Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 4/22 kur. 5-8
  • Mambo Tupaswayo Kujua Kuhusu Magenge

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Mambo Tupaswayo Kujua Kuhusu Magenge
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Sababu kwa Nini Wao Hujiunga na Magenge
  • Ni Vigumu Kujiondoa
  • Maisha Yaliyo Bora Yawezekana
  • Je! Nijiunge na Genge?
    Amkeni!—1992
  • Kuwalinda Watoto Wetu na Magenge
    Amkeni!—1998
  • Tatizo Laenea
    Amkeni!—1998
  • “Nilikuwa Nikijichimbia Kaburi”
    Biblia Inabadili Maisha
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 4/22 kur. 5-8

Mambo Tupaswayo Kujua Kuhusu Magenge

Wade, mshiriki wa hapo zamani wa genge la California, alisema: “Tulikuwa tu wajamaa walioishi katika ujirani mmoja. Tulianza shule ya msingi pamoja. Hatukufanya tu maamuzi yaliyofaa.”

MARA nyingi magenge yalianza yakiwa vikundi vya kijirani. Watu waliokuwa katika umri wao wa utineja wa mapema au wachanga zaidi walikusanyika katika pembe moja ya mtaa. Walifanya mambo pamoja kisha wakaungana ili kujilinda na kikundi cha karibu kilichokuwa imara zaidi. Lakini upesi kikundi chao kikaanza kudidimia na kuwa chenye jeuri kama washiriki wake, na kikahusika katika utendaji wa jinai ulio hatari.

Genge la upinzani kutoka mtaa mwingine huenda lilikiona kikundi hiki kipya kuwa adui wake. Kisha hasira ikaongoza kwenye jeuri. Walanguzi wa dawa za kulevya walitumia genge hilo kuuza dawa hizo haramu. Utendaji mwingine wa jinai ulifuata.

Luis alikuwa na umri wa miaka 11 wakati marafiki wake wakubwa walipounda genge. Alipofikisha umri wa miaka 12 alianza kutumia dawa za kulevya. Alipofikisha umri wa miaka 13 alikamatwa kwa mara ya kwanza. Alishiriki katika wizi wa magari, uvunjaji wa nyumba, na unyang’anyi wa kutumia silaha. Na alifungwa jela mara kadhaa kwa sababu ya mapigano ya genge na ghasia.

Nyakati fulani twaweza kushangazwa na washiriki wa magenge. Martha, mwenye sura ya kupendeza, mwanafunzi wa shule ya upili mwenye kufanya vizuri katika masomo, alipata maksi nzuri na alikuwa mwenye tabia nzuri shuleni. Hata hivyo, alikuwa kiongozi wa genge lililoshughulika na bangi, heroini, na kokeini. Haikuwa mpaka mmoja wa marafiki wake alipopigwa risasi mara kadhaa na kuuawa kwamba aliogopeshwa na kutaka kubadili maisha yake.

Sababu kwa Nini Wao Hujiunga na Magenge

Kwa kushangaza, washiriki fulani wa magenge husema walijiunga na magenge hayo ili kupata upendo. Walikuwa wakitafuta urafiki, undani ambao hawakuupata nyumbani. Gazeti la habari Die Zeit la Hamburg, Ujerumani, lilisema kwamba katika magenge ya mitaa vijana hujaribu kutafuta usalama ambao hawawezi kuupata mahali pengine. Eric, aliyekuwa mshiriki wa genge hapo zamani, alisema kwamba ikiwa hupati upendo nyumbani, “unaenda nje kwa watu wasio washiriki wa familia ukitafuta jambo fulani lililo bora zaidi.”

Baba mmoja, aliyekuwa mshiriki wa genge wa hapo zamani, aliandika kuhusu mambo aliyopata katika maisha yake ya mapema: “Nilifungwa jela mara kadhaa kwa sababu ya mwenendo mbaya, mapigano ya genge, ghasia na hatimaye kwa kujaribu kuua kimakusudi kwa kumpiga risasi mtu fulani nikiwa naendesha gari.” Baadaye, alipopata mwana wake Ramiro, alikuwa na wakati mchache sana wa kutumia na mwana huyo. Ramiro alipokua, yeye pia alijiunga na genge, na alikamatwa na polisi baada ya pigano la genge. Wakati baba yake aliposisitiza atoke kwenye genge hilo, alipaaza sauti: “Sasa wao ni familia yangu.”

Muuguzi mmoja katika hospitali ya Texas, ambaye alizungumza na wahasiriwa wachanga 114 waliokuwa wamepigwa risasi kwa kipindi kilichozidi kidogo mwaka mmoja, alisema: “Ni ajabu. Sifikiri nimewahi kusikia mmoja wao akiulizia mama yake au mshiriki yeyote wa familia.”

Jambo la maana ni kwamba, si watoto watokao kwenye sehemu za mji zilizo maskini tu ambao hujiunga na magenge. Miaka kadhaa iliyopita gazeti la Kanada Maclean’s liliwanukuu polisi wakisema kwamba walikuwa wamewapata vijana kutoka sehemu zote mbili za jiji zilizo tajiri sana na za ujirani zilizo maskini sana wakiwa katika genge lilelile. Wachanga hawa kutoka malezi mbalimbali huungana pamoja kwa sababu inayofanana—wanatafuta hisi ya familia ya udugu ambayo hawaipati nyumbani.

Katika maeneo fulani vijana hukua wakiona ushiriki wa genge kuwa njia ya kawaida ya maisha. Fernando mwenye umri wa miaka 16 alieleza: “Wanafikiri kujiunga na genge kutawasaidia watatue matatizo yao. Wao hufikiri: ‘Nitapata marafiki kadhaa. Wao ni wakubwa na hubeba bunduki. Watanilinda, na hakuna mtu atakayenidhuru.’” Lakini punde si punde washiriki wapya hugundua kwamba kuwa katika genge huwafanya wawe shabaha ya maadui wa genge.

Mara nyingi magenge hupatikana katika ujirani ambao kuna pesa kidogo na bunduki nyingi sana. Ripoti za habari husema juu ya madarasa ya shule ya jiji kubwa ambayo wanafunzi 2 kati ya 3 huishi katika nyumba za mzazi asiye na mwenzi. Nyakati nyingine, mzazi wa mwanafunzi ni mraibu wa dawa za kulevya ambaye huenda asije nyumbani usiku, na nyakati nyingine mwanafunzi huyo mchanga akiwa mama asiye na mwenzi lazima ampeleke mtoto wake kwenye kituo cha kutunzia watoto kabla hajaenda shuleni asubuhi.

Gavana wa California, Pete Wilson, alisema: “Tuna tatizo kubwa sana kwa sababu watoto wengi wanakua bila baba, bila kigezo cha kiume cha kuwapa upendo, mwongozo, nidhamu na maadili—bila hisi ya kwa nini wanapaswa kujistahi au kuwastahi wengine.” Alisema kwamba kutoweza huku kwa vijana hawa kushiriki hisia na wengine ni sababu inayofanya “waweze kulipua mtu fulani [kuwapiga risasi hadi wafe] bila kutikisika kwa majuto.”

Ijapokuwa ukosefu wa udugu wa familia, mazoezi ya kibinafsi, na kielelezo thabiti cha adili ni mambo makuu yanayochangia ukuzi wa magenge, mambo mengine pia huhusika. Mambo haya hutia ndani vipindi vya televisheni na sinema ambazo huonyesha jeuri kuwa utatuzi rahisi wa matatizo, jamii ambayo huwaona maskini kuwa watu walioshindwa kufanikiwa maishani na kuwakumbusha sikuzote kwamba hawawezi kufanya mambo ambayo wengine hufanya, na idadi inayokua ya familia za mzazi asiye na mwenzi ambazo mama mchanga mwenye kufanyizwa kazi kupita kiasi lazima ajikaze kutegemeza mtoto mmoja au zaidi wasiosimamiwa. Muungano wa mengi ya mambo haya au wa yote, na labda mengine bado, umeongoza kwenye kukua kwa tatizo la magenge ya mitaani ulimwenguni pote.

Ni Vigumu Kujiondoa

Kweli, baada ya muda fulani washiriki fulani wa genge huondoka pole kwa pole kutoka kwenye genge lao, wakijishughulisha na utendaji mwingine. Wengine waweza kwenda kuishi na jamaa zao katika eneo jingine na hivyo kuponyoka maisha ya genge. Lakini mara nyingi, kujiondoa kutoka kwenye genge haliwi jambo rahisi.

Kwa kawaida, washiriki wa genge lazima wapatwe na mapigo yenye jeuri kutoka kwa washiriki kadhaa kabla ya kuruhusiwa kuliacha genge wakiwa hai. Kwa kweli, watu waliotaka kuondoka kwenye magenge fulani kwa hakika walilazimika kuteseka kwa kupigwa risasi. Ikiwa waliokoka, waliruhusiwa kuondoka! Je, inastahiki kutendwa vikali namna hiyo ili kuondoka kwenye genge?

Mshiriki mmoja wa genge wa hapo zamani alieleza kwa nini alitaka kutoka: “Marafiki wangu watano tayari wamekufa.” Kwa kweli, maisha ya kuwa mshiriki wa genge yaweza kukaribia kuwa yenye hatari isivyoaminika. Gazeti Time liliripoti kuhusu mshiriki mmoja wa genge la Chicago wa hapo zamani: “Katika kazi-maisha yake ya miaka saba, amepigwa risasi tumboni, akapigwa kichwani na chuma ya kuunganishia reli, akavunjwa mkono wake katika pigano na kufungwa jela mara mbili kwa wizi wa gari . . . Lakini sasa kwa kuwa hatimaye hahusiki na utendaji wa jinai hata marafiki wake wa zamani wananuia kumdhuru.”

Maisha Yaliyo Bora Yawezekana

Eleno, Mbrazili, wakati mmoja alikuwa mshiriki wa Headbangers, genge lililopigana kwa visu na nyakati nyingine bunduki. Akihisi kuwa amenyimwa haki za kimsingi za kijamii, alipata uradhi kwa kuvunja vitu na kuwashambulia watu. Mfanyakazi mwenzi alizungumza naye kuhusu Biblia. Baadaye Eleno alihudhuria kusanyiko la Mashahidi wa Yehova, ambapo alikutana na washiriki wa hapo zamani ambao walikuwa wametoka katika genge lake na vilevile mshiriki wa hapo zamani wa genge la upinzani. Walisalimiana kama ndugu—tofauti kabisa na vile ingaliweza kutokea hapo awali.

Je, kwa kweli jambo hili hutukia? Kwa kweli hutukia! Hivi karibuni mwakilishi wa Amkeni! aliketi pamoja na washiriki wa hapo zamani wa magenge makubwa katika Los Angeles ambao sasa hutumika pamoja na makutaniko ya Mashahidi wa Yehova. Baada ya saa kadhaa za mazungumzo, mmoja wao alitua, akaegemea kiti chake, na kusema: “Ona jambo hili! Washiriki wa hapo zamani wa magenge ya Bloods na Crips wakiketi hapa wakipendana kama ndugu!” Walikubali kwamba badiliko lao kutoka kuwa washiriki wakatili wa genge hadi kuwa wanaume wenye fadhili na upendo lilikuwa tokeo la uhakika wa kwamba walikuwa wamejifunza kanuni za kimungu kupitia funzo lenye uangalifu la Biblia.

Je, jambo hili lingeweza kutukia katika miaka ya 1990? Je, washiriki wa magenge kwa kweli waweza kufanya mabadiliko sasa? Wanaweza ikiwa wako tayari kutafuta kitia-moyo chenye nguvu kinachoandaliwa katika Neno la Mungu kisha kupatanisha maisha zao na kanuni za Biblia. Ikitukia kwamba wewe ni mshiriki wa genge, kwa nini usifikirie kufanya badiliko?

Biblia hutuhimiza ‘tuweke mbali utu wa hapo zamani unaofuatana na njia yetu ya kwanza ya mwenendo’ na ‘tuvae utu mpya ulioumbwa kulingana na mapenzi ya Mungu katika uadilifu wa kweli na uaminifu-mshikamanifu.’ (Waefeso 4:22-24) Huo utu mpya husitawishwaje? “Kupitia ujuzi sahihi,” Biblia husema, utu wa mtu waweza ‘kufanywa kuwa mpya kulingana na mfano wa Mungu aliyeuumba.’—Wakolosai 3:9-11.

Je, inastahili kujaribu kufanya badiliko kama hilo? Ndiyo, inastahili! Ikiwa wewe ni mshiriki wa genge, huenda utahitaji kufanya badiliko hilo. Kuna watu katika ujirani wako ambao wataterema kukusaidia. Lakini, mara nyingi wazazi huwa katika nafasi ya kudhihirisha uvutano unaofaa ulio mkubwa zaidi juu ya watoto wao. Kwa hiyo sasa tutafikiria yale wazazi wawezayo kufanya ili kuwalinda watoto wao na magenge.

[Picha katika ukurasa wa 7]

Washiriki wa hapo zamani wa magenge yenye kushindana sasa wameunganishwa na kweli ya Biblia

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki