Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 3/8 kur. 13-18
  • Ni Nini Kilichowapata Wale Waapache?

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Ni Nini Kilichowapata Wale Waapache?
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • “Simbamarara wa Spishi ya Kibinadamu”
  • Kuokoka kwa Mapema
  • Ni Nani Waliokuwa wa Kwanza Kukata Vichwa?
  • Je, Maeneo Yaliyotengwa Yalikuwa Suluhisho?
  • Ni Matatizo Gani Wanayokabili Leo?
  • Maendeleo ya Kiuchumi ya Waapache
  • Wakati Ambapo Haki ya Kweli Itadumu
  • “Katika Lugha Yetu Hakuna Matusi”
    Amkeni!—2005
  • Jinsi Ulimwengu Wao Ulivyopotea
    Amkeni!—1996
  • Wakati Wao Ujao Una Nini?
    Amkeni!—1996
  • Mwanadamu Amemkandamiza Mwanadamu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 3/8 kur. 13-18

Ni Nini Kilichowapata Wale Waapache?

NI NANI aliyesemekana kuwa, “Uso wenye ukatili zaidi uliopata kuwako”? Na bado, ni nani aliyejulikana kwa moyo mkuu na azimio lake lenye kutokeza? Alikuwa kiongozi wa mwisho wa Waapache kujisalimisha kwa Jeshi la Marekani. Aliishi kufikia umri wa karibu miaka 80 na alikufa katika mwaka wa 1909 katika Oklahoma, anadhaniwa kuwa alikuwa mshiriki wa Dutch Reformed Church. Alikuwa Goyathlay (hutamkwa Goyahkla), alijulikana vizuri zaidi kuwa Geronimo, kiongozi mkubwa wa mwisho wa Waapache.

Inasemekana kuwa alikuja kuitwa Geronimo baada ya askari-jeshi wa Mexico kuita kwa woga “Mtakatifu” Jerome (Jerónimo) wakati Goyathlay alipowashambulia. Karibu na mwaka wa 1850, vikosi vya wanajeshi vya Mexico viliwaua wanawake na watoto Waapache 25 waliokuwa wamepiga kambi kwenye viunga vya Janos, Mexico. Kati yao walikuwa mama ya Geronimo, mke wake mchanga, na watoto wake watatu. Inasemekana kwamba “kwa maisha yake yote Geronimo aliwachukia Wamexico.” Akichochewa na tamaa ya kulipiza kisasi, akaja kuwa mmoja wa machifu Waapache walioogopewa zaidi.

Lakini twajua nini kuwahusu Wahindi Waapache, ambao kwa kawaida huonyeshwa wakiwa wenye mtindo wa wahalifu katika sinema za Hollywood. Je, wangali wapo? Ikiwa wapo, wao huishije na wanakabili wakati ujao ulioje?

“Simbamarara wa Spishi ya Kibinadamu”

Waapache (yaelekea jina lao latokana na neno la Kizuni apachu, linalomaanisha “adui”) walijulikana kuwa wanavita wasiohofu na werevu. Mhindi mwanavita wa karne ya 19 aliyejulikana sana Jenerali George Crook aliwaita “simbamarara wa spishi ya kibinadamu.” Lakini, mamlaka moja husema kwamba “hakuna wakati wowote baada ya 1500 ambapo makabila yote ya Waapache yakijumlishwa pamoja yalipita idadi ya watu elfu sita.” Lakini makumi machache tu ya wapiganaji wangeweza kuzuia jeshi zima katika pigano la kuvizia!

Hata hivyo, chanzo kimoja cha Waapache hutaarifu: “Tofauti na dhana zijulikanazo sana zilizobuniwa na Wahispania, Wamexico, na Wamarekani, Waapache si watu wa vita wenye kiu cha damu. Tulivamia kwa ajili ya chakula tu wakati kulipokuwa na upungufu. Vita havikufanywa kama matendo yasiyo na mpango maalumu, bali kwa ujumla vilikuwa kampeni iliyopangwa vizuri ya kulipiza kisasi dhidi ya ukosefu wa haki kutuelekea.” Na ukosefu huo wa haki, ulikuwa mwingi!

