Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 4/22 kur. 21-23
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mzuolojia wa Kwanza Atangulia
  • Babuloni Ipo Kila Mahali
  • Kuendelea Hatua kwa Hatua
  • Naam, Wagiriki Hao Waliopo Kila Mahali
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Waweza Kuitumaini Sayansi Kadiri Gani?
    Amkeni!—1998
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 4/22 kur. 21-23

Sehemu ya 2

Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Jitihada ya Kutafuta Yaanza

“HAKUNA mtu ajuaye ni nani aliyekuwa wa kwanza kugundua moto, kuvumbua gurudumu, kutengeneza uta na mshale, au kujaribu kueleza macheo na machweo ya jua,” yasema The World Book Encyclopedia. Lakini ziligunduliwa, zikavumbuliwa, zikatengenezwa, na kuelezwa, na tokea wakati huo, ulimwengu haujapata kuwa kama ulivyokuwa.

Matimizo hayo yalikuwa hatua za mapema katika safari ya jitihada ya kutafuta kweli ambayo kufikia sasa imechukua karibu miaka elfu sita. Wanadamu wamekuwa wadadisi sikuzote, wakitaka kuelewa viumbe hai na visivyo hai katika ulimwengu unaowazunguka. Pia wametaka kutumia yale wanayojifunza, wakiyatumia kwa njia inayotumika ili kujinufaisha. Kiu hiyo ya kindani ya maarifa na tamaa ya kuitumia zimekuwa vichocheo vikubwa katika jitihada inayoendelea ya ainabinadamu ya kutafuta kweli ya kisayansi.

Bila shaka, jitihada hizo za kwanza za kutumia maarifa ya kisayansi kwa njia inayotumika hazikuitwa tekinolojia, kama inavyoitwa leo. Kwa habari hiyo, hata wale watu mmoja mmoja waliofanya majaribu hayo hawakuitwa wanasayansi. Kwa hakika, sayansi katika umaana wayo wa kisasa hata haikuwapo kwa sehemu kubwa ya kuwapo kwa ainabinadamu. Baadaye sana kama karne ya 14, wakati mshairi Mwingereza Chaucer alipotumia neno “sayansi,” yeye alimaanisha tu aina tofauti-tofauti za maarifa. Hilo lilipatana na asili ya neno hilo, ambalo chanzo chalo ni neno la Kilatini linalomaanisha “kujua.”

Mzuolojia wa Kwanza Atangulia

Hata iwe sayansi iliitwa nini awali, sayansi ilianza katika bustani ya Edeni mara tu binadamu walipoanza kuchunguza ulimwengu uliowazunguka. Hata kabla ya Hawa kuumbwa, Adamu alipewa utume wa kuwapa wanyama majina. Ili awape majina yanayofaa ilihitaji kwamba achunguze kwa uangalifu sifa zao na tabia zao. Leo, tunaita sayansi hiyo zuolojia.—Mwanzo 2:19.

Mwana wa kwanza wa Adamu na Hawa, Kaini, ‘alijenga mji,’ kwa hiyo ni lazima alikuwa na maarifa ya kisayansi ya kutosha kutengeneza vyombo vya kazi vilivyohitajiwa. Baadaye, mmoja wa uzao wake Tubal-kaini, aliitwa “mfua kila chombo cha kukatia, cha shaba na cha chuma.” Kufikia wakati huo, maarifa ya kisayansi na ya kitekinolojia kwa wazi ilikuwa imeongezeka.—Mwanzo 4:17-19, 22.

Kufikia wakati Misri ilikuja kuwa mamlaka kuu ya ulimwengu—ya kwanza kutajwa katika Biblia—maarifa ya kisayansi yalikuwa yameendelea kwa kiasi cha kwamba Wamisri waliweza kujenga piramidi kubwa-kubwa sana. Ubuni wa hizo piramidi, yasema The New Encyclopœdia Britannica, “uliwezekana baada tu ya majaribio mengi, ambayo yalihitaji matatizo makubwa ya uhandisi yasuluhishwe.” Kusuluhisha matatizo hayo kulihitaji maarifa mengi ya hesabu na kulionyesha stadi nyinginezo zilizohusiana za kisayansi.

Bila shaka, si Wamisri pekee waliokuwa na udadisi wa kisayansi. Wababuloni, kuongezea kuanzisha kalenda, walianzisha mifumo ya kuhesabu na kupima. Katika Mashariki ya Mbali, ustaarabu wa Wachina ulichangia sana mambo ya kisayansi. Na mababu wa mapema wa Wainka na Wamaya wa Amerika, walisitawisha ustaarabu ulioendelea sana ambao baadaye uliwagutusha wavumbuzi kutoka Ulaya, ambao hawakutarajia matimizo kama hayo kutoka kwa “wenyeji wasiostaarabika.”

Hata hivyo, si kila kitu watu hao wa kale waliona kuwa kweli ya kisayansi kilikuja kuwa sahihi kisayansi. The World Book Encyclopedia yatuambia kwamba pamoja na vyombo muhimu ambavyo Wababuloni walitokeza kwa ajili ya utafiti wa kisayansi, “walibuni pia sayansi ya ubandia ya unajimu.”a

Babuloni Ipo Kila Mahali

Kwa wanafunzi wa Biblia, Babuloni inashirikishwa na ibada bandia. Katika unajimu uliokuwa ukifanywa huko, mungu tofauti aliaminiwa kuwa anatawala kila sehemu ya mbingu. Biblia, inayofundisha kwamba kuna Mungu mmoja tu wa kweli, ni sahihi kisayansi inapokataa sayansi ya ubandia inayoitwa unajimu.—Kumbukumbu la Torati 18:10-12; 1 Wakorintho 8:6; 12:6; Waefeso 4:6.

Dini ilikuwa sehemu isiyotenganika ya binadamu wa mapema. Kwa hiyo, ni jambo linaloeleweka kwamba maarifa ya kisayansi hayakusitawi mbali na itikadi na mawazo ya kidini. Jambo hilo laweza kuonwa sanasana katika ulimwengu wa sayansi ya tiba.

“Hati za kale zinazoonyesha jumuiya ya Misri na dawa za tiba wakati wa Ufalme wa Zamani,” yasema The New Encyclopœdia Britannica, “zaonyesha kwamba uchawi na dini zilishirikiana pamoja bila kuachana na tiba isiyohusu sayansi na kwamba mganga mkuu wa jumba la farao mara nyingi pia alitumika akiwa tabibu mkuu.”

Katika utawala wa tatu wa Misri, mstadi wa ujenzi aliyeitwa Imhotep alipata umashuhuri akiwa tabibu stadi. Muda unaopungua karne moja baada ya kifo chake, aliabudiwa akiwa mungu wa dawa wa Misri. Kufikia mwisho wa karne ya sita K.W.K., alikuwa amepandishwa cheo kuwa mungu mkuu. Britannica yasema kwamba mahekalu yaliyowekwa wakfu kwa ajili yake “mara nyingi yalijaa watu waliokuwa wakiteseka waliosali na kulala humo wakiamini kwamba mungu huyo atawafunulia tiba katika ndoto zao.”

Waponyaji wa Misri na wa Babuloni walishawishwa sana na mawazo ya kidini. “Nadharia ya maradhi iliyoenea wakati huo, na kwa vizazi vilivyofuata,” chasema The Book of Popular Science, “ilikuwa kwamba homa, maambukizo, maumivu, na uchungu yalisababishwa na roho waovu, au mashetani, waliovamia mwili.” Kwa sababu hiyo, utibabu sanasana ulihusu matoleo ya kidini, ulozi, au maneno ya uchawi.

Baadaye, katika karne ya nne na ya tano K.W.K., tabibu Mgiriki aliyeitwa Hipokrate alipinga maoni hayo. Yeye anajulikana sana hasa kwa ajili ya kile kiapo cha Hipokrate, ambacho bado huonwa kwa kawaida kuwa kina kanuni ya mwelekezo wa kitiba. Kitabu Moments of Discovery—The Origins of Science chaeleza kwamba Hipokrate alikuwa pia “miongoni mwa watu wa kwanza kushindana na makuhani katika kutafuta sababu ya ugonjwa wa binadamu.” Akitibu kwa njia ya sayansi, alitafuta sababu za asili zinazoleta maradhi. Kutoa sababu na ujuzi ukaanza kuchukua mahali pa ushirikina wa kidini na makisio.

Katika kutenganisha tiba na ushupavu wa kidini, Hipokrate alichukua hatua ya kuelekea upande ufaao. Hata hivyo, hata leo tunakumbushwa juu ya chanzo cha kidini cha tiba. Ishara yayo yenyewe, ufito wa Asklepio wenye kupindwa na nyoka, mungu wa Kigiriki wa tiba, yaweza kufuatiwa mpaka kwenye mahekalu ya kale ya kutibu ambapo nyoka watakatifu waliwekwa. Kulingana na The Encyclopedia of Religion, nyoka hao walikuwa na “uwezo wa kurudiwa upya kwa uhai na kuzaliwa tena katika afya.”

Baadaye Hipokrate alikuja kujulikana kuwa mwanzilishi wa tiba. Lakini jambo hilo halikumfanya asikosee kisayansi nyakati nyingine. The Book of Popular Science chatueleza kwamba baadhi ya mawazo yake yenye makosa “leo yanatushangaza sana” lakini chatahadharisha dhidi ya upumbavu wa kitiba, kinaposema hivi: “Baadhi ya nadharia za kitiba ambazo ni thabiti sana sasa huenda baadaye zikashangaza sana watu wa kizazi cha wakati ujao.”

Kuendelea Hatua kwa Hatua

Hivyo, kuvumbua kweli ya kisayansi kumekuwa mwendo wa hatua kwa hatua, kukitia ndani kuchagua mambo ya hakika kutokana na nadharia zisizo za kweli kwa muda wa karne nyingi. Lakini ili jambo hilo liwezekane, magunduzi ya kizazi kimoja yalihitaji kupitishwa kwa kizazi kilichofuata kwa usahihi. Kwa wazi, njia moja ya kufanya hivyo ilikuwa ni kwa neno la mdomo, kwa sababu wanadamu waliumbwa na uwezo wa usemi.—Linganisha Mwanzo 2:23.

Hata hivyo, njia hiyo ya kupitishia uchunguzi, haingeweza kutegemeka sana katika kuandaa usahihi ambao maendeleo ya kisayansi na ya kitekinolojia yanahitaji. Kulikuwa na uhitaji wa wazi wa kuhifadhi habari kwa namna ya maandishi.

Haijulikani ni lini hasa wanadamu walipoanza kuandika. Lakini walipoanza, walikuwa na mfumo bora sana wa kupitishia habari ambayo wengine wangeweza kutumia. Kabla ya karatasi kuvumbuliwa—labda katika Uchina karibu 105 W.K.— uandikaji ulifanywa kwa mabamba ya udongo, mafunjo, na ngozi.

Maendeleo makubwa ya kisayansi hayangewezekana bila mifumo ya kuhesabu na kupima. Kusitawishwa kwayo ni kwa umaana mkubwa sana. Kikiita matumizi ya hesabu kuwa “ya ulimwenguni pote,” The Book of Popular Science chatukumbusha kwamba “machunguzo yayo yameongoza kwa maendeleo makubwa ya kisayansi.” Hesabu hutumika pia “kuwa chombo muhimu kwa mkemia, mfizikia, mwastronomia, mhandisi na wengine.”

Kwa karne ambazo zimepita, mambo mengine yameongezea nguvu ile jitihada ya kutafuta kweli ya kisayansi. Kwa mfano usafiri. The Book of Popular Science chaeleza: “Mtu anayeenda nchi za kigeni aelekea kupata udadisi wake ukiamshwa kwa kuona vitu vipya, sauti, harufu na ladha. Atashawishwa aulize mbona vitu ni tofauti sana katika nchi hiyo ya kigeni; na katika jitihada yake ya kutosheleza udadisi wake, atapata hekima. Ndivyo ilivyokuwa na Wagiriki wa kale.”

Naam, Wagiriki Hao Waliopo Kila Mahali

Soma historia ya dini, siasa, au biashara na utapata mengi zaidi juu ya Wagiriki. Na ni nani ambaye hajasikia juu ya wanafalsafa wao mashuhuri, neno linalotokana na neno la Kigiriki phi.lo.so.phiʹa, linalomaanisha “upendo wa hekima”? Upendo wa hekima wa Wagiriki na kiu yao ya maarifa ulijulikana sana katika karne ya kwanza wakati mtume Mkristo Paulo alipozuru nchi yao. Alirejezea wanafalsafa Waepikureo na Wastoiko, ambao kama ilivyokuwa na “Waathene na wageni waliokaa huko walikuwa hawana nafasi kwa neno lo lote ila kutoa habari na kusikiliza habari za jambo jipya.”—Matendo 17:18-21.

Kwa hiyo haishangazi kwamba kati ya watu wote wa kale, Wagiriki walichangia sana sayansi. The New Encyclopœdia Britannica chafafanua hivi: “Jitihada ya falsafa ya Kigiriki ya kuandaa nadharia ya ulimwengu wote mzima kuchukua mahali pa hekaya za elimu za ulimwengu wote mzima hatimaye iliongoza kwa mavumbuzi halisi ya kisayansi.”

Kwa kweli, baadhi ya wanafalsafa Wagiriki walichangia sana ile jitihada ya kutafuta kweli ya kisayansi. Walijitahidi kuondoa mawazo na nadharia zenye makosa za wale waliowatangulia, na wakati uo huo wakijenga juu ya msingi wa zile walizopata kuwa kweli. (Ona mifano katika sanduku) Hivyo, wanafalsafa Wagiriki wa wakati uliopita walikaribia zaidi kufikiri kama wanasayansi wa leo kushinda watu wengineo wote wa kale. Kwa kutukia tu, ilikuwa ni hivi karibuni kwamba maneno “falsafa ya asili” yalitumiwa kueleza sehemu mbalimbali za sayansi.

Baadaye, Ugiriki yenye kupenda falsafa ilishindwa kisiasa na ile Milki ya Warumi iliyotoka kuanzishwa. Je! jambo hilo liliathiri kwa vyovyote maendeleo ya kisayansi? Au kuja kwa Ukristo kungebadili mambo? Sehemu ya 3 katika toleo litakalofuata itatoa majibu.

[Maelezo ya Chini]

a Unajimu, masomo ya mienendo ya vitu vya angani kwa kuamini kwamba vinaathiri maisha za watu au kutabiri wakati ujao, usichukuliwe kimakosa kuwa astronomia, ambayo ni masomo ya kisayansi ya nyota, sayari, na vitu vingine vya asili vilivyoko angani bila kutia ndani mambo yoyote ya uwasiliani-roho.

[Sanduku katika ukurasa wa 22]

“Wanasayansi” Wagiriki wa Kabla ya Ukristo

THELO wa Mileto (karne ya sita), alijulikana hasa kwa kazi yake ya hesabu na kwa imani yake kwamba maji hufanyiza asili ya mata, alikuwa na maoni ya kuchambua nadharia ya ulimwengu wote mzima ambao unatajwa na The New Encyclopœdia Britannica kuwa “muhimu sana katika ukuzi wa mawazo ya kisayansi.”

Sokrate (karne ya tano) aitwa na The Book of Popular Science “mwanzilishi wa njia ya uchunguzi—kimahoji—inayokaribia kufanana sana na njia ya kweli ya kisayansi.”

Demokrato wa Abdera (karne ya tano hadi ya nne) alisaidia kuweka msingi wa nadharia ya atomu ya ulimwengu wote mzima na vilevile nadharia za kutoweza kuharibika kwa mata, na hifadhi ya nishati.

Plato (karne ya tano hadi ya nne) alianzisha Chuo katika Athene kikiwa chuo cha kutafiti kwa utaratibu mambo ya kifalsafa na kisayansi.

Aristotlo (karne ya nne), mwanabiyolojia mwenye maarifa, alianzisha ile Lyceum, chuo cha kisayansi kilichofanya utafiti katika nyanja nyingi. Kwa zaidi ya miaka 1,500, maoni yake yalijaa sana katika mawazo ya kisayansi, naye alionwa kuwa mamlaka kuu katika mambo ya kisayansi.

Euklidi (karne ya nne), aliyekuwa mwanahesabu mashuhuri zaidi wa nyakati za kale, anajulikana zaidi kwa kukusanya maarifa ya jiometria, neno la Kigiriki linalomaanisha “kipimo cha ardhi.”

Hiparko wa Nikaya (karne ya pili), mwastronomia mwenye kutokeza sana na mwanzilishi wa trigonometria, aliorodhesha nyota katika vikundi kulingana na uangavu, mfumo ambao kwa msingi bado unatumiwa. Alikuwa mtangulizi wa Ptolemy, mwanajiografia na mwastronomia mashuhuri wa karne ya pili W.K., aliyepanua magunduzi ya Hiparko na kufundisha kwamba dunia ilikuwa ndiyo kitovu cha ulimwengu wote mzima.

[Picha katika ukurasa wa 23]

Ule ufito wa Asklepio wenye kupindwa na nyoka, kikumbusho kwamba sayansi haikusitawi bila uvutano wa kidiniyy

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki