Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 5/22 kur. 13-15
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Mabaradhuli Watia Giza ile Njia
  • Mabaradhuli Bado Wako
  • Ni Nani Wanaathiriwa?
  • Umeme Ukikatwa
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli
    Amkeni!—1993
  • Mageuzi Yajaribiwa
    Mnara wa Mlinzi Unaotangaza Ufalme wa Yehova—1994
  • Kitabu Chashangaza Ulimwengu
    Amkeni!—1995
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 5/22 kur. 13-15

Sehemu ya 4

Sayansi—Jitihada Inayoendelea ya Ainabinadamu ya Kutafuta Kweli

Kufufuliwa kwa Sayansi Kupitia Mapinduzi

MSUKOSUKO uliupata ulimwengu katika sehemu ya pili ya karne ya 18 wakati mapinduzi yalipobadili hali ya kisiasa, kwanza katika Amerika, kisha katika Ufaransa. Wakati uo huo, aina nyingine ya mapinduzi ilianza katika Uingereza, yale mapinduzi ya kiuchumi. Yalihusika sana na aina nyingine ya mapinduzi, yale ya kisayansi.

Wengine huona kufufuliwa kwa sayansi kuwa kulianza katika miaka ya 1540, wakati mwastronomia wa Polandi Nicolaus Copernicus na mwanatomia Mbelgiji Andreas Vesalius walipochapisha vitabu vilivyokuwa na uvutano sana juu ya mawazo ya kisayansi. Wengine huona badiliko hilo kuwa lilitokea mapema zaidi, katika 1452, wakati Leornado da Vinci alipozaliwa. Akiwa mchunguzi mwenye bidii aliyetoa michango mingi ya kisayansi, Leornado alisitawisha mawazo ambayo katika hali nyinginezo yalikuwa mwanzo wa uvumbuzi uliopata kukamilishwa karne za baadaye, kama vile eropleni, kifaru cha vita, na parachuti.

Lakini sayansi kama tunavyoijua sasa, asema Ernest Nagel, profesa aliyestaafu kutoka Chuo Kikuu cha Kolumbia, “haikuimarika ikiwa mpango wenye kuendelea katika jamii ya Magharibi mpaka wakati karne za kumi na saba na kumi na nane zilipofika.” Mara ilipoimarika, hatua kubwa ya mabadiliko katika historia ya binadamu ilikuwa imefikiwa. Chasema hivi kitabu The Scientist: “Katikati ya karibu 1590 na 1690 watu wengi wenye akili . . . walitokeza utafiti mwingi sana ambao haukufikiwa hata kidogo katika kipindi kingine chochote cha miaka 100.”

Mabaradhuli Watia Giza ile Njia

Sayansi za bandia zilisitawi pia, kama mabaradhuli ambao nadharia zao zilizuia maendeleo ya kweli ya kisayansi. Ile nadharia ya mwako ya flojistoni ilikuwa moja yayo. “Flojistoni,” kwa Kigiriki, linamaanisha “-ungua.” Nadharia hiyo ilianzishwa katika 1702 na George Ernst Stahl, aliyeamini kwamba flojistoni ni kitu kinachotoweka wakati vitu vinavyoweza kushika moto vinapoungua. Alidhani kwamba flojistoni ni kanuni badala ya kuwa kitu cha kweli, lakini imani ya kwamba ilikuwa ni kitu cha kweli ilisitawi katika miaka iliyofuata. Nadharia hiyo iliendelea mpaka miaka kati ya 1770 na 1790 wakati Antoine-Laurent Lavoisier alipotilia shaka nadharia hiyo.

The Book of Popular Science chakiri kwamba ingawa nadharia ya flojistoni “ilikosea sana, hata hivyo kwa wakati fulani iliandaa nadharia inayofanya kazi iliyoeleza kwa wazi sababu ya matukio mengi ya asili. Ilikuwa tu ni mojapo nadharia nyingi za sayansi ambayo imepimwa katika mizani na kuonekana kuwa imepungukiwa kwa muda wa miaka iliyopita.”

Alkemia ilikuwa baradhuli jingine. Kamusi Harrap’s Illustrated Dictionary of Science yaifasili kuwa “mchanganyiko wa falsafa, fumbo, na tekinolojia ya kemikali, iliyoanza kabla ya enzi ya Ukristo, ikitafuta kwa njia nyingi kubadili madini zisizo na thamani kubwa kuwa dhahabu, urefusho wa uhai na siri ya kutoweza kufa.” Kabla haijakataliwa, alkemia ilisaidia kuweka msingi wa kemia ya kisasa, badiliko lililomalizwa kufikia mwisho wa karne ya 17.

Kwa hiyo ingawa zilikuwa mabaradhuli, nadharia za flojistoni na alkemia zilikuwa na mafaa fulani. Lakini, haikuwa hivyo kwa mabaradhuli wa kibinadamu ambao kwa sababu ya imani za kidini waliendeleza mielekeo isiyo ya kisayansi. Upinzani kati ya sayansi na theolojia—zote mbili zikidai kuwa na mamlaka ya pekee katika masuala ya ulimwengu wote mzima—mara nyingi umeongoza kwenye mzozo wa moja kwa moja.

Kwa mfano, katika karne ya pili W.K., mwastronomia mashuhuri Ptolemy alibuni nadharia ya jionsentriki, inayomaanisha kwamba sayari zizungukapo katika duara, kitovu cha duara hiyo, kinachoitwa episaiko (duara ya ndani), huzunguka pia katika mzingo wa duara nyingine. Huo ulikuwa ujuzi wa hesabu wa hali ya juu sana na ulieleza sababu ya ule unaoonekana kuwa mwendo wa jua, mwezi, sayari, na nyota angani na ambao ulikubaliwa sana hadi karne ya 16.

Copernicus (1473-1543) alikuza nadharia nyingine. Aliamini kwamba ingawa sayari, kutia ndani dunia, zilizunguka jua, jua limetulia. Wazo hilo—la dunia inayosonga kuwa si kitovu tena cha ulimwengu wote mzima—kama lingalikuwa kweli, lingalileta mabadiliko mengi sana. Miaka inayopungua mia moja baadaye, mwastronomia Mwitalia Galileo Galilei alitazama angani kwa kutumia darubini, na yale aliyoyaona yalimhakikishia kwamba nadharia ya Copernicus ya kwamba dunia huzunguka jua ilikuwa kweli kabisa. Lakini Kanisa Katoliki lilikataa maoni ya Galileo kuwa ni uzushi na kumlazimisha akanushe maoni hayo.

Makosa ya kidini yalikuwa yamefanya wanatheolojia wa kanisa wakatae kweli ya kisayansi. Kanisa halikumwondolea Galileo mashtaka ya uzushi mpaka karibu miaka 360 baadaye. Gazeti LʼOsservatore Romano, katika toleo lalo la kila juma la Novemba 4, 1992, lilikiri “kosa la uamuzi” katika kesi dhidi ya Galileo.

Mabaradhuli Bado Wako

Vilevile, katika karne hii ya 20, dini za Jumuiya ya Wakristo pia hazistahi kweli. Zinafanya hivyo kwa kupendelea nadharia za kisayansi zisizothibitishwa kuliko kupendelea kweli, ya kisayansi na ya kidini. Mfano bora zaidi ni ile nadharia isiyoweza kuthibitishwa ya mageuzi, kwa msingi ikiwa uzao mbaya wa “ujuzi” wa kisayansi wenye hitilafu kubwa na mafundisho bandia ya kidini.a

Charles Darwin alitangaza kitabu chake On the Origin of Species by Means of Natural Selection mnamo Novemba 24, 1859. Lakini wazo la mageuzi lilianzia hasa kabla ya nyakati za Ukristo. Kwa mfano, mwanafalsafa Mgiriki Aristoto aliwazia kuwa mtu alikuwa wa juu katika mstari wa uhai unaopitia mageuzi kutoka kwa wanyama wenye aina ya uhai wa chini. Mwanzoni, makasisi walikataa nadharia ya Darwin, lakini The Book of Popular Science chataarifu hivi: “[Baadaye] mageuzi yakawa kitu kubwa zaidi ya nadharia ya kisayansi . . . Yakawa ndiyo shime na hata falsafa.” Wazo la kuokoka kwa walio bora zaidi pekee lilivutia watu waliotaka kufikia hali ya maisha ya juu zaidi.

Upesi upinzani wa makasisi ukaisha. The Encyclopedia of Religion yasema kwamba “na-dharia ya Darwin haikukubaliwa tu bali ilisifiwa sana,” na kwamba “kufikia wakati wa kifo chake katika 1883, makasisi wenye kufikiri zaidi na wenye kusema sana walikuwa wamefikia mkataa wa kwamba mageuzi yalipatana kabisa na uelewevu wenye kutiwa nuru wa andiko.”

Hilo lilikubaliwa kujapokuwa kukiri huku kwa The Book of Popular Science: “Ilibidi hata waungaji mkono washupavu zaidi wa fundisho la mageuzi ya viumbe wakiri kwamba kulikuwa na makosa na mapengo makubwa katika nadharia ya awali ya Darwin.” Kikisema kwamba “sehemu kubwa ya nadharia ya awali ya Darwin imesahihishwa au kuondolewa,” hata hivyo kitabu hicho kinasema kwamba “uvutano [wa mageuzi] juu ya kila nyanja ya utendaji wa kibinadamu umekuwa mkubwa sana. Historia, akiolojia, na ethnolojia zimebadilika sana kwa sababu ya nadharia hiyo.”

Leo, wanasayansi wengi wenye kufikiri wanatilia shaka sana nadharia ya mageuzi. Bwana Fred Hoyle, mwanzilishi wa Taasisi ya Cambridge ya Nadharia ya Astronomia na mshiriki wa Chuo cha Kitaifa cha Amerika cha Sayansi, aliandika hivi karibu miaka kumi iliyopita: “Kwangu binafsi, sina shaka kwamba wanahistoria wa kisayansi wa wakati ujao watapata ugumu wa kuelewa kwamba nadharia inayoonekana kuwa haifai ilikuja kuaminiwa na wengi sana kadiri hiyo.”

Nadharia hiyo ikishambulia msingi hasa wa kuwapo kwa wanadamu, inamnyang’anya Muumba sifa anayostahili. Pia inapinga dai layo la kuwa ni ya kisayansi na haifaidi kitu ile jitihada inayoendelea ya ainabinadamu ya kutafuta kweli ya kisayansi. Karl Marx alifurahi kujua nadharia ya mageuzi na pia ‘kuokoka kwa walio bora zaidi’ ili aimarishe mwinuko wa Ukomunisti. Lakini nadharia ya mageuzi ni baradhuli la aina mbaya zaidi.

Ni Nani Wanaathiriwa?

Mtu yeyote anayedanganywa aamini nadharia bandia za kisayansi huathiriwa. Lakini hata kuamini kweli za kisayansi kwaweza kutokeza hatari. Maendeleo ya kustaajabisha ya kisayansi yaliyotokana na mapinduzi ya kisayansi yalidanganya wengi waamini kwamba sasa sayansi ingeweza kutimiza kitu chochote.

Imani hiyo iliongezeka sana wakati maendeleo ya kisayansi yalipoendelea kubomoa mwelekeo wa kupinga sayansi uliokuwa umeendelezwa wakati mmoja na dini bandia. Biashara na siasa zikaanza kutambua sayansi kuwa chombo chenye nguvu ambacho zinaweza kutumia katika kutimiza miradi yazo, uwe mradi huo ni mapato ya kifedha au kuimarisha mamlaka ya kisiasa.

Ikisemwa waziwazi, sayansi ilikuwa inaendelea polepole kuwa mungu, ikitokeza usayansi. Kamusi Webster’s Ninth New Collegiate Dictionary yafasili neno hilo kuwa “kutumaini kupita kiasi manufaa ya njia za sayansi ya asili ikitumiwa katika nyanja zote za utafiti.”

Karne ya 19 ilipokaribia kwisha, watu walijiuliza karne ya 20 ingeleta nini. Je! sayansi ingeleta ‘maendeleo mazuri ajabu’ kama vile wengi walivyodhania ingeweza kufanya? Au mabaradhuli wayo wangeendelea kujaza miili ya majeruhi wayo katika uwanja wa vita ya mapinduzi ya kisayansi? Makala “Kufanya ‘Miujiza’ Katika Karne ya 20,” inayotokea katika toleo letu linalofuata, itatoa majibu.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Umeme Ukikatwa

HIVI karibuni kufikia karne ya 19, umeme ulionekana kuwa ajabu kubwa yenye kupendeza lakini isiyokuwa na matumizi mengi. Hata hivyo, wanaume kutoka nchi tofauti-tofauti na malezi mbalimbali, kutia ndani H. .C. Ørsted (1777-1851), M. Faraday (1791-1867), A. Ampère (1775-1836), na B. Franklin (1706-90) walifanya mavumbuzi makubwa yaliyothibitisha mambo tofauti, hivyo wakiwekea msingi ulimwengu wa leo wa umeme—ulimwengu ambao hauwezi kutenda bila umeme.

[Maelezo ya Chini]

a Fundisho moja kama hiyo ni wazo la Wafandamentali kwamba lile “juma” la uumbaji linalotajwa katika Mwanzo ni mfululizo wa siku halisi zenye saa 24. Biblia yaonyesha kwamba kwa kweli vilikuwa ni vipindi vinavyojumlika kuwa maelfu mengi ya miaka.

[Picha katika ukurasa wa 15]

Nicolaus Copernicus

Galileo Galileiy

[Hisani]

Picha zilizotolewa kwa Giordano Bruno and Galilei (toleo la Ujerumani)y

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki