Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g98 12/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—1998
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Msitu wa Mvua Unaotoweka
  • Wanawake na Maradhi ya Moyo
  • Mvunjiko wa Familia Katika Bolivia
  • Nutrino Yapatikana Kuwa na Uzito
  • Jiwe la Sanisia la Kale
  • Tahadhari Wakati wa Kupika
  • Msiwatume Watoto Tu
  • Je, Ni Wonyesho wa Upendo?
  • Muziki Huathiri Wanunuzi
  • Faida za El Niño
  • Kujaribu Kurudisha Washiriki Kwenye Zizi
  • El Niño Ni Nini?
    Amkeni!—2000
  • Mali za Asili za Dunia Zinapungua
    Amkeni!—2005
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—1996
  • Kuutazama Ulimwengu
    Amkeni!—2001
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—1998
g98 12/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Msitu wa Mvua Unaotoweka

Msitu wa mvua wa Amazon unazidi kutoweka kwa kiwango chenye kuogofya. Katika kila mmoja wa miaka mitatu iliyopita, ekari milioni 4.8 zilipotea, ambazo karibu zinatoshana na “viwanja saba vya mpira wa miguu kwa dakika moja,” laripoti gazeti Natural History. Baada ya miti yenye thamani kukatwa, kwa kawaida mimea inayobakia huchomwa ili ardhi itumiwe kwa kilimo. Hata hivyo, “miti na mimea mingine inapokatwa au kuliwa na vijiumbe-maradhi, inatokeza kiasi kikubwa cha kaboni dioksidi, methani, na oksidi nitrasi kwenye angahewa, na kuongezea halijoto.” Tokeo la kutokezwa kwa gesi hizi laweza kuwa “sawa na kuharibu ekari nyinginezo milioni 1 hadi 3 za msitu wa mvua kila mwaka,” lasema gazeti hilo.

Wanawake na Maradhi ya Moyo

Mpaka miaka ya 1960, katika Brazili maradhi ya moyo hasa yalikuwa tatizo la kitiba la wanaume, laripoti gazeti Veja. Hata hivyo, mambo yalianza kubadilika wanawake walipoanza kufanya kazi ya kuajiriwa. Wakati wanawake walipopatwa na “mkazo kazini, kuvuta sigareti na kula vyakula vinavyotayarishwa haraka-haraka,” kama wanaume, wanawake wengi zaidi walianza kupatwa na maradhi ya moyo. Ingawa watu fulani huamini kwamba wanawake wana kinga ya kiasi fulani ya homoni ya kuzuia matatizo ya mishipa, “baada ya kufikisha umri wa miaka 35, kinga ya homoni hupungua, ikiwafanya wanawake wakabili hatari zilezile kama wanaume,” lasema gazeti hilo. Katika mwaka wa 1995, mshtuko wa moyo uliwaua wanawake Wabrazili mara mbili zaidi ya walivyouawa na kansa ya matiti na kansa ya tumbo la uzazi zikiunganishwa.

Mvunjiko wa Familia Katika Bolivia

Zaidi ya asilimia 70 ya wakazi wa Bolivia huishi katika umaskini, laripoti Bolivian Times. Tokeo ni kwamba watoto wengi “huacha familia zao zilizovunjika ili wakaishi kwenye mazingira yaliyo hatari zaidi ya mitaani.” Wakiwa humo wanaonyeshwa namna ya kutumia kokeini na kunusa vitu kama vile mafuta ya rangi na gundi. Inakadiriwa kwamba asilimia 88 ya watumiaji wa dawa za kulevya katika Bolivia ni vijana walio na umri wa kati ya miaka 5 na 24. Hivyo, matumizi haramu ya dawa za kulevya yameongezeka karibu asilimia 150 zaidi ya miaka 15 iliyopita. Kulingana na Times, “wengi wanafikiri kwamba kisababishi kikuu cha ongezeko hili ni mvunjiko wa familia ya kizamani.”

Nutrino Yapatikana Kuwa na Uzito

Nutrino ni punje ya kimsingi isiyokuwa na chaji yoyote, inayosafiri kwa mwendo unaokaribia wa nuru, na huchangamana kwa nadra sana na mata ya aina yoyote. Inasemekana kwamba nutrino zaweza kupita katikati ya dunia bila kugonga atomu hata moja. Ijapokuwa hivyo, hivi karibuni chembe hizi zilipata kujulikana kimataifa wakati wanasayansi katika Takayama, Japani, walipotangaza kwamba nutrino imethibitishwa ina uzito. Kwa kuwa ulimwengu umejaa nutrino, wanasayansi fulani wanasisitiza kwamba jumla ya uzito yake yaweza kuongeza uzito wa kutosha kwenye ulimwengu kupunguza mpanuko wake.

Jiwe la Sanisia la Kale

Waakiolojia wamevumbua uthibitisho wa kwanza wa jiwe lililotengenezwa na mwanadamu, katika Mashkan-shapir, jiji la kale ambalo magofu yake yanapatikana kusini mwa Iraq ya kisasa. Wanajiolojia na waakiolojia wanasema kwamba jiwe hilo lilitengenezwa kwa kuchoma mchangatope kutoka mito Tigri na Frati mpaka uyeyuke na kisha kuupoesha polepole “ili kutokeza vigae vigumu kama mawe mithili ya jiwe la volkano linaloitwa gumawesi,” laripoti The New York Times. Kulikuwa na upungufu wa mali ghafi za ujenzi katika eneo hilo, kwa hiyo gumawesi ya sanisia “yaonekana kuwa ilitengenezwa kwa kiasi fulani kuchukua mahali pa gumawesi ya asili.” Jiwe hilo lililotengenezwa na mwanadamu lilitumiwa kujenga Mashkan-shapir miaka ipatayo 4,000 iliyopita.

Tahadhari Wakati wa Kupika

Kuanzia mwaka wa 1990 hadi 1994, kisababishi kikuu cha kifo miongoni mwa wanawake waliochomeka katika Sumner Redstone Burn Center, katika Hospitali Kuu ya Massachusetts, kilikuwa nguo zilizoshika moto wakati wa upishi, lasema Tufts University Health & Nutrition Letter. Mara nyingi, waliochomeka walikuwa wanawake waliokuwa na umri wa miaka 60 au zaidi na ambao mikono ya mavazi yao ilining’inia juu ya moto wa jiko walipokuwa wakichukua birika. Madokezo yafuatayo yalitolewa ili kuzuia watu wasichomeke vibaya. Unapopika, (1) usivalie mavazi ya kushindia nyumbani au mavazi mengine makubwa. (2) tumia meko yaliyo katika sehemu ya mbele inapowezekana ili kupunguza hatari za kuchomeka wakati wa kuchukua sufuria na vikaango. (3) valia mavazi yasiyoshika moto kwa wepesi.

Msiwatume Watoto Tu

Mwanafunzi wa kidato cha tatu katika somo la kidini alipolalamika kwamba kulikuwa na sheria nyingi mno kwa watoto ilhali watu wazima hawakuwa na zozote, mwalimu aliitikia kwa kuwaomba wanafunzi waandike Amri Kumi zao kwa watu wazima. Kulingana na gazeti la kila siku la Kikatoliki la Ujerumani Christ in der Gegenwart, wanafunzi wengi walihangaikia wema, amani, kutopendelea, ufuatiaji-haki, na ukweli. Orodha ya mtoto mmoja ilisema hivi: “1. Msipendelee. 2. Msikemee sana. 3. Msituharakishe. 4. Msitusumbue sikuzote. 5. Msituchekelee. 6. Msitulazimishe. 7. Mwe mkikiri kwamba tuko sawa mara mojamoja. 8. Msijibunie sheria zenu wenyewe. 9. Mpatane. 10. Nyinyi wenyewe mwende kanisani, msiwatume watoto tu.”

Je, Ni Wonyesho wa Upendo?

“Upendo na kufanya ngono ni mambo yanayohusiana kwa ukaribu kwa wavulana,” yasema ripoti moja katika nyongeza ya gazeti la habari la Afrika Kusini Witness Echo, “na wasichana waliobalehe huelekea kupigwa wanapokataa kufanya ngono.” Utafiti uliofanyiwa vijana katika kitongoji kimoja cha Cape Town ulifunua kwamba “wanaume ndio hudhibiti mahusiano hayo, mara nyingi wakitumia jeuri kuwalazimisha wasichana wafanye ngono nao.” Uchunguzi mmoja ulionyesha kwamba asilimia 60 ya wasichana walikuwa wamepigwa na wenzi wao, hata kwa kuongea na wanaume wengine. “Kushambuliwa kimwili ni kwa kawaida sana,” yaongezea ripoti hiyo, “hivi kwamba wengi wa marika wao wa kike hukuona kuwa wonyesho wa upendo.”

Muziki Huathiri Wanunuzi

Katika nchi ya Uingereza, kikundi cha wanasaikolojia kutoka Chuo Kikuu cha Leicester kiligundua kwamba muziki wa chinichini ungeweza kuathiri uchaguzi wa wanunuzi wa divai. “Muziki wa kodiani wa Ufaransa ulipochezwa, divai ya Ufaransa iliuzwa kwa wingi wa chupa tano kwa kila chupa moja ya Ujerumani,” lasema gazeti National Geographic. “Lakini muziki wa Ujerumani ulipochezwa, wanunuzi walinunua chupa mbili za divai ya Ujerumani kwa kila chupa moja ya Ufaransa.” Kwa kupendeza, ni wanunuzi wachache tu waliotambua kwamba “muziki ulichangia fungu kubwa katika uamuzi wao,” asema mmoja wa watafiti hao.

Faida za El Niño

Tukio la maji moto linaloitwa El Niño “limelaumiwa kwa kila kitu kuanzia dhoruba zenye kuua huko Marekani hadi mioto ya porini katika Brazili na mazao haba ya kahawa nchini Kenya,” laripoti shirika la habari la Reuters. Hata hivyo, licha ya dhoruba na ukame, wataalamu wanadai kwamba El Niño ilileta faida pia. Kulingana na ripoti hiyo, uzalishaji wa kahawa nchini Brazili “unatazamiwa kufikia magunia milioni 35 msimu huu, kiwango cha juu zaidi katika mwongo huu,” na “mvua zisizotazamiwa katika sehemu zisizotazamiwa zimejaza tena mabwawa ya maji ulimwenguni pote.” Mkurugenzi wa Kituo cha Kutabiri Tabia ya Nchi cha Marekani Ants Leetmaa alisema: “Katika sehemu nyingi za ulimwengu kuna tatizo la upungufu wa maji. Mengi ya maeneo haya yalihitaji maji. . . . Mameneja wa maji walikuwa wakitazamia El Nino.”

Kujaribu Kurudisha Washiriki Kwenye Zizi

Watu wanaokadiriwa kuwa 1,500 huacha kwenda makanisani kila juma nchini Uingereza. Ijapokuwa zaidi ya asilimia 50 ya watu wa Uingereza hudai kuwa Wakristo, ni asilimia 10 tu wanaoenda kanisani kwa ukawaida. Kwa nini? Makanisa nchini Uingereza “mara nyingi yamelaumiwa kuwa yasiyofaa, yasiyowasiliana na watu na yenye kuchosha,” asema kasisi Steve Chalk. Katika jitihada za “kuwatia moyo watu waanze kwenda kanisani,” Askofu Mkuu wa Canterbury na Askofu Mkuu wa Westminster “wanaunga mkono njia mpya inayokusudiwa kusaidia makanisa yafurahishe zaidi, yahusishe jamii na yavutie zaidi,” laripoti shirika la habari la BBC News. Kufikia Januari 2, 2000, makanisa yanatumaini kutekeleza “miradi 10 iwezayo kutumika.” Inatia ndani: “Tutawafurahisha, tutakuwa wenye fadhili na wenye nia njema, tutahakikisha kwamba mnasikia waziwazi, . . . tutawasaidia mpate majibu ya maswali yenu ya kina kirefu, . . . tutahakikisha kuja kwenu kutakuwa kwenye kusaidia lakini kwenye kuvutia.”

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki