Uvutio wa Tufeni Pote wa Muziki wa Kilatini
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA MEXICO
ZAIDI ya watu milioni 400 ulimwenguni pote huzungumza lugha ya Kihispania. Lugha ya Kihispania hufuata Kimandarin na Kihindi kwa kuwa na wasemaji wenyeji wengi zaidi kuliko lugha nyingineyo. Basi haishangazi kwamba watu wengi wanafahamu muziki wa Amerika ya Latini. Ulimwenguni pote watu wamefurahia kusikiliza na kucheza dansi muziki wa mambo, cha-cha, merengue, au salsa.
Kwa nini muziki huu wapendwa sana? Sababu moja ni kwamba ni muziki motomoto wenye kuchangamsha. Waamerika wengi wa Kilatini hupenda muziki wa haraka-haraka wa kitropiki. Baadhi ya midundo hii ililetwa Amerika ya Latini na watumwa wa Afrika Magharibi mamia ya miaka iliyopita. Ni kweli kwamba watu fulani ambao si Walatini hupata ugumu wa kufurahia baadhi ya muziki wa haraka-haraka wenye midundo inayojirudia-rudia.
Muziki wa Kilatini pia waweza kuwa wa polepole, wa kimahaba, na hata wa kuhuzunisha. Kwa kielelezo, bolero ya Amerika ya Latini imependwa sikuzote katika nchi nyingi. Kwa kawaida bolero ilichezwa na watu watatu na ilijulikana kwa namna yake ya kimahaba na ya kishairi. Ilipendwa sana katika miaka ya 1940 na 1950, na hivi majuzi bolero imeanza kupendwa sana na wanamuziki wachanga. Wachezaji wa bendi za mitaani za Mexico, wenye mavazi yenye kupendeza, chapeo kubwa, na muziki wa kipekee, pia wanatambuliwa ulimwenguni pote.
Merengue, Salsa, na Muziki wa Mexico-Amerika
Muziki wa merengue na salsa umependwa sana katika nchi nyingi. Huo si muziki mpya. Muziki wa merengue ulianza katika Jamhuri ya Dominika na Haiti. Umefafanuliwa kuwa ‘muziki wa haraka sana, wa kujirudia, wa kushawishi, na wa kupendeza.’ Neno la Kihispania merengue lamaanisha ule mchanganyiko ambao umekorogwa sana wa sukari na ute wa mayai. Baada ya kutazama namna wachezaji wa dansi hiyo hucheza kwa nguvu, mtazamaji aweza kuona kwa urahisi kwamba jina hilo lafaa.
Kuna aina nyingi za muziki wa salsa, nyingi zikiwa zimetokea Kuba na Puerto Riko. Neno la Kihispania salsa humaanisha “mchuzi.” Kulingana na watu fulani, muziki wa salsa ni mchanganyiko wa muziki uliotokea katika New York City, ambapo mchanganyiko wa wanamuziki kutoka Karibea yote walichangamana. Kutoka hapo ukaenea ulimwenguni pote.
Mauaji ya Selena aliyekuwa mwanamuziki wa asili ya Amerika ya Latini katika Marekani, katika mwaka wa 1995, yalifanya nyimbo zake zipendwe zaidi ya zilivyopendwa alipokuwa hai. Alijulikana kuwa malkia wa muziki wa Mexico-Amerika, ambao umefafanuliwa kuwa mchanganyiko wa muziki wa Amerika na wa norteño (Mexico kaskazini). Nyimbo hizi huimbwa katika Kiingereza, Kihispania, au kwa kuchanganya Kihispania na Kiingereza. Muziki huu umependwa sana na Walatini walioko Marekani na Amerika ya Latini.
Mtazamo Uliosawazika wa Muziki na Kucheza Dansi
Muziki, kama vile vitu vingine viwezavyo kuleta raha, waweza kufurahiwa zaidi ukiwa wenye kiasi. (Mithali 25:16) Wakristo ni wateuzi wa muziki. Biblia huonya kwa upole: “Fulizeni kuangalia sana kwamba jinsi mnavyotembea si kama wasio na hekima bali kama watu wenye hekima, mkijinunulia kabisa wakati unaofaa, kwa sababu siku ni za uovu.” (Waefeso 5:15, 16) Inajulikana sana kwamba nyimbo fulani zina ujumbe wa kukufuru, usio wa kiadili, au hata wa kishetani. Muziki wa Kilatini umeathiriwa na mambo hayo.
Nyimbo fulani za Kilatini zina maneno machafu. Nyingine zina maneno yenye maana mbili, huku nyingine zikiwa za mahaba sana au kutaja wazi mambo ya kingono. Masuala ya kisiasa, jeuri na uasi hukaziwa sana katika nyimbo kadhaa. Kwa kielelezo, wimbo wa Kimexico unaoitwa corrido umependwa sana na Walatini wengi. Hata hivyo, hivi karibuni namna mpya ya corrido uitwao narco corrido unazidi kupendwa. Nyimbo hizi husimulia hadithi zenye jeuri za walanguzi wa dawa za kulevya na kuwaonyesha kuwa mashujaa. Nyimbo nyingine za bendi za mitaani za Mexico pia huendeleza ujumbe wenye kuudhi, zikitukuza ulevi, utukuzo wa wanaume, au utukuzo wa taifa. Kuna mahangaiko kama hayo kuhusu maneno ya nyimbo katika muziki wa merengue, salsa, na aina nyinginezo za muziki wa Kilatini.
Watu fulani ambao hupendezwa na muziki wa Kilatini hawaelewi maneno ya nyimbo hizo. Bila kujua wanaweza kujipata wakifurahia nyimbo ambazo hutukuza ukosefu wa adili katika ngono, jeuri, au hata mambo ya kimafumbo. Wale wanaojua lugha ya Kihispania waweza kukosa kutambua maneno ya nyimbo zenye kutiliwa shaka wanapocheza dansi kwa kufuatana na muziki wenye kuvutia na wenye kufurahisha. Hata hivyo, kustahi sana viwango vya Biblia, kwapaswa kutusukuma kuchunguza kwa makini kila wimbo uchezwao nyumbani mwetu na katika vikusanyiko vya kirafiki. Hili litatuzuia kutosikiliza au kucheza dansi kwa kufuatana na midundo ya nyimbo zilizo na maneno yanayomchukiza Mungu.
Pia twapaswa kuwa waangalifu tusije tukawakwaza wengine kwa namna tunavyocheza dansi. (1 Wakorintho 10:23, 24) Wakristo huwa waangalifu wasicheze dansi kwa kujiachilia mno kwa njia inayopoteza adhama yao. Wala hawangecheza dansi ya kujinengua kimakusudi. Wenzi waliofunga ndoa hudhihirisha uamuzi unaofaa ili kwamba kucheza dansi kwao kusiwe wonyesho wa hadharani wa usiri wa ndoa.
Usawaziko wa Kikristo huhitaji kiasi kuhusu kiasi cha sauti ya muziki unaochezwa na muda unaotumiwa katika vikusanyiko vya kirafiki. Bila shaka, waabudu wa Yehova wanaweza kufurahia uchaguzi wao wa muziki bila kujihusisha katika “sherehe zenye kelele za ulevi na ulafi” ambazo huendelea hadi usiku wa manane na ambazo huwa na muziki wenye vishindo vikuu. Biblia hutuhimiza hivi: “Wakati ambao umepita watosha kwenu kuwa mmefanyiza mapenzi ya mataifa wakati mlipoendelea katika vitendo vya mwenendo mlegevu, uchu, mazidio ya kunywa divai, sherehe zenye kelele za ulevi, mashindano ya kunywa, na ibada haramu za sanamu.”—1 Petro 4:3.
Ujapokuwa mweneo wa mambo yasiyo ya kiadili katika vitumbuizo vya leo, bado kuna namna nyingi za muziki unaofaa ambao mtu aweza kufurahia. Muziki ni zawadi nzuri kutoka kwa Mungu, na Biblia husema kwamba kuna “wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu . . ., wakati wa kuomboleza na wakati wa kucheza.” (Mhubiri 3:1, 4) Ikiwa wapenda muziki wenye uchangamfu na wenye kupendeza, bila shaka utafurahia kusikiliza na kucheza dansi muziki wenye kuvutia wa Kilatini, ukifanya hivyo kwa kiasi na usawaziko wa Kikristo.—1 Wakorintho 10:31; Wafilipi 4:8.