Uvutio wa Vitabu Vidogo Sana
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
KUZIDI mipaka huvutia sana—mlima mrefu zaidi, bahari yenye kina kirefu zaidi, jengo refu zaidi, mtaro mrefu zaidi—hivyo, namna gani kitabu kilicho kidogo zaidi? Vitabu vidogo sana huvutia! Mamilioni yavyo yamechapishwa, kuhusu kila somo linaloweza kufikirika kwa angalau lugha 20. Ikiwa hujavinjari ulimwengu wa vitabu vidogo sana, sasa pata habari fupi kuuhusu.
Twaweza kufasilije kitabu kidogo sana? Kanuni inayokubalika huwa ni kitabu kisichozidi milimeta 76 kwa urefu au upana. Vipimo hivi hutia ndani jalada, ijapokuwa wakusanyaji fulani wenye uangalifu hupendelea zaidi kutia ndani tu kurasa za kitabu. Kwa nini mabuku ya vitabu vidogo sana hivi yalichapishwa?
Pande za Ufundi Huu
Kinyume cha vile mtu angetarajia, vingi vya vitabu hivi vidogo sana ni vyenye kusomeka kabisa. Vijitabu-mwaka, maandishi yaliyo maarufu, riwaya, tamthilia, kamusi, na maandishi matakatifu yaweza kuchukuliwa na kutumiwa kwa jitihada kidogo. Ijapokuwa miaka kadhaa iliyopita hii ingekuwa sababu kuu ya kuwa na mabuku hayo yaliyo madogo sana, mkusanyaji wa kisasa anahangaikia zaidi jambo jingine linalohusu vitabu vidogo sana: ufundi wa wale ambao walivichapisha na kuvijalidi.
Wachapishaji walihitaji kukabili matatizo mengi ya kiufundi ili kuunda na kupiga chapa herufi ambazo zingesomeka, kwa kutumia au bila kutumia kiookuzi. Nyingi ya kazi yao imetokeza vitabu vilivyo na uzuri mwingi. Watengenezaji wa karatasi na wino pia walitoa ujuzi wao ili kuhakikisha uwazi ulio safi kabisa wa ukurasa uliochapwa.
Baada ya kitabu kuchapishwa, kinajalidiwa; na kujalidi vitabu vidogo sana kwaweza kuwa bora sana. Ufundi wa msanii huonekana wazi katika kutokezwa kwa jalada ndogo sana zilizotiwa nakshi za ngozi, dhahabu au temsi ya fedha, gamba la kobe, au gamba la jino lililorembeshwa. Jalada nyingine ni za hariri au mahameli au zimetariziwa au hata kurembeshwa na lulu na puleki, na vitabu fulani vina bweta la kuvihifadhi linalofunuka upande mmoja.
Watiaji nakshi waliotolea kielezi maandishi hayo walibuni picha zilizokuwa na mambo mengi isivyoaminika, mara nyingi zikisambaa kwenye sentimeta mbili na nusu mraba za karatasi! Kielelezo kimoja ni ile picha ya Dakt. Samuel Johnson, mtunga-kamusi Mwingereza, katika kitabu chenye kurasa 368 Bryce’s Thumb English Dictionary, kilichochapishwa katika miaka ya 1890; na kingine katika kielezi kinachoelekeana na ukurasa wenye kichwa wa kitabu cha Shakespeare King Richard III, kilichotolewa katika mwaka wa 1909 kwa heshima ya mchezaji Mwingereza Ellen Terry.
Kile kitabu Bibliothèque Portative du Voyageur, kilichochapishwa huko Paris, ni maktaba ndogo ambayo inafikiriwa kuwa ilichukuliwa na Napoléon Bonaparte wakati wa kampeni zake za kijeshi. Mabuku yake 49 ya maandishi ya Kifaransa yaliyo bora sana huwekwa ndani ya sanduku lililofunikwa kwa ngozi, ambalo linapofungwa huonekana kama kitabu kikubwa kinachotoshana na folio.
Biblia Gumba
Biblia Gumba si lazima ziwe Biblia nzima. Nyingine ni “Agano Jipya tu.” Nyingine ni muhtasari wa hadithi za Biblia au huwa na historia nzima ya Biblia ikiwa imefupishwa kufikia karibu maneno 7,000, na zilibuniwa hasa kwa ajili ya kusomwa na watoto. Zina vichwa kama vile The Bible in Miniature, The History of the Holy Bible, na The Child’s Bible.
Biblia gumba ilipataje jina lake? Ufafanuzi ulio wazi ni kwamba Biblia hiyo ni kubwa kidogo tu zaidi ya ncha ya kidole gumba cha mwanadamu. Na bado kitabu Three Centuries of Thumb Bibles hudokeza kwamba maneno hayo huenda yalitungwa kufuatia ziara ya Mmarekani mmoja mfupi sana Charles Stratton huko Uingereza, anayejulikana vyema kuwa Jenerali Tom Thumb. Jambo linalounga mkono dai hili ni uhakika wa kwamba Tom Thumb alizuru Uingereza katika mwaka wa 1844 na maneno “Biblia gumba” yaonekana kuwa yalitumiwa kwa mara ya kwanza katika London katika mwaka wa 1849.
Mabuku ya Maandiko Yasiyo ya Kawaida
Tunu iliyoongezewa kwenye ulimwengu wa Biblia ndogo ni The Finger New Testament, iliyochapishwa karibu mwanzoni mwa karne ya 20. Ina upana wa sentimeta tatu tu na urefu wa sentimeta tisa—urefu wa kidole—kwa hiyo, ikapewa jina hilo. Hata hivyo, kwa kuwa ina urefu unaozidi milimeta 76, tukisema kwa kweli, si kitabu kidogo sana, ijapokuwa kwa kawaida huainishwa pamoja na Biblia kama hizo. Herufi zake ndogo sana za chapa, zilizotumiwa katika buku hili ndogo ni dhahiri kabisa na huweza kusomwa na wengi bila kuzikuza.
Kielelezo kimoja kisicho cha kawaida kina kichwa The Illustrated Bible, chenye mashairi yaliyo na kichwa Railway to Heaven. Kiliendelea kuchapishwa kwa zaidi ya miaka 50 wakati wa siku za mapema za ujenzi wa reli za Uingereza. Mwandishi akitumia reli kujifaidi aliandika shairi la kurasa mbili, lenye kichwa “Kuwaelekeza Kwenye Njia Nyingine.” Njia hiyo nyingine inatambulishwa kuwa “Yesu Kristo, Mwana wa Yehova.” Shairi hilo lamalizia: “Mwana wangu, asema Mungu, elekeza moyo wako kwangu. Fanya hima—ama sivyo utaachwa na gari moshi.”
Pia buku lisilokuwa la kawaida ni lile lililoitwa My Morning Counsellor, la mwaka wa 1900. Linakazia andiko la kila siku la Biblia, na kila mwezi hutangulizwa na namna fulani ya jina la Mungu. Kwa kielelezo, namna ya Februari, ni “Yehova-Shalom.” Vyote viwili kitabu hiki na The Illustrated Bible, kilichotangulia kutajwa, huonyesha uhakika wa kwamba Yehova, jina la Mungu, lilitumiwa kwa ukawaida katika Uingereza miaka mia moja iliyopita.
Ni Kitabu Kipi Kilichokuwa Kidogo Zaidi?
Kwa karne kadhaa madai yamefanywa kuhusu ni kitabu kipi kilichokuwa kidogo zaidi kuchapishwa. Dai halali la kwanza lilifanywa katika mwaka wa 1674 wakati kitabu cha C. van Lange kilipochapishwa kwa chapa ndogo sana. Kilifafanuliwa na Miniature Books kuwa “ukubwa wa ukucha wa kidole,” na kilishikilia rekodi kwa zaidi ya miaka 200.
