Kutoka kwa Wasomaji Wetu
Uumbaji Dhidi ya Mageuzi Ule mfululizo “Tulikujaje Kuwapo? Kwa Aksidenti au kwa Ubuni?” (Mei 8, 1997) ulitolewa waziwazi, kwa usahili, na kwa njia ya kimantiki. Nililipata kuwa jambo lenye kusisimua kuona ukurasa baada ya ukurasa ulio na uthibitisho wa kisayansi juu ya uumbaji. Vielezi vilikuwa vyenye kusadikisha. Nilifurahia hasa kusoma tena juu ya chembe na sehemu zake zote. Sijafikiria kwa uzito juu ya utendaji wa mitokondria na Golgi tangu nilipokuwa shuleni, na nilifurahi kufanya hivyo kikamili.
J. S., Marekani
Nikiwa mwanafunzi mtaalamu wa biolojia na mwagnosti wa maisha, nataka kuwashukuru kwa ajili ya makala hizo. Ijapokuwa makala hizo zilirahisisha kupita kiasi mambo fulani . . . , hata hivyo zilielekeza uangalifu kwenye tatizo halisi ambalo sasa linakabili nadharia ya mageuzi: dhana ya karibu ulimwenguni pote ya jumuiya ya wanasayansi ya kutoa heshima yenye kutokeza kwa mageuzi kupitia uteuzi asilia, licha ya matatizo yanayoletwa na kutofautiana kabisa kwa uthibitisho. Sikuzote lazima sayansi ivumilie jaribu linalotokana na wenye kushuku ikiwa itaitwa kwa usahihi sayansi. Kwa kuelekeza uangalifu kwenye udhaifu katika nadharia mpya ya Darwin, hamtoi tu hoja ya kuwa na imani katika Yehova bali pia mnatokeza jambo la kufanyiwa kazi na utafiti wa sayansi wa wakati ujao. Asanteni.
A. S., Marekani
Kuhama Kwa kweli nilithamini sana ile makala “Hesabu Gharama za Kuhama!” (Mei 8, 1997) Ninashuhudia mambo mengi ambayo mliandika juu yake. Nikiwa nimehama kutoka Afrika hadi Ulaya, mimi hukabiliwa daima na mambo yenye kuhuzunisha yanayohusisha jamii, lugha, rangi na, zaidi ya yote, ubaguzi. Vyombo vya habari vinavyopendwa na wengi vimewapa watu maoni yaliyopotoka kuhusu Waafrika na wageni kwa ujumla.
P. A., Ujerumani
Vitumbuizo Asanteni kwa ajili ya makala “Ni Nini Kimepata Vitumbuizo?” (Mei 22, 1997) Nina umri wa miaka 12, na wakati wa mapumziko yangu ya shule, nimekuwa nikitazama televisheni sana. Makala hiyo ilinisaidia nione kwamba kuna mambo mengine ya kutumbuiza niwezayo kufanya.
J. L., Uingereza
Kuhubiri Katika Sehemu za Mashamba ya Afrika Ningependa kuwashukuru kwa ajili ya makala “Afukuzacho Kuku Kwenye Mvua . . . ” (Mei 22, 1997) Ninathamini ujitoaji na uvumilivu wa ndugu zetu katika Nigeria. Hata ingawa walihitaji kukabili nyoka, mamba, na ruba, upendo wao kuelekea watu uliwachochea waendelee. Wakati ambapo nitatoka kwenda kuhubiri na kuhisi joto au uchovu, nitawafikiria ndugu zetu wapendwa katika Nigeria.
S. S., Marekani
Mwenendo wa Kingono—Mitazamo Inayobadilika Ningependa kutoa shukrani zangu za moyo mweupe kwa ajili ya mfululizo “Mwenendo wa Kingono—Kinachomaanishwa na Mitazamo Inayobadilika.” (Juni 8, 1997) Mfululizo huo uliimarisha sana imani yangu. Hivi karibuni mwanamume mmoja katika ujirani aliniambia [mwanamke] kwamba ‘nilikuwa nimelemaa kimwili’ kwa sababu nina umri wa miaka 19 na bado mimi ni bikira. Ninaterema niliweza kumjulisha kwamba mimi ni mwenye afya ya kimwili na ya kiroho machoni pa Yehova.
W. M. C. C., Zimbabwe
Rejezo lenu katika ukurasa wa 10 lisemalo “urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo” si sahihi. Nikiwa mwanafunzi wa Chuo Kikuu wa shahada ya kwanza katika somo la sayansi-biolojia, naweza kuwaambia kwamba “urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo” hurejezea kwenye jeni katika chembeuzi ambayo hujongea ndani ya chembeuzi au kuhamia kwenye chembeuzi mpya. Haihusiani kwa vyovyote na tabia.
L. P., Kanada
Ile taarifa kwamba Mungu hakutufanya tukiwa na “urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo” kwa kweli ilikuwa inarejezea kwenye hotuba iliyotolewa na askofu wa Anglikana wa Edinburgh, Scotland, ambayo sehemu yake ilinukuliwa katika ukurasa wa 4 wa makala hiyo ya “Amkeni!” Askofu huyo alisema kwamba “Mungu . . . ametupatia urithi unaotufanya tufanye ngono ovyoovyo”—kwa wazi likiwa ni jaribio la kutolea udhuru tabia isiyo ya adili. Makala yetu ilifichua upumbavu wa madai ya namna hiyo.—Mhariri.