dai au ubishi waweza kuthibitishwa kuwa ama kweli ama si kweli na wataalamu wa kisayansi. “Kweli ya kisayansi huamuliwa na angalau maoni yanayoenea kijamii katika wakati fulani kama tu inavyoamuliwa na kusababu kuzuri na mambo yapatanayo na akili pekee,” chasema kitabu Paradigms Lost. Michael Fumento, amalizia suala la dioksini kwa kusema: “Ikitegemea ni nani unayemsikiliza, ama sisi sote tunaweza kuwa wahasiriwa wa kusumishwa ama tunaweza kuwa wahasiriwa wa udanganyifu mbaya sana.”
Lakini, misiba fulani ijulikanayo sana ya kisayansi haiwezi kutolewa udhuru. Ni lazima sayansi itoe hesabu kwa hiyo misiba.
“Msiba Wenye Madhara Sana”
Katika taarifa “Ujumbe kwa Wataalamu,” iliyotolewa Agosti 29, 1948, Albert Einstein alionyesha mambo yasiyopendeza ya sayansi aliposema hivi: “Kwa mambo machungu tuliyojionea tumejifunza kwamba kufikiri kuzuri hakutoshi kusuluhisha matatizo ya maisha yetu ya kijamii. Utafiti wa kina na kazi ya kisayansi yenye kufanywa kwa makini mara nyingi zimehusu wanadamu kwa njia yenye msiba sana, . . . zikifanyiza njia za binadamu kujiangamiza mwenyewe kwa wingi. Kwa kweli, huu ni msiba wenye madhara sana!”
Taarifa ya karibuni ya shirika la habari la Associated Press yasema hivi: “Uingereza Lakiri Kufanya Majaribio ya Mnururisho kwa Wanadamu.” Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilithibitisha kwamba hiyo serikali tayari ilikuwa imefanya majaribio ya mnururisho kwa wanadamu kwa karibu miaka 40. Mojawapo ya majaribio hayo lilihusu kujaribiwa kwa bomu la atomu katika Maralinga, Australia Kusini, katikati ya miaka ya 1950.
Maralinga ni jina litokanalo na neno la Wenyeji wa Australia limaanishalo “radi,” na eneo hilo lililojitenga liliandaa mahali pazuri sana pa Uingereza kufanya majaribio yake ya kisayansi. Baada ya mlipuko wa kwanza, furaha kwa ajili ya mafanikio hayo iliijaza anga. Ripoti ya gazeti moja la habari la Melbourne ilisema: “Wingu lenye [mnururisho] lilipofifia, misafara ya malori na magari aina ya jip ilileta wanajeshi wa Uingereza, Kanada, Australia, na New Zealand ambao walikuwa wamekabili mlipuko huo wakiwa katika mashimo yaliyochimbwa kilometa nane tu kutoka mahali pa mlipuko. Na kila uso ulitabasamu. Ilikuwa ni kana kwamba wametoka kujifurahisha.”
Mleta-habari wa mambo ya kisayansi wa gazeti la habari la Uingereza Daily Express, Chapman Pincher, hata alitunga wimbo wenye kichwa “Kutamani Sana Mlipuko wa Nyuklia.” Kwa kuongezea, kulikuwa na uhakikisho wa waziri wa serikali ambaye alisema kwamba jaribio hilo lilifaulu kabisa na kwamba hakungekuwa na hatari ya mnururisho kwa mtu yeyote katika Australia. Lakini miaka kadhaa baadaye, zile tabasamu zilitoweka usoni mwa wale waliokuwa wakifa kutokana na kufunuliwa kwa mnururisho, kisha madai mengi sana ya kutaka kulipwa ridhaa yakafuata. Hakuna mtu aliyekuwa ‘Akitamani Sana Mlipuko wa Nyuklia’ sasa! Maralinga ingali eneo ambalo watu hawaruhusiwi kwenda kwa sababu ya uchafuzi wa mnururisho.
Maono ya Marekani ya majaribio ya bomu la atomi huko Nevada pia yanafanana na hiyo. Wengine huhisi kwamba kinachohusika ni suala la kisiasa wala si kosa la kisayansi. Robert Oppenheimer, ambaye alikuwa msimamizi wa kutengenezwa kwa bomu la Marekani la kwanza la atomu, katika Los Alamos, New Mexico, alisema: “Si daraka la mwanasayansi kuamua kama bomu la hidrojeni linapasa kutumiwa. Hilo ni daraka la watu wa Marekani na wawakilishi wao waliochaguliwa.”