Maonyesho katika Kitovu cha Kitamaduni cha Waapache katika San Carlos, katika Peridot, Arizona, hueleza historia ya Waapache kwa maoni yao: “Kuwasili kwa watu kutoka nje katika eneo hilo kulileta uhasama na badiliko. Wageni hawa hawakuwa na staha kwa vifungo vyetu vya kiasili kwa nchi hii. Katika juhudi za kulinda mapokeo na tamaduni zetu, babu zetu walipigana na kushinda mapigano mengi dhidi ya wanajeshi na raia wa Hispania, Mexico, na Marekani. Lakini wakishindwa nguvu na wingi na tekinolojia ya kisasa, babu zetu na babu zetu wa zamani walilazimishwa hatimaye kukubali madai ya Serikali ya Marekani. Tulilazimishwa kuacha maisha yetu ya kutangatanga na kuishi katika maeneo yaliyotengwa.” Maneno ‘kulazimishwa kuishi katika maeneo yaliyotengwa’ huamsha hisia nyingi za wakazi karibu nusu milioni walioishi katika maeneo yaliyotengwa (kati ya Wenyeji Wamarekani milioni mbili) katika yale makabila 554 katika Marekani na yale makundi 633 huko Kanada. Waapache wako karibu 50,000.a

Kuokoka kwa Mapema

Wataalamu wengi wa historia ya Wenyeji Wamarekani wa zamani hukubali ile nadharia ya kwamba makabila ya awali yalitoka Asia kupitia Mlango-Bahari wa Bering kisha polepole yakasambaa kuelekea kusini na mashariki. Wanasayansi wa lugha huhusianisha lugha ya Waapache na ile ya watu wanaosema lugha ya Athapaska wa Alaska na Kanada. Thomas Mails aandika: “Wakati wa kuwasili kwao Kusini-Magharibi mwa Marekani kwa sasa kwakadiriwa kuwa kati ya A.D. 1000 na 1500. Njia barabara waliyofuata na mwendo wa kuhama kwao wanaanthropolojia wangali hawajakubaliana.”—The People Called Apache.

Katika karne za zamani Waapache waliendeleza maisha kwa kupanga vikosi vya kuvamia dhidi ya majirani wao Wahispania-Wamexico. Thomas Mails aandika: “Mashambulio kama hayo yaliendelea kwa karibu miaka mia mbili, yakianza karibu mwaka wa 1690 na kuendelea hadi karibu mwaka wa 1870. Mashambulio hayo hayakuwa ya kushangaza, kwani Mexico ilithibitika kuwa kwa kweli na wingi wa vitu vilivyohitajika.”

Ni Nani Waliokuwa wa Kwanza Kukata Vichwa?

Likiwa tokeo la mapambano ya daima kati ya Mexico na taifa la Waapache, serikali ya taifa la Sonora Mexico “ilirudia njia ya zamani ya Kihispania” ya kutoa zawadi za vichwa. Hili halikuwa utokezo wa Wahispania tu—Waingereza na Wafaransa walikuwa wamefuata desturi hii katika nyakati za mapema.

Wamexico walikata vichwa ili wapate zawadi ya pesa taslimu, na nyakati nyingine halikuwa jambo la maana kama kichwa kilikuwa cha Mwapache au la. Katika mwaka wa 1835 sheria ya zawadi za kichwa ilipitishwa katika Mexico ambayo ilitoa peso 100 kwa kila kichwa cha mpiganaji. Miaka miwili baadaye zawadi hiyo ilitia ndani peso 50 kwa kichwa cha mwanamke na peso 25 kwa kichwa cha mtoto! Katika kitabu chake The Conquest of Apacheria, Dan Thrapp aandika: “Sera hiyo kwa wazi ilitafuta kuangamiza, uthibitisho wa kwamba mizizi ya maangamizi ya jamii ilikuwa imeenea na haukuwa ubuni wa kisasa wa taifa moja.” Aendelea: “Waapache wenyewe hawakukata vichwa.” Hata hivyo, Mails asema kuwa nyakati nyingine Wachiricahua walichukua vichwa—lakini si mara nyingi, “kwa sababu ya kuhofu kifo na mazimwi.” Aongezea: “Kukata vichwa kulifanywa tu katika kulipiza kisasi baada ya Wamexico kuanzisha rasmi mbinu hiyo.”

Thrapp asema kwamba wachimba-madini “mara nyingi walijipanga pamoja . . . na wakaenda kuwawinda Wahindi. Wakati ambapo wangewatega, waliua wanaume wote na, nyakati nyingine waliua wanawake na watoto wote. Kwa asili, Wahindi, pia walifanya vivyo hivyo kwa wazungu na makabila mengine.”

Ulifika wakati ambapo vita na Waapache ilikuwa yenye faida kwa jimbo la Arizona, asema Charles Lummis, kwani “kuendeleza vita na Waapache [kulimaanisha] dola zaidi ya milioni 2 kwa mwaka [zilikuwa] zikitolewa kati ya mipaka ya Arizona na Idara ya Vita.” Thrapp ataarifu: “Kulikuwa na watu wenye nguvu na wenye uangalifu mno ambao hawakutaka amani pamoja na Waapache, kwani kulipokuwa na amani, fedha zilizokuwa zikipatikana kwa kuendelea na zikitumiwa na wanajeshi ziliisha.”

Je, Maeneo Yaliyotengwa Yalikuwa Suluhisho?

Mapigano ya daima kati ya wazungu-wakazi waliovamia na wenyeji Waapache yaliongoza kwenye suluhisho la serikali ya shirika la kuwaweka Wahindi katika maeneo yaliyotengwa—mara nyingi ardhi ambayo haikutoa kinga na riziki ambapo walitarajiwa kuendelea kuwa hai. Katika mwaka wa 1871-1872 maeneo yaliyotengwa yaliwekwa kwa ajili ya Waapache.

Kuanzia 1872 hadi 1876, Waapache wa Chiricahua walikuwa na eneo lao wenyewe lililotengwa. Wahamahamaji hawa wenye kuzunguka kwa uhuru walijihisi kuwa wamefungiwa. Hata ingawa walikuwa na eka 2,736,000 kati ya watu 400 na 600, eneo hili ambalo ni kavu sana halikuwapa nafasi ya kutosha kupata chakula kwa kuwinda na kukusanya. Ilikuwa lazima serikali igawe chakula kila baada ya siku 15 ili kuzuia kufa njaa.

Hata hivyo, masetla wazungu walifikiri kuwa Eneo Lililotengwa kwa Wachiricahua ilikuwa ni kupoteza ardhi na kwamba Waapache walipaswa kuwekwa katika eneo moja lililotengwa. Hisi ya kukosa urafiki ya masetla wazungu iliongezeka baada ya kifo cha chifu mstahiki Cochise katika mwaka wa 1874. Walihitaji kisababu ili wawafukuze Waapache wa Chiricahua kutoka kwenye eneo hilo lililotengwa. Kulitokea nini? “Katika mwaka wa 1876, kisingizio kilijitokeza. Wauzaji mvinyo haramu wawili waliuawa na Wachiricahua wawili walipokataa kuuza [mvinyo] zaidi. Badala ya kuwakamata washukiwa, mwakilishi wa [serikali] wa eneo la San Carlos alifika akiwa na wanaume wenye silaha na kusindikiza [kabila] la Chiricahua hadi San Carlos. Eneo Lililotengwa la Chiricahua lilifungwa.”

Hata hivyo, Wahindi bado waliruhusiwa kutembea-tembea kwa uhuru kupita mipaka ya eneo lililotengwa. Masetla wazungu hawakuipenda sera hiyo. “Kwa kuitikia madai ya masetla, serikali iliwahamisha Waapache wa San Carlos, White Mountain, Cibecue, na Tonto pamoja na makundi mengi ya jumla ya Waapache wa Chiricahua, kwenye sehemu ya San Carlos.”—Creation’s Journey—Native American Identity and Belief.

Katika wakati mmoja maelfu ya Waapache wa Yavapai, Chiricahua, na wa Magharibi walizuiliwa katika eneo hilo lililotengwa. Hili lilileta mvutano na shuku, kwani baadhi ya makabila yalikuwa maadui wa muda mrefu. Waliitikiaje vizuizi vya maeneo hayo yaliyotengwa? Jibu la Waapache ni, “Tulikatiliwa mbali kutoka kwa maisha yetu ya kitamaduni, tulikufa njaa kimwili, kihisia-moyo, na kiroho. Uhuru wetu ulikuwa umechukuliwa.”

Hata hivyo, kikundi cha Chiricahua, kikiongozwa na chifu maarufu Geronimo, kilikimbia kutoka kwenye eneo hilo lililotengwa katika mwaka wa 1885 na kutorokea Mexico. Waliwindwa na Jenerali Nelson Miles pamoja na askari-jeshi karibu 5,000 kuongezea maskauti Waapache 400—wote wakijaribu kuwatafuta na kuwatokeza, kufikia wakati huo, wanavita 16, wanawake 12, na watoto 6 tu!

Mwishowe, katika Septemba 4, 1886, Geronimo alijisalimisha. Alikuwa tayari kurudi kwenye Eneo Lililotengwa la San Carlos. Lakini haikuwa hivyo. Aliambiwa kuwa Waapache wote waliokuwa huko walikuwa wamehamishwa kuelekea mashariki, wakiwa wafungwa, huko Florida, ambako pia yeye alipaswa kwenda. Alisema katika lugha yake ya Apache: “Łahn dádzaayú nahikai łeh niʹ nyelíí k’ehge,” ikimaanisha, “Wakati mmoja tulienda kwa uhuru kama upepo.” Geronimo mwenye majivuno na hila, sasa akiwa mfungwa, hangeweza tena kwenda kwa uhuru kama upepo.

Mwishowe aliruhusiwa kusonga kuelekea magharibi, hadi kufikia Fort Sill, Oklahoma, ambapo alikufa katika mwaka wa 1909. Sawa na wengi wa viongozi wa Wenyeji Wamarekani, chifu huyu wa Waapache alikuwa amelazimishwa kujinyenyekeza kwa hali zenye kukomesha maisha gerezani na katika maeneo yaliyotengwa.

Ni Matatizo Gani Wanayokabili Leo?

Waapache huishi katika maeneo kadhaa yaliyotengwa katika Arizona na New Mexico. Amkeni! lilitembelea Eneo Lililotengwa la San Carlos na kuwahoji viongozi fulani Waapache. Simulizi la ziara hiyo lafuata.

Punde baada ya kuingia katika eneo hilo lililotengwa siku yenye joto, kavu katika Mei, tulikaribishwa na Harrison Talgo na mke wake. Harrison, msemaji mwenye ufasaha, mwenye urefu wa zaidi ya futi sita, na mwenye masharubu, ni mshiriki wa baraza la kikabila la San Carlos. Tulimuuliza: “Ni yapi baadhi ya matatizo yanayowakabili Waapache leo?”

“Tunapoteza kanuni zetu za kitamaduni. Televisheni imekuwa na uvutano hasi, hasa kwa vijana wetu. Kielelezo kimoja ni kuwa hawajifunzi lugha yetu. Tatizo jingine kubwa ni ukosefu wa kazi za kuajiriwa, ambalo hufikia asilimia 60 katika maeneo mengine. Ni kweli kwamba tuna majumba ya kuchezea kamari, lakini hayatoi kazi za kuajiriwa kwa wengi wa watu wetu. Na tokeo hasi ni kwamba wengi wa watu wetu wenyewe huenda huko na kucheza kamari wakitumia hundi zao za msaada, ambazo huwakilisha pesa za kulipia nyumba na kununulia chakula.”

Alipoulizwa kuhusu matatizo ya afya kwa kabila hilo, Harrison hakusita kujibu. “Ugonjwa wa kisukari,” alisema. “Zaidi ya asilimia 20 ya watu wetu wana ugonjwa wa kisukari. Katika sehemu nyingine ni zaidi ya asilimia 50.” Alikiri kwamba tatizo jingine kubwa ni pigo lililoletwa na wazungu zaidi ya miaka 100 iliyopita—alkoholi. “Dawa za kulevya pia zawaathiri watu wetu.” Ishara za barabara kwenye eneo hili lililotengwa hutoa ushuhuda ulio wazi kwa matatizo haya, zikisema: “Acha Kufikiri Kukuongoze—Uwe Huru na Dawa za Kulevya” na, “Hifadhi Ardhi Yetu. Hifadhi Afya Yetu. Usiharibu Mali Yetu.”

Tuliuliza ikiwa UKIMWI umeathiri kabila hilo. Kwa chukizo lililoonekana wazi alijibu: “Hatari iko kwa ugoni-jinsia-moja. Ugoni-jinsia-moja unapenya kuingia katika eneo hili lililotengwa. Televisheni na mabaya ya mzungu yanadhoofisha baadhi ya vijana wetu Waapache.”

Tuliuliza jinsi ambavyo hali zimebadilika katika eneo hili lililotengwa katika miaka ya majuzi. Harrison alijibu: “Katika miaka ya 1950 hii ndiyo iliyokuwa orodha ya mambo ya kutangulizwa na adhari: Kwanza ilikuwa dini; pili, familia; tatu, elimu; nne, msongo wa marika; na, mwishowe, televisheni. Leo, utaratibu huo umebadilika, televisheni ikiwa uvutano unaoongoza. Msongo wa marika ndio uvutano wa pili wenye nguvu zaidi—msongo wa kuacha kufuata njia za Waapache na kufuata za Wamarekani zilizo kuu. Elimu ingali ya tatu, na Waapache wengi wanajifaidi kwa nafasi katika chuo cha elimu na kuongezeka kwa shule na shule za sekondari kwenye eneo hili lililotengwa.”

“Namna gani uvutano wa kifamilia?” tukauliza.

“Kwa kuhuzunisha, familia sasa imeshushwa hadi nafasi ya nne, na sasa dini iko mwisho—iwe ni dini yetu ya kitamaduni au dini za wazungu.”

“Mwazionaje dini za Jumuiya ya Wakristo?”

“Hatupendezwi na dini kujaribu kuwageuza watu wetu kutoka kwa itikadi zetu za kitamaduni.b Walutheri na Wakatoliki wamekuwa na wamishonari wao hapa kwa zaidi ya miaka 100. Pia kuna vikundi vya Kipentekoste ambavyo huwa na uvutio wa kihisia-moyo.

“Tunahitaji kurudisha utambulisho wetu wa kitamaduni kupitia familia na kuanza tena kutumia lugha ya Waapache. Kwa sasa, inapotezwa.”

Maendeleo ya Kiuchumi ya Waapache

Tulitembelea mwenye mamlaka mwingine wa Waapache ambaye alizungumza kwa uhakika kuhusu matazamio ya kiuchumi kwa ajili ya Eneo Lililotengwa la San Carlos. Hata hivyo, alieleza kwamba haikuwa rahisi kupata watega-uchumi ili watumie kiasi kikubwa cha pesa katika miradi hapa. Ishara moja nzuri ni makubaliano na kampuni moja kubwa ya simu ili kufanyiza Kampuni ya Simu na Mawasiliano ya Waapache wa San Carlos. Inasimamiwa kifedha na Shirika la Kiuchumi la Mashambani na itatokeza kazi kwa waajiriwa Waapache vilevile kupanua na kuboresha mfumo wa simu katika eneo hili lililotengwa.

Ofisa huyu pia alizungumza kwa majivuno kuhusu kituo cha tiba ya kuondoa uchafu katika damu ambacho kingeanzishwa katika hospitali ya eneo hilo lililotengwa, ambacho kitatoa uangalifu bora na wa karibu zaidi wa kitiba. Kisha akatuonyesha mipango ya kuendeleza upya kituo cha biashara katika San Carlos, ambacho kinapaswa kuanza kujengwa karibuni. Alikuwa na matumaini mema kuhusu wakati ujao lakini akasisitiza kwamba elimu lazima iwe msingi. ‘Elimu yamaanisha mishahara bora, ambayo huongoza kwenye viwango bora vya kuishi.’

Wanawake Waapache wanajulikana kwa ustadi wao wa kufuma vikapu. Kitabu cha kuwaongoza watalii chasema kuwa “kuwinda, kuvua samaki, kufuga wanyama, ukataji wa miti, uchimbaji wa madini, tafrija za nje, na utalii” ni mambo makuu katika uchumi wa wenyeji.

Waapache wanajaribu kufikia kiwango sawa cha maendeleo na ulimwengu ulio nje ya eneo hilo lililotengwa, ijapokuwa magumu mengi wanayoyakabili. Sawa na watu wengine wengi, wanataka haki, staha, na maisha ya adabu.

Wakati Ambapo Haki ya Kweli Itadumu

Mashahidi wa Yehova huwatembelea Waapache kuwaambia kuhusu ulimwengu mpya ambao Yehova Mungu ameahidi kwa ajili ya dunia yetu, ulioelezewa vizuri sana katika kitabu cha Biblia cha Isaya: “Maana, tazama, mimi naumba mbingu mpya na nchi mpya, na mambo ya kwanza hayatakumbukwa, wala hayataingia moyoni. Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake. Hawatajitaabisha kwa kazi bure.”—Isaya 65:17, 21, 23; 2 Petro 3:13; Ufunuo 21:1-4.

Wakati uko karibu ambapo Yehova Mungu atachukua hatua ya kusafisha dunia kutokana na ubinafsi wote na ufisadi vilevile utumizi mbaya wa dunia. (Ona Mathayo 24; Marko 13; Luka 21.) Watu wa mataifa yote, kutia ndani Wenyeji Wamarekani, wanaweza sasa kujibariki kwa kumgeukia Mungu wa kweli, Yehova, kupitia Kristo Yesu. (Mwanzo 22:17, 18) Mashahidi wa Yehova hutoa elimu ya Biblia bila malipo kwa watu wanyoofu wowote wanaotaka kuirithi dunia iliyorudishwa na wako tayari kumtii Mungu.—Zaburi 37:11, 19.

[Maelezo ya Chini]

a Waapache wamegawanyika katika vikundi mbalimbali vya kikabila kama vile Waapache wa Magharibi, ambao hutia ndani Watonto wa Kaskazini na Kusini, Mimbreño, na Coyotero. Waapache wa Mashariki ni Waapache wa Chiricahua, Mescalero, Jicarilla, Lipan, na Kiowa. Migawanyiko zaidi ni Waapache wa White Mountain na Waapache wa San Carlos. Leo, makabila haya hasa huishi kusini-mashariki ya Arizona na New Mexico.—Ona ramani kwenye ukurasa wa 15.

b Nakala ya wakati ujao ya Amkeni! itachunguza itikadi na dini za Wenyeji Wamarekani.

[Picha katika ukurasa wa 15]

AMERIKA KASKAZINI

Eneo lililoongezwa ukubwa kulia

Maeneo Yaliyotengwa ya Waapache

ARIZONA

NEW MEXICO

Jicarilla

Ngome ya Waapache (White Mountain)

San Carlos

Mescalero

[Hisani]

Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.

[Picha katika ukurasa wa 13]

Geronimo

[Hisani]

Kwa hisani ya Arizona Historical Society/Tucson, AHS#78167

[Picha katika ukurasa wa 16]

Harrison Talgo, mwanabaraza wa kikabila

[Picha katika ukurasa wa 17]

Chifu Cochise alizikwa katika ngome yake ya Chiricahua

Sahani za setilaiti huleta programu za televisheni kwa watu wa eneo hili lililotengwa

[Picha katika ukurasa wa 18]

Kwenye maziko ya Waapache jamaa huweka mawe kuzunguka kaburi. Tepe hewani hutoa ishara ya zile sehemu nne za mwelekezo

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki