Alama Usoni ‘Kitambulisho’ cha Nigeria Kinachotoweka
NA MLETA-HABARI WA AMKENI! KATIKA NIGERIA
ASUBUHI moja mwishoni-mwishoni mwa miaka ya 1960, Danjuma mwenye umri wa miaka sita alimwendea baba yake na kusisitiza apate chanjo ambazo Waigala walionea fahari nyusoni mwao. Danjuma alihisi kwamba hangeweza kuvumilia tena kamwe dhihaka za wanashule wenzake waliomdhihaki kwamba hakuwa na alama usoni. Ijapokuwa kwa kawaida vitoto vichanga vya Waigala visivyoweza kuhofu utendaji huo ndivyo huchanjwa, wavulana waliziona alama hizo kuwa ishara ya ujasiri. Waliwaona wasiokuwa nazo kuwa waoga ambao hawangeweza kustahimili makali ya kisu.
Hadi wakati huo, baba ya Danjuma alikuwa amekataa kumchanja mwanawe usoni. Lakini asubuhi hiyo, akisongwa na azimio la mwanawe la kuthibitisha ujasiri wake, alichukua kisu na kufanyiza mikato mitatu ya mlalo yenye kina pande zote mbili za uso wa kijana huyo, juu kidogo ya kona za mdomo wake.
Baba ya Danjuma alijua kwamba umuhimu hasa wa chanjo hizo za chale haukuwa hasa ujasiri. Badala yake, chanjo hizo zingepona na kuwa makovu ya utambulisho. Zingekuwa ‘kitambulisho’ cha kudumu ambacho hakingepotea wala kuigwa. Zingemtambulisha mwana wake mara moja kwa watu wa ukoo, zikimfanya astahili kupata haki na mapendeleo ya Waigala. Vilevile alama hizo zingemtofautisha na makabila mengine ya Nigeria yapatayo 250.
Ijapokuwa chanjo haziko Afrika pekee, zina historia ndefu barani Afrika. Katika karne ya tano K.W.K., mwanahistoria Mgiriki Herodotus aliandika juu ya Wakaria walioishi Misri hivi: “[Wao] huchanja vipaji vya nyuso zao kwa visu, hivyo, wakijithibitisha kuwa wageni wala si Wamisri.” Vichwa vilivyotengenezwa kwa shaba vilivyoundiwa Ife, Nigeria, miaka mia saba iliyopita vyaonyesha alama zionwazo na wengi kuwa za kikabila. Alama usoni pia zaweza kuonekana katika sanamu za kuchongwa katika Benin, ufalme wa kale wa Nigeria.
Si alama zote usoni zinazotambulisha kabila la mtu. Alama fulani zilikuwa, na zingali zahusianishwa na mazoea ya uasiliani na roho waovu na ya kidini. Nyingine ni ishara ya hadhi katika jamii za kitamaduni. Nyingine nazo ni alama za mapambo.
Alama usoni hutofautiana sana zifanywapo na wataalamu katika jumuiya. Nyingine ni michibuo midogo kwenye ngozi, hali nyingine ni mikato mikubwa iwezayo kupanuliwa kwa vidole. Nyakati nyingine rangi fulani ya kienyeji hutiwa kwenye donda ili kuzitia rangi alama hizo. Kila kabila lina alama zake za kipekee. Kwa mfano, alama za wima, moja kwa kila shavu, huwatambulisha wanaume na wanawake Waondo. Alama tatu za mlalo kwa kila shavu huwatambulisha Waoyo. Kwa wenye ujuzi wa alama hizi, kule kutazama tu uso wa mtu, kwatosha kujua kabila, mji, au hata familia ya mtu.
Mitazamo Yenye Kutofautiana
Kama tu vile alama hizo na sababu zake zinavyotofautiana sana, ndivyo ilivyo na mitazamo inayozihusu. Watu wengi huzionea fahari alama hizo. Mhariri mmoja wa gazeti Daily Times la Nigeria alitaarifu hivi: “Watu fulani huziona alama hizo kama ishara ya uzalendo. Huwafanya wajihisi kuwa wana wa kweli wa mababu zao.”
Haya ndiyo maoni ya Jimoh, Mnigeria, asemaye hivi: “Sijawahi kuonea haya alama zangu za Oyo kwa kuwa hunitambulisha kuwa Myoruba halisi mzaliwa wa Alafin.” Aeleza zaidi jinsi mwaka wa 1967 alama hizo zilivyomwokoa wakati wa Vita vya Wenyewe kwa Wenyewe vya Nigeria: “Nyumba niliyoishi . . . ilivamiwa na [wengine] wote wakauawa. Wauaji hawakunigusa kwa sababu ya alama usoni mwangu.”
Wengine huchukizwa sana na alama hizo. Tajudeen asema juu ya alama usoni mwake hivi: “Naichukia, tena nailaani siku niliyochanjwa.” Naye msichana tineja humsifu mamaye kwa kutomruhusu kuchanjwa alipokuwa mtoto. Yeye asema hivi: “Ningefikiria kujiua iwapo ningetiwa alama hizo.”
Kukabiliana na Dhihaka
Danjuma, aliyetajwa kwenye utangulizi, alidhihakiwa kwa sababu hakuwa na alama hizo. Kwa kawaida hali huwa tofauti. Zaidi ya miaka 45 iliyopita, G. T. Basden aliandika hivi katika kitabu chake Niger Ibos: “Kuchanjwa na kupigwa chale kwaelekea kuwa kwa kikale. Vijana wengi . . . wangefurahia kuondolewa [alama zao]. Linaloonekana kuwa jambo la fahari, miongoni mwa watu wa ukoo, huwa aibu kwa sababu ya dhihaka na dharau anayopata mtu katika sehemu nyingine za nchi.”
Maneno hayo ni ya kweli kabisa leo. Ajai, aliyetunukiwa shahada ya saikolojia kwenye Chuo Kikuu cha Lagos, hivi majuzi alijifunza juu ya alama usoni nchini Nigeria. Yeye asema hivi: “Walio na alama usoni, siku hizi, angalau katika majiji kama vile Lagos, ndio wachache zaidi, nao hukutana na watu wanaowadhihaki. Kwa kielelezo, ni kawaida kuwasikia watu wakimrejezea mtu kuwa kanali, na kumbe hata si mwanajeshi, lakini kwamba idadi ya mistari mashavuni mwake yalingana na mistari ipatikanayo kwenye yunifomu ya kanali katika Jeshi. Wengine huitwa simbamarara kwa sababu ya mashavu yao yenye mistari au wengine huitwa machozi ya milele. . . . Wazia jinsi ile hali ya kujistahi ya mtu inavyoweza kuathiriwa na hilo.”
Labda mitihani migumu zaidi hukabiliwa shuleni. Samuel ndiye peke yake aliyekuwa na alama usoni darasani. Aeleza hivi: “Shuleni nilidhihakiwa sana. Wanashule wenzangu waliniita ‘reli,’ na ‘kijana mwenye reli.’ Nyakati zote walinidhihaki na kuinua vidole vitatu. Jambo hilo lilinifanya nijihisi duni.”
Yeye alikabilianaje na hilo? Samuel aendelea kusema: “Siku moja dhihaka hizo zilikuwa nyingi mno hivi kwamba nilimwendea mwalimu wangu wa biolojia na kumwuliza iwapo ingewezekana kuziondoa alama hizo. Aliniambia ingewezekana kupitia kurekebishwa uso, lakini nisijali kwani watu wengi katika Nigeria wana alama. Aliniambia marika wangu walinifanyia mzaha kwa sababu wao hawakuwa wakomavu, lakini kwamba tutakapokua, dhihaka zote hizo zitakoma. Alisema pia kwamba alama hizo hazingeamua nilikuwa mtu wa aina gani, au ningekuwa mtu wa aina gani baadaye.
“Hilo lilinifanya nijihisi nafuu zaidi, na zile hisia mbaya nilizokuwa nazo zikatokomea. Watu hawazungumzii sana alama zangu sasa. Hata wanapozirejezea, mimi hutabasamu tu. Uhusiano wangu na wengine haujadhoofika. Watu huniheshimu kwa jinsi nilivyo, si kwa sababu ya kuwa na alama.”
Desturi Inayofifia
Kwa sababu ni wachanga wanaochanjwa, Wanigeria wengi wenye nyuso zenye alama za kikabila hawangeepuka hili. Hata hivyo, wanapokuwa wazazi, ni lazima waamue iwapo watawachanja watoto wao au la.
Watu wengine huamua kufanya hivyo. Kulingana na gazeti Times International la Lagos, kuna sababu kadhaa za kufanya uamuzi huu. Gazeti hilo lataarifu hivi: “Watu fulani bado huona hilo kuwa jambo lenye kurembesha. Wengine huamini alama za kikabila zaweza kusaidia kujua asili ya mwenye alama kwa makusudi ya kumwonyesha upendeleo. Utumizi mwingine ni katika kutambua uhalali wa mtoto katika mazingira ya kitamaduni.”
Hata hivyo, leo, wazazi wanaozidi kuongezeka hawachochewi na sababu hizi. Hata miongoni mwa waoneao fahari alama zao, ni wachache walio tayari kuhatarisha nyuso za watoto wao kwa kisu cha mtiaji wa alama wa kikabila. Hasa hivi ndivyo ilivyo majijini. Yale maumivu na hatari ya kuambukizwa pamoja na dharau na ubaguzi ambao mtoto aweza kukabili baadaye maishani, zote hizo ni sababu ziwafanyazo wazazi kukataa alama usoni.
Kwa wazi, kupendwa na watu wengi, na kukubalika kwa alama usoni kunatoweka upesi. Yaonekana kwamba katika Nigeria ya wakati ujao, ‘kitambulisho’ kitakuwa kitu kinachobebwa na watu katika vibeti vyao, wala si nyusoni mwao.
[Picha katika ukurasa wa 23]
Alama usoni hutambulisha makabila
[Picha katika ukurasa wa 24]
Kutiwa alama usoni ni utamaduni unaotoweka