Mimea Dhidi ya Uchafuzi
KUONDOA vichafuzi kutoka kwenye udongo na maji zilizochafuliwa, mara nyingi huwa ni kazi inayochukua muda mrefu, ghali, na ngumu. Hata hivyo, mimea ya kawaida imeweza kujifanyia kazi hiyo.
Wanasayansi wanafikiria kutumia aina ya kawaida ya magugu yapatikanayo katika vidimbwi na namna ya ua dogo liitwalo periwinkle kusafisha maeneo ya zamani ya kuwekea silaha na kurudisha ardhi katika hali nzuri. Katika majaribio, aina ya magugu ya vidimbwi yaliyoondolewa vijidudu, parrot feather na ua la periwinkle zilitoa sumu ya TNT vizuri sana hivi kwamba katika juma moja hakukuwa na dalili yoyote ya vilipukaji vilivyosalia katika tishu za mimea hiyo, wala kuchoma mimea hiyo hakukutokeza mlipuko! Watafiti wengine waligundua kwamba chembe za mimea ya kawaida ya kiazi-sukari na vitolewaji vyake vyaweza kufyonza na kuvunja-vunja aina ya sumu iitwayo nitroglycerin.
Vipi juu ya maji yaliyochafuliwa sana na unururifu? Yaonekana alizeti husaidia. Alizeti za majuma sita zilitumiwa kushughulikia tatizo la maji machafu yaliyokuwa katika kiwanda kisichotumiwa cha urani katika Ohio, Marekani. Tokeo lilikuwa nini? Uchafuzi wa urani ulipunguzwa kutoka wastani wa mikrogramu 200 kwa lita moja hadi chini ya kiwango cha usalama cha mikrogramu 20 kwa lita moja. Majaribio mengine yaliyofanywa kwenye tanuri ya Chernobyl karibu na Kiev, yalionyesha kwamba alizeti zilifyonza asilimia 95 ya nururishi ya strontium na cesium katika siku kumi!
Huenda hivi karibuni wakulima wakaanza kutumia airisi ya manjano na aina ya unyasi katika jitihada za kuepuka kuchafua vijito vya maji kwa dawa za kuua wadudu na za kuua mimea. Hatua hii ya kuondoa uchafu hasa hufanywa na vijiumbe-maradhi vilivyo katika mizizi ya mimea ambavyo huvunja-vunja vichafuzi hivyo na kusafisha maji.
Vielelezo vilivyo juu vinatoa kielezi cha uwezo wenye kustaajabisha wa dunia kuweza kujisafisha yenyewe.