Chapa iliyopendwa sana ya Dante La Divina Commedia ilichapishwa kwa herufi ndogo sana, na ilifikiriwa kuwa chapa iliyo ndogo zaidi kutumiwa—ambayo ilikuwa ngumu sana kusomeka kwa kutumia macho tu bila kifaa chochote. Kitabu hicho kilitolewa katika Padua, Italia, mwaka wa 1878. Ilichukua muda wa mwezi mmoja kuchapisha kurasa 30, na chapa mpya ilikuwa ya lazima kwa ajili ya kila mtindo wa maandishi. Licha ya hilo, nakala 1,000 zilichapishwa.
Kupunguzwa kwa ukubwa kuliendelea. Katika mwaka wa 1978, beti za watoto Three Blind Mice zilizotolewa na Matbaa ya Gleniffer huko Paisley, Scotland, zikawa “kitabu kidogo sana ulimwenguni.” Chapa hii ndogo ilishindwa katika mwaka wa 1985 na wachapishaji walewale wakati walipotoa nakala nyingine 85 za beti za watoto, zilizoitwa Old King Cole! Kila nakala ilikuwa na kipimo cha milimeta moja kwa milimeta moja tu. Kurasa zaweza kufunguliwa—kwa kutumia sindano!
Vitabu hivyo vilivyo vidogo sana, vilivyofafanuliwa na Louis Bondy kuwa “kama mavumbi madogo sana,” hutoa uthibitisho kemkem wa saburi na usanii. Hata hivyo, vitabu hivi vidogo sana, vimezidi kusudi la awali la vijitabu ambalo lilikuwa kutoa vitabu ambavyo vingesomeka na kutumiwa kwa utayari.
Mkusanyo mzuri wa mabuku ya vitabu hivi vidogo sana vyenye kupendeza waweza kuonwa katika majumba ya makumbusho vingine vingi vinamilikiwa na watu binafsi. Ikiwa kwa vyovyote utazuru ulimwengu wao wenye kuvutia, kumbuka kuvitumia vitabu hivi vidogo kwa makini sana. Kwa kweli ni kazi ya akili ya kiufundi!
[Sanduku/Picha katika ukurasa wa 14]
Kupunguza Ukubwa wa Chapa kwa Mashine
Biblia ya “Agano Jipya” iliyo ndogo zaidi kupata kutolewa ilikuwa ya David Bryce, wa Glasgow, Scotland, katika mwaka wa 1895. Ina urefu wa sentimeta 1.9 kwa upana wa sentimeta 1.6 na unene wa sentimeta 0.8! Iliwezekanaje kuichapisha? “Ilichapishwa vizuri sana kwa kutumia njia ya kupunguzia ukubwa wa chapa kwa mashine,” aeleza Louis Bondy katika Miniature Books. Upigaji wa picha ukiwa umeanzishwa tu miaka mia moja iliyopita, hili lilikuwa fanikio kubwa sana.
Pia David Bryce alichapisha idadi kadhaa za Biblia Gumba akitumia njia hiihii. Kwa wale walio na tatizo la kusoma nakala ndogo sana, kila Biblia ina kiookuzi kidogo kilichotiwa ndani ya jalada la kuunganisha. Wakitumia msaada huu, kusoma kwawezekana kwa wale wanaostahimili.
Inafaa kuangaliwa kwamba njia ya kuchapisha vichapo vilivyopunguzwa ukubwa kwa kutumia mashine ilitumiwa kwa kufaa na Mashahidi wa Yehova wakati waliponyanyaswa na Wanazi wakati wa Vita ya Ulimwengu ya Pili na baadaye na Wakomunisti. Unaoonekana katika kielezi kinachoandamana ni msaada wa kujifunzia Biblia uliochapishwa kwa kutumia njia hii. Kikiwa kimefichwa ndani ya ganda la kiberiti, kiliingizwa kisiri ndani ya kambi ya mateso ya Nazi kwa ajili ya Mashahidi waliokuwa katika kambi hiyo.
Hiki hutoshea ndani ya ganda la kiberiti na kiliingizwa kisiri ndani ya kambi ya mateso
[Picha katika ukurasa wa 13]
Ijapokuwa ni vidogo, vitabu vidogo sana vyaweza kusomeka
[Picha katika ukurasa wa 15]
Maktaba ya vitabu vidogo sana