Watchtower MAKTABA KWENYE MTANDAO
Watchtower
MAKTABA KWENYE MTANDAO
Kiswahili
  • BIBLIA
  • MACHAPISHO
  • MIKUTANO
  • g01 6/8 kur. 28-29
  • Kuutazama Ulimwengu

Hakuna video yoyote kwa sasa.

Samahani, haikuwezekana kupakia video.

  • Kuutazama Ulimwengu
  • Amkeni!—2001
  • Vichwa vidogo
  • Habari Zinazolingana
  • Watoto Wadogo na Muziki Mchafu
  • “Mtakatifu” Columbus?
  • Kuepuka Deni
  • Ustadi wa Kutumia Tena Vitu Vilivyotumiwa
  • Vijusi Hujifunza na Vina Kumbukumbu
  • Wanawake na Ugonjwa wa Moyo
  • Wanawake Waingereza na Kansa ya Mapafu
  • Kuhifadhi Chakula Kisiharibike Bila Kutumia Friji
  • Aina Mbili za Wanyama Hutoweka Kila Juma Ulimwenguni
  • Mambo Ambayo Wanawake Wapaswa Kujua Juu ya Kansa ya Matiti
    Amkeni!—1994
  • Kansa ya Matiti Utazamie Nini? Ukabiliane Jinsi Gani?
    Amkeni!—2011
  • Njia za Kuokoka Kansa
    Amkeni!—1994
  • Sigareti—Je, Wewe Huzikataa?
    Amkeni!—1996
Pata Habari Zaidi
Amkeni!—2001
g01 6/8 kur. 28-29

Kuutazama Ulimwengu

Watoto Wadogo na Muziki Mchafu

Gazeti la Chicago Tribune laripoti kwamba watoto wa umri wa miaka saba au minane wanasikiliza muziki mchafu, wenye maneno yanayokazia ngono, na ujeuri. “Zamani, watoto wa shule ya wachanga hadi wale wa shule ya msingi walikuwa na muziki wao wa ‘kitoto,’” lakini “yamkini watoto wengi wa shule za msingi leo, husikiliza vipindi vilevile vya redio ambavyo wazazi wao na ndugu zao matineja husikiliza.” Ingawa ni lazima kampuni za kurekodi muziki huko Marekani ziweke vibandiko vya kuonya juu ya diski za muziki wenye maneno ya ujeuri au yanayokazia ngono ili watoto wasizinunue, watoto wanaweza kusikiliza muziki huo kwa urahisi kwenye maduka ya kusikilizia kanda za muziki. Diane Levin, wa Chuo cha Wheelock huko Boston, ambaye ni mtaalamu wa vitumbuizo na tabia za watoto, alionya hivi: “Mambo yanapozidi kupita kiasi hatushtuki tena.”

“Mtakatifu” Columbus?

“Vatikani inahimizwa imfanye Christopher Columbus kuwa mtakatifu,” laripoti gazeti The Times la London. Wasomi wanaochunguza hifadhi za nyaraka za Vatikani wanadai kwamba si Mfalme Ferdinand na Malkia Isabella wa Hispania waliogharimia safari za Columbus, bali Papa Innocent wa Nane ndiye aliyemtuma kwa siri ili akusanye fedha za kutegemeza zile Krusedi na “kuwabadilisha watu kuwa Wakristo.” Ujumbe ulioandikwa na Papa Pius wa Tisa katika mwaka wa 1851, wasema hivi: “Kuna uthibitisho ulio wazi kabisa kwamba Columbus alitimiza mradi wake bora sana kwa msaada na utegemezo wa papa huyo.” Papa aliyefuata, aliyeitwa Leo wa 13, alimtaja Columbus kuwa “mtu wa Kanisa.” Hata hivyo, Columbus aliporudi Hispania katika mwaka wa 1493, haki za mavumbuzi yake zilipitishwa rasmi kwa milki ya Hispania na Papa Alexander wa Sita aliyekuwa Mhispania wa Borgia. Alikuwa mwandamizi wa Innocent wa Nane.

Kuepuka Deni

Kikundi kinachochunguza ununuzi katika Muungano wa Uingereza “kimeanzisha kampeni kubwa yenye kichwa, Usiruhusu mkopo uwe deni, ili kuwaonya watu kuhusu hatari za kuwa na madeni mengi,” yaripoti Newstream.com. Kwa mujibu wa Shirika la Biashara ya Haki (OFT), mikopo inayotolewa katika Muungano wa Uingereza imeongezeka kwa zaidi ya asilimia 60 katika miaka minne iliyopita. Isitoshe, sasa raia wa kawaida ana deni lisilo na dhamana la dola 3,700 hivi za Marekani. Shirika la OFT ladokeza ufanye jambo lifuatalo kabla ya kupata mkopo: “Jiulize ikiwa kweli unaweza kulipa.” Pili, tafuta kiwango cha riba kilicho nafuu. Watu wengi hutafuta bei nafuu wanaponunua bidhaa lakini wanapotafuta mkopo wanakubali kiwango chochote cha riba kinachotozwa na mkopeshaji. Linganisha viwango vya riba vinavyotozwa kila mwaka na benki au makampuni ya kadi za mkopo, ili uone ikiwa utapata mkopo unaotozwa riba nafuu. Na tatu, ukilemewa na madeni, omba msaada.

Ustadi wa Kutumia Tena Vitu Vilivyotumiwa

Kwa kutumia chupa za plastiki ambazo kwa kawaida hutumiwa mara moja tu, kikundi cha wakulima kilijenga mfereji wa maji wa kilometa nane karibu na Trujillo, kaskazini mwa Peru. Kwa mujibu wa gazeti la Lima El Comercio, wakulima 81 walinunua ardhi kame na wakapata sehemu yenye maji. Lakini hawakuweza kununua bomba la kupeleka maji kwenye ardhi yao. Ili kulitatua tatizo hilo, mkulima mmoja alidokeza jambo fulani. Walinunua chupa za maji zilizotupwa na wakatumia siku 14 kukata sehemu za juu na za chini na kuunganisha chupa 39,000 ziwe mfereji mmoja. Mfereji huo utatumiwa kusambaza maji kwa muda kabla ya kisima kuchimbwa.

Vijusi Hujifunza na Vina Kumbukumbu

“Watoto hawajifunzi tu wanapokuwa tumboni lakini pia wana kumbukumbu la muda mfupi la mambo yaliyotukia dakika 10 zilizopita na vilevile kumbukumbu la muda mrefu la mambo yaliyotukia saa 24 zilizopita,” laripoti shirika la habari la Reuters. Wachunguzi Waholanzi kwenye Hospitali ya Chuo Kikuu huko Maastricht, walitumia mitetemo na sauti kuviamsha “vijusi 25 vyenye umri wa kati ya majuma 37 na 40 katika tumbo la uzazi.” “Walichunguza jinsi vilivyoitikia kupitia mashine inayopiga picha sehemu mbalimbali za mwili kwa kutumia mawimbi ya sauti.” Baada ya majaribio ya kwanza kufanywa, vijusi hivyo viliamshwa tena baada ya kila dakika 10 na saa 24. “Iwapo mtoto angesogeza mguu sekunde moja baada ya kuamshwa, hilo lingeonyesha kwamba hakukumbuka,” lasema shirika la Reuters. Lakini “ikiwa mtoto hakuitikia baada ya kuamshwa mara nne mfululizo, hiyo ilionyesha alikuwa amekumbuka sauti na mitetemo hiyo.” Wanasayansi waliona kuwa majaribio yaliporudiwa, vijusi vilizoea sauti hiyo na havikuisogeza miguu tena. Hiyo ilionyesha kwamba vilikumbuka sauti na mitetemo hiyo.

Wanawake na Ugonjwa wa Moyo

“Kwa kawaida, ugonjwa wa moyo huonwa kuwa ugonjwa unaowapata wanaume, hata ingawa idadi ileile ya wanaume na wanawake hufa kutokana na ugonjwa huo kila mwaka,” laripoti gazeti la The Toronto Star. Gazeti hilo lasema kuwa wanawake hugunduliwa na ugonjwa huo inapokuwa kuchelewa mno. Dalili za ugonjwa wa moyo—ambao ndio kisababishi kikuu cha kifo kule Amerika Kaskazini—huwa tofauti katika wanaume na wanawake. “Wanaume huhisi maumivu kifuani yanayoweza kusambaa hata kwenye shingo, mgongo na mabega, lakini mara nyingi wanawake huumwa na taya, hupata matatizo ya kupumua na kichefuchefu,” lasema gazeti la Star. Wanawake walio na miaka zaidi ya 55 hasa wanapata dalili hizo wakati estrojeni inapokwisha. ‘Estrojeni inapokwisha mwilini idadi ya wanawake wanaoumia kutokana na ugonjwa wa moyo huwa sawa na idadi ya wanaume,’ asema Dakt. Stephanie Brister, mpasuaji wa moyo kwenye Hospitali Kuu ya Toronto.

