Kuutazama Ulimwengu
Ndoa Zapungua
Katika Kanada, ndoa ikiwa kama shirika inapungua kwa kasi sana. Kulingana na ripoti ya shirika la Statistics Canada, kwa miaka 15 iliyopita, “idadi ya Wakanada wanaoishi pamoja bila ya kufunga ndoa imekuwa karibu mara tatu kutoka 700,000 hadi milioni 2—ukuzi wa mwaka ulio mara sita zaidi ya ndoa,” lasema gazeti la The Toronto Star. Kwa kuongezea, “nusu ya muungano wa kwanza katika Kanada sasa ni ndoa za kienyeji na idadi yapanda kuwa nne kati ya kila ndoa tano katika Quebec.” Kwa nini badililko hilo? Ndoa za kienyeji “kwa wazi ni sehemu ya mabadiliko ya kijamii, moja kati ya mifululizo ya kukataa mashirika yaliyokubaliwa katika utaratibu wa jamii ambao unapitwa na wakati,” yasema ripoti hiyo. Makala katika gazeti hilo ilisema kwamba “zamani kuishi pamoja bila ndoa kulionwa kuwa ndoa ya kujaribu, lakini sasa inaonekana kuwa badala ya hiyo.”
“Tokeo la Musa”
Wanafizikia wawili kutoka Japani wamefanikiwa kutenganisha maji katika maabara, laripoti gazeti la New Scientist. Masakazu Iwasaka na Shogo Ueno, wa Chuo Kikuu cha Tokyo, walitumia koili ya umeme yenye nguvu sana kutokeza uga sumaku wenye nguvu kuzunguka neli iliyolazwa na iliyowekwa maji kidogo. Uga sumaku huo, ulio na nguvu karibu mara 500,000 zaidi ya ule wa dunia, ulilazimisha maji kwenda pembeni mwa mcheduara, ukitokeza eneo kavu katikati. Hali hiyo, ambayo wanasayansi waliigundua kwanza katika mwaka 1994, imeigizwa na wanafizikia katika Ulaya na Marekani. Inafanyaje kazi? Kulingana na Koichi Kitazawa, mshiriki katika Chuo Kikuu cha Tokyo, maji “hayapendi kuvutwa na sumaku. Hivyo sumaku yenye nguvu hutawanya maji, na huyaondosha mbali kutoka mahali ambapo uga sumaku ni mkubwa hadi mahali ambapo upo mdogo.” Kitazawa ameiita hali hiyo kuwa “Tokeo la Musa.”
Watalii Wenye Tabia Mbaya
Utajiri mwingi wa kitamaduni wa Italia huifanya kuwa sehemu ipendwayo sana kutembelewa. Kwa kusikitisha, waenda-likizo huko mara nyingi hawawi waangalifu linapokuja suala la tabia njema. Kulingana na Mario Lolli Ghetti, kamishna wa Florence wa mazingira na urithi wa usanifuujenzi, “wengi wahisi wako huru kufanya mambo ambayo kamwe wasingefikiria kufanya wakiwa nyumbani.” Kwa hiyo, jiji la Florence limetengeneza “Hati ya Haki na Wajibu wa Watalii,” ambayo huwakumbusha wageni kile wawezacho na wasichoweza kufanya, laripoti gazeti la La Repubblica. Hivi ni baadhi ya vikumbusha: Usioge au kuweka miguu yako katika vibubujiko vya maji; usifanye mandari mbele ya makumbusho na majumba ya makumbusho; usitupe makopo au chingamu katika ardhi; usivae fulana isiyo na mikono utembeleapo majumba ya makumbusho; na usiote jua ukiwa umevaa nguo ya kuogelea katika bustani za ukumbusho na katika makutano ya barabara. Bila shaka, watalii wenye tabia njema bado wanathaminiwa na kukaribishwa.
Tatizo la Ulishaji wa Mtoto Mchanga
“Kwa miongo kadhaa, madaktari na mashirika ya afya ya umma wamekuwa wakitoa shauri linalofanana kwa akina mama wapya katika nchi maskini zaidi: Nyonyesheni watoto wenu wachanga maziwa ya mama ili kulinda afya zao,” lasema gazeti la The New York Times. “Lakini sasa, UKIMWI wenye kuenea unabadilisha shauri hilo. Uchunguzi unaonyesha kwamba katika visa vingi akina mama wanaonyonyesha waweza kupitisha virusi ya UKIMWI kwa njia ya kunyonyesha maziwa. . . . Hivi karibuni Umoja wa Mataifa ulikadiria kwamba thuluthi moja ya watoto wachanga sana wenye H.I.V. walipata virusi hiyo kupitia maziwa ya mama zao.” Njia ya badala ni mchanganyiko wa maziwa kumlisha mtoto, lakini hiyo pia ina matatizo yake. Katika mataifa mengi akina mama hawana fedha kuweza kununua maziwa ya mtoto au kuchemsha chupa na hawana njia za kupata maji safi. Tokeo ni kwamba, watoto wachanga hupatwa na ugonjwa wa kuharisha na kuishiwa na maji mwilini, hali kadhalika kutokana na magonjwa ya kupumua na magonjwa ya tumbo na utumbo. Familia maskini huongeza maji mengi ili kupata kiasi kikubwa zaidi, ikitokeza utapiamlo kwa watoto wachanga. Maofisa wa afya sasa wanajitahidi kusawazisha mambo yote mawili. Ulimwenguni pote, kuna visa vipya 1,000 vya maambukizo ya HIV miongoni mwa watoto wachanga sana na watoto kila siku.
Hali ya Usafi wa Kutunza Afya Ulimwenguni Yaendelea Kuwa Mbaya Zaidi
“Karibu watu bilioni tatu, zaidi ya nusu ya idadi ya watu ulimwenguni, hawana hata njia ya kupata choo safi kilicho cha hali ya chini kabisa,” laripoti The New York Times. Matokeo ya uchunguzi huo, ambao ni sehemu ya uchunguzi wa kila mwaka wa Progress of Nations ulioendeshwa na UNICEF (Hazina ya Watoto ya Umoja wa Mataifa), pia wafunua kwamba “takwimu za kiwango cha usafi wa kutunza afya kinaendelea kuwa kibaya zaidi, si bora.” Kwa kielelezo, baadhi ya nchi ambazo zimefanya maendeleo katika kuandaa maji safi kwa watu maskini zimeshindwa kutokeza mifumo ya maji machafu. Ukosefu wa usafi wa msingi waongeza kwa kiasi kikubwa katika kuenea kwa magonjwa mengi ya kuambukiza na kurudi upya kwa magonjwa ya zamani, yasema ripoti hiyo. Inakadiriwa kwamba zaidi ya watoto milioni mbili hufa kila mwaka kutokana na maradhi yahusianayo na hali za ukosefu wa afya. Akhtar Hameed Khan, mbuni wa uchunguzi huo, asema hivi: “Uwapo na kiwango kidogo cha usafi wa kutunza afya, ndipo uwapo na kiwango kikubwa cha magonjwa.”
Nyumbani Ni kwa Maana Zaidi
Je, utunzaji wa mchana—uangalizi wa watoto ufanywao na watu wengine wazazi wafanyapo kazi—ni mzuri kwa watoto? Hilo ndilo jambo ambalo uchunguzi uliofanywa Marekani na Taasisi ya Afya ya Watoto na Maendeleo ya Kibinadamu ulitaka kujua. Watafiti maarufu wa afya ya mtoto kutoka vyuo vikuu 14 walifuatilia watoto 1,364 kutoka kuzaliwa hadi umri wa miaka mitatu. Zaidi ya asilimia 20 ya watoto hao walitunzwa na mama zao nyumbani; waliobaki walipelekwa katika vituo vya utunzaji wa watoto au katika nyumba za watunza-watoto wanaolipwa. Matokeo? “Watafiti hao waligundua kwamba watoto katika vituo vilivyo bora vya utunzaji wa watoto—ambavyo katika hivyo watu wazima huongea nao sana katika njia ya kuitikia—walikuwa na faida zaidi kidogo ya watoto katika vituo vyenye uangalifu kidogo kwa habari ya suala la lugha na uwezo wa kujifunza,” lilisema gazeti la Time. “Lakini mkataa mkubwa ulikuwa kwamba matokeo ya utunzaji wa mchana uliathiri kidogo sana maendeleo ya kiakili na kihisia-moyo ya watoto kuliko ubora wa maisha ya familia zao. . . . Watafiti hao walikadiria kwamba kiasi cha asilimia 1 tu ya tofauti miongoni mwa watoto ingeweza kufuatiliwa kuwa kutokana na utunzaji wa mchana lakini asilimia 32 ingeweza kuelezwa kuwa kutokana na hali zinazotofautiana na mambo yaliyowapata katika familia zao. Ujumbe ni nini? Nyumbani ndipo mahali panapofaa sana kujifunzia.”
Urafiki Usio wa Kawaida
Kwa muda mrefu wanasayansi wamekuwa wakistaajabu kuhusu uhusiano kati ya mchwa na miti ya mikakaya ya Afrika. Miti hii huandalia mchwa chakula na kivuli. Mchwa kwa upande mwingine, hushambulia wadudu ambao hutokeza hasara kwa miti hiyo na huwauma wanyama ambao hula majani yake. Yaonekana kwamba miti hii yategemea ulinzi huu ili kuwa hai. Lakini miti hiyo pia yahitaji wadudu warukao kwa ajili ya kuchavua maua yao. Hivyo basi, ni jinsi gani wadudu wanaochavua hupata nafasi ya kufanya kazi zao? Kulingana na jarida moja la sayansi Nature, “miti hiyo inapokuwa katika kilele chake cha kutokeza maua,” hiyo hutoa kemikali fulani ambayo yaonekana kuzuia mchwa. Jambo hili huruhusu wadudu kutembelea maua hayo “kwa wakati ulio muhimu kabisa.” Kisha, baada ya maua kuwa yamechavushwa, mchwa hurudi katika zamu yao ya ulinzi.
Biblia ya Gutenberg Yagunduliwa
Sehemu ya Biblia iliyochapishwa katika karne ya 15 na Johannes Gutenberg katika nyaraka za kanisa katika Rendsburg, Ujerumani. Kufuatia ugunduzi wake mwanzoni mwa mwaka wa 1996, sehemu hiyo ya Biblia yenye kurasa 150 ilichunguzwa kwa uangalifu sana kabla haijatangazwa rasmi kuwa ni Gutenberg halisi, laripoti gazeti la Wiesbadener Kurier. Ulimwenguni pote, Biblia 48 za Gutenberg zinajulikana kuwa zipo, ambapo 20 kati ya hizo ni kamili. “Biblia maarufu za mabuku mawili zilizochapishwa na Johannes Gutenberg zaonwa kuwa kazi ya kwanza ya maana sana katika uchapishaji wa vitabu,” lasema gazeti hilo. Ugunduzi huu wa mwisho “bado una mnyororo wa awali wa kitabu hicho ukiwa mahali pake, ambapo Biblia hiyo ilifungwa katika mimbari ili kuilinda isiibiwe.”
Kuishi Maisha Marefu Zaidi
Jambo gani husaidia mtu kubaki mwenye afya na kuishi maisha marefu zaidi? “Mwelekeo wa utu katika kulinda hali ya moyo isiyobadilika ambayo kwa kiasi kikubwa haina mikazo ya kisaikolojia huendeleza afya ya kimwili zaidi ya vile kufanya mazoezi au tabia za kula zifanyazo,” asema Dakt. George Vaillant wa Brigham na Hospitali ya Wanawake katika Boston. Maoni ya Vaillant yana msingi wa uchunguzi unaoendelea wa wanaume zaidi ya 230 ambao waliandikishwa awali katika mwaka wa 1942. Katika umri wa miaka 52, wanaume ambao walikuwa na afya nzuri waligawanywa katika vikundi vitatu: wale waliofikiriwa kuwa “wamesononeka” (walikuwa wametumia vibaya alkoholi, kwa kawaida walitumia dawa za kutuliza maumivu, au walimwona daktari wa magonjwa ya akili), “wasiosononeka” (kamwe hawakuwa wametumia vibaya alkoholi, hawakumeza dawa za kubadilisha hali ya moyo, au kumwona daktari wa magonjwa ya akili), na “wa katikati” (walikuwa kati ya makundi hayo mawili). Katika umri wa miaka 75, “asilimia 5 tu ya [wasiosononeka] walikuwa wamekufa, kulinganisha na asilimia 25 ya kikundi cha katikati, na asilimia 38 ya wanaume waliosononeka,” laripoti gazeti la Science News. Bila shaka, kudumisha mlo wenye kufaa na kufanya mazoezi kwa kawaida husaidia kutokeza afya njema. Lakini, kuishi maisha “marefu, angalau kwa wanaume, kwaonekana kwategemea mwelekeo wa uimara kihisia-moyo ambao ungefukuzia mbali maumivu makali ya mshuko-moyo,” lasema Science News.