Usanifu-Ramani—Msingi wa Kuufahamu Ulimwengu
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA KANADA
“Paradiso iko sehemu fulani katika Mashariki ya Mbali. Yerusalemu ndicho kitovu cha mataifa yote na nchi zote, na ulimwengu wenyewe ni diski bapa iliyozungukwa na bahari za maji. Ndivyo watawa wa kiume, watayarishaji wa ramani wa Enzi za Kati, walivyouona ulimwengu walimoishi ndani yake.”
MANENO hayo yalitumiwa katika utangulizi wa The Reader’s Digest Great World Atlas na wahariri wake. Itikadi hiyo ya kidini, ambayo haiungwi mkono na Biblia, kwa sehemu yaeleza sababu kwa nini usanifu-ramani, au utayarishaji wa ramani uliendelea kwa kiwango kidogo katika mwanzo-mwanzo wa Enzi za Kati.
Ramani ni muhimu katika kujua jiografia, ambayo yenyewe ni ya maana katika kuuelewa ulimwengu unaotuzunguka. Na bado, kwa watu wengi, ujuzi juu ya jiografia haujawa wa hali ya juu sana tangu enzi za kati. Yapata miaka mia moja iliyopita, mwandishi Mark Twain alitumia mhusika wa kubuni Huck Finn ili kuonyesha tatizo hilo katika siku zake. Wakiwa wanaelea juu wakitumia puto, Huck alimhakikishia rafiki yake Tom Sawyer kwamba hawakuwa wamefika kwenye jimbo la Indiana kwa sababu dunia ilikuwa bado na rangi ya kijani-kibichi. Huck alikuwa ameona Indiana kuwa yenye rangi ya waridi katika ramani.
Katika nyakati za karibuni, mwalimu Mmarekani wa shule ya upili angeanza somo lake la jiografia kwa kumwomba mwanafunzi aonyeshe mahali ilipo Marekani katika ramani ya ulimwengu. Alianzisha somo lake kwa njia hiyo kwa kipindi cha miaka kumi. Aliripoti kwamba katika kipindi hicho hakuna mwanafunzi wala wa kwanza—wala wa pili—aliyepata kufaulu kuonyesha mahali ilipo Marekani! Labda jambo la kushangaza kuliko hilo, ni kwamba “Wamarekani 3 kati ya 10 hawawezi kutofautisha kaskazini na kusini kwenye ramani,” kulingana na gazeti Time.
Tarihi za Utayarishaji wa Ramani
Utayarishaji wa ramani ni mojawapo wa njia za kale zaidi na zisizo za kawaida za kuwasiliana. Ramani zimechongwa kwenye mawe na mbao; zikachorwa kwenye udongo, kwenye karatasi, zikachorwa kwenye ngozi na kwenye vitambaa; na hata zikaundwa kwenye theluji.
Kichapo The World Book Encyclopedia chataja kwamba ramani ya kale zaidi inayojulikana ni ya karibu mwaka wa 2300 K.W.K., kikiifafanua kuwa “bamba dogo la udongo kutoka Babiloni ambalo huenda laonyesha eneo la makazi lililo katika bonde lenye milima.” Wababiloni walitumia michoro ya udongo inayofanana na hiyo ya kuta za jiji katika jitihada za mapema za kuendeleza jumuiya.
Mwanajiografia Mgiriki Ptolemy wa Alexandria wa karne ya pili alijua kwamba dunia ilikuwa duara, kama ilivyofunua Biblia katika karne ya nane K.W.K. ilipomtaja Mungu kuwa “Anayeketi juu ya duara ya dunia.” (Isaya 40:22, italiki ni zetu.) Kulingana na gazeti Equinox, michoro ya Ptolemy ni “baadhi ya majaribio ya kwanza yaliyorekodiwa ya kosmografia—ramani ya sura ya ulimwengu unaojulikana.”