Wanawake Waingereza na Kansa ya Mapafu

Gazeti la The Daily Telegraph la London laripoti kuwa ‘kwa mara ya kwanza, wanawake Waingereza wanaokufa kutokana na kansa ya mapafu ni wengi zaidi kuliko wanaokufa kutokana na kansa ya matiti. Basi kati ya magonjwa yote ya kansa yanayowakumba wanawake, ugonjwa huo ndio unaowaua zaidi.’ Wanawake wanaokufa sasa kutokana na ugonjwa huo ni wale walioanza kuvuta sigareti miongo minne iliyopita wakati zoea hilo lilipotangazwa kuwa njia ya kupunguza uzito. Kampeni ya Uchunguzi wa Kansa huko Uingereza ilisema kuwa katika miaka 20 iliyopita, idadi ya wanawake wanaokufa kutokana na kansa ya matiti ilipungua kwa asilimia 5, ilhali idadi ya wale wanaokufa kutokana na kansa ya mapafu iliongezeka kwa asilimia 36. Katika kipindi hichohicho, idadi ya wanaume waliokufa kutokana na kansa ya mapafu ilipungua kwa asilimia 31, ikionyesha kuwa wanaume wengi wanaacha kuvuta sigareti. Profesa Gordon McVie, msimamizi wa kampeni hiyo, anasema kwamba licha ya maonyo yanayotolewa “wasichana wengi zaidi ya wavulana wanaanza zoea hilo.”

Kuhifadhi Chakula Kisiharibike Bila Kutumia Friji

Kuhifadhi na kudumisha chakula kikiwa baridi bila kutumia friji ni jambo gumu. Hata hivyo, njia rahisi na ya bei nafuu ya kuhifadhi vitu, inawafaidi watu sana katika eneo lisilo kame sana, kaskazini mwa Nigeria. Inahusisha kuingiza chungu cha udongo ndani ya chungu kingine na kujaza nafasi iliyo katikati kwa mchanga wenye unyevunyevu. Chakula kinawekwa ndani ya kile chungu kidogo, kisha chungu kinafunikwa kwa kitambaa chenye unyevunyevu. ‘Hewa yenye joto huvuta mvuke nje ya vyungu, kisha unavukizwa,’ lasema gazeti la New Scientist. “Mvuke wa maji hutoka pamoja na joto, basi utendaji huu wa kukausha hufanya joto liendelee kutoka ndani ya chungu maadamu mchanga na kitambaa vinadumishwa vikiwa na unyevunyevu.” Mbinu hii inapotumiwa, nyanya na pilipili zaweza kubaki bila kuharibika kwa zaidi ya majuma matatu na biringanya kwa mwezi mmoja hivi. Mohammed Bah Abba, aliyebuni njia hii ya “kuweka chungu ndani ya chungu,” asema kwamba sasa wakulima wanaweza kuuza mazao yao wakati yanapohitajiwa. Na binti zao, ambao kwa kawaida walikuwa wanabaki nyumbani kila siku ili kuuza chakula, wanaweza kuenda shule.

Aina Mbili za Wanyama Hutoweka Kila Juma Ulimwenguni

Gazeti la Italia la Corriere della Sera laripoti kwamba aina mbili za wanyama wa kufugwa hutoweka kila juma, na huenda aina 1,350 zitatoweka. Wachunguzi kutoka kwenye Shirika la Chakula na Kilimo la UM (FAO) walitumia miaka kumi kuchunguza wanyama na ndege 6,500 wa kufugwa katika nchi 170. Kulingana na Dakt. Keith Hammond, ofisa mkuu wa Kundi la Uchunguzi wa Chembe za Urithi za Wanyama la FAO, “iwapo hakuna hatua itakayochukuliwa, theluthi moja ya aina ya wanyama wanaozaa watatoweka katika miaka 20 inayokuja.” Ripoti moja ya Reuters kutoka Roma yaeleza kuwa kuwauza wanyama wa nchi zilizositawi katika nchi nyingine kumechangia sana tatizo hilo. Wanyama wanaoingizwa ndani ya nchi nyingine wanaweza kujamiiana na wanyama wa nchi hiyo, na kusababisha jamii za nchi hiyo zitoweke. “Hata hivyo, tatizo ni kwamba wanyama hao wamezoea mazingira ya nchi waliyotolewa na hupata ugumu wa kukabiliana na mazingira magumu ya nchi zinazositawi,” asema Dakt. Hammond.

    Maktaba Kwenye Mtandao (1980-2025)
    Toka
    Ingia
    • Kiswahili
    • Shiriki
    • Mapendezi
    • Copyright © 2025 Watch Tower Bible and Tract Society of Pennsylvania
    • Masharti ya Utumiaji
    • Sera ya Faragha
    • Mpangilio wa Faragha
    • JW.ORG
    • Ingia
    Shiriki