Kushona Sweta—Katika Patagonia
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA ARGENTINA
“NAHISI baridi!” Katika maeneo yaliyo na halijoto ya wastani, ni nani ambaye hajatamka maneno hayo wakati fulani? Na huenda itikio lilikuwa, ‘Sweta yangu iko wapi?’
Ikiwa wewe ni mmoja wa mamilioni ya watu wanaovalia sweta, je, umewahi kuwazia jinsi ilivyoshonwa? Sufu husokotwa namna gani? Rangi hupatikana namna gani? Hapa katika Argentina tuna Wahindi wenyeji ambao hufanya kazi hii yote kwa mkono. Hebu tuwazuru tuone jinsi wanavyoifanya.
Kushona Sweta kwa Mtindo wa Zamani
Idadi fulani ya watu wa Mapuche, kabila la Kihindi la watu wa Araucania, huishi kusini ya Patagonia, katika Argentina. Wao hutumia njia za kitamaduni za kusokota sufu na kuitia rangi. Katika majira ya masika ya Kizio cha Kusini, kuelekea mwisho wa Novemba na mwanzoni mwa Desemba, wao hunyoa kondoo, wakitumia makasi ya pekee yaliyotengenezwa kwa feleji. Unyoaji-kondoo ni ufundi unaostahili kuonwa!
Bila shaka, sufu itokapo kwa kondoo, huwa na nyasi, mimea, na madonge ya udongo. Hivyo inapasa kufuliwa kikamili. Hili hufanywa kwa kuilowesha ndani ya maji moto kisha kuianika ili ikauke. Kisha, taka zilizobakia huondolewa. Hatua hii hujulikana kuwa escardado, au kuchambua sufu. Hatua hii ifanywapo sawasawa, sufu itakuwa safi, itakauka, na kuwa nyororo sana. Hii yamaanisha kwamba lundo la manyoya ya kondoo liko tayari kugeuzwa kuwa sufu ya kufumia, au kitani.
Kuna njia mbili za kitamaduni za kusokota kitani. Katika njia moja, pia hutumiwa. (Ona picha 1.) Msokotaji hugeuza sufu kuwa kitani kwa kuisokota kwenye pia huku akisugua sufu kwenye miguu yake kwa mkono mmoja na kuisuka. Kisha kitani hurundikana kwenye pia. Unene wa kitani huamuliwa na kiasi cha sufu iliyozungushwa kwenye pia.
Katika njia ile nyingine ya kufuma kitani, gurudumu la kusokotea nyuzi hutumiwa, ambalo msokotaji hulizungusha kwa kukanyaga kifaa cha miguu. Sufu huingizwa ndani ya gurudumu hilo kupitia kwenye tundu, na msokotaji huamua unene wa kitani. (Ona picha 2.) Mara kitani kinapofanyizwa, chaweza kufanywa kuwa mpira halisi wa sufu ambao wanawake wengi hununua. Lakini namna gani kutia sufu rangi tofauti? Jambo hili hufanywa jinsi gani?
Watu wa Mapuche hutengeneza rangi kutokana na mizizi au mimea fulani kwa kuichemsha kwa muda wa karibu nusu saa ndani ya maji yenye chumvi kidogo. Njia hii hufanana na namna Wahindi fulani wa Navajo katika Arizona, Marekani, hutengeneza rangi za blanketi ambazo wao hufuma. Katika Argentina, ili kupata rangi ya kimanjano, watu wa Mapuche huchemsha mizizi ya mti mfupi unaoitwa michai, jina la Kihindi kwa mmea ujulikanao kuwa Berberis darwinii; ili kupata rangi ya kikahawia yenye madoa meupe, wao hutumia majani ya mti mfupi unaojulikana kuwa radal, au kokwa za mwitu; ili kupata rangi nyekundu, wanatumia viazisukari vyekundu. Ingawa mtindo huu huchosha, rangi hizo hazichujuki kwa urahisi. Sasa, vitani vyote vikiwa vimetiwa rangi, twaweza kuanza kufuma sweta.
Kufuma—Kwa Mitindo Mbalimbali
Kwa karne kadhaa wanawake wametumia sindano za kufumia ili kuunganisha sufu kuwa kitambaa bapa ambacho baadaye chaweza kushonwa kuwa vazi. Sindano nne zaweza kutumiwa kufuma soksi, mikono, na maumbo ya neli. Chanzo kimoja husema kwamba huenda ufumaji ulianzia Arabia karibu mwaka wa 200 W.K. Kisha ufundi huu ulisambaa Ulaya, na kisha Wahispania wakapeleka ufumaji katika Amerika Kusini na Kati katika karne ya 16, ijapokuwa ufundi huu huenda ulijulikana mapema na baadhi ya wakulima wadogo waliokuwa wenyeji.
Mfumaji wetu mwenye urafiki sasa auliza, “Ungependa sweta iwe na uzito wa kadiri gani?” Jibu lake litaamua upana wa sindano na unene wa sufu atakayotumia. Kisha, “Ungependa rangi zipi?” Jambo hilo likishaamuliwa, sasa anaweza kuanza kufuma.
Linalowashangaza watu wasiofahamiana na ufumaji ni kwamba ufundi wa ufumaji waweza kutia ndani mishono miwili ya msingi—mshono usio na mapambo, na wa kupindwapindwa. Mshono wa kupindwapindwa ni mshono usio na mapambo uliogeuzwa ili kutokeza matuta. Kwa kuiunganisha, mishono hii miwili ikitumiwa pamoja yaweza kutokeza sampuli mbalimbali.
Mfumaji wetu hushona sweta kwa sehemu, kisha hizi huunganishwa pamoja—sehemu ya mbele, ya nyuma, mikono, na shingo—kufanyiza bidhaa iliyomalizika. Bila shaka, huchukua saa kadhaa, hata siku, kushona vazi. Hivyo upokeapo moja kama zawadi, usiione kuwa ya kawaida! Wakati mwingi na jitihada yenye subira zilitiwa ndani.
Njia za Kisasa
Tangu mvuvumko wa kiviwanda, mashine zimevumbuliwa ambazo zaweza kufuma maelfu ya sweta kwa muda mfupi sana. Leo mashine hizi za kufumia za kiviwanda mara nyingi huendeshwa na kompyuta. Wanawake wengi hutumia mashine ndogo zaidi nyumbani, ambayo huokoa wakati mwingi sana.
Katika Patagonia, ufumaji bado ni jambo kubwa la familia ambamo mama hufuma na mume na watoto husaidia kukamilisha kikorokoro kilichomalizika. Mara nyingi, wao hutumia mashine ya kufumia ya nyumbani na kisha kuuzia kiwanda cha kushonea sweta zao lao la ziada. Jambo hili hutegemeza bajeti ya familia.
Je, Utanunua Sweta?
Ni jambo gani upaswalo kufikiria ikiwa wataka kununua sweta? Ikiwa wataka sweta iliyoshonwa kwa mkono, labda utalipa pesa zaidi, kwa hiyo waweza kupata iliyo bora zaidi uwezayo kwa bei hiyo. Chagua sweta yako kwa uangalifu, kulingana na mahitaji yako, na chunguza thamani yake. Unaweza kufanyaje hivyo? Chunguza uone jinsi vipande vilivyofumwa vya vazi vilivyomalizwa na ikiwa shingo yatoshea vizuri. Tazama msokotano na mchanganyiko wa kitani. Je, ni sufu safi asilimia 100? Je, ni mchanganyiko? Inapovutwa, je, hupoteza unyumbuko wake na kubaki ikiwa imevutika, au hurudi kwenye umbo lake la awali? Baada ya kufanya ununuzi wako, kila wakati uvaapo sweta yako, fikiri juu ya kazi yote iliyohusika, hasa ikiwa ilishonwa kwa mkono katika Patagonia!
[Ramani katika ukurasa wa 22]
AMERIKA KUSINI
ARGENTINA
Patagonia
[Hisani]
Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.
[Picha katika ukurasa wa 23]
1. Kutumia pia kufanyiza kitani
2. Gurudumu la kusokotea nyuzi ndiyo njia ya haraka zaidi ya kusokota kitani
3. Uchunguzi wa jinsi ambavyo sufu huingizwa ndani ya gurudumu la kusokotea nyuzi
4. Kufuma kwa njia ya kitamaduni
5. Vipande vya mbele vya sweta
6. Mashine ya kufumia ya kisasa inayoendeshwa na kompyuta