Msiba wa Aina Nyingine
Matumizi ya damu katika tiba yakawa zoea baada ya Vita ya Ulimwengu ya Pili. Sayansi iliisifu kuwa kiokoa-uhai na kutangaza kwamba ni salama kuitumia. Lakini kuibuka kwa UKIMWI kukazindua ulimwengu wa tiba. Kwa ghafula, ule umajimaji uliosemekana kwamba ulikuwa wenye kuokoa uhai ukageuka kuwa muuaji kwa wengine. Msimamizi mmoja wa hospitali moja kubwa ya Sydney, Australia, aliambia Amkeni!: “Kwa miongo mingi tumeingiza mwilini kitu ambacho hatukujua mengi kukihusu. Hata hatukujua baadhi ya maradhi ambayo kilibeba. Ni nini kingine tunachoingizia watu mwilini, hatujui bado kwa sababu hatuwezi kupima kitu ambacho hatukijui.”
Kisa chenye msiba hasa kilihusu matumizi ya homoni za ukuzi katika kutibu wanawake walio tasa. Wakitazamia kupata uradhi mkubwa zaidi maishani kwa kupata mtoto, wanawake hao waliona tiba hii kuwa yenye kunufaisha sana. Miaka fulani baadaye, baadhi yao walikufa kutokana na hali zisizoeleweka kwa maradhi yaitwayo Creutzfeldt-Jakob (CJD) yenye kuharibu ubongo. Watoto waliotibiwa kwa homoni iyo hiyo kwa sababu ya kutoweza kukua walianza kufa. Watafiti waligundua kwamba wanasayansi walikuwa wamepata homoni hizo katika matezi ya pituitaria ya wafu. Baadhi ya maiti hizo zaonekana zilikuwa zina virusi vya CJD, na matungo ya homoni yakaambukizwa. Jambo lenye kuhuzunisha hata zaidi ni kwamba baadhi ya wanawake waliotibiwa kwa hiyo homoni wakawa wenye kuchanga damu kabla ya dalili za CJD kuonekana. Kuna hofu za kwamba virusi hivyo huenda sasa vipo katika akiba za damu, kwa kuwa hakuna njia iwezekanayo ya kupima damu ili kuvigundua.
Sayansi yote huhusisha kujasiria kwa kiasi fulani. Basi, si ajabu kwamba kama kitabu The Unnatural Nature of Science kisemavyo, sayansi “yaonwa kwa mchanganyiko wa kusifiwa na kuhofiwa, kwa tumaini na kwa kukata tumaini, inaonwa kuwa chanzo cha matatizo mengi ya leo yaliyotokezwa na jamii ya kisasa ya kiviwanda na vilevile kuwa chanzo kitakachotokeza suluhisho la matatizo mengi yajayo.”
Lakini tunaweza kupunguzaje kujihatarisha kibinafsi? Tunaweza kudumishaje maoni yenye usawaziko juu ya sayansi? Makala ifuatayo itakuwa yenye msaada.
[Maelezo ya Chini]
a Hiyo Agent Orange ni dawa ya kuua magugu ambayo ilitumiwa katika vita ya Vietnam ili kuondoa majani ya miti ya maeneo ya msitu.
[Blabu katika ukurasa wa 6]
Waziri wa serikali alisema kwamba hakungekuwa na hatari ya mnururisho
[Blabu katika ukurasa wa 7]
Mahali pa majaribio pa Maralinga pamechafuliwa na mnururisho
[Blabu katika ukurasa wa 8]
“Si daraka la mwanasayansi kuamua kama bomu la hidrojeni linapasa kutumiwa.”—Robert Oppenheimer, mwanasayansi wa atomu
[Hisani]
Hulton-Deutsch Collection/Corbis
[Picha katika ukurasa wa 9]
“Kwa mambo machungu tuliyojionea tumejifunza kwamba kufikiri kuzuri hakutoshi kusuluhisha matatizo ya maisha yetu ya kijamii.”—Albert Einstein, mwanafizikia
[Hisani]
Picha ya U.S. National Archives
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 5]
Richard T. Nowitz/Corbis
[Picha katika ukurasa wa 8, 9 zimeandaliwa na]
Picha ya USAF