Ni wachache waliojua ramani za Ptolemy mpaka wakati zilipochapishwa katika atlasi katika mwisho-mwisho wa miaka ya 1400. Baada ya hapo, zikawa chanzo cha habari za jiografia kwa mabaharia kama vile Columbus, Cabot, Magellan, Drake, na Vespucci. Hata leo, ramani ya ulimwengu ya Ptolemy inayofanana na tufe yafanana na ramani za ulimwengu za kisasa, ingawa katika ramani yake bara Ulaya-Asia ni kubwa mno. Kichapo Reader’s Digest Atlas of the World chasema kwamba ukubwa huo wa kupita kiasi “ulimfanya Columbus akosee umbali wa kufika Asia alipoondoka kuvuka Atlantiki, na hivyo akashindwa kung’amua kwamba alikuwa amevumbua Mabara Mapya yaliyokuwa katikati.” Yaliyoitwa Mabara Mapya, yaani Amerika, yaliyoitwa hivyo kutokana na Amerigo Vespucci, yalitiwa katika ramani ya ulimwengu kwa mara ya kwanza katika mwaka wa 1507.
Safari za baharini zilizofuata katika enzi za ugunduzi, kati ya 1500 na 1700 hivi, ziliwaandalia wasanifu-ramani habari kamili. Chati au ramani zao, zikawa hati muhimu na zimetambuliwa kuwa “vifaa vya mamlaka za serikali” na “silaha za vita.” Watayarishaji wa ramani waliapishwa kisiri, wakafanya kazi wakiwa wamejitenga, na kulinda ramani zao hata ikiwa ingewagharimu uhai wao. Ikiwa adui angeingia ndani ya meli, ramani ziliwekwa ndani ya magunia yaliyowekewa uzito, zilitupwa baharini. Kwa muda mrefu, mataifa yalilinda sana ramani zao rasmi, na katika nyakati za vita, ni watu wachache tu ambao wangeweza kuziona.
Mabara mapya yalipogunduliwa, mipaka ya zamani ilihitaji kuwekwa tena. Mwanajiografia Mflemi Gerardus Mercator (1512-1594) alishughulikia uhitaji huu kwa kuchora kitabu cha kwanza cha kisayansi cha ramani. Katika kitabu chake Mercator alitumia jitu la kubuniwa Atlas the Titan, na tangu wakati huo neno “atlasi” limekuja kutumiwa kwa mkusanyo wa ramani.
Usanifu-Ramani wa Kisasa
Ujuzi wa kijiografia ulipokua, ndivyo ramani zilivyozidi kuwa bora. Mbinu mpya za kuchora ramani zilichangia sehemu kubwa katika ukuzi huu. Kichapo Canadian Geographic chafafanua kazi ngumu ya masoroveya katika mwisho-mwisho wa karne ya 19 na mwanzo wa karne ya 20: “Kwa joto na baridi, kwa kusafiri kwa farasi, mtumbwi, chelezo na mguu . . . , walikagua majiji na nyumba, misitu na mashamba, barabara zilizojaa matope na kinamasi zilizojaa wadudu. Walitumia minyororo kupima umbali na kipimapembe kupima mipindo. Waliweka alama kwenye vitu vya kudumu kwa kutumia nyota . . . na kukadiria vina vya maji ya mwambao.”
Katika karne ya 20, utayarishaji wa ramani uliendelea sana kwa sababu ya picha za kupigwa kutoka angani. Ndege zilizokuwa na kamera zilianza kupiga picha za angani. Kisha, setilaiti zinazozunguka angani za miaka ya 1950 zilifanya utayarishaji wa ramani upige hatua ya kufikia tekinolojia ya uvumbuzi wa anga. Kufikia mwisho wa miaka ya 1980, masoroveya wa ardhi wakiwa na vipokezi vilivyoelekezwa tufeni pote wangeweza kutambua pande zote za ulimwengu kwa muda wa saa moja, jambo ambalo lilichukua miezi kadhaa kutimiza, miaka michache iliyotangulia.
Leo wasanifu-ramani huchora kwa msaada wa elektroni. Wanafanyia marekebisho ramani zao kwa kutumia vifaa vilivyo katika setilaiti zinazozunguka dunia, vinavyokamilishwa na vifaa tata vilivyo duniani. Kompyuta zenye programu za pekee huwaruhusu watayarishaji wa ramani wahifadhi habari nyingi kwelikweli, zinazohusu usanifu-ramani na nyinginezo. Hivyo, ramani ya kupimwa yaweza kutokezwa kwa muda wa dakika chache, bila kupoteza wakati mwingi kwa kutumia mkono.
Kwa kutumia mfumo wa habari wa kijiografia (GIS), karibu habari yoyote yaweza kuwekwa kwenye ramani. Mfumo wa GIS waweza kutokeza ramani ya barabara ya jiji katika dakika hiyohiyo ili kusaidia magari yasonge kwa haraka wakati wa msongamano. Waweza pia kufuata na kuelekeza lori zinazosafiri kwenye barabara kuu za taifa, na hata waweza kusimamia uzalishaji wa nyasi kavu kwa wafugaji wa ng’ombe.
Ramani—Je, Hudhihirisha Mambo Halisi?
“Ramani yaweza kukosea lakini haiwezi kamwe kuchekesha,” akaandika mshairi Howard McCordin. Kwa kielelezo, wakati ramani iliyochorwa kwa mkono kwenye karatasi ikosapo kuonyesha mteremko wa kuelekea unakoenda, haliwi jambo la kuchekesha. Tumetarajia ramani zote ziwe za kweli na zionyeshe mambo halisi. Lakini ukweli ni kwamba si zote za kweli, wala zote hazionyeshi mambo kihalisi.
Mhifadhi-nyaraka mmoja alijipatia ramani nzuri sana ya ukutani ya Quebec, Kanada, na baadaye akatambua lililoonekana kuwa kosa dhahiri. “Labrador yote ilitiwa ndani ya Quebec,” akaeleza. “Nilipomwonyesha mfanyakazi mwenzangu tatizo hilo, nilishangaa aliposema labda halikuwa kosa la kupitiwa ila ni lilifanywa kimakusudi.” Inaonekana kwamba Quebec haikupendezwa kamwe na uamuzi wa 1927 kuhusu kuwekwa kwa mpaka kati ya Labrador na Quebec, na kwa hiyo ramani hiyo haikuonyesha ukweli huu usiotakikana.
Mfanyakazi mwenzi wa mhifadhi-nyaraka huyo alitaja vielezi vingine vya ramani ambazo zilidanganya kwa kukusudia. Baadaye mhifadhi-nyaraka huyo aliandika makala katika gazeti Canadian Geographic iliyokuwa na kichwa “Ramani Zinazodanganya,” iliyokazia kwamba “usanifu-ramani waweza kutumiwa vibaya kwa urahisi ili kuunga mkono oni fulani.” Aliandika: “Sikuzote nilifundishwa kwamba ramani ziliwakilisha uhalisi wa mambo kikweli na bado kulikuwako ramani zilizojaa uwongo!”
Katika mwaka wa 1991, The Globe and Mail, la Toronto, liliripoti kwamba “ujumbe wa maofisa wa Japani, ambao serikali yao hudai inamiliki Visiwa vya Kurile vinavyodhibitiwa na Sovieti, uliomba shirika la [National Geographic Society] liteue rangi tofauti kwa eneo hili linalozozaniwa.” Kwa nini walitaka badiliko la rangi? Mkuu wa usanifu-ramani wa shirika la National Geographic, John Garver, Jr., alieleza: “Walitaka rangi ibadilishwe iwe ya kijani kibichi kwa sababu Japani ina rangi ya kijani kibichi kwenye ramani.”
Kwa hiyo, rangi zilizo katika ramani zaweza kutumiwa kuonyesha mashirika fulani au kukazia jambo fulani hususa. Kwa kielelezo, katika mwaka wa 1897, dhahabu ilipogunduliwa kandokando ya mto unaoingia Mto Klondike, ramani zilisaidia hasa katika kuendeleza mbio za watafutaji wa dhahabu waliokadiriwa kuwa 100,000. Wafanyiza- ramani walipaka Alaska na Yukon rangi ya manjano sana ili kudokeza uwezekano mkubwa wa kufanikiwa.
Mitazamo mingine yaweza kuathiri mwonekano wa ramani kwa njia kubwa hata zaidi. Kwa kielelezo, katika mwaka wa 1982 “Ramani Iliyopinduliwa” ilitokezwa, ikiwa imeweka Kizio cha Kusini kuwa juu. Kwa nini? Kwa sababu ilionekana kwamba kuwa katika sehemu ya juu kulionyesha ukuu na fahari na kwamba ramani hiyo ingeathiri ifaavyo nchi maskini zaidi ulimwenguni zilizo katika Kizio cha Kusini.
Kipingamizi kwa Watayarishaji wa Ramani
Hata wakati msanifu-ramani atakapo kuwakilisha ukweli wa mambo, kubuni ramani kwenye sehemu iliyo bapa hutokeza tatizo. Hii ni kwa sababu kuchora uso wa duara kwenye sehemu iliyo bapa hupotosha. Ni sawa na kujaribu kufanya ganda lote la chungwa liwe bapa. Huenda maumbo ya mabara yakawa sahihi, lakini ukubwa wake hauna uwiano. Hivyo, John Garver, Jr., alisema: “Ramani iliyo sahihi pekee ni tufe.” Lakini kwa sababu ni vigumu kubeba tufe kila mahali, ramani bapa yenye kupendeza ya ulimwengu huthaminiwa na hunufaisha.
Katika mwaka wa 1988, shirika la National Geographic lilitoa ramani mpya ya ulimwengu. Likiripoti juu ya tukio hili, gazeti Time lilieleza tatizo linalowakabili watayarishaji wa ramani: “Mara nyingi mifano iliyo katika ramani haidhihirishi miundo halisi na ukubwa wenye kuwiana wa mabara na bahari.” Unaweza kutambua jambo hili kwa urahisi kwa kulinganisha ramani ya ulimwengu iliyotolewa na shirika la National Geographic Society katika mwaka wa 1988 na ramani za ulimwengu zilizotolewa na shirika hili hili katika miaka iliyotangulia.
Likizungumzia tofauti kubwa sana zilizoko katika ramani hizo, gazeti Time lilisema: “Kwenye ramani mpya ya ulimwengu ambayo shirika la [National Geographic Society] linawapelekea wanachama wake milioni 11, Muungano wa Sovieti umepoteza kilometa za mraba milioni 47—zaidi ya thuluthi mbili za eneo lililokuwa nalo kwenye ramani za National Geographic za nusu karne iliyopita.”
Tangu nyakati za Ptolemy, wasanifu-ramani wamepambana na tatizo la kutokeza ukubwa unaowiana wa maeneo ya ulimwengu. Kwa kielelezo, katika ramani iliyotumiwa na shirika la National Geographic kwa miaka 66, Alaska inazidi ukubwa wake halisi kwa mara tano! Matatizo ya namna hiyo yenye kupotosha yaweza kukusaidia uelewe kwa nini Arthur Robinson, anayefikiriwa na wengi kuwa mshauri wa wasanifu-ramani wa Marekani, alisema: “Utayarishaji wa ramani unafanana sana na sanaa kama vile sayansi.” Ramani iliyotumiwa na shirika la National Geographic Society katika mwaka wa 1988, kulingana na Garver, ilikuwa “usawaziko bora kati ya jiografia na sanaa.”
Kuna Wakati Ujao Gani kwa Utayarishaji wa Ramani?
Kwa wazi, mengi yanahusika katika utayarishaji wa ramani kuliko wanavyotambua watu wengi. Kadiri ujuzi zaidi juu ya dunia upatikanavyo, ndivyo ramani ziwezavyo kuwa sahihi zaidi. Na bado, huenda ujuzi huo usipatikane kwa urahisi. Hivyo, kama alivyosema mwandishi Lloyd A. Brown miaka kadhaa iliyopita, “mpaka wakati watu wote watakapoabiri hadi kwenye pwani za majirani bila hofu, na kusafiri au kuruka kwa ndege bila kuangushwa au kusimamishwa, ramani kuu ya ulimwengu ambayo watu wameota juu yake kwa karne nyingi itazidi kungojewa. Labda itakamilika siku fulani.”
Kwa kufurahisha, kulingana na unabii wa Biblia, hatimaye tufe nzima itaunganishwa chini ya utawala wa Mfalme aliyewekwa na Mungu, Yesu Kristo. Unabii wa Biblia watangaza hivi kumhusu: ‘Atakuwa na enzi toka bahari hata bahari, toka mto hata miisho ya dunia.’ (Zaburi 72:8) Wakati mabishano ya mipaka yatakapoisha na ushindani wa kisiasa utakapoondolewa hatimaye na kutokuwepo kwa tawala za kitaifa, ndipo ramani kamilifu ya ulimwengu iwezapo kutokezwa.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
Ptolemy na ramani yake ya ulimwengu
Gerardus Mercator
[Hisani]
Ptolemy na Mercator: Culver Pictures; ramani ya ulimwengu ya Ptolemy: Gianni Dagli Orti/Corbis; tufe: Mountain High Maps® Copyright © 1997 Digital Wisdom, Inc.; background on pages 16-19: The Complete Encyclopedia of Illustration/J. G. Heck