Sehemu ya Kwanza
Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
“MTAIFAHAMU kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.” (Yohana 8:32) Maneno hayo ya hekima yanayonukuliwa mara kwa mara yalisemwa na mtu ambaye mamilioni humwona kuwa yule mtu mkuu zaidi aliyepata kuishi.a Ingawa msemaji huyo alikuwa anarejezea kweli ya kidini, katika njia fulani kweli katika uwanja wowote wa utendaji yaweza kuweka watu huru.
Kwa mfano, kweli ya kisayansi imeweka watu huru na mawazo mengi ya uwongo, kama vile kwamba dunia ni tambarare, kwamba dunia ndiyo kitovu cha ulimwengu wote mzima, kwamba joto ni umaji-maji uitwao kaloriki, kwamba hewa chafu huleta magonjwa, na kwamba atomu ndio sehemu ya mata iliyo ndogo zaidi. Utumizi halisi wa kweli ya kisayansi katika biashara, kutia na katika nyanja za uwasiliano na usafiri, umeweka watu huru na kazi nzito isiyo ya lazima na, kwa kadiri fulani, na mipaka ya wakati na umbali. Kweli ya kisayansi inayotumiwa katika dawa za kuzuia magonjwa na matibabu imesaidia kuweka watu huru na kifo cha mapema au mawazo ya kuhofu magonjwa.
Sayansi—Hiyo ni Nini?
Kulingana na The World Book Encyclopedia, “sayansi inatia ndani uwanja mkubwa wa maarifa ya kibinadamu unaohusu mambo hakika yanayoshikamanishwa na kanuni (sheria).” Kwa kueleweka, kuna aina tofauti za sayansi. Kitabu The Scientist chadai: “Kinadharia, karibu kila aina ya maarifa yaweza kufanywa iwe ya kisayansi, kwa kuwa fasili ya sehemu fulani ya maarifa huwa sayansi inapochunguzwa kwa njia ya kisayansi.”
Hilo hutokeza ugumu katika kufasili, kwa usahihi wowote, mahali ambapo sayansi moja huanza na nyingine huishia. Kwa kweli, kulingana na The World Book Encyclopedia, “katika visa fulani, sayansi mbalimbali zaweza kufanana sana hivi kwamba nyanja zinazofanana zimeanzishwa ambazo zinaunganisha sehemu za sayansi mbili au zaidi.” Hata hivyo, vitabu vingi vya marejezo husema juu ya sehemu nne kuu: sayansi za asili, sayansi za biolojia, sayansi za jamii, na sayansi ya hisabati na kutoa sababu.
Eti hisabati ni sayansi? Ndiyo, bila njia fulani moja ya kupimia, njia fulani ya kujua kadiri ya ukubwa, udogo, wingi, uchache, umbali, ukaribu, joto, na baridi, utafiti wa kisayansi wenye matokeo haungewezekana. Kwa sababu hiyo, hisabati imeitwa “Malkia na Mtumishi wa Sayansi Mbalimbali.”
Kuhusu sayansi za asilia, hizo zinatia ndani kemia, fizikia, na astronomia. Sayansi kuu za biolojia ni botania na zuolojia, ilhali sayansi za jamii zinatia ndani anthropolojia, sosholojia, Ikonomia, sayansi ya siasa, na saikolojia. (Ona sanduku ukurasa 8.)
Ni lazima tofauti ifanywe kati ya sayansi halisi na sayansi-tumizi. Sayansi halisi hushughulika hasa na mambo hakika na kanuni zenyewe za kisayansi; sayansi-tumizi, hushughulika na utumizi halisi. Leo sayansi-tumizi huitwa pia tekinolojia.
Kujifunza kwa Kujaribu na Kukosea
Dini na sayansi ni mifano miwili ya tamaa ya ainabinadamu kujua kweli. Lakini kuna tofauti kubwa kati ya jinsi kweli ya kidini inavyotafutwa kutoka chanzo kimoja na jinsi kweli ya kisayansi inavyotafutwa kutoka chanzo kingine. Labda mtafutaji wa kweli ya kidini atatumia Biblia Takatifu, Korani, Talmudi, Vedas, au Tripitaka, ikitegemea ikiwa yeye ni Mkristo, Mwislamu, Myahudi, Mhindu, au Mbuddha. Humo atapata kile kinachoonwa na dini yake kuwa ufunuo wa kweli ya kidini, labda ikitoka kwa chanzo cha kimungu na hivyo ikionwa kuwa mamlaka kamili.
Hata hivyo, mtafutaji wa kweli ya kisayansi hana mamlaka kamili kama hiyo ambayo anaweza kutumia—si kitabu wala mtu fulani. Kweli ya kisayansi haifunuliwi; inavumbuliwa. Hiyo hufanya kuwe mfumo wa kujaribu na kukosea, huku mtafutaji wa kweli ya kisayansi akikosa kufanikiwa mara nyingi. Lakini kwa kufuata hatua nne kwa utaratibu, yeye afanya utafutaji wenye mafanikio. (Ona sanduku “Kupata Kweli kwa Njia ya Kisayansi.”) Hata hivyo, ushindi wa kisayansi husherehekewa baada ya kukosa kufanikiwa kisayansi huku maoni yaliyokuwa yamekubaliwa mwanzoni yanapokataliwa na yale mapya yanayoonwa kuwa sahihi zaidi yanapokubaliwa.
