Ramani za Kutimiza Mahitaji Yako
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA UINGEREZA
KUFAHAMU njia katika nchi ama jiji geni si rahisi. Kwanza, ni lazima ufahamu ulipo. Kisha, uamue ni njia ipi iliyo afadhali zaidi. Unaweza kuipataje hiyo njia? Unachohitaji ni ramani!
Ramani—Tangu Lini, na kwa Nini?
Kuchora ramani, ama katografia kama kunavyoitwa, kumekuwa na historia ndefu ya kupanda na kushuka. Wenye mamlaka fulani hufuatilia uchoraji ramani hadi huko nyuma miaka 4,300 iliyopita kwenye mabamba ya udongo yaliyochorwa katika Babilonia. Lakini Wagiriki wa kale ndio walichora chati ambazo zilikuwa tangulizi za ramani za kisasa. Baada ya ramani za ulimwengu wa kale zilizochorwa na Claudius Ptolemy katika karne ya pili W.K., ubora wa katografia uliyoyomea kwa sababu ya Enzi za Giza. Maeneo yaliyokuwa bado kuvumbuliwa yalionyeshwa kuwa makazi ya dubwana na majitu. Dini ziliathiri sana uchoraji wa ramani hivi kwamba ramani nyingi zilionyesha mahali bustani ya Edeni ilikuwa. Yerusalemu na Mashariki ya Kati zilianza kutokea kwenye ramani za ulimwengu uliojulikana kwa wakati huo.
Ramani za mapema za Uingereza pia zilionyesha athari ya kidini. Ramani moja ya aina hiyo ilifuatilia njia ambayo wapilgrimu walifuata wakielekea maeneo matakatifu ya kidini ya Uingereza. Kwa kutoa maelezo ya kindani ya “Barabara Kuu ya Kaskazini ya Wapilgrimu,” ramani hii iliweka njia kutoka mji wa kaskazini wa Durham hadi bandari ya pwani ya kusini ya Dover.
Mwanzilishi wa katografia ya kisasa alikuwa Gerardus Mercator (1512-1594). Yeye alibuni mbinu ya ramani yenye mistari iliyosifika sana miongoni mwa mabaharia kwa usahihi wayo, na ramani nyingi zilizochorwa kulingana na mistari ya Mercator zatokea katika atlasi za kisasa.
Kwa wenye mashamba, ramani zilikuja kuwa baraka. Rejezeo kwa mistari iliyochorwa vizuri ya mipaka lilisaidia kusuluhisha magombano ya kisheria. Upendezi wa serikali katika ramani uliongezeka, kwa sababu uchanganuzi wa kodi ulitegemea kuweka rekodi sahihi za umiliki wa ardhi.
Leo, ramani zatimiza mahitaji ya kila siku. Atlasi husaidia watoto wa shule kushika mambo ya msingi ya jiografia. Chati huwezesha watabiri wa hali ya hewa kuonyesha kwa michoro kile huenda tutazamie kuhusu hali za hewa. Ramani yaweza kutusaidia kutumia usafiri wa umma kwa njia bora zaidi. Na kwa ajili ya tafrija za familia, ramani yaweza kuonyesha njia ya kufuata yenye mandhari nzuri zaidi.
Wastadi hawajapuuzwa kamwe. Kuna ramani za msongamano wa watu kwa ajili ya waratibu-mji. Ramani za sakafu ya bahari husaidia wale wanaotafuta meli zilizovunjika ama kutafuta rasilimali za madini. Ramani za kiakiolojia ni kielekezi kwa wale wanaochimba kutafuta habari za kale. Ala, kwa watafiti wa anga hata kuna ramani za mwezi na sayari nyinginezo! Kukiwa na habari kemkem kama hizo kwenye ramani, ni kwa faida yako kusitawisha na kuboresha stadi zako katika kuzisoma.
Jinsi ya Kusoma Ramani
Kupata mengi kutoka kwa ramani zako ni sawa na kujifunza lugha ngeni. Unapojifunza lugha nyingine, unapata msamiati mpya na sarufi tofauti. Katika lugha ya ramani, ishara zaweza kufananishwa na neno, ilihali skeli za mistari ya kontua na mistari ya ramani huwa kama sarufi. Ramani nyingi huchorwa pamoja na kisanduku chenye ufunguo wa kufahamu ishara zitumiwazo kwenye ramani. Hiki hutumika kama kamusi, kikifafanua hizo ishara.
Ishara huchaguliwa kwa makini ili kuwasilisha maana yazo. Kwa kielelezo, ili kupata mnara wa taa, tafuta ishara inayofanana nao. Makanisa na misikiti huenda yakaonyeshwa kwa miraba myeusi ama miviringo iliyowekwa misalaba ama vizingo vya mwezi.
Unaweza kufahamuje maana ya ishara kama hizo? John Wilson, mtungaji wa Follow the Map, apendekeza “kipitisha-wakati chenye kupendeza cha ‘kupitia ramani.’” Yeye aongezea hivi: “Acha jicho lako lirande-rande kwenye ramani bila haraka, nawe zifasiri hizo ishara kadiri uzionapo.”
Je, unapata kwamba makao yako yaonekana tofauti kabisa na kile ramani yako inachoonyesha? Kwa nini? Kwa kawaida sisi hutazama mazingira yetu kutoka kwa kimo chetu, meta 1.5 hadi 1.8 kutoka ardhini. Lakini ramani huonyesha ardhi kutoka mtazamo, kwa ulalo ikiwa juu kila mwinuko. Ili kufahamu wazo hili, ni muhimu kwamba uelewe sarufi ya ramani.
Skeli, Kimo, na Mahali
Jambo gumu kwa wachora ramani ni kurekodi utofautiano wa mwinuko kutoka usawa wa bahari na kitu kinginecho chochote ardhini kilichotengenezwa na mwanadamu. Yote haya lazima yachapishwe kwenye karatasi ya saizi ya kadiri. Ili kutimiza hili, ramani huchorwa kwa skeli. Ramani fulani maarufu za Uingereza huonyesha nchi ikiwa katika skeli ya 1:50,000—jambo linalomaanisha kwamba kila sentimeta kwenye ramani huwakilisha sentimeta 50,000 kwenye uso wa dunia.
Hata hivyo, ramani iliyo kwenye karatasi yaweza kuonyeshaje utofautiano wa mwinuko? Mistari yenye ukaribiano inayoonyesha mteremko ni njia moja ya kuonyesha uhalisi wa hali. Jua huonekana kuangaza mahali fulani kwenye pembe ya kushoto juu ya ramani. Miteremko inayokabili mashariki na kusini-mashariki, ikiwa kwenye uvuli, huchorwa kwa rangi zilizo nyeusi zaidi. Ramani za kisasa mara nyingi huwa na mistari ya kontua ikiunganisha maeneo yaliyo na kimo kinacholingana juu ya wastani wa usawa wa bahari. Kuchapa alama hizi kwa rangi nyepesi huwezesha kuona vizuri sehemu zile nyingine kuu za ramani bila kukengeuka.
Ramani nyingi hutumia mifumo ya mistari inayopitana ili kukusaidia kutambua mahali ulipo. Mstari ramani huu, kama unavyoitwa, huwezesha mahali popote kupewa jozi ya visawazishi vya kialfabeti ama kinambari ambavyo huonyesha mahali hususa katika mistari ya ramani. Kwa kielelezo, mji fulani huenda uwe kwenye G-13, yaani G kwenye upande wa mistari-wima na nambari 13 kwenye upande wa mistari ilalayo. Mahali ambapo vionyeshi hivi viwili hukutana ndipo mahali utapata huo mji. Hata hivyo, unaweza kuwa na uhakika namna gani kwamba ramani yako itakupa picha iliyo sahihi?
Ramani Katika Enzi ya Kompyuta
Mahitaji ya kijeshi mara nyingi yametokeza uchapishaji wa ramani zilizo sahihi kabisa. Wakati wa miaka 40 iliyopita, kuchora ramani zilizo sahihi kwa kutumia mlinganisho wa picha ya kupigwa kutoka angani kumekuja kuwa uhalisi, nchi nyingi zikifuata mbinu kama hizo.
Tayari, kuna ramani za kusonga zijionyeshazo kwa kompyuta katika magari fulani pamoja na ramani za kusafiria zenye mambo ya ndani-ndani kwa minajili ya kompyuta za nyumbani. “Kompyuta Zaelekeza Dereva,” kikasomeka kichwa kimoja katika The Observer. Hiyo ripoti ilieleza mradi mmoja wa majaribio ambao hutumia diski za kompyuta zenye habari za ramani zilizounganishwa na kitoa-sauti cha kielektroni. Dereva huweka maneno ya kuelekeza kwenye kiwambo cha ramani ya kompyuta ili kuonyesha anakoelekea. Hakuna haja ya kuhangaika kuhusu njia panda za barabarani! Kwa nini? Kwa sababu gari linapokaribia kila njia panda, sauti fulani humwambia dereva upande wa kuelekea. Dira pamoja na kihisi-magurudumu hufuatilia mkondo wa gari. Maendeleo ya hivi karibuni hata ni yenye kutegemeka na sahili zaidi.
Hili litamaanisha nini kuhusu wakati ujao wa ramani? Je, ramani za karatasi zitakuja kuwa vitu vya kukusanya kwa ajili ya kukumbukwa? Wakati utaonyesha. Katika hali yoyote ile, ramani itaendelea kuwa kifaa muhimu katika kutimiza mahitaji yako ya usafiri.
[Ramani/Picha katika ukurasa wa 23]
Ramani nyingi hutia ndani ufunguo, ama chati, ili kufafanua zile ishara zinazotumiwa
Utofautiano katika mwinuko huonyeshwa na mistari ya kontua, kwa kawaida kwa rangi zilizo nyepesi
Mfumo wa mistari ya ramani huwezesha mahali papatikane kwenye ramani
Ramani mara nyingi huonyesha ulinganifu wa sentimeta moja kwenye uso wa dunia (hauonyeshwi hapa)
Skeli ya kilometa huwezesha kupima umbali kati ya mahali mbalimbali
[Hisani]
Haki za Kunukuu Zimehifadhiwa na Crown
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 22]
Kutoka kwa kitabu Die Heiligkeit der Gesellschaft Jesu