Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g93 5/8 kur. 13-17
  • Kifo Katika Mabawa Mepesi

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kifo Katika Mabawa Mepesi
  • Amkeni!—1993
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Utafutaji Wenye Subira wa Adui
  • Madhara Makubwa ya Malaria
  • Vita vya Kupata Ushindi
  • Silaha mpya
  • Mashambulizi Zaidi Yenye Matarajio Mazuri
  • Malaria Yapigana Pia
  • Unayopaswa Kujua Kuhusu Malaria
    Amkeni!—2015
  • Kuyarudia Mambo ya Msingi Katika Kupigana na MALARIA
    Amkeni!—1997
  • Silaha Mpya Dhidi ya Malaria
    Amkeni!—1993
  • Kwa Nini Maradhi “Yanayoponyeka” Yamerudi?
    Amkeni!—1993
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1993
g93 5/8 kur. 13-17

Kifo Katika Mabawa Mepesi

Hii si vita inayotangazwa sana katika magazeti; na bado imechukua mamilioni mengi ya uhai wa kibinadamu. Si vita ya mabomu na risasi; na bado kwa habari ya huzuni inayoleta na uhai inayochukua, inafikia au hata kupita vile vita vingine. Katika vita hii, kifo hakiji kwa sehemu ya kubeba shehena ya ndege za kivita za adui zenye kulipua mabomu, bali huja kwa mabawa mepesi ya mbu-jike.

Na mleta habari za Amkeni! katika Nigeria

NI USIKU; wenye nyumba wamelala usingizi. Mbu apeperuka ndani ya chumba cha kulala, mabawa yake yakipigapiga kati ya mara 200 na 500 kwa sekunde moja. Ana njaa ya damu ya binadamu. Atua kwa upole juu ya mkono wa kivulana. Kwa kuwa uzito wake ni gramu 3/1,000 tu, kivulana hasikii. Kisha atoa sindano kama msumeno inayotokea kwenye sehemu ngumu ya midomo yake, ambayo apasua nayo ngozi ya kivulana huyo ili afikie mshipa wa damu. Pampu mbili katika kichwa chake zanyonya damu yake. Kwa wakati uo huo, vijidudu vya malaria vyapita kutoka tezi za mate za mbu huyo na kuingia katika mkondo wa damu wa kivulana huyo. Tendo hilo lamalizika upesi; asihisi chochote. Mbu huyo aruka na kwenda zake, akiwa amevimba kwa damu kiasi cha mara tatu ya uzito wa mwili wake. Siku chache baadaye, kivulana huyo ni mgonjwa mahututi. Ana malaria.

Ni kitendo ambacho kimerudiwa mara maelfu ya mamilioni. Tokeo limekuwa huzuni na kifo kwa kiwango kikubwa sana. Bila shaka yoyote, malaria ni adui mkatili asiyekoma wa binadamu.

Utafutaji Wenye Subira wa Adui

Mmojawapo mavumbuzi makubwa ya malaria haukufanywa na wanasayansi mashuhuri wa Ulaya, bali ulifanywa na daktari-mpasuaji wa Jeshi la Uingereza aliyekuwa India. Wanasayansi na madaktari wa karne ya 19, wakiamini mawazo ya miaka elfu mbili iliyopita, waliamini kwamba watu waliambukizwa ugonjwa huo kwa kuvuta hewa mbaya ya bwawa.a Kwa kutofautisha, Dkt. Ronald Ross aliamini kwamba ugonjwa huo ulipitishwa kwa mtu na mbu. Hata baada ya kujulikana kwamba malaria ulihusisha vijidudu katika mkondo wa damu ya binadamu, watafiti waliendelea kutafuta chanzo chao katika hewa na maji ya bwawa. Wakati uo huo, Ross alikuwa akichunguza matumbo ya mbu.

Ukifikiria vifaa vya kale vya maabara ambavyo alilazimika kufanya kazi nazo, kuchunguza matumbo ya mbu hakukuwa jambo rahisi. Mbu wengi walimjaa huku akifanya kazi, wakiazimia, kulingana na Ross, kulipiza kisasi kwa ajili ya “vifo vya marafiki wao.”

Hatimaye, mnamo Agosti 16, 1897, Ross aligundua katika ngozi ya matumbo ya mbu aina ya anofales, vitu vyenye umbo la mviringo ambavyo vilikuwa vimekua vikawa vikubwa kwa usiku mmoja. Vijidudu vya malaria!

Akiwa amechachawa, Ross aliandika katika kitabu chake cha habari kwamba alikuwa amegundua siri ambayo ingeokoa “mamiriadi ya watu.” Pia aliandika mstari kutoka kitabu cha Biblia cha Wakorintho: “U wapi, Ewe mauti, uchungu wako? Ku wapi, Ewe mauti, kushinda kwako?”—Linganisha 1 Wakorintho 15:55.

Madhara Makubwa ya Malaria

Uvumbuzi wa Ross ulikuwa hatua kubwa katika vita dhidi ya malaria, uvumbuzi ambao ulifungulia wanadamu njia ya kufanya mashambulizi makubwa ya kwanza dhidi ya ugonjwa huo na wadudu wanaoubeba.

Kwa sehemu kubwa ya historia, hasara ya binadamu kutokana na malaria imekuwa kubwa sana na yenye kuendelea. Maandishi ya michoro na ya mafunjo ya Misri yathibitisha madhara makubwa ya malaria miaka 1,500 kabla ya Yesu kuja duniani. Iliharibu kabisa majiji mazuri katika nyanda ya chini ya Ugiriki ya kale na kumwua Aleksanda Mkuu akiwa katika upeo wa maisha yake. Ilipunguza sana idadi ya watu wa majiji ya Warumi na kuwafanya matajiri wahamie milimani. Katika vita vya kruse-di, vita ya Amerika ya Wenyewe kwa Wenyewe, na katika vita viwili vya ulimwengu, malaria iliua watu zaidi ya mapigano yoyote makubwa.

Katika Afrika malaria ilisaidia kupatia Afrika Magharibi sifa ya “Kaburi la Wazungu.” Kwa kweli, ugonjwa huo ulizuia ule mng’ang’ano wa nchi za Ulaya kutwaa Afrika hivi kwamba chuo kikuu kimoja cha Afrika Magharibi kilitawaza mbu kuwa shujaa wa taifa! Katika Amerika ya Kati, malaria ilisaidia kushinda jitihada za Wafaransa za kujenga Mfereji wa Panama. Katika Amerika Kusini, ilisemekana kwamba malaria iliua mtu kwa kila taruma ya reli iliyolazwa wakati wa kujenga reli ya Mamoré-Madeira katika Brazili.

Vita vya Kupata Ushindi

Ulinzi dhidi ya mbu, lakini pasipo kujua dhidi ya malaria, umetumika kwa mamileani ya miaka. Katika karne ya 16 K.W.K., Wamisri walitumia mafuta ya mti Balanites wilsoniana kukinza mbu. Miaka elfu baadaye, Herodoto aliandika kwamba wavuvi Wamisri walifunga nyavu zao kuzunguka vitanda vyao wakati wa usiku ili kuzuia wadudu hao. Karne kumi na saba baadaye, Marco Polo aliripoti kwamba wakazi matajiri wa India walilalia vitanda vyenye mapazia ya kukinga yanayoweza kufungwa wakati wa usiku.

Katika sehemu nyinginezo, watu walivumbua dawa za asili zenye thamani kubwa. Kwa muda wa zaidi ya miaka 2,000, malaria katika Uchina ilikuwa imetibiwa kwa mafanikio kwa mmea unaoitwa qinghaosu, dawa ya mmea ambayo imegunduliwa tena katika miaka ya karibuni. Katika Amerika Kusini, Wahindi wa Peru walitumia ganda la mti sinchona. Katika karne ya 17, mti huo ulikuja Ulaya, na katika 1820 wakazi wawili wa Paris ambao walikuwa wataalamu wa dawa walitoa kutokana na mti huo aina ya dawa inayoitwa kwinini.

Silaha mpya

Thamani ya kwinini ya kuzuia na kutibu malaria ilikubaliwa polepole, lakini ilipokubaliwa kabisa, ikawa ndiyo dawa ya kutumiwa kwa miaka mia moja. Kisha mapema katika vita ya ulimwengu ya pili, majeshi ya Japan yaliteka mashamba ya maana ya mti sinchona katika Mashariki ya Mbali. Matokeo ya ukosefu mkubwa wa kwinini katika United States yalichochea utafiti mkubwa wa kutengeneza dawa isiyo ya asili ya malaria. Matokeo yakawa chloroquine, dawa iliyokuwa salama kutumiwa, yenye matokeo sana, na isiyokuwa ghali kutengeneza.

Upesi chloroquine ikawa silaha kubwa dhidi ya malaria. Dawa ya kuua wadudu inayoitwa DDT, mwuaji hatari wa mbu, pia ilitokezwa katika miaka ya 1940. DDT haiui tu mbu wakati wa kunyunyizwa bali baadaye masalio yake kwenye kuta zilizonyunyiziwa huua wadudu.b

Mashambulizi Zaidi Yenye Matarajio Mazuri

Baada ya vita ya ulimwengu ya pili, wanasayansi wakiwa na DDT na chloroquine walipanga mashambulizi zaidi dhidi ya malaria na mbu. Hiyo ingekuwa ni vita yenye pande mbili—dawa zingetumiwa kuua vijidudu mwilini mwa wanadamu, na kunyunyizwa kwingi kwa dawa za kuua wadudu kungetowesha mbu kabisa.

Mradi ulikuwa ni ushindi kabisa. Malaria ingeondoshwa kabisa isiwepo. Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) lililotoka tu kufanyizwa, na ambalo lilifanya kuangamizwa kwa malaria kuwa mradi walo mkuu, lingeongoza shambulizi hilo. Azimio la shirika hilo lilitegemezwa na pesa. Kati ya 1957 na 1967, mataifa yalitumia dola bilioni 1.4 za U.S. katika kampeni yayo ya duniani pote. Matokeo ya mapema yalikuwa ya kustaajabisha. Ugonjwa huo ulimalizwa katika Ulaya, Amerika ya Kaskazini, Muungano wa Sovieti, Australia, na baadhi ya nchi fulani katika Amerika ya Kusini. Profesa L. J. Bruce-Chwatt, mtaalamu wa kupambana na malaria, alionenelea hivi: “Ni vigumu kueleza leo ule msisimuko mkubwa sana ulioletwa na wazo la kuangamiza [malaria] ulimwenguni pote katika siku hizo za amani.” Malaria ilikuwa ikishindwa! Shirika la WHO lilijisifu hivi: “Kuangamizwa kwa malaria ni jambo halisi tunaloweza kutimiza.”

Malaria Yapigana Pia

Lakini ushindi haukutokea. Vizazi vya mbu vilivyookoka yale mashambulizi ya kemikali vilisitawisha kinga kwa dawa za kuua wadudu. DDT haikuweza kuwaua kwa urahisi kama ilivyofanya hapo awali. Vivyo hivyo, vijidudu vya malaria katika miili ya wanadamu vilisitawisha kinga kwa chloroquine. Matatizo hayo pamoja na mengine yalibadili mambo kwa njia ya kuhofisha sana katika baadhi ya nchi fulani ambamo ushindi ulikuwa umeonekana kuwa jambo la hakika. Kwa mfano, Sri Lanka, ambako ilifikiriwa kuwa malaria ilikuwa imeangamizwa katika 1963, ilipatwa na mweneo mkubwa wa ugonjwa huo miaka mitano tu baadaye ambao uliathiri mamilioni ya watu.

Kufikia 1969 ilikuwa imejulikana wazi kwamba malaria ilikuwa adui ambaye haingeweza kushindwa. Badala ya neno ‘angamiza,’ neno “kudhibiti” lilianza kutumiwa. Ni nini kinachomaanishwa na “kudhibiti”? Dkt. Brian Doberstyn, mkuu wa idara ya malaria ya shirika la WHO, aeleza hivi: “Yale tuwezayo kufanya sasa ni kujaribu kupunguza vifo na kuteseka kwa kiwango cha chini.”

Ofisa mwingine wa shirika la WHO aomboleza hivi: “Baada ya jitihada za kuondoa Malaria zilizofanywa katika miaka ya 1950 na utumizi wa dawa ya DDT dhidi ya wadudu, jumuiya ya kimataifa imepunguza mwendo. Umaskini, ukosefu wa mpango bora, kinga dhidi ya dawa za kutibu na za kuua wadudu vimefanya ugonjwa huo udumu. Kwa hakika, tumeshindwa na ugonjwa huo.”

Jambo jingine ni kwamba makampuni ya dawa yameacha utafiti wayo. Mwanasayansi mmoja wa malaria asema hivi: “Tatizo ni kwamba inahitaji fedha nyingi, lakini haileti faida na hakuna kitia-moyo.” Naam, ingawa vita vingi vimeshindwa, vita dhidi ya malaria bado haijakwisha. Hata hivyo Biblia yaelekeza kwenye wakati ulio karibu ambapo “hapana mwenyeji atakayesema, Mimi mgonjwa.” (Isaya 33:24) Mpaka wakati huo, ugonjwa na kifo bado vitakuja katika mabawa mepesi.

[Maelezo ya Chini]

a Neno “malaria” latokana na neno la Kiitalia mala (mbaya) aria (hewa).

b Ilipatikana kuwa DDT ilikuwa inadhuru mazingira na hivyo imepigwa marufuku au kuzuiwa sana katika nchi 45.

[Sanduku katika ukurasa wa 14]

Mbu dhidi ya Binadamu

Mbu anatisha kwa njia ya moja kwa moja karibu nusu ya ainabinadamu, zaidi ya nchi mia moja, sanasana katika tropiki. Afrika hasa ni ngome kubwa ya mbu.

Inajulikana kwamba mbu hupanda ndege kutoka sehemu za tropiki na wameambukiza watu wanaoishi karibu na viwanja-ndege vya kimataifa.

Wanaoambukizwa. Malaria huambukiza watu milioni 270 kila mwaka, ikiua kufikia watu milioni 2. Ni hatari hasa kwa wanawake wenye mimba na watoto, na kwa wastani inaua watoto wawili kila dakika.

Hushambulia wageni wanaozuru nchi za tropiki. Kila mwaka karibu visa 10,000 za malaria “iliyoingizwa nchini” huripotiwa katika Ulaya na zaidi ya 1,000 katika Amerika ya Kaskazini.

Mbinu. Mbu-jike aina ya anofales hushambulia binadamu sana-sana wakati wa usiku. Malaria pia hupitishwa kupitia kutiwa damu mishipani na, mara chache sana, kupitia sindano zenye vijidudu.

Ni miaka ya karibuni tu ndipo wanadamu walipata maarifa ya kupigana naye. Zijapokuwa jitihada za pamoja za nchi 105 zinazojaribu kuishinda malaria, wanadamu wanaendelea kushindwa katika vita hiyo

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 15]

Jilinde Dhidi ya Kuumwa na Mbu

Lala kitanda chako kikiwa kimefunikwa kwa chandarua. Vyandarua vilivyowekwa dawa za kuua wadudu ni bora zaidi.

Tumia kisawazisha hewa ikiwezekana, au lala katika chumba chenye madirisha na milango yenye kusetiriwa. Kama hakuna kisetiri, basi funga milango na madirisha.

Baada ya jua kushuka, inapendekezwa uvae mavazi yenye mikono mirefu na suruali ndefu. Mavazi meusi huvutia mbu.

Paka dawa ya kufukuza wadudu katika sehemu za mwili zisizofunikwa na mavazi. Chagua kizuizi kinachoitwa deet au chenye chumvi ya asidi ya phthalic.

Tumia vinyunyizo vya kuzuia mbu, dawa za kuua wadudu, au uvumba wa kufukuzia mbu.

Chanzo: Shirika la Afya Ulimwenguni.

[Hisani]

H. Armstrong Roberts

[Sanduku katika ukurasa wa 16]

“Hakuna ‘Risasi ya Ajabu’”

Ingawa tarajio la ushindi ni dogo sana, vita dhidi ya malaria inaendelea. Katika mkutano wa kimataifa juu ya malaria katika Brazzaville, Kongo, mnamo Oktoba 1991, wawakilishi wa shirika la WHO walitaja kwamba “mwelekeo wa sasa” uachwe na wakapendekeza utaratibu mpya wa duniani pote wa kudhibiti malaria. Jitihada kama hizo zitafanikiwa kadiri gani?

“Hakuna ‘risasi ya ajabu’ kwa malaria,” akasema mkurugenzi-mkuu wa WHO Hiroshi Nakajima hivi karibuni. “Kwa hiyo, ni lazima tupigane kutoka pande nyingi.” Hapa pana pande tatu za vita ambazo karibuni zimezungumziwa sana:

Machanjo: Wanasayansi wamekuwa wakifanya kazi kwa miaka mingi katika jitihada za kutafuta chanjo dhidi ya malaria, na mara moja-moja vyombo vya habari huripoti juu ya “kufaulu” katika utafiti. Likiondoa matazamio mazuri yasiyofaa, WHO latahadharisha dhidi ya “ndoto ya kupatikana kwa chanjo ya malaria katika wakati ujao ulio karibu.”

Mojapo matatizo ya kutengeneza chanjo ni kwamba vijidudu vya malaria vimefanikiwa sana katika kuepa jitihada za kuviharibu za mfumo wa kinga wa binadamu. Hata baada ya miaka mingi ya kuambukizwa tena na tena, watu husitawisha kinga kidogo tu kwa ugonjwa huo. Dkt. Hans Lobel, mtaalamu wa kudhibiti magonjwa katika Vituo vya Kudhibiti Magonjwa vya U.S. katika Atlanta alisema hivi: “Huwezi kusitawisha kinga baada ya kushambuliwa mara chache tu. Kwa hiyo, [kwa kujaribu kutokeza chanjo] unajaribu kufanya zaidi ya asili.”

Dawa. Kwa sababu ya kinga inayoendelea ya vijidudu vya malaria dhidi ya dawa zinazopatikana sasa, WHO linatokeza dawa inayoitwa arteether, inayotokana na umaji-maji wa Uchina unaoitwa qinghaosu.c Shirika la WHO latumaini kwamba qinghaosu huenda utakuwa ndio chanzo cha aina mpya kabisa ya dawa za asili, zinazoweza kupatikana kwa jumuiya yote ya ulimwengu katika muda wa miaka kumi hivi ijayo.

Vyandarua vya kitanda. Ulinzi huu wa miaka elfu mbili bado unatumika dhidi ya mbu. Mbu wa malaria mara nyingi hushambulia wakati wa usiku, na chandarua huwazuia. Vyandarua vilivyoingizwa ndani ya dawa ya kuua wadudu, kama vile permethrin, ni vyenye matokeo zaidi. Uchunguzi mbalimbali katika Afrika waonyesha kwamba katika vijiji ambamo vyandarua vilivyoingizwa ndani ya dawa vilitumiwa, vifo vya malaria vilishuka kwa asilimia 60.

[Maelezo ya Chini]

c Qinghaosu latokana na mmea wa pakanga, Artemisia annua.

[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 17]

Je! Wasafiri Kwenda Nchi za Tropiki?

Ikiwa unasafiri kwenda eneo ambalo malaria ni tisho, wapaswa kufanya yafuatayo:

 1. Mwone daktari wako au enda katika kituo cha chanjo.

 2. Fuata kabisa maagizo unayopewa, na ikiwa unatumia dawa ya malaria basi endelea kufanya hivyo mpaka majuma manne yapite baada ya wewe kuondoka sehemu ya malaria.

 3. Jikinge dhidi ya kuumwa na mbu.

 4. Ujue ishara za malaria: homa, maumivu ya kichwa, maumivu ya misuli, kutapika/au kuhara. Ukumbuke kwamba malaria inaweza kujionyesha kufikia mwaka mmoja baada ya wewe kutoka katika eneo la malaria hata kama ulikuwa ukitumia dawa za malaria.

 5. Ukiwa na ishara hizo, mwone daktari. Malaria inaweza kuzidi kwa haraka na inaweza kuua kwa muda unaopungua saa 48 baada ya ishara za kwanza kuonekana.

Chanzo: Shirika la Afya Ulimwenguni.

[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 13]

H. Armstrong Roberts

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki