Ufundi wa Kupamba Bakora
Na mleta-habari wa Amkeni! katika Uingereza
“SIKUZOTE mimi hushangaa kujua kwamba kuna maeneo mazima ya Visiwa vya Uingereza ambamo hakuna mtu yeyote ajuaye unalomaanisha unaposema kwamba hobi yako ni kupamba bakora,” asema mtaalamu mmoja wa ufundi huo.
Wengi wanajua bakora au fimbo ya mchungaji. Upambaji wa bakora hugeuza vifaa hivi vya kawaida viwe vifaa vya kipekee vya kiufundi. Kwa karne kadhaa, wachungaji na wafanyakazi wa shamba wamepata kwamba ufundi huu wenye kuvutia sana huhitaji ustadi mwingi—na subira nyingi sana. Lakini ni nini kinachohusika katika kupamba bakora?
Kuteua Mti
Hatua ya kwanza ni kuteua mti. Mti wowote ulio na vipimo vinavyofaa waweza kutumiwa—blackthorn, mtofaa, au mpea. Mara nyingi mti uitwao holly huteuliwa kwa sababu ya mafundo yake yenye kutokeza na kuvutia. Lakini wengi wa wapambaji wa bakora hupendelea kutumia mbao ya mti hazel. Wakati mwingine mti huwa na mche unaokua pembeni kidogo mwa tawi au mzizi. Hii huwezesha kutengeneza bakora nzima—mahali pa kichwa na mpini—kutokana na sehemu moja ya mti.
Ni wakati upi unaofaa wa kukata mpini? Kwa kawaida wakati mti unapokuwa bwete na utomvu hautiririki, ijapokuwa wengi wa wapambaji wa bakora wanasisitiza kwamba wakati unaofaa ni mara unapoipata—kabla mtu mwingine hajaupata! Kwa vyovyote vile, mara tu mpambaji wa bakora anaporidhika kwamba amekata kipande kinachofaa cha mti, ni lazima apake grisi au atie rangi sehemu zilizokatwa, ili mbao isipasuke. Kisha mbao hiyo lazima ipakwe dawa ya kuihifadhi, hatua ambayo inaweza kuchukua miaka miwili au zaidi. Ndipo basi mpambaji wa bakora anapoweza kuanza kuchonga.
Kuchonga Kichwa
Wakati mti hauna sehemu ya kushikilia ya asili, au kichwa, mpambaji aweza kutengeneza kishikilio akitumia pembe ya ng’ombe, ya kondoo, au ya mbuzi. Kama mpini, pembe hiyo lazima itiwe dawa ya kuihifadhi, kwa kawaida kwa mwaka mmoja. Kisha, akitumia jiliwa, mpambaji wa bakora huunda pembe hiyo kwa njia anayotaka. Kwa karne kadhaa wachungaji wangetumia moto wa mhunzi, maji yaliyochemka, makaa moto ya mboji, au hata joto lililo juu ya taa ya mafuta ili kufanya pembe hiyo ipindike kwa urahisi. Kisha itakuwa tayari kutengenezwa iwe kitu chochote ambacho wazo na ustadi wa mchungaji ungeweza kutokeza. Kwa kielelezo, angechonga mpini ufanane na mbwa, ndege, samaki, kichwa cha kwale, au mnyama mdogo.
Pembe ichongwapo, mpambaji wa bakora huwa makini sana kwa kila jambo. Ikiwa, kwa kielelezo, anaunda mfano wa samaki, mkia na mifupa ya mapezi huchongwa kwa chuma moto na panchi ya mviringo hutumiwa kufanyiza gamba mojamoja. Macho yaweza kutengenezwa kutokana na pembe ya nyati mweusi. Wino, hutumiwa kuupaka mwili badala ya rangi. Zaidi ya mpako mmoja utahitajiwa, na matumizi ya wino kwenye sehemu zilizong’arishwa huenda yakachosha. Hatua ya mwisho ni kuzuia rangi hiyo isitoke kwa kupaka pembe vanishi.
Kazi ya Kiufundi Iliyomalizika
Pembe hiyo huunganishwa na mpini kwa kutumia komeo ya chuma, msumari, au kijiti. Kisha mpambaji wa bakora kwa ustadi husugua kifaa chake cha kiufundi kwa kutumia kitu cha kusugulia sufuria kilicho bora. Halafu, hung’arisha na kuupaka vanishi mpini wake. “Ili kuunda samaki, kukata mapezi, na kadhalika, na ili kuujaza magamba mwili wa samaki, kuupaka rangi ya mwisho ya vanishi kwa ustadi ili iwe nzuri vya kutosha kushinda tuzo katika shindano ingenichukua karibu muda wa saa 100,” aandika mpambaji mmoja wa bakora mwenye uzoefu.
Pasipo shaka upambaji wa bakora ni kazi inayotia ndani mambo mengi. Lakini tokeo la mwisho laweza kuwa kitu kizuri sana cha kiufundi, nyingine hata hupelekwa kwenye mashindano. Kwa vyovyote vile, mpambaji wa bakora huona ufundi wake kuwa kumbukumbu la muhula ulio shwari zaidi, kitu kinachomaliza mikazo na misongo ya maisha ya kisasa.