Kujapokuwa njia hiyo ya kujaribu na kukosea, wanasayansi wamepata kiasi kikubwa ajabu cha maarifa ya kisayansi kwa muda wa karne zilizopita. Ingawa mara nyingi wanakosea, wameweza kusahihisha maamuzi mengi yasiyo sahihi kabla ya hasara kubwa kufanywa. Kwa kweli, maadamu maarifa yasiyo sahihi yanadumu katika uwanja wa sayansi halisi, hakuna hatari kubwa ya kufanya madhara makubwa. Lakini majaribio yanapofanywa ili kubadili sayansi halisi yenye makosa makubwa kuwa sayansi-tumizi, matokeo yaweza kuwa ya msiba.
Chukua kwa mfano, maarifa ya kisayansi yaliyowezesha kufanyizwa kwa dawa za kuua wadudu. Hayo yalithaminiwa sana hadi utafiti zaidi wa kisayansi ulipofunua kwamba baadhi yazo huacha mabaki yanayodhuru afya ya kibinadamu. Katika jumuiya fulani karibu na bahari ya Aral, zilizo katika Uzbekistan na Kazakhstan, uhusiano umethibitishwa kati ya utumizi mwingi wa dawa hizo za wadudu na kadiri ya kansa ya koromeo iliyo mara saba zaidi ya ile ya wastani wa kitaifa.
Kwa sababu ya manufaa zilizopatikana, erosoli (bidhaa zinazoshindiliwa katika mkebe) zilipendwa na wengi—hadi uchunguzi wa kisayansi ulipodokeza kwamba zilikuwa zikichangia uharibifu wa tabaka ya ozoni inayolinda dunia, kwa kweli kwa upesi zaidi, kuliko vile ilivyofikiriwa hapo mwanzoni. Kwa hiyo, jitihada ya kutafuta kweli ya kisayansi ni jambo linaloendelea. “Kweli” ya kisayansi ya leo huenda kesho ikawa mawazo yenye makosa, na hata yenye hatari.
Sababu kwa Nini Sayansi Yapaswa Itupendeze
Sayansi na tekinolojia zimefanya mengi katika kujenga muundo wa ulimwengu wetu wa kisasa. Frederick Seitz, aliyekuwa msimamizi wa Chuo cha Kitaifa cha Sayansi cha U.S. alisema: “Sayansi, ambayo ilianza kwa msingi ikiwa msisimko wa akili, sasa inakuwa mojawapo nguzo muhimu katika njia yetu ya maisha.” Hivyo, utafiti wa kisayansi leo umefungamanishwa na maendeleo. Mtu yeyote anayeshuku uvumbuzi wa kisayansi wa hivi karibuni anajihatirisha kuitwa “adui wa maendeleo.” Kwa vyovyote, yale ambayo wengine huita maendeleo ya kisayansi huonwa kuwa yanatofautisha watu walioendelea na wale wasioendelea.
Basi haishangazi kwamba mtunga mashairi Mwingereza wa karne ya 20 W. H. Auden alionelea hivi: “Wanaume halisi wenye kutenda katika wakati wetu, wale wanaobadili ulimwengu, si wanasiasa na wakuu, bali wanasayansi.”
Ni watu wachache wanaoweza kukana kwamba ulimwengu unahitaji mabadiliko. Lakini je, sayansi inaweza kufanya hivyo? Je! hiyo yaweza kuvumbua kweli ya kisayansi inayohitajiwa ili kuwezana na matatizo ya kipekee yanayozushwa na karne ya 21? Na je, kweli hiyo yaweza kuvumbuliwa upesi vya kutosha ili kuweka wanadamu huru na hofu ya msiba wa tufeni pote unaokaribia?
Mshindi wa tuzo la Nobeli mara mbili Linus Pauling alisema: “Kila mtu anayeishi ulimwenguni ahitaji kupata ufahamu juu ya asili na matokeo ya sayansi.” Ni kwa kusudi la kuandalia wasomaji wetu baadhi ya ufahamu unaohitajiwa kwamba tunatoa mfululizo “Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli.” Hakikisha kusoma Sehemu ya 2, katika toleo letu linalokuja.
[Maelezo ya Chini]
a Kristo Yesu. Ona kitabu Yule Mtu Mkuu Zaidi Aliyepata Kuishi, kilichotangazwa katika 1991 na Watchtower Bible and Tract Society of New York, Inc.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 7]
KUPATA KWELI KWA NJIA YA KISAYANSI
1. Chunguza yale yanayotukia.
2. Ikitegemea uchunguzi huo, fanyiza nadharia juu ya jambo linaloweza kuwa la kweli.
3. Tahini nadharia hiyo kwa uchunguzi zaidi na kwa majaribio.
4. Tazama uone ikiwa utabiri mbalimbali uliotegemea nadharia hiyo umetimizwa.
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 8]
SAYANSI ZAFASILIWA
ANTHROPOLOJIA ni masomo juu ya binadamu kama wanavyoonwa kibiolojia, kijamii, na kitamaduni.
ASTRONOMIA ni masomo juu ya nyota, sayari, na vitu vingine vya asili angani.
BIOLOJIA ni masomo juu ya jinsi vitu vilivyo hai hufanya kazi na kutofautishwa kwa mimea na wanyama
BOTANIA, ambayo ni mojayapo sehemu kuu mbili za biolojia, ni masomo juu ya uhai wa mimea.
FIZIKIA ni masomo juu ya nguvu na vitu kama vile nuru, sauti, kanieneo, na nguvu za uvutano.
HISABATI ni masomo juu ya nambari, wingi, maumbo, na mahusiano.
KEMIA ni masomo juu ya tabia na muundo wa vitu na jinsi vinavyoitikiana.
SAIKOLOJIA ni masomo juu ya akili ya kibinadamu na sababu za tabia ya kibinadamu.
ZUOLOJIA, ambayo ni sehemu kuu ya pili ya biolojia, ni masomo juu ya uhai wa wanyama.yyy