Sababu Inayofanya Wengi Wakatae Damu
KATIKA ule ulioitwa uamuzi wenye maana sana, mahakama ya Ontario ilitangaza shirika la Msalaba Mwekundu la Kanada kuwa lenye hatia kwa ambukizo la HIV kwa watu wawili waliopokea damu—hao wawili walipokea damu yenye viini kutoka kwa mpaji yuleyule mmoja. “Kitu kinachoweza kuleta msiba kama vile damu isiyo safi kinapotisha uhai wa watu,” akasema Hakimu Stephen Borins, “hatua ya dharura huhitajiwa.”
Katika miaka ya 1980, Wakanada wapatao 1,200 waliambukizwa HIV, na wengine 12,000 zaidi waliambukizwa mchochota-ini aina ya C—maambukizo yote yalitokana na damu isiyo safi. Ili kusaidia kupunguza idadi ya maambukizo, watoaji-damu wanachunguzwa kwa uangalifu hata zaidi. Lakini si watoaji-damu wote walio wanyoofu kuhusu maisha yao ya kingono. Kwa kielelezo, uchunguzi uliofanywa Marekani ulifunua kwamba mtoaji-damu 1 kati ya 50 alikosa kuripoti mambo yenye kuhatarisha, kama vile ugoni-jinsia-moja au kufanya ngono na kahaba.
Jambo linalotatanisha hata zaidi ni kwamba kuchuja damu hakukosi hitilafu. Kulingana na gazeti New Scientist, “mtu atoapo damu katika muda unaopungua majuma matatu baada ya kuambukizwa HIV, upimwaji wa kisasa hukosa kugundua virusi hivyo. Huenda upimwaji wa damu ukakosa kugundua mchochota-ini aina ya C zaidi ya miezi miwili baada ya kuambukizwa.”
Katika miaka ya juzijuzi, kumekuwako upungufu mkubwa wa Wakanada walio tayari kutoa—au kupokea—damu. Mwandikaji wa makala za gazeti Paul Schratz aandika: “Kukiwa na upungufu wa wale wanaopendezwa kutoa damu, na ongezeko la wanaokataa kutoa damu, tunashukuru kwamba Mashahidi wa Yehova wamekuwa kwenye mstari wa mbele katika utafiti wa vibadala vya damu.”
Kwa kupendeza, The Toronto Star laripoti kwamba katika mwaka mmoja hivi karibuni, watu wapatao 40 “waliingia katika hospitali za Kanada wakidai kwa uwongo kuwa Mashahidi wa Yehova kwa sababu hawakutaka kutiwa damu mishipani.” Uchunguzi waonyesha kwamba karibu asilimia 90 ya Wakanada wangependelea tiba ya badala kuliko kutiwa damu. Kwa hiyo, matumizi ya damu si suala la kidini tena.