Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 5/8 kur. 18-21
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Ulaya ya “Kikristo” Yapoteza Uongozi Wayo
  • Maendeleo ya Kisayansi
  • Urahisisho wa Hesabu ya Kiarabu
  • Kuamsha Kupendezwa Tena Katika Ulaya
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Jinsi Kiarabu Kilivyokuja Kuwa Lugha ya Wasomi
    Amkeni!—2012
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 5/8 kur. 18-21

Sehemu ya 3

Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Dini na Sayansi—Mchanganyiko Mbovu

MAELFU ya miaka ya kutafuta kweli ya kisayansi yaonekana yalikuwa yameweka msingi thabiti kwa utafiti ambao ungefuata. Kwa kweli hakuna kitu kingezuia maendeleo zaidi. Na bado The Book of Popular Science chasema, “sayansi ilifanya vibaya sana katika karne ya tatu, ya nne, na ya tano W.K.”

Matukio mawili yalichangia sana hali hiyo. Wakati wa karne ya kwanza, enzi mpya ya kidini ilikuwa imeletwa na Yesu Kristo. Na miongo mingi ya miaka iliyotangulia, katika 31 K.W.K., enzi mpya ya kisiasa ilikuwa imeanza kwa kusimamishwa kwa Milki ya Warumi.

Wakiwa tofauti na wanafalsafa Wagiriki waliowatangulia, Warumi “walipendezwa hasa na kusuluhisha matatizo ya kila siku kuliko kupendezwa na kweli inayowaziwa tu,” chasema kitabu cha marejezo kilichotajwa hapo juu. Kwa wazi basi, “mchango wao kwa sayansi-halisi ulikuwa mdogo sana.”

Hata hivyo, Warumi walichangia sana kupitisha maarifa ya kisayansi yaliyokuwa yamejulikana kufikia wakati huo. Kwa mfano, Pliny Mkubwa, alikusanya mambo ya kisayansi wakati wa karne ya kwanza katika kitabu kilichoitwa Natural History. Ingawa kilikuwa na makosa-makosa, kilihifadhi aina mbalimbali za habari za kisayansi ambazo labda hazingepatwa na vizazi vilivyofuata.

Kwa habari ya dini, kundi la Kikristo lenye kupanuka kwa kasi halikujihusisha katika utafutaji wa kisayansi wa wakati huo. Si kwamba Wakristo waliupinga utafutaji huo, bali jambo kuu kwa Wakristo, kama lilivyoelezwa na Kristo mwenyewe, kwa wazi lilikuwa ni kuelewa na kueneza kweli ya kidini.—Mathayo 6:33; 28:19, 20.

Kabla ya mwisho wa karne ya kwanza, Wakristo waasi-imani walikuwa tayari wameanza kupotosha kweli ya kidini waliokuwa wamepewa waieneze. Baadaye jambo hilo liliwafanya watokeze namna ya Ukristo wenye uasi-imani, kama ilivyokuwa imetabiriwa. (Matendo 20:30; 2 Wathesalonike 2:3; 1 Timotheo 4:1) Matukio yaliyofuata yalionyesha kwamba kukataa kwao kweli ya kidini kuliandamana na mwelekeo wa kutojali—wakati mwingine hata kupinga—ile kweli ya kisayansi.

Ulaya ya “Kikristo” Yapoteza Uongozi Wayo

The World Book Encyclopedia yaeleza kwamba wakati wa Enzi za Katikati (kutoka karne ya 5 hadi 15), “wanachuo katika Ulaya walipendezwa zaidi na theolojia, au masomo ya dini, kuliko masomo ya asili.” Na “mkazo huo wa wokovu badala ya kuchunguza asili,” Collier’s Encyclopedia yaelezea, “ulikuwa sana-sana kizuizi badala ya kuwa kichocheo kwa sayansi.”

Mafundisho ya Kristo hayakukusudiwa yatumike kuwa kizuizi kama hicho. Lakini, mawazo bandia ya kidini yanayotatanisha ya Jumuiya ya Wakristo, kutia ndani kukazia kupita kiasi wokovu wa ile inayodhaniwa kuwa nafsi isiyoweza kufa, yaliendeleza kizuizi hicho. Masomo mengi yalidhibitiwa na kanisa na yalifanywa sana-sana katika nyumba za watawa. Mwelekeo huo wa kidini ulipunguza mwendo wa jitihada ya kutafuta kweli ya kisayansi.

Mambo ya kisayansi yalichukua nafasi ya pili yakilinganishwa na theolojia tokea mwanzo kabisa wa Wakati wa Kawaida Wetu. Kwa kweli, maendeleo pekee ya kisayansi yanayoweza kutajwa yalikuwa katika uwanja wa tiba. Kwa mfano, mwandikaji wa tiba Mrumi Aulus Celsus wa karne ya kwanza W.K., aliyeitwa “Hipokrato wa Warumi,” aliandika kile kinachoonwa kuwa kitabu bora cha kitiba. Mfanyiza-dawa Mgiriki Pedanius Dioscorides, aliyekuwa daktari-mpasuaji katika majeshi ya Warumi ya Nero, alikamilisha kitabu bora sana cha maelezo ya kufanyiza dawa kilichotumiwa sana kwa karne nyingi. Galen, Mgiriki wa karne ya pili, kwa kuanzisha fiziolojia (elimu ya mwili) ya majaribio, alivutia elimu na matumizi ya tiba ya kutokea wakati wake kufikia Enzi za Katikati.

Kipindi cha kukwama kwa sayansi kiliendelea hata baada ya karne ya 15. Ni kweli, wanasayansi wa Ulaya walivumbua vitu wakati huo, lakini kwa sehemu kubwa vilikuwa vimejulikana awali. Gazeti Time lasema: “[Wachina] walikuwa ndio mabwana wa sayansi ulimwenguni. Muda mrefu kabla ya Wazungu, tayari walikuwa wamejua jinsi ya kutumia dira, kutengeneza karatasi na baruti, [na] kupiga chapa kwa chapa zenye kusonga.”

Hivyo, kwa sababu ya ukosefu wa mawazo ya kisayansi katika Ulaya ya “Kikristo,” tamaduni zisizo za Kikristo zikachukua uongozi.

Maendeleo ya Kisayansi

Kufikia karne ya tisa, wanasayansi Waarabu walikuwa wanainuka kwa kasi kuwa mabwana wa sayansi. Hasa katika karne za 10 na 11—wakati Jumuiya ya Wakristo ilipotenda bila maendeleo—hao walifurahia enzi bora sana ya matimizo mengi. Walitoa mchango mkubwa kwa tiba, kemia, botania, fizikia, astronomia, na zaidi ya yote, hesabu. (Ona sanduku, ukurasa 20.) Maan Z. Madina, profesa mshirika wa lugha ya Kiarabu katika Chuo Kikuu cha Columbia, asema kwamba “trigonometria ya kisasa pamoja na algebra na geometria kwa sehemu kubwa zimeanzishwa na Waarabu.”

Mengi ya maarifa hayo ya kisayansi hayakuwa yamejulikana awali. Lakini baadhi yayo yalitegemezwa kwa msingi mkubwa wa falsafa ya Kigiriki na, kwa kushangaza sana, yalitokezwa na kujihusisha kwa kidini.

Hapo awali katika Wakati wetu wa Kawaida, Jumuiya ya Wakristo ilienea ndani ya Uajemi na baadaye katika Arabia na India. Wakati wa karne ya tano, Nestorio, baba wa Konstantinopo, alijiingiza katika ubishi uliotokeza farakano katika kanisa la Mashariki. Jambo hilo lilitokeza kuanzishwa kwa kikundi kilichojitenga cha Wanestorio.

Katika karne ya saba, wakati dini mpya ya Uislamu ilipotokea ghafula ulimwenguni na kuanza kampeni yayo ya upanuzi, Wanestorio walifanya haraka kupitisha maarifa kwa Waarabu hao waliowashinda. Kulingana na Encyclopedia of Religion, “Wanestorio ndio waliokuwa wa kwanza kuendeleza sayansi na falsafa ya Kigiriki kwa kutafsiri maandishi ya Kigiriki katika Kisiria na kisha katika Kiarabu.” Pia walikuwa wa kwanza kuleta tiba za Kigiriki katika Baghdad.” Wanasayansi Waarabu walianza kujenga juu ya mambo waliyojifunza kutoka kwa Wanestorio. Kiarabu kikachukua mahali pa Kisiria kuwa lugha ya sayansi katika milki ya Uarabu nayo ikathibitika kuwa lugha iliyofaa kutumiwa kwa maandishi ya kisayansi.

Waarabu walipokea na pia kutoa maarifa. Wamoor walipoingia Ulaya kupitia Uhispania—wakakae kwa miaka zaidi ya 700—walikuja na utamaduni wenye elimu wa Kiislamu. Na wakati wa zile zilizoitwa eti Krusedi za Kikristo nane, kati ya 1096 na 1272, wanakrusedi wa Magharibi walivutiwa na maendeleo makubwa ya Kiislamu waliyoona. Walirudi, kama vile mwandikaji mmoja wa vitabu anavyosema wakiwa, na “mawazo mengi mapya.”

Urahisisho wa Hesabu ya Kiarabu

Mmojawapo michango mikubwa ambayo Waarabu walitolea Ulaya ulikuwa ni kuanzishwa kwa tarakimu za Kiarabu kuchukua mahali pa matumizi ya herufi za Kirumi. Kwa hakika maneno, “tarakimu za Kiarabu” hayafai. Maneno sahihi zaidi labda ni “tarakimu za Kihindu na Kiarabu.” Ni kweli, Mwarabu wa karne ya tisa aliyekuwa mtaalamu wa hesabu na astronomia, al-Khwārizmī, aliandika juu ya mfumo huo wa tarakimu, lakini alikuwa ameupata kutoka kwa wataalamu wa hesabu Wahindu wa India, walioufanyiza zaidi ya miaka elfu moja iliyokuwa imepita, katika karne ya tatu K.W.K.

Mfumo huo wa tarakimu haukujulikana katika Ulaya mpaka mtaalamu mashuhuri wa hesabu Leonardo Fibonacci (aitwaye pia Leornado wa Pisa) alipouanzisha katika 1202 katika Liber abaci (Kitabu cha Abacus). Akionyesha mafaa ya mfumo huo, alieleza: “Tarakimu tisa za Kihindi ni: 9 8 7 6 5 4 3 2 1. Kwa tarakimu hizi tisa pamoja na ishara 0 . . . nambari yoyote yaweza kuandikwa.” Mwanzoni Wazungu waliitikia polepole. Lakini kufikia mwisho wa Enzi za Katikati, walikuwa wamekubali mfumo huo mpya wa kuhesabu, na usahili wao ukaendeleza maendeleo ya kisayansi.

Ikiwa una shaka kwamba tarakimu za Kihindu na Kiarabu si rahisi zaidi ya taraki-mu za Kirumi zilizokuwa zikitumiwa hapo awali, ebu jaribu kuondoa LXXIX kutoka MCMXCIII. Je! umepigwa bumbuazi? Labda kuondoa 79 kutoka 1,993 kunaweza kuwa rahisi zaidi.

Kuamsha Kupendezwa Tena Katika Ulaya

Kuanzia na karne ya 12, tamaa kubwa ya masomo iliyowaka sana katika ulimwengu wa Waislamu ilianza kupoa. Hata hivyo, iliamshwa katika Ulaya wakati vikundi vya wanachuo walipoanza kuanzisha vyuo vikuu vya awali vilivyotangulia vya kisasa. Katikati ya karne ya 12, vyuo vikuu vya Paris na Oxford vilianzishwa. Chuo Kikuu cha Cambridge kikafuata mapema katika karne ya 13, na vile vya Prague na Heidelberg vyote viwili vikafuata katika karne ya 14. Kufikia karne ya 19, vyuo vikuu vilikuwa vimekuwa vitovu vikuu vya utafiti wa kisayansi.

Hapo mwanzoni, shule hizo zilikuwa na uvutano mkubwa sana wa dini, masomo mengi yakitegemea au kuegemea upande wa theolojia. Na kwa wakati uo huo, shule hizo zilikubali falsafa za Kigiriki, hasa maandishi ya Aristoto. Kulingana na Encyclopedia of Religion, “Mtindo wa masomo . . . kupitia Enzi za Katikati . . . ulifanyizwa kulingana na mawazo ya Aristoto ya kufasili, kugawanya, na kusababu katika kueleza andiko na kutatua mambo magumu.”

Mwanachuo mmoja wa karne ya 13 aliyeazimia kuchanganya mafunzo ya Aristoto na theolojia ya Kikristo alikuwa Thomas Aquinas, aliyeitwa baadaye “Aristoto Mkristo.” Lakini kwa mambo mengine alitofautiana na Aristoto. Kwa mfano, Aquinas alikataa nadharia ya kwamba ulimwengu umekuwapo nyakati zote, akikubaliana na Maandiko kwamba uliumbwa. Kwa “kushikilia imani kwamba ulimwengu wote mzima ni wenye utaratibu unaoweza kufahamika kwa kutoa sababu,” chasema The Book of Popular Science, “alitoa mchango mkubwa katika maendeleo ya sayansi ya kisasa.”

Hata hivyo, kwa sehemu kubwa, mafundisho ya Aristoto, Ptolemy, na Galen yalikubaliwa hata na kanisa kuwa kweli isiyoweza kukosea. Kitabu hicho cha marejezo kilichotajwa hapo juu chaeleza hivi: “Katika Enzi za Katikati, wakati kupendezwa kwa majaribio ya kisayansi na uchunguzi wa moja kwa moja ulipokuwa chini sana, neno la Aristoto lilikuwa sheria. Ipse dixit (‘yeye mwenyewe alisema’) ulikuwa ndio ubishi uliotumiwa na wanashule hao wa enzi za katikati ili kuthibitisha kweli ya machunguzi mengi ya ‘kisayansi.’ Chini ya hali hizo makosa ya Aristoto hasa katika fizikia na astronomia, yalikawiza maendeleo ya kisayansi kwa karne nyingi.”

Mmoja aliyepinga kushikilia bila akili maoni ya zamani alikuwa ni mtawa wa Oxford Roger Bacon. Akiitwa “mtu mashuhuri zaidi katika sayansi ya enzi ya katikati,” Bacon alikuwa karibu peke yake katika kupendekeza kujaribu mambo kuwa ndiyo njia ya kujifunza kweli za kisayansi. Inasemekana kwamba mapema kama 1269, kwa wazi karne nyingi mbele ya wakati wake, alitabiri kwamba kungekuwa na magari, eropleni, na meli zenye kuendeshwa kwa mitambo.

Hata ingawa alikuwa na uwezo wa kuona kimbele na akili nyingi, Bacon hakuwa na maarifa ya mambo ya hakika. Aliamini sana katika unajimu, uchawi, na alkimia. Jambo hilo lathibitisha kwamba sayansi kwa kweli ni jitihada inayoendelea ya kutafuta kweli, sikuzote ikihitaji kusahihishwa.

Ingawa ilionekana kwamba uchunguzi wa kisayansi ulipoa katika karne ya 14, wakati karne ya 15 ilipokaribia mwisho wayo, jitihada ya ainabinadamu ya kutafuta kweli ya kisayansi ilikuwa ingali inaendelea. Kwa kweli, miaka 500 iliyofuata ingepita kwa mbali sana yale yote yaliyotangulia. Ulimwengu ulifikia mwanzo wa mapinduzi makubwa ya kisayansi. Na kama ilivyo na mapinduzi mengine yoyote, haya pia yangekuwa na mashujaa wayo, mabaradhuli wayo, na zaidi ya yote, majeruhi wayo. Jifunze mengi zaidi katika Sehemu ya 4 ya “Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli” katika toleo letu linalokuja.

[Sanduku katika ukurasa wa 20]

Enzi Bora ya Sayansi ya Kiarabu

Al-Khwārizmī (karne za nane na tisa), mtaalamu wa hesabu na astronomia kutoka Iraq; ajulikana kwa kuanzisha neno “algebra,” kutokana na al-jebr, linalomaanisha katika Kiarabu “muungano wa vipande vilivyovunjika.”

Abū Mūsā Jābir ibn Ḥayyān (karne za nane na tisa), mwalkemia; anayeitwa baba ya kemia ya Kiarabu.

Al-Battānī (karne za tisa na kumi), mwastronomia na mtaalamu wa hesabu; alifanya hesabu za Ptolemy kuwa bora zaidi, hivyo akitambua kwa usahihi zaidi mambo kama vile urefu wa miaka na wa majira.

Ar-Rāzī (Rhazes) (karne za tisa na kumi), mmoja wa matabibu mashuhuri zaidi wa Uajemi; wa kwanza kutofautisha kati ya ugonjwa wa ndui na surua na kuainisha vitu vyote kuwa chini ya ama mnyama, mboga, ama madini.

Abū ‘Alī al-Ḥasan ibn al-Haytham (Alhazen) wa Basra (karne za 10 na 11), mtaalamu wa hesabu na fizikia; alitoa michango mikubwa kwa nadharia za elimu ya nuru, kutia ndani kugeuka njia kwa nuru, kurudishwa kwa nuru, kuona mara mbili, na kugeuzwa kwa hewa; wa kwanza kueleza kisahihi kwamba mwono ni matokeo ya nuru inayotoka kwa kitu kwenda kwenye jicho.

Omar Khayyám (karne za 11 na 12), mtaalamu Mwajemi aliyekuwa mashuhuri kwa hesabu, fizikia, astronomia, utibabu, na falsafa; ajulikana zaidi katika Magharibi kwa sababu ya mashairi yake.

[Picha katika ukurasa wa 18]

Aristoto (juu) na Plato (chini) walivuta sana kweli ya kisayansi kwa karne nyingi

[Hisani]

National Archeological Museum of Athens

Musei Capitolini, Romay

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki