Gutenberg—Jinsi Alivyounufaisha Ulimwengu!
NA MLETA-HABARI WA AMKENI!KATIKA UJERUMANI
NI UVUMBUZI upi wa miaka elfu moja iliyopita ambao umeathiri maisha yako? Je, ni simu, televisheni, au gari? Labda si mojawapo ya vitu hivi. Kulingana na wataalamu wengi, ni uchapishaji kwa kutumia mashine. Mtu anayepewa sifa ya kuvumbua njia ya kwanza yenye kutumika ni Johannes Gensfleisch zur Laden, anayejulikana vizuri zaidi kuwa Johannes Gutenberg. Alikuwa mkabaila na kwa hiyo hakulazimika kutumikia akiwa mwanagenzi wa kawaida.
Uvumbuzi wa Gutenberg umefafanuliwa kuwa “mchango mkubwa sana wa Ujerumani kwa ustaarabu.” Kila nakala iliyookoka ya kazi yake bora ya uchapaji—inayoitwa Biblia ya Gutenberg ya mistari 42—ina thamani ya fedha nyingi.
Mainz Wenye Ufanisi
Gutenberg alizaliwa Mainz, katika au karibu mwaka wa 1397. Ukiwa katika kingo za Mto Rhine, Mainz ulikuwa mji wenye wakazi wapatao 6,000. Ulijulikana kuwa Mainz wenye Ufanisi, ukiwa kitovu cha shirika lenye nguvu la miji. Maaskofu wakuu katika Mainz walikuwa wapiga kura wa Milki ya Roma Takatifu. Mainz ulijulikana kwa ufuaji wa dhahabu. Johannes mchanga alijifunza mengi kuhusu kufua chuma, kutia ndani namna ya kutunisha maandishi ya chuma. Kwa sababu ya mizozo ya kisiasa, alienda uhamishoni kwa miaka kadhaa hadi Strasboug, ambapo alikuwa sonara na kufundisha kazi ya sonara. Lakini jambo alilojishughulisha nalo zaidi lilikuwa kazi yake ya siri kuhusu uvumbuzi mpya. Gutenberg alijaribu kusitawisha ufundi wa kupiga chapa kwa kutumia mashine.
Kipaji cha Gutenberg na Misaada ya Kifedha ya Fust
Gutenberg alirudi Mainz na kuendelea na majaribio yake. Ili kupata misaada ya kifedha alimwendea Johann Fust, aliyemkopesha gulden 1,600—kiasi kikubwa cha fedha wakati huo ambapo msanii stadi alipata gulden 30 tu kwa mwaka. Fust alikuwa mfanyabiashara mwerevu aliyeona angepata faida kwa kujasiria jambo hili. Gutenberg alikuwa akifikiria jambo gani?
Katika mawazo yake Gutenberg aliona kwamba vitu fulani vilitokezwa kwa idadi kubwa, kila kimoja kikifanana na kingine. Mathalani, sarafu zilipigwa chapa, na risasi zilimiminwa katika kalibu ya metali. Kwa hiyo kwa nini kurasa nyingi zinazofanana zisichapishwe na kisha kupanga kurasa kwa utaratibu wa nambari na kuwa vitabu vinavyofanana? Vitabu gani? Alifikiri juu ya Biblia, kitabu ghali sana ambacho ni wachache waliopendelewa ndio waliokuwa na nakala za kibinafsi. Gutenberg alikusudia kutokeza Biblia nyingi zinazofanana, kukizifanya ziwe za bei nafuu zaidi kuliko nakala zilizoandikwa kwa mkono bila kuondoa umaridadi wake wowote. Jambo hili lingefanywaje?
Vitabu vingi vilinakiliwa kwa mkono, jambo lililohitaji bidii na wakati. Uchapishaji ulikuwa umejaribiwa kwa mabamba ya mbao zilizochongwa kwa mkono, kila moja likiwa na ukurasa wa kuandikia. Mtu mmoja Mchina aliyeitwa Pi Sheng hata alikuwa amefanyiza herufi mojamoja za udongo ili kutumiwa katika uchapishaji. Katika Korea, herufi zilizotengenezwa kwa shaba zilikuwa zimetumiwa katika matbaa ya kuchapishia ya serikali. Lakini kuchapisha kwa kutumia uchapaji wa mashine—herufi mojamoja zilizofanyizwa zinazoweza kupangwa kwa kila ukurasa mpya—zilitaka herufi nyingi sana, na hakuna mtu yeyote aliyekuwa amebuni njia ya kuzitokeza. Jambo hili lingefanywa na Gutenberg.
Akiwa mfua chuma mwenye uzoefu, aliona kwamba kuchapisha kungewezekana kwa njia nzuri zaidi kwa kuwa na herufi zinazoweza kusonga zilizotengenezwa si kwa udongo au mbao, bali kwa metali. Zingetupwa ndani ya kalibu, si kuchongwa au kuokwa ndani ya joko. Gutenberg alihitaji kalibu ambazo zingetumiwa kukalibu herufi zote 26 za alfabeti—zikiwa ndogo na kubwa—kuongezea herufi zilizounganishwa, vituo vya uandishi, ishara, na nambari. Kwa ujumla, alipiga hesabu kwamba herufi mbalimbali 290 zilihitajiwa, kila moja ikiwa na makumi ya nakala.
Aanza Kazi Yake
Gutenberg alichagua kutumia maandishi ya mtindo wa Gothic kwa kitabu chake katika Kilatini, kilichotumiwa na watawa wa kike katika kunakili Biblia. Akitumia uzoefu wake wa kufua chuma, kwenye kipande kidogo cha feleji alichonga kila herufi na ishara iliyogeuka, yaani, mfano wa mchongo kwenye uso wa feleji. (Picha ya 1) Kisha muhuri huu wa feleji ulitumiwa kupigilia mfano ndani ya metali nyororo zaidi, ama shaba au shaba nyeupe. Tokeo lilikuwa mfano halisi wa herufi iliyoshindiliwa ndani ya metali nyororo zaidi, iliyoitwa herufi ya msingi.
Hatua iliyofuata ilihusisha chuma cha kukalibu, kilichokuwa tokeo la kipaji cha Gutenberg. Chuma hicho cha kalibu kilitoshana na ngumi ya mwanadamu na sehemu yake ya juu na ya chini ilikuwa wazi. Herufi ya msingi ilishikanishwa kwenye sehemu ya chini ya kalibu, na muungano wa metali hizo ulioyeyushwa ulimwagwa katika sehemu ya juu. (Picha ya 2) Mchanganyiko huo wa metali—bati, risasi, stibi, na bisimathi—ulipoa na ukawa mgumu upesi.
Mchanganyiko wa metali uliotolewa kwenye kalibu ulikuwa herufi iliyoandikwa kwa kinyume ya ile herufi iliyowekwa ndani ya kalibu, nayo iliitwa chapa. Hatua hiyo ilirudiwa mpaka idadi iliyotakikana ya vipande vya herufi hiyo ilipotokezwa. Kisha ile herufi ya msingi iliondolewa na kubadilishwa na herufi nyingine ya msingi. Hivyo, idadi yoyote ya vipande vya chapa ya kila herufi na ishara ingeweza kutokezwa kwa muda mfupi. Chapa zote zilitoshana kwa urefu, kama alivyotaka Gutenberg.
Sasa kuchapisha kungeweza kuanza. Gutenberg alichagua kifungu cha Biblia alichotaka kunakili. Akiwa na kijiti cha kupanga mkononi, alitumia chapa kuandika tahajia za maneno, na kufanyiza maneno kuwa mistari ya maandishi. (Picha ya 3) Mistari yote ilifanywa itoshane. Akiwa amepanga chapa, alipanga mistari kuwa safu ya maandishi, safu mbili kwa kila ukurasa. (Picha ya 4)
Ukurasa huu wenye maandishi ulifungiwa mahali pake kwenye sehemu ya matbaa iliyo bapa kisha ukatiwa unyevu kwa wino mweusi. (Picha ya 5) Matbaa hiyo—inayofanana na zile zinazotumiwa kutengenezea divai—ilihamisha wino kutoka kwenye chapa hadi kwenye karatasi. Ukurasa uliochapwa ukatokea. Wino zaidi na makaratasi zaidi yalitumiwa na hatua hiyo ikarudiwa mpaka idadi ya nakala za kuchapishwa zilizohitajiwa zilipotokezwa. Kwa kuwa chapa hiyo iliweza kusogezwa, ingeweza kutumiwa tena kupanga ukurasa mwingine.
Uchapishaji Bora
Karakana ya Gutenberg iliyoajiri kati ya watu 15 hadi 20, ilimaliza kuchapisha Biblia ya kwanza katika mwaka wa 1455. Nakala zipatazo 180 zilifanyizwa. Kila Biblia ilikuwa na kurasa 1,282, na mistari 42 kwa kila ukurasa, uliochapishwa katika safu mbili. Kujalidiwa kwa vitabu hivyo—kila Biblia ilikuwa na mabuku mawili—na madoido ya vichwa vilivyopakwa rangi kwa mkono na herufi ya kwanza ya kila sura kulifanywa baadaye katika karakana nyinginezo.
Je, twaweza kuwazia ni vipande vingapi vya chapa vilivyohitajiwa ili kuchapisha Biblia? Kila ukurasa una herufi zipatazo 2,600. Tukichukua kwamba Gutenberg alikuwa na watayarishaji-chapa sita, kila mmoja akifanyia kazi kurasa tatu mara moja, wangehitaji vipande vipatavyo 46,000 vya chapa. Twaweza kuelewa kwa utayari kwamba kalibu ya Gutenberg ilichangia sana kuchapisha kwa kutumia herufi zinazosonga.
Watu walishangaa walipolinganisha Biblia hizo: Kila neno lilikuwa mahali palepale. Jambo hilo halingewezekana kwa hati zilizoandikwa kwa mkono. Günther S. Wegener aandika kwamba Biblia hiyo yenye mistari 42 ilikuwa na “usare na ulinganifu, upatano na umaridadi, hivi kwamba wachapishaji katika miaka yote walishangazwa na ubora wa kazi hiyo.”
Maangamizi ya Kifedha
Hata hivyo, Fust alipendezwa zaidi na pesa kuliko kazi bora. Ilichukua muda mrefu kuliko alivyotarajia kupata faida kutokana na kitega-uchumi chake. Wenzi hao wakaachana, na katika mwaka wa 1455—wakati tu Biblia zilipokuwa zikikamilishwa—Fust akakataa kutoa mikopo. Gutenberg hakuweza kulipa mkopo na akapoteza kesi ya mahakamani iliyofuata. Alilazimishwa kusalimisha kwa Fust angalau vifaa fulani vya kuchapishia na chapa kwa ajili ya Biblia. Fust alifungua kiwanda chake cha kuchapisha pamoja na mfanyakazi stadi wa Gutenberg Peter Schöffer. Biashara yao, Fust na Schöffer, ilitambuliwa kwa kazi bora ambayo kwa kweli ilikuwa ya Gutenberg na ikawa matbaa ya biashara ya kwanza yenye mafanikio ulimwenguni.
Gutenberg alijaribu kuendeleza kazi yake kwa kuanzisha kiwanda kingine cha uchapishaji. Wasomi fulani wasema aliandika vitabu fulani vilivyochapishwa vya tarehe za karne ya 15. Lakini hakuna kitu kilichopokea ukuu na fahari kama Biblia ya mistari 42. Balaa ilitokea tena katika mwaka wa 1462. Kutokana na mng’ang’ano wa mamlaka miongoni mwa wakuu wa Katoliki, mji wa Mainz ulichomwa na kuporwa. Kwa mara ya pili Gutenberg alipoteza karakana yake. Alikufa miaka sita baadaye, mnamo Februari 1468.
Urithi wa Gutenberg
Uvumbuzi wa Gutenberg ulienea haraka. Kufikia mwaka wa 1500, kulikuwa na matbaa katika miji 60 ya Ujerumani na nchi nyingine 12 za Ulaya. “Ukuzi wa uchapishaji ulitokeza maendeleo makubwa ya mawasiliano,” yasema The New Encyclopædia Britannica. “Zaidi ya miaka 500 iliyofuata kulikuwa na maendeleo mengi yaliyofanywa katika mbinu za kuchapisha, lakini hatua za msingi zilibaki zikiwa zilezile.”
Uchapishaji ulibadili hali ya maisha ya Ulaya, kwa kuwa ujuzi haukubaki kuwa kitu cha waliopendelewa. Habari zikaanza kuwafikia watu wa kawaida, ambao walianza kufahamu zaidi mambo yaliyokuwa yakiendelea. Kuchapisha kulifanya iwe lazima kuipa kila lugha ya kitaifa kiwango fulani cha maandishi ambacho kila mtu angeweza kuelewa. Hivyo, lugha za Kiingereza, Kifaransa, na Kijerumani zilifanywa kuwa sanifu na kuhifadhiwa. Wengi sana wakataka vitabu vya kusoma. Wakati uliotangulia Gutenberg kulikuwako maelfu machache ya hati katika Ulaya; miaka 50 baada ya kifo chake, kulikuwako mamilioni ya vitabu.
Marekebisho ya karne ya 16 hayangalifaulu bila mashine za kuchapishia. Biblia ilitafsiriwa katika lugha za Kicheki, Kifaransa, Kiholanzi, Kiingereza, Kiitalia, Kijerumani, Kipoland, na Kirusi na matbaa ilirahisisha kazi ya kuchapisha makumi ya maelfu ya nakala. Martin Luther alitumia matbaa ifaavyo kueneza ujumbe wake. Jitihada zake zilifanikiwa ilhali wengine, walioishi kabla ya matbaa ya Gutenberg walikuwa wameshindwa. Haishangazi kwamba Luther aliiita matbaa kuwa njia ya Mungu ya “kueneza dini ya kweli ulimwenguni pote”!
Nakala Zilizookoka za Biblia ya Gutenberg
Ni Biblia ngapi za Gutenberg zilizookoka? Mpaka hivi majuzi iliaminiwa kuwa zilikuwa 48—nyinginezo zikiwa hazijakamilishwa—zikiwa zimesambaa kote katika Ulaya na Amerika ya Kaskazini. Mojawapo ya nakala nzuri zaidi ni Biblia ya hati ya ngozi katika Maktaba ya Congress katika Washington, D.C. Kisha, katika mwaka wa 1996, uvumbuzi wenye kugusa hisia ulifanywa: Kisehemu zaidi cha Biblia ya Gutenberg kiligunduliwa katika hifadhi ya vitu vya kale ya kanisa katika Rendsburg, Ujerumani.—Ona Amkeni! la Januari 22, 1998, ukurasa wa 29.
Jinsi tunavyoweza kuwa wenye shukrani kwamba sasa Biblia inaweza kupatikana kwa mtu yeyote! Bila shaka, hii haimaanishi kwamba tunaweza kwenda na kununua Biblia ya mistari 42 ya Gutenberg! Moja ina thamani ya kiasi gani? Jumba la Makumbusho la Gutenberg katika Mainz lilijipatia nakala moja katika mwaka wa 1978 kwa deutsche mark milioni 3.7 (leo ni dola zipatazo milioni 2). Biblia hiyo sasa ina thamani inayopita kiasi hicho mara kadhaa.
Ni nini kinachoifanya Biblia ya Gutenberg iwe ya kipekee? Profesa Helmut Presser, aliyekuwa mkurugenzi wa hapo awali wa Jumba la Makumbusho la Gutenberg alidokeza sababu tatu. Kwanza, Biblia ya Gutenberg ilikuwa kitabu cha kwanza kuchapishwa katika Magharibi kikiwa na herufi zinazosonga. Pili, ilikuwa Biblia ya kwanza kupata kuchapishwa. Tatu, ina umaridadi wa kustaajabisha. Profesa Presser aandika kwamba katika Biblia ya Gutenberg, twaona “kiwango cha juu kabisa cha maandishi aina ya Gothic.”
Watu wa tamaduni zote wamenufaika na kipawa cha Gutenberg. Aliunganisha matumizi ya chuma cha kukalibu, mchanganyiko wa metali, wino, na matbaa. Alibuni uchapishaji na kuunufaisha ulimwengu.
[Picha katika ukurasa wa 16, 17]
1. Muhuri wa feleji ulitumiwa kushindilia mfano wa herufi ndani ya herufi ya msingi yenye shaba
2. Mchanganyiko wa metali ulimwagwa ndani ya chuma ya kalibu. Mchanganyiko huo ulipofanywa kuwa mgumu, chapa iliyotolewa ilikuwa na herufi ya awali ikiwa kinyume
3. Chapa iliwekwa ndani ya kijiti cha kutahajia maneno, kikifanyiza mstari wa maandishi
4. Mistari ilipangwa kuwa safu katika trei ndefu ya kupangia chapa
5. Ukurasa wa maandishi uliwekwa juu ya sehemu ya matbaa iliyo bapa
6. Bamba la shaba lililotiwa nakshi la Gutenberg, la tarehe ya tangu 1584
7. Leo, nakala moja ya Biblia ya Gutenberg ina thamani ya mamilioni ya dola
[Hisani]
Picha ya 1-4, 6, na ya 7: Gutenberg-Museum Mainz; picha ya 5: Courtesy American Bible Society
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 16]
Mandharinyuma: By Permission of the British Library/Gutenberg Bible