Mipango ya UM ya Kuwasaidia Vijana—Je, Ina Mafanikio Kadiri Gani?
MIAKA 15 hivi iliyopita, UM ulitangaza mwaka wa 1985 kuwa Mwaka wa Kimataifa wa Vijana. Kwa kuongezea, miaka minne hivi iliyopita, UM ulianzisha Mpango wa Ulimwengu wa Kuwasaidia Vijana Kufikia Mwaka wa 2000 na Kuendelea. Ilidhaniwa kwamba mipango hii ingesaidia kupunguza matatizo na kuongeza fursa za kujiendeleza kwa vijana wanaozidi bilioni moja ulimwenguni pote. Je, mipango hii iliboresha maisha ya vijana?
Bila shaka mipango hii ilifanikiwa katika maeneo fulani. Gazeti Choices, linalochapishwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo, latoa mifano: Nchini Thailand mwaka wa 1982, zaidi ya nusu ya watoto ambao hawakuwa wamefikia umri wa kwenda shule waliugua utapiamlo. Hata hivyo, katika muda unaopungua miaka kumi, utapiamlo wa kadiri na ule mbaya sana ulikuwa karibu umemalizwa. Nchini Omani, kulikuwa na shule tatu pekee mwaka wa 1970 na ni wavulana 900 tu waliohudhuria shule hizo. Lakini mwaka wa 1994, karibu watoto 500,000 katika nchi hiyo walikuwa wakienda shule, na asilimia 49 ya idadi hiyo walikuwa wasichana. Bila shaka, hayo ni mafanikio kwa kiasi fulani.
Ingawa hivyo, kichapo cha UM kiitwacho United Nations Action for Youth chaeleza kwamba hasa katika mataifa yanayositawi, mafanikio hukumbwa na matatizo yasiyokoma yanayohusu elimu, kazi ya kuajiriwa, na umaskini, na haya ni maeneo machache tu ambayo hilo Shirika la Ulimwengu linajitahidi kuboresha.
Kwa mfano, mataifa mengi yanayositawi hayatafikia mradi wa kuwapa watoto wote elimu ya msingi kufikia mwaka wa 2000. Wazazi wengi katika nchi hizi hawawezi kuwasomesha watoto wao kwa sababu shule haziko au hawawezi kugharimia karo. Tokeo ni kwamba, chasema kichapo United Nations Action for Youth, “idadi ya watu wasiojua kusoma na kuandika itaendelea kuongezeka.” Na kutojua kusoma na kuandika huchangia ukosefu wa kazi ya kuajiriwa, na ukosefu wa kazi ya kuajiriwa hutokeza matatizo ya kijamii, kama vile “kukosa kujistahi, kutengwa na jamii,” kupoteza vipawa vya ujanani, na umaskini wa kupita kiasi. Na ingawa umaskini huwapata wote vijana kwa wazee, wenye kudhuriwa zaidi ni vijana. Kichapo hichohicho cha UM chafikia mkataa kwamba licha ya juhudi nyingi, “njaa na utapiamlo zingali miongoni mwa matatizo makubwa sana kwa binadamu yasiyoweza kuondolewa kwa urahisi.”
Ingawa mipango mingi yenye nia njema na wataalamu wanaofanya kazi kwa bidii wanatokeza maendeleo fulani, hawawezi kuondoa visababishi vya matatizo ya kijamii. Mengi zaidi yanahitajika ili kutimiza hilo. Kama vile kitabu Mensenrechten en de noodzaak van wereldbestuur (Haki za Binadamu na Uhitaji wa Utawala wa Ulimwengu) chasema, matatizo ya ulimwengu yatatatuliwa tu ‘ikiwa serikali ya ulimwengu itakayokuwa na uwezo wa kuchukua hatua imara itapatikana.’ Basi, haishangazi kwamba Wakristo—vijana kwa wazee—wanautazamia Ufalme wa Mungu unaokaribia, serikali ya ulimwengu ambayo Yesu aliwaambia wanafunzi wake wasali juu yake. (Danieli 2:44; Mathayo 6:9, 10) Serikali hiyo kwa kweli italeta mabadiliko!
[Picha katika ukurasa wa 31]
Elimu ni haki ya msingi na watoto wote wanaihitaji
[Hisani]
WHO photo by J. Mohr
[Hisani ya Picha katika ukurasa wa 31]
FAO photo/F. Mattioli
Logo: